Je, Ni Haki kwa Serikali Kuwaweka Rumande Washtakiwa Halafu Kufuta Kesi Bila Kuwalipa Fidia?

Wadau wanasema siyo haki, wataka mageuzi yafanyike kwenye mfumo wa utoaji haki jinai nchini.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Wadau wa haki jinai nchini Tanzania wamekosoa utaratibu wa Serikali wa kuwafungulia mashtaka wananchi na kuwaweka rumande kwa kuwanyima dhamana halafu kuja kufuta kesi kwa kigezo cha kwamba haina nia ya kuendelea nazo huku washtakiwa wakiachwa bila kupewa haki yoyote, kama vile fidia.

Wadau hao wamesema siyo haki kwa Serikali kufanya hivyo, wakitaka mageuzi ya msingi kufanyika kwenye mfumo mzima wa utoaji wa haki jinai Tanzania ili kuepusha aina hizo za usumbufu kujitokeza mara kwa mara.

The Chanzo haikufanikiwa kupata majibu kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Sylvester Mwakitalu baada ya simu yake kuita bila kupokelewa. Hali ilikuwa hivyo hivyo kwa Waziri wa Katiba na Sheria Dk Damas Ndumbaro.

“Suala hili lote, kwa ujumla, siyo sawa, siyo haki,” Tito Magoti, mwanaharakati aliyemstari wa mbele kupigania mageuzi kwenye mfumo wa utoaji haki jinai nchini, alisema kwenye mahojiano na The Chanzo. “Hii ni kwa sababu suala hili linakiuka misingi ya utu na haki za binadamu.”

SOMA ZAIDI: Hivi Ndivyo Serikali Inavyoweza Kuuboresha Mfumo wa Haki Jinai Tanzania

Kuachiwa Mahabusu

Maoni ya wanaharakati hao yanakuja wakati ambao Serikali imeendelea kuwaachia huru watu mbalimbali waliokuwa wamewekwa magerezani kwa miezi kadhaa wakishtakiwa kwa makosa mbalimbali.

Miongoni mwao ni wanachama na viongozi wa CHADEMA waliopewa kesi mbalimbali kabla na baada tu ya Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Mnamo Agosti 4, 2022, kwa mfano, Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Sumbawanga ilimuachia huru kada wa CHADEMA na aliyekuwa diwani wa kata ya Isengule Oscar Sangu na wenzake watano baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kutosha wa kuwatia hatiani.

Walioachiwa huru kwenye kesi hiyo pia ni Emanuel S. John, Respic J. Namwala, Busiga Clement, January Katuhu na Mickson Makatale.

SOMA ZAIDI: Ben Ishabakaki: Katiba Mpya Italeta Mageuzi Kwenye Mfumo wa Utoaji Haki Tanzania

Kuachiwa kwao kulikuja siku chache baada ya Mahakama jijini Mbeya kuwaachia huru vijana saba wa CHADEMA waliokuwa wanakibiliwa na kesi za mauaji.

Kuachiwa kwa makada hawa wa CHADEMA kunafanya idada ya vijana wa chama hicho cha upinzani wanaoendelea kusota rumande kuwa saba, ambao wanakabiliwa na kesi nne tofuati.

Hii ni kwa mujibu wa Mwenyekiti wa CHADEMA taifa Freeman Mbowe aliyetoa takwimu hizo Agosti 12, 2022, akizungumza mkoani Shinyanga kuazimisha Siku ya Vijana Duniani.

Sababu kubwa mbili zimekuwa zikitolewa kuhalalisha uachiliwaji wa watu ambao wamekaa gerezani kwa siku nyingi kama washtakiwa: DPP hana nia ya kuendelea na kesi husika au kumekosekana ushahidi wa kuwatia hatiani washtakiwa.

SOMA ZAIDI: Kuachiwa kwa Mbowe na Mapungufu ya Mfumo wa Utoaji Haki Tanzania

Uachiliwaji huu, hata hivyo, huja baada ya mshtakiwa kusota gerezani kwa kipindi kirefu.

Hali hii imepelekea wadau kupongeza hatua hizo lakini pia kupendekeza mageuzi ya msingi kwenye mfumo wa utoaji haki, ikiwemo suala la kuyafanya makosa yote yawe na dhamana.

Ulipaji fidia

Fatma Karume ni wakili na mwanaharakati ambaye ameutafsiri uamuzi wa Serikali wa kuwaachia huru watu wasiopaswa kuwepo gerezani kama kuanza kustaaribika kwa Serikali, akisema lakini haipaswi kuishia kwenye kuachilia tu watu bali iwalipe fidia pia.

“Kitu cha kwanza ni kwamba Serikali imeona ni sawa kuwaachia hawa watu; hicho ni kitu muhimu na lazima tuone kwamba Serikali inaanza kustaraabika,” anasema Rais huyo wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

“Sasa hatua ya pili ya ustaarabu ni kuhakikisha hawa watu wanapewa haki zao [kulipwa fidia],” aliongeza Fatma.

SOMA ZAIDI: Tito Magoti: Tukiwa Tunaadhimisha Wiki ya Sheria, Tuwafikirie Wanaoendelea Kusota Gerezani Bila Kutiwa Hatiani

Serikali haijatangaza utaratibu wa kuwalipa fidia watu ambao waliwekwa magerezani kwa makosa – angalau mpaka sasa.

Ndumbaro pia hakupokea simu yetu tulipotaka kufahamu kama utaratibu huo unaweza kutegemewa siku chache zijazo. Lakini uwezekano ni upi kwa watu hawa kulipwa fidia?

Uwezekano mdogo

Kwa mujibu wa Benedict Ishabakaki, moja kati ya mawakili mashuhuri nchini Tanzania wanaosimamia kesi za jinai, uwezekano ni mdogo sana.

Hii ni kwa sababu ingawaje sheria inamruhusu mtu kufungua kesi kama anahisi ameshtakiwa pasi na sababu za msingi, sheria hiyo haitoa mwanya kwa kesi ambazo DPP amezifuta.

Anachosema Ishabakaki ni kwamba unaweza kufungua shtaka dhidi ya kushtakiwa pasi na sababu za msingi pale tu baada ya kushinda kesi uliyofunguliwa, ikasikilizwa mpaka ikaisha.

Kwa watu wanaoachiwa na DPP– kama hawa vijana wa CHADEMA – kesi zao hazikufuata utaratibu huo kwani zimekoma baada tu ya DPP kuamua kutokuendelea nazo.

“Kwa hiyo,” anahitimisha Ishabakaki, “Kwa hawa ambao unaona wameachiwa na DPP inakuwa ni ngumu kidogo kwenda kufungua kesi kama hiyo ya madai.”

SOMA ZAIDI: Mjane wa Katibu wa Zamani wa Bunge Anayepigania Haki Yake kwa Miaka 23

Mageuzi makubwa

Lakini suala la fidia ni suala dogo sana kwenye madai ya wadau wa haki jinai chini Tanzania.

Dai lao kubwa ni kuona mfumo mzima wa utoaji haki jinai unafumuliwa ili kuepusha uwezekano wa watu kudhulumiwa haki zao.

“Serikali kuendelea kuweka makosa yasiyokuwa na dhamana ni kinyume na kila kitu cha busara, haki za binadamu na ustaarabu; ni kinyume kabisa,” anasema Fatma Karume, mjukuu wa Rais wa kwanza wa Zanzibar Abeid Amani Karume.

Fatma anasema ni lazima Serikali ifute makosa yote ambayo kwa sasa hayana dhamana.

“Kila kosa lazima liwe na dhamana, iwe unaweza kuomba dhamana,” anapendekeza Fatma. “Mtu mmoja tu ndiyo aweze kukukatalia dhamana: Mahakama. Na hapo baada ya Mahakama kuona kwamba hustahili kupewa dhamana.”

Magoti, ambaye mnamo Aprili 15, 2021, alimuandikia Rais Samia Suluhu Hassan barua ya wazi ikimtaka atupie jicho mfumo wa utoaji wa haki jinai nchini, anasema kwamba ni wakati sasa wa Mahakama iingilie kati kwenye suala zima la dhamana.

SOMA ZAIDI: Tito Magoti: Barua ya Wazi kwa Rais Samia Kuhusu Hali ya Haki Jinai Tanzania

“Ni muda muafaka kwa Mahakama kuona heri tukipeleka maombi ya namna hiyo Mahakama iwe na utayari wa kufanya hivyo.

“Mahakama imepelekewa kesi ya kuruhusu dhamana, angalau kwa mamlaka yake, lakini Mahakama ya Rufaa ilijivua katika hili suala,” alisema Magoti.

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts