The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kikosi Kazi cha Mwinyi Chataka Mamlaka Zaidi kwa Z’bar Ndani ya Muungano

Mnyukano unaonekana ulikuwa mkali kwenye siasa za ndani ya Zanzibar tu, huku maoni ya wadau yakionekana kufanana linapokuja suala la Muungano.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Mapendekezo mengi ya kikosi kazi cha Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi juu ya namna bora ya kupata maridhiano ya kisiasa visiwani humo yanaonekana kujikita kwenye kuitaka Serikali iiwezeshe Zanzibar kuwa na mamlaka makubwa zaidi ya iliyonayo sasa kwenye Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Rais Mwinyi aliunda kikosi kazi hicho chenye watu 11 hapo Oktoba 10, 2022, na kukipa kazi ya kuchambua maoni yaliyotolewa na wadau wa vyama vya siasa, asasi za kiraia pamoja wananchi kwenye mkutano uliofanyika mnamo Oktoba 6, 2022, kujadili hali ya siasa visiwani humo.

Akiwasilisha mapendekezo ya kikosi kazi hicho kilichopewa siku 15 kufanya uchambuzi wa maoni hayo wakati wa hafla iliyofanyika leo, Novemba 2, 2022, katika Ikulu ya Zanzibar, Mwenyekiti wa Kikosi Kazi Dk Ali Uki alisema kwamba haikuwa kazi rahisi kwa wajumbe wa kikosi kazi hicho kujadiliana juu ya mambo kadhaa lakini waliweza kukubaliana juu ya mengi kwa njia ya muafaka badala ya kura.

Wakati inaonekana kwenye mapendekezo yaliyowasilishwa kulikuwa na mnyukano mkali wa kimawazo, mnyukano huo hata hivyo unaonekana kutokea pale tu siasa za ndani za Zanzibar zilipohusika huku ikidhihirika kwamba wajumbe wa kikosi kazi hicho walikuwa na mtazamo karibu unaofanana linapokuja suala la nafasi ya Zanzibar kwenye Jamhuri ya Muungano.

Mapendekezo ya Muungano

Kwa mfano, kikosi kazi kinataka kwamba pale ikitokea kufanyika marekebisho yoyote ya Katiba, au wakati wa kutungwa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, suala la mafuta na gesi asilia liwekwe sawa. Zanzibar siku zote imekuwa ikitaka suala la mafuta na gesi asilia lisiwe la Muungano.

Dk Uki aliwasilisha pia kwamba suala la hisa za Benki Kuu lifanyiwe kazi kwa kupatikana mfumo wa kudumu kwani mfumo wa sasa ni wa muda. Kikosi kazi kinataka mfumo wa kudumu uzingatie hisa za kila upande zilizoanzisha Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Hii ni moja kati ya “kero” za siku nyingi za Muungano. 

“Mheshimiwa Rais, kamati ilipendekeza pia Serikali zote mbili zilifanyie kazi suala la mipaka ya umiliki wa kisiwa cha Fungu M’baraka, au kinaitwa Fungu Kizimkazi, au kinaitwa Latham Island,” Dk Uki aliwasilisha. “Ili mipaka ya kiutawala kati ya Zanzibar na Tanzania bara ifahamike vizuri.”

Kikosi kazi pia kinataka makubaliano yaliyofanyika kuruhusu Zanzibar kukopa na kufanya mikataba na nchi, au taasisi, za nje ya nchi yawekewe utaratibu wa utekelezaji. 

“Aidha, Mheshimiwa Rais, [kamati] inapendekezwa kutungwa kwa sheria iliyotafsiri matumizi bora ya mamlaka ya pamoja ya dola, yaani Jamhuri ya Muungano, hapa kwa lugha ya kigeni wanaita ‘shared sovereignty,’” alisema Dk Uki. “Kwa manufaa ya pande zote mbili [za Muungano].”

Kikosi kazi cha Dk Mwinyi pia kimependekeza tume ya pamoja ya fedha ifanye kazi kwa mujibu wa matakwa ya Katiba na sheria ya kuanzishwa kwake ili iweze kuleta manufaa kwa pande zote mbili za Muungano. 

Pia, kikosi kazi kimependekeza akaunti ya pamoja ya fedha ianzishwe kwa mujibu wa katiba na sheria.

“Kamati pia imependekeza mgawanyo wa nafasi za ajira zinazotokana na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, yaani asilimia 21 kwa upande wa Zanzibar na asilimia 79 kwa upande wa Tanzania Bara utekelezwe ipasavyo na zitungwe kanuni maalumu zitakazorahisisha utekelezaji wake,” Dk Uki alisema akiwasilisha maoni ya kikosi kazi. 

“Kamati inapendekeza kuwe na muongozo utakaoweka uwiano baina ya pande mbili za Muungano katika uteuzi wa mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” aliongeza Dk Uki. “Na maamuzi yaliyofanyika kuhusu kuondoa kero katika suala la kodi na ushuru kwa bidhaa zinazotoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara yatekelezwe ipasavyo.”

Maridhiano ya kisiasa

Kuhusu maridhiano ya kisiasa, inaonekana ni kama vile kikosi kazi imelichukua pendekezo la Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo Ismail Jussa alilolitoa kwenye mkutano huo wa Oktoba 6 la haja ya kuundwa kwa tume maalum ya kusimamia maridhiano ya kisiasa pale yanapofikiwa ili kufanya usuluhishi.

TAZAMA: Jussa: Zanzibar Tunahitaji Tume ya Kudumu ya Utengamano

Kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kikosi kazi kimependekeza kuundwa kwa mpango maalumu wa kuielimisha jamii kuhusu utendaji kazi na umuhimu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa maendeleo ya Zanzibar na vizazi vijavyo.

“Pili, muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa uendelee kuwepo Zanzibar kutokana na umuhimu wake katika kujenga jamii yenye amani, umoja na maridhiano ya kweli,” Dk Uki aliwasilisha maoni ya kikosi kazi.

Kikosi kazi pia kinataka uteuzi wa watumishi wa umma uzingatie weledi na utaalamu bila kujali itikadi za siasa ili kutoa taswira halisi ya Umoja wa Kitaifa kwa lengo la kudumisha maridhiano ya Wazanzibar.

Pia, Serikali ivishirikishe vyama vya siasa katika mambo ya utendaji wa nchi ili kuimarisha mazingira ya maelewano na kuaminiana, ikiwa ni pamoja na ushiriki wao katika ziara rasmi za kiserikali za ndani na nje ya nchi.

Kikosi kazi pia kimeshauri muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa uwe mpaka katika ngazi ya chini ya utawala.

“Uteuzi wa masheha uzingatie uwezo wa kutambua mazingira na hali halisi ya sheria husika pamoja na mchanganyiko wa watu wake,” Dk Uki alisema. “Pili, uteuzi wa Sheha uzingatie uwezo wa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria zilizopo bila kujali itikadi za kisiasa, dini, kabila au eneo la kijiografia.”

Uchaguzi

Kikosi kazi cha Rais Mwinyi kimependekeza kwamba nafasi za mwenyekiti na wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) zitangazwe na wanaoona wanafaa, wanazo sifa, waombe.

Pia, kimependekeza kuundwa kwa kamati maalumu ya uteuzi wa nafasi ya mwenyekiti na wajumbe wa ZEC ambayo itakuwa na jukumu la kupokea maombi ya watu.

“Kamati imependekeza matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Zanzibar yahojiwe mahakamani kwa utaratibu lakini uliowekwa na demokrasia na kuongeza uwazi katika kusimamia masuala ya uchaguzi,” Dk Uki alisema, akimalizia orodha ya mapendekezo ya kikosi kazi hicho.

Kwa upande wake, Rais Mwinyi aliwapongeza wajumbe wa kikosi kazi hicho kwa kazi hiyo waliyofanya, akisema sasa Serikali itaipeleka ripoti hiyo ya kikosi kazi kwa wataalamu ili washauri ni kwa jinsi gani ya kuyatekeleza mapendekezo yaliyotolewa katika muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu.

“Lengo kuu [la kutafuta maridhiano ya kisiasa] ni kuendeleza amani katika nchi yetu. Lazima tufanye kila litakalowezekana tuendeleze amani tuliyonayo. Tujenge umoja tulionao. Na tuhakikishe kwamba maridhiano tuliyonayo basi tunayatafutia njia ya kuyaendeleza ili yaweze kudumu,” Dk Mwinyi alisema. 

“Hii ni muhimu. Ni muhimu sana kwa sababu hatuwezi kukuza uchumi kama ndani ya nchi hakuna amani. Hakuna umoja. Hakuna mshikamano. Hakuna maridhiano kati ya wananchi,” aliongeza Rais huyo wa Zanzibar.

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *