Dar es Salaam. Hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kutengua katazo lililokuwepo dhidi ya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa imethibitisha utabiri wa baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa kwamba mwaka huu wa 2023 unaweza kushuhudia mageuzi makubwa ya kisiasa yakitokea Tanzania.
Rais Samia alitengua katazo hilo ambalo vyama vya upinzani wamekuwa wakililalamikia kwa siku nyingi hapo Januari 3, 2023, wakati wa kikao chake na viongozi wa vyama 19 vyenye usajili wa kudumu nchini kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
“Ni haki ya vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara,” Rais Samia alitamka wakati wa kikao hicho. “Kwa hiyo, niko hapa mbele yenu leo kutengua katazo lililokuwa limewekwa dhidi ya mikutano ya hadhara.”
Katika hotuba yake hiyo, kiongozi huyo mkuu wa nchi pia alidokeza kwamba michakato ya kuzifanyia maboresho sheria za uchaguzi pamoja na kufufuliwa kwa mchakato uliokwama wa kuandika Katiba Mpya inaendelea, akiahidi kwamba yote hayo yatatekelezwa ndani ya muda muafaka.
Hii ni hatua ambayo baadhi ya wachambuzi waliiambia The Chanzo kwamba wanaitegemea kutokea ndani ya mwaka 2023, walipokuwa wakielezea matarajio yao makubwa kwenye eneo la siasa na utawala kwa mwaka huu. (Wachambuzi hao waliongea kabla ya Rais Samia kutangaza uamuzi huo).
Dk Muhidin Shangwe, Mhadhiri wa Siasa na Utawala wa Umma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kwa mfano, aliiambia The Chanzo hapo Disemba 30, 2022, kwamba anatabiri mageuzi ya msingi yakifanyika 2023 kwani Watanzania hawataendelea kuvumilia kuona viongozi wa kisiasa wakiendelea kuzungumza pasipo na matokeo.
Kitaeleweka
“Rais Samia ameonesha dhamira ya kuzungumza, kwa hiyo, watu wanaelewa kwamba tunazungumza lakini subira inakwisha,” alieleza Dk Shangwe. “Sina uhakika kama mwaka 2023 wote uishe pia hakuna chochote. Nadhani kuna msukumo mkubwa kwamba hayo maridhiano yakamilike watu waelewe wanachokifanya.”
“Nategemea kuwe na matokeo kwenye hayo maeneo, watu wanaanza kuchoka kwa kitu ambacho kimsingi ni haki kabisa, kipo kwenye Katiba, lakini inakubidi upige magoti ili kukiomba,” aliongeza msomi huyo akizungumzia suala la mikutano ya hadhara.
“Sasa watu walivumilia kwamba ni utawala mpya, tunahitaji kuongea, lakini mpaka sasa subira imekwisha. Ndiyo maana nasema mwaka 2023, watu hawatavumilia tena uishe, bado mnazungumza, watu watahoji mnazungumza nini?
“Hiyo ndiyo inanifanya niamini kwamba kuna kitu kitatokea mwaka 2023, sijui mwanzoni sijui katikati. Kwa lugha ya mtaani [wanasema] kitaeleweka, kama ni kusuka au kunyoa, kwa maana kwamba kama tuna mikutano au hakuna.”
Tangu aingie madarakani hapo Machi 19, 2021, Rais Samia ameshuhudia michakato miwili ya kutafuta maridhiano ya kisiasa ikifanyika chini ya Serikali yake. Kwanza, kuna ule unaoratibiwa na Kikosi Kazi cha Rais cha Kuratibu Maoni ya Wadau Juu ya Namna Bora ya Kuboresha Demokrasia ya Vyama Vingi Nchini.
SOMA ZAIDI: Yaliyowapatanisha, Kuwafarakanisha Serikali, Upinzani 2022
Mchakato wa pili ni ule unaokihusisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali uliotokana na hatua ya CHADEMA kususia mchakato unaoratibiwa na Kikosi Kazi cha Rais, kikidai kwamba wajumbe wake hawana mamlaka ya kimaadili ya kuratibu majadiliano ya kidemokrasia.
Michakato yote miwili, hata hivyo, kwa kiasi kikubwa inahusu mambo matatu makubwa ambayo ni kuondolewa kwa katazo dhidi ya mikutano ya hadhara; sheria na kanuni za uchaguzi kufanyiwa mageuzi ili kuweka mazingira ya chaguzi huru na za haki; na kufufuliwa kwa mchakato wa kuandika Katiba Mpya.
Alipokuwa akitamka kwamba katazo dhidi ya mikutano ya hadhara limefutwa, Rais Samia aliahidi kwamba haya mengine yapo kwenye orodha ya mambo ambayo amepanga kuyakamilisha.
Dk Paul Luisulie, Mhadhiri wa Siasa na Utawala wa Umma kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), aliiambia The Chanzo hapo Disemba 30, 2022, kwamba hiki ndicho anachokitarajia.
SOMA ZAIDI: Hatua Tano Muhimu Kufikia Upatikanaji wa Katiba Mpya Tanzania
“Sijawa na wasiwasi, pamoja na changamoto zilizopo, sijawa na wasiwasi kwamba kutakuwa na matukio mabaya ya kisiasa [mwaka 2023]. Mimi nauona wakati ujao utakua mzuri katika masuala ya kisiasa,” alieleza msomi huyo.
Luisulie alitaja utayari uliooneshwa na Rais Samia kwenye maridhiano kama moja ya sababu zinazomfanya afikie hitimisho hilo.
“Nikisema hivyo simaanishi kwamba ni mteremko, hapana,” anaonya Dk Luisulie. “Hakuna mteremko, lakini kutokana na sababu hizo nilizozitaja, mimi naona kuna wakati mzuri ujao wa kisiasa katika nchi yetu.”
Hakuna kikubwa kitafanyika
Lakini wapo wachambuzi ambao matarajio yao ya 2023 hayakuwa chanya sana. Rashid Abdallah, mwandishi wa habari za siasa wa kujitegemea, kwa mfano, ameiambia The Chanzo kwamba hategemei kuona mageuzi makubwa ya kisiasa yakitokea 2023.
“Haya mambo yataendelea kubaki tu kwamba ni ajenda zinazozungumzwa taratibu na ajenda zinazosukumwa polepole, lakini kwa hakika sitarajii kwamba mambo haya yatafanyiwa kazi, ama yatatekelezwa, kwa asilimia mia moja kabla ya uchaguzi wa mwaka 2025,” alieleza Abdallah.
“Kwa sababu, hali ya kisiasa ilivyo Tanzania hivi sasa, inapendelea upande wa chama tawala. Kwa hiyo, kurekebisha mambo haya tafsiri yake ni kwamba unauweka uwanja sawa wa kisiasa kuelekea uchaguzi wa mwaka 2025.
“Kwa hakika, sidhani kama Rais Samia atataka kuona changamoto kubwa ya kisiasa, au changamoto kubwa wakati anaelekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025,” alitabiri mchambuzi huyo.
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.