The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Haki ya Kusahaulika ni Nini na Kwa Nini ni Muhimu?

Una haki ya kusahaulika, usikubali ichezewe, Maxence Melo wa JamiiForums anawasihi wananchi.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Mnamo Novemba 21, 2022, The Chanzo ilifanya mahojiano maalum na Mkurugenzi wa JamiiForums Maxence Melo kuhusiana na haki ya msingi ya binadamu ambayo watu wengi hawaifahamu: haki ya kusahaulika.

Melo, ambaye ni moja kati ya wadau wakubwa wa haki za kidijitali nchini Tanzania, amesema haki hiyo ni muhimu kama zilivyo haki zingine, akisema kwamba ana matumaini kwamba Serikali itaijumuisha kwenye Muswada Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya Mwaka 2022.

Yafuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo yaliyofanyika katika ofisi za The Chanzo, zilizopo Msasani, Dar es Salaam. Endelea …

The Chanzo: Nini haswa maana ya haki ya kusahaulika?

Maxence Melo: Haki ya kusahaulika, kwa wengine wanasema the right of erasure, au haki ya kufutwa, ni haki ambayo kwa wengi wanaichukulia kama si haki ya msingi. Lakini ni haki ya msingi ya binadamu.

Kuna taarifa zimekusanywa na mkusanya taarifa yoyote, au mchakata taarifa, anaweza kwenda kuomba kwamba taarifa hizi mlizokuwa nazo kuhusu mimi sitaki muendelee kuwa nazo kwa sababu labda matumuzi yake yameisha au kwa namna moja au nyingine inaweza ikasababisha madhara kwake.

Kwa hiyo, ni haki ambayo katika nchi zenye sheria ni haki ya msingi sana na kwa wengine wanaichukulia poa lakini ina madhara makubwa. Na baadaye ninaweza nikatoa mifano ya madhara yanayoweza kupatikana.

The Chanzo: Kwa hiyo, katika ule mtiririko wa haki za msingi za binadamu, kuna chapisho ambalo limeongeza hii haki ya kusahaulika?

Maxence Melo: Tunapoongelea haki za binadamu kwa sasa hivi haki ya faragha ndiyo ambayo ninaweza kusema hadi Umoja wa Mataifa (UN) wameichukua [na] kuiingiza [kwenye orodha ya haki za binadamu]. Sasa tunapoongelea haki ya faragha ni pamoja na kusahaulika, au taarifa zako kulindwa, kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, haki ya faragha inaingiza hizo haki za kusahaulika na nyinginezo.

Kwa hiyo, haki kubwa kabisa tunayoongelea mara nyingi tunayoipigia chapuo ni haki ya faragha. Kwa hiyo, kimataifa haki ya faragha ipo kama haki ya msingi ya binadamu na Umoja wa Mataifa wameiweka.

The Chanzo: Kwa hiyo, tunaweza tukasema kwamba katika haki ya faragha, haki ya kusahaulika imewekwa kama haki ndogo?

Maxence Melo: Siyo haki ndogo ni haki ya msingi katika haki za faragha. Kwa mantiki hiyo kuna haki nyingi sana katika haki za faragha lakini moja wapo ni haki hiyo ya kusahaulika.

The Chanzo: Asante sana.

Maxence Melo: Shukrani.

The Chanzo: Na vipi sasa kuhusiana na Watanzania, wanauelewa kuhusiana na haki ya kusahaulika?

Maxence Melo: Tukienda kwenye faragha, Watanzania wengi wanatamani kusahaulika, nadhani wanatamani iwe hivyo, lakini hawajui wafanye nini. Na nikisema hawana uelewa nitakua nawaonea kwa sababu najua kutakuwa na Watanzania wengi wenye uelewa, lakini kutakuwa na kundi la Watanzania wengi wasiokua na uelewa.

Na tunafika maeneo mengi tunatoa taarifa zetu, tunatoa kwa nia njema yawezekana wanaozikusanya pia nao wanazikusanya kwa nia njema lakini matumizi yanaweza yakafika mwisho wake.

Waliokusanya taarifa zetu bado wanabakia nazo na hawaziachii, wanazitumia kwa shughuli gani? Hatujui. Kwa hiyo, hapo baada ya nia njema kinachofuata hapo sasa haki yako ya kusahaulika baada ya matumuzi ya taarifa zako ndiyo inapopotea.

Na ninaweza nikasema labda kama wengi watataka kuelewa kuna maeneo mengi unaenda unakutana na taarifa zako ambazo ukiziangalia unabaini huyu si mimi ila ni mimi wa miaka 15 iliyopita, ila kwa wakati huu huyu si mimi na sitakiwi kukuta taarifa kama hizi bado mnazo.

The Chanzo: Sasa ili kuwaelewesha watazamaji haki ya kusahaulika ina fanya kazi katika mazingira gani?

Maxence Melo: Haki ya kusahaulika inaweza ikapatikana kwa utaratibu huu. Moja inawezekana wewe umetumia mitandao ya kijamii na wakati unaweka taarifa zako kuna baadhi ya vitu uliviweka ambavyo unabaini kwamba vinaweka maisha yako hatarini.

Na ukajaribu kuwaonesha, au ukawaelezea, wahusika waweze kujua madhara yanayoweza kupatikana kwa taarifa zako hizi kuendelea kubakia kwenye uwazi wa umma na ukishafanya hivyo, unawaelewesha kwamba wakati najaza taarifa, au wakati natiki boksi kwenye mtandao, tunaingia kwa kutiki boksi wakati nikijaza niliafiki kwamba mfanye hivyo lakini sikujua  madhara yake ni moja mbili tatu.

Kama hawana matumizi tena na taarifa hizi wataziondoa, lakini wakiwa na matumizi nayo watakufahamisha taarifa hizi bado zina faida kwa sababu ya moja mbili tatu.

Lakini pia kampuni yawezekana ni ya simu, au benki, umewahi kujiandikisha, au kutumia huduma zao, wanaweza wakabaini, au wewe mwenyewe unaweza ukabaini, kwamba benki hii A nilikua nikifanya nayo biashara lakini imefika wakati naenda kufunga akaunti yangu.

Wengi hawajui kwamba hata ukienda kufunga akaunti, benki bado ina mawasiliano yako, bado ina kila kitu karibia vyote kuhusu wewe. Na ukafika wakati ukasema hii kampuni ya mawasiliano hii ya simu nimeacha kutumia laini yao naachana nayo, lakini wengi hawajui kwamba kampuni za simu zina taarifa zetu kwa takribani miaka 10 kuhusiana na sisi.

Lakini kama unajua kabisa mimi naachana na kampuni A au kampuni B ya mawasiliano, au benki, una haki ya kwenda kuwaambia kwamba kwa sasa kama hamna lolote kuhusu mimi nahitaji taarifa zangu zote mlizonazo ziondolewe kwenye mifumo yenu.

Na unatakiwa kuweka utaratibu wa wazi ili kama wakikataa ni haki yako iko wazi kabisa. Kwamba haya matumizi waliyokuwa wamekwambia mwanzoni ndiyo walikua wanalenga kutumia.

Na wala usilenge benki tu, yawezekana ni hata Asasi ya Kiraia (AZAKI) ilikuja kwako ikakwambia tunafanya utafiti, utafiti huu ni kwa ajili ya ugonjwa wa kipindupindu unaoendelea katika mtaa wako.

Sasa ukakuta taarifa kama hizo wanazo miaka 15 baadaye. Mambo uliyoyaongea wakati ule hayahusiani na wewe lakini bado wanazo [hizo taarifa], wanasema huyu ndiye Hadija, na Hadija ana hofu ya mbu wakati ule ulikua na hofu ya mbu lakini kwa kipindi hiki hofu ya mbu haipo tena, yawezekana mambo yamebadilika.

Kwa mantiki, kwa sababu tunajua binadamu anaenda anabadilika na ana haki ya kusema kwamba kwa kweli acha kuchakata taarifa hizi. Ndiyo maana mara nyingi tunawaambia watu kabla hujatoa taarifa zako jaribu kusoma hawa watu wanaochukua taarifa zako wanakua wanataka nini na nini na kwa matumizi yapi na mwisho wa matumizi hayo ni lini.

Ni vizuri ujue mwisho wa matumizi ili ikifika mwisho wa matumuzi uweze kwenda kuomba sasa mwisho wa matumizi umefika kama unadhani bado wanazitumia na una haki ya kwenda kuuliza kama bado wana taarifa zako kuonesha walichonacho na ukiona bado wana kitu ambacho kweli hutamani kiwepo na kiondolewe. Nadhani nimeelezea kwa kirefu kidogo.

The Chanzo: Sasa kuna dhana hapo niliisikia kwamba unaweza ukaenda ukawaambia kwamba taarifa zangu sitaki zitumike. Na vipi sasa mwanzo wakati tuseme labda kama unajisajili kwenye mtandao fulani, wamekuandikia pale mwisho [wa kutumika taarifa hizi ni] miaka 10 labda tuseme. Sasa wewe hutaki zile taarifa zitumike miaka 10, [ikiwa] haijafika [miaka 10] na hapo unaweza pia ukawafuata?

Maxence Melo: Sasa ndiyo maana tunawaambia watu soma kabla hujajiunga, jiridhishe kwanza na masharti ya ushiriki kwenye programu fulani kabla hujachukua hatua.

Kwa sababu wanapokwambia kwamba tutatumia taarifa zako kwa muda wa miezi sita au tunatumia taarifa hizi kwa ajili ya moja,mbili, tatu, ukaafiki labda wao waende nje ya kile walichokwambia kwamba watatumia kwa ajili ya hicho.

Kwa mfano, mtu anaweza kusema tunachukua taarifa hizi kwa ajili tu ya kujua jinsi ambavyo tukikuhitaji tutawasiliana na wewe. Wakimaliza kukwambia hivyo ghafla ukaanza kupokea meseji za matangazo sijui mjukuu wangu sijui vitu gani.

Wakaanza kutumia meseji za ajabu ajabu ni baada ya wewe kujiandikisha kwenye hiyo huduma. Hapo una haki ya kwenda kuwawahi kwamba sikiliza tulichoafikiana sicho mnachokifanya na taarifa zangu, ninyi mmevunja mkataba kwa sababu huko ni kuvunja mkataba.

Lakini kama wamekwambia tutatumia miaka miwili na wewe ukaridhia na ukaanza kufanya wakakupa karatasi ukasaini sasa mimi nimeridhia kimsingi mwenye makosa ni wewe uliyeamua kuingia huko bila ya kuwa umejiridhisha na huduma unayokaribia kujiandikisha.

The Chanzo: Asante sana. Kwa hiyo, ikitokea wameenda kinyume na hivyo mtu anaweza akafanya hatua za kisheria zaidi?

Maxence Melo: Kwa sababu nchi yetu kwa sasa hivi haikuwa na sheria, na tuna bahati kwamba mswada umepelekwa bungeni umesomwa, na kwa bahati mbaya mswada huo haukuwa na haki hiyo, bahati nzuri tumesikia kwamba Serikali imefikiria maoni ya wadau na ikaona kuna haja ya kulinda utu wa Watanzania kwa kuwapa haki ya kusahaulika.

Endapo kwenye mswada huu ambao unaenda kuwa sheria utakua imeingizwa basi haki hii inaweza ikawa imempa nguvu Mtanzania kwamba sikiliza kwa mujibu wa sheria hii mpya mimi niliongea na nyinyi tukakubaliana kwamba taarifa zangu mtazitumia miezi sita kwa ajili ya moja, mbili, tatu, nyinyi mmekiuka haki yangu ni kwamba mnatakiwa muondoe.

Wasipo iondoa kuna kulipwa fidia. Kwa mujibu wa sheria mpya inayokuja watalipwa pesa nyingi sana. Mwanzoni mswada wa Serikali haukuwa unatambua kwamba aliyeathiriwa ndiye alipwe ilikua ni kwamba labda mamlaka za Serikali ndiyo zilipwe.

Sisi tukasema hapana, mwenye madhila au madhara yanayomkuta ni mwenye taarifa, wanamwita mhusika wa taarifa. Kwa kuwa taarifa hizi ni za kwangu, na aliyezitumia kazitumia vibaya wa kulipwa ni mimi na wala si Serikali.

Bila shaka Serikali inaweza kupokea gawio lake lakini mimi niliyeathirika kwanza nipate malipo kwa yule aliotumia taarifa zangu vibaya. Lakini kwa kuwa mpaka dakika hii nchi yetu haina sheria basi hiyo haki haipo.

The Chanzo: Kwa hiyo, unaweza ukasema kwamba taifa kwa ujumla bado hatuna mifumo inayohakikisha watu wanapata haki ya kusahaulika?

Maxence Melo: Mpaka sasa hatuna sheria ya kulinda faragha za watu. Hatuna sheria za kulinda taarifa za watu. Tuna mswada, na wala siyo sheria, na mpaka sasa taarifa zako ukizitoa, umetoa. Zimetumika visivyo huna la kufanya utabakia kulalamika tu.

The Chanzo: Sawa. Na vipi sasa kuhusiana na mswada ambao ulipitishwa hivi karibuni bungeni ambao unahusiana na haki binafsi. Je, haki ya kusahaulika imewekwa katika mswada huo?

Maxence Melo: Kama nilivyosema awali kwenye mswada wa Serikali ambao upo mtandaoni kwa sasa hivi wengi wanauona hauna hiyo haki na tuna haki nyingi ambazo tuliona Serikali ikawa imezisahau tukaziingiza kwa ajili ya kulinda utu wa Watanzania.

Na tukasema tunatambua kwa kufanya hivi kuna watu wataanza kusema sasa hawa watu watataka kujiondoa hata benki, atataka afunge. Hapana. Kutakuwa kuna ukomo, kuna haki na wajibu.

Lakini pia utapochukua haki ya kusahaulika hii ya faragha ya kusahaulika kama unaenda kujiandikisha, tuseme kampuni za simu ambacho kitatokea sasa ni kwamba kampuni ya simu ikiingia makubaliano na wewe utaeleweshwa kabisa kwamba taarifa zako zitatumika moja,mbili, tatu.

Lakini mwishowe itakapotaka kwamba hiyo haki ya kusahaulika utaratibu utakua ukoje.

Kuna watu hata tukiwa bungeni tulijaribu kuwaelezea, hata waheshimiwa wabunge, kuna wabunge waliwahi kuwa ni wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na sasa hivi wako upinzani. Kuna wabunge waliwahi kuwa wa upinzani sasa hivi wako CCM.

Lakini wakienda kwenye vyama walikotoka bado wao ni wanachama. Yaani tunatumia mfano rahisi sana kuweza kuelewa kwamba haki ya kusahaulika inaanzia wapi na ukomo wake unaweza ukajaje.

Pale unapofika tamati na mwenzio, au na wenzako, au na mwenye kukupa huduma, au mchukua taarifa, au mchakata taarifa, mnatakiwa kufika wakati wa kusema sasa sikiliza kila kitu kilichopo kuhusiana na mimi, hasa vinavyohusiana moja, mbili, tatu kuna mipaka, mipaka yake inakujaje?

Mipaka ipo kwenye upande huu kama taarifa unazozitaka ziondolewe iwe ni kwenye injini ya utafutaji, iwe ni kwenye hata huduma ulizojiandikisha kama zina maslahi mapana ya umma taarifa hizo zinaweza zisifutwe.

Kwa sababu mwisho wa siku umma unashinda dhidi yako hata kama una haki ya faragha lakini umma utakuja kushinda dhidi yako.

Sasa muswada wa Serikali haukua na hii haki baada ya kuielezea kwa kirefu waheshimiwa wabunge waliona kwamba kwa kweli inaleta maana na hata kama mliangalia mjadala bungeni ilikua ni miongoni mwa haki ambazo wabunge walipigia kelele isije ikaachwa.

The Chanzo: Kwa hiyo, tutegemee kuiona haki ya kusahaulika inapewa uzito katika mswada?

Maxence Melo: Mimi nina matumaini makubwa kwamba Serikali sitarajii ishupaze shingo kwamba iache kuiweka. Natarajia itaiweka, isipoiweka basi Watanzania wajue kwamba bado pamoja na kwamba kuna haki ya faragha bado tutakuwepo sana hapo.

Kwenye ulimwengu huu wa digitali na ulimwengu kwa ujumla tutakua tupo kwenye changamoto kubwa sana.

The Chanzo: Sawa, lakini kuna kitu ambacho nilihitaji uongezee, nahisi wengi watakua wanadhani kwamba haki ya kusahaulika ipo kwenye mtandao tu na labda inaenda upana upi?

Maxence Melo: Haki ya kusahaulika haipo mitandaoni tu kwa sababu taarifa zetu binafsi zinakusanywa mitandaoni na nje ya mitandao. Haki ya kusahaulika iko kila mahala. Kwamba inafika wakati taarifa ulizonazo kuhusu mimi hazihusiani, yaani hazina uhalisia na mimi.

Moja yawezekana pia taarifa ulizokuwa nazo kuhusu mimi zikawa zinahatarisha usalama wangu na zinaharibu mtarajio yangu. Yaani achana na usalama kwamba kwa maslahi mapana ya ukuaji wangu saikolojia yangu taarifa ulizonazo kuhusu mimi naomba ziondolewe.

Na ukajenga hoja lazima ujenge hoja kwanza kwamba kwa nini taarifa hizi ziondolewe. Sisi kama JamiiForums, kuna wateja ambao wanakuja wanaomba baadhi ya vitu kuondolewa, taarifa zinazowahusu wao binafsi, ukiziangalia unasema ama kweli hii baadae inaweza ikawa na madhara kwake.

Lakini ukibaini pamoja kwamba hii taarifa ipo kwa sababu inawezekana ikawa ni mtumishi wa umma, inawezekana ni mtu aliwahi kuwa na nafasi kubwa hata siyo mtumishi wa umma lakini alishawahi kuwa na nafasi kubwa kwenye jamii.

Ambapo jamii ina haki ya kufahamu masuala anuwai kuhusu yeye. Huyu haki yake ya kusahaulika inakuwa iko na uwanda mdogo sana. Kwa sababu mwisho wa siku huyu si yeye huyu ni mali ya umma, sijui kama naeleweka?

Lakini mtu binafsi, mwananchi kama mwananchi, yeye mwenyewe taarifa zake binafsi au haki yake hii ya faragha, faragha yake inalindwa na sheria lakini ni nje na ndani ya mtandao si mtandaoni peke yake.

Kwa sababu watu wengi wanadhani tunafanya hivi kwa sababu ya mitandao, [hapana] hata nje ya mitandao. Kwa hiyo, tunapoongelea masuala ya haki ya faragha ni ndani ya mtandao na nje ya mtandao.

Ukitaka kujua kwamba faragha yako ni muhimu kumbuka labda umesoma shule ya msingi, naamini umesoma shule ya msingi, nikachukua makaratasi yako ya mitihani kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba halafu nikaweka iwe mitandaoni au nikapeleka sehemu wanayouza maandazi nikasema watu wafungie.

Nadhani povu litaanza kukutoka na povu likianza kukutoka ujue, kwamba hapo sasa unaanza kutokwa povu si kwa sababu labda ulifeli, hapana, kwa sababu faragha yako sasa iko wazi mno kupitiliza.

Kwa hiyo, tunapopigania haki ya faragha tunapigania watu waweze kulindwa utu wao ili kama mtu anakua amekusanya taarifa, moja aweke utaratibu mzuri unaoeleweka wa kiusalama wa kulinda taarifa za mtu.

Pili, faragha yake ilindwe, ikitokea yeye ana hofu, au ana mashaka na mifumo yako, ana haki ya kuja kusema sasa sikiliza naomba muache kuchakata taarifa zangu na kuanzia sasa naomba taarifa zote mlizonazo kuhusu mimi ziondolewe, au kwenda kuuliza naomba kujua mna nini kuhusu mimi.

Yawezekana wewe umeenda kule kuomba huduma wakakwambia sisi tunakupa simu ongea tu. Ukienda kwenye kampuni yako ya simu unakuta kumbe inakusanya hadi popote unakokatiza, wanajua mitaa yote unayoishi, wanarekodi  maongezi yako. Makubaliano yenu hayakuwa hayo.

Kwa hiyo,  una haki ya kusema wakati nikiomba mawasiliano na wewe ili kutumia huduma yako hukunambia mtakua mnanirekodi, hukunambia jumbe zangu zote utazitunza, basi naomba futa kila kitu kuhusu mimi, sitaki kutumia huduma yako tena.

Kwa hiyo, tunapoongelea haki ya kusahaulika ipo nje na ndani ya mtandao.

The Chanzo: Sasa hapo kuna jambo nimelipata. Kwa mfano, ukitembea sehemu mbalimbali unaweza ukakuta mitihani yetu labda ya mock iliyopita, unaweza ukakuta imezungushwa ipo inatumika watu wanafungia vitu kumbe nayo unaweza ukachukua sheria?

Maxence Melo: Kabisa, unaweza ukachukulia sheria na ni haki yako ya msingi kwa sababu hiki kitu watu wengi walikua wanakiona cha kawaida.

Lakini niseme kinaingilia utu wako, kinakushushia hadhi katika jamii na kimsingi kwa sababu ya uwepo wa digitali mtu akiamua kukichukua na kukuiweka kwenye mtandao, kikaanza kusambaa madhara yake ni makubwa sana kuliko watu wengi wanavyodhania.

Kwa mantiki hiyo, ni wakati sahihi tuwe na sheria lakini ni wakati sahihi tuanze kuelewesha wananchi haki zao inapokuja kuhusiana na masuala haya ya faragha. Suala la faragha ni utu wako, siyo suala la kuchukulia poa.

The Chanzo:  Wito wako kwa wananchi kuhusiana na hii haki ya kusahaulika?

Maxence Melo: Wito wangu kwa wananchi ni kwamba haki zipo nyingi. Haki ya faragha ni miongoni mwa haki muhimu sana kuhusiana na utu wetu. Na haki ya kusahaulika ni miongoni mwa vitu vinavyoifanya haki ya faragha kuwa na maana zaidi.

Usichukulie poa, yoyote anayechukua taarifa kwako anatakiwa akueleze atatumia hizo taarifa kwa ajili ya nini na akizitumia nje ya makubaliano yenu tafadhali hakikisha kwamba unaenda kwenye mamlaka husika ili faragha yako ilindwe, ili mamlaka zikusaidie kupata haki yako.

Una haki na usikubali ichezewe!

Mazungumzo haya yamebadilishwa kutoka kwenye sauti kwenda kwenye maneno na mwandishi wa The Chanzo Hadija Said na kuhaririwa na Lukelo Francis. Stephan Gimbi amesimamia na kuzalisha mahojiano haya.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *