The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Polisi Zanzibar: Suala la Vijana Kutoweka Tunalichukulia kwa Uzito Mkubwa

Waitaka jamii kutoa ushirikiano kusambaratisha mtandao unaohusika na kutorosha vijana visiwani humo.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Kamishna wa Polisi Zanzibar Hamad Khamis Hamad amesema kwamba Jeshi la Polisi linalichukulia suala la vijana kutoweka kwenye mazingira ya kutatanisha visiwani humo kwa “umakini mkubwa sana.” 

Kamishna huyo ameongeza kwamba mpaka sasa jumla ya kesi tatu zinazohusiana na suala hilo zimefikishwa kwenye chombo hicho chenye dhamana ya kudumisha ulinzi wa watu na mali zao nchini.

Hamad alisema hayo wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo yaliyofanyika ofisini kwake, Makao Makuu ya Polisi, Kilimani, Zanzibar, hapo Septemba 13, 2022, majira ya saa 11:30 za jioni.

“Suala hili tumelipa uzito sana kwa sababu hata viongozi wa nchi wamelizungumza hili jambo,” Kamishna Hamad alisema wakati wa mahojiano hayo. 

“Lakini tatizo linaloonekana ni kuwa huko mtaani linazungumzwa kama ni tatizo kubwa sana wakati watu wachache sana ndiyo wanaripoti hizo kesi kwenye vituo vya polisi,” aliongeza.

Mahojiano hayo na afisa huyo mwandamizi wa Jeshi la Polisi yamefanyika takriban siku 10 baada ya The Chanzo kuchapisha habari iliyoonesha uwepo wa mtandao unaowasajili vijana wa Kizanzibari kwenda kujiunga na yanayoshukiwa kuwa ni makundi ya kigaidi nje ya sehemu hiyo ya Jamhuri ya Muungano.

Kwenye taarifa yake hiyo, The Chanzo iliongea na wazazi waliopotelewa na watoto wao na wake waliopotelewa na waume zao ambao walielezea maswaibu ya kupotelewa na wapendwa wao hao kwenye mazingira ya kutatanisha, wakiviomba vyombo vya ulinzi na usalama viwasaidie kuwapata wapendwa wao.

SOMA ZAIDI: Vijana Zanzibar Watoweka Katika Mazingira Tatanishi. Wazazi, Polisi Watoa Kauli Kinzani

Akijibu swali juu ya namna Jeshi la Polisi limezipokea taarifa hizo, Kamishna Hamad aliiambia The Chanzo:

“Kimsingi niseme hizo taaarifa za vijana kupotea tumezipata na mpaka tunapozungumza hivi sasa tuna kesi kama tatu, nadhani, ambazo ndiyo zimeripotiwa kwenye vituo vya polisi na upelelezi unaendelea kuona hao watu wameondokaje na pengine kwa ushirikiano wa jamii tunaweza kujua hao watu wameenda wapi.

“Kama ni kweli, kama inavyozungumzwa, kwamba hao vijana wamejiunga na vikundi vya kigaidi, ukweli utabainika tu. Lakini tutambue kuwa upelelezi ni mchakato na siyo suala la siku moja au siku mbili. Unaweza kuchukua muda mfupi na unaweza kuchukua muda mrefu. Lakini tunafuatilia.”

SOMA ZAIDI: CCM, Wanaharakati Walaani Vijana Kutoweka Zanzibar. Wataka Hatua Zichukuliwe

Kufuatia habari kwamba baadhi ya watu kuitwa polisi na kuhojiwa kuhusiana na suala hilo, Hamad alisema:

“Ni kweli kuna baadhi ya vijana wameitwa kituo cha polisi kwa ajili ya mahojiano maana ni kama nilivyozungumza kuwa upelelezi ni mchakato na ni lazima watu wakamatwe na wahojiwe. 

“Pale tutakapopata taarifa kuwa fulani anaweza kuwa na taarifa  fulani zinazoweza kutusaidia katika upelelezi ataitwa kituo cha polisi, siyo lazima akamatwe, ataitwa tu kituo cha polisi. 

“Tutahojiana naye na akitupa taarifa ambayo itapelekea kumkamata mwengine ndivyo upelelezi unavyokwenda. 

“Kwa hiyo, mpaka sasa siwezi kusema ni watu wangapi ambao wamekamatwa, au ni watu wangapi ambao wanaitwa vituo vya polisi, wanahojiwa, ili kuweza kupata taarifa kuhusiana na hizi tuhuma zinazoendelea.”

SOMA ZAIDI: Zanzibar Yaimarisha Ulinzi Kufuatia Taarifa za Vijana Kutoweka Katika Mazingira Tatanishi

Kamishna Hamad ametoa wito kwa jamii kutokuacha kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi, akisema ni kwa kufanya hivyo tu ndipo vyombo vya ulinzi na usalama visiwani humo vinaweza kukomesha suala hilo.

“Mimi ningependa kutoa rai kwa kila mwenye kesi, au taarifa, inayohusiana na upotevu wa watu kama inavyozungumzwa, hebu aje polisi tushiriakiane naye kutafuta ukweli wa hili jambo,” alisema Hamad kwenye mahojiano hayo. 

“Polisi tuna kesi chache lakini huku mtaani kila kona linazungumzwa kwamba watu wanapotea lakini taarifa hazifiki polisi,” alilalama Hamad. “Basi tushirikiane kuona kwamba tunaweza kulipatia ufumbuzi hili jambo.”

Najjat Omar ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts