The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Deni la Taifa Kuendelea Kuwa Gumzo 2023?

Deni la taifa limegeuka kaa la moto, likiwaunguza watu mbalimbali wanaojaribu kutahadharisha juu ya athari zake.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Deni la taifa limeendelea kuzua gumzo miongoni mwa Watanzania, huku Serikali ikiendelea kusisitiza kwamba kukopa hakukwepeki kama kweli Tanzania, kama nchi, inataka kufanikisha mipango yake ya maendeleo.

Ni mjadala ambao unaweza kusema umegeuka kuwa kaa la moto, likiwaunguza watu wanaojaribu kuuibua na kutahadharisha juu ya athari ambazo nchi inaweza kukutana nazo endapo kama itaendelea na kasi ya sasa ya ukopaji.

Mtu wa hivi karibuni kabisa kujikuta matatani ni mtangazaji wa redio ya EFM Gerald Hando ambaye akizungumza kwenye kipindi chake cha asubuhi kiitwacho Joto la Asubuhi, cha Disemba 27, 2022, alikosoa kile alichokiita “kukopa sana” kwa Serikali.

“Mimi binafsi sipendi Serikali inavyokopa kopa hovyo,” alisema Hando, moja kati ya watangazaji mashuhuri nchini Tanzania. “Na Serikali inakopa sana. Tunaona kila siku na yenyewe-, hata Rais [Samia Suluhu Hassan] kafafanua, lakini mimi bado nasema hivi, tunakopa sana.”

Kauli hiyo haikumuacha Hando salama, kwani baada ya siku chache kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, mwajiri wake alijitokeza hadharani na kujitenga na kauli hiyo, huku mmiliki wa EFM na TVE Francis Majjizo akiita kauli hiyo “maoni binafsi ya mtangazaji” kwenye taarifa yake kwa umma.

Kufuatia maoni yake hayo, Hando alisimamishwa kazi kwa siku saba, huku mwajiri wake akiwaomba radhi wale wote “waliokwazika” na kauli ya Gerald Hando. Hando alitoa kauli hiyo katika muktadha wa kumtetea aliyekuwa Spika wa Bunge Job Ndugai, mhanga mwengine wa mjadala wa deni la taifa.

Ndugai, ambaye pia ni mbunge wa Kongwa (Chama cha Mapinduzi – CCM), alilazimika kujiuzulu kwenye nafasi ya Spika wa Bunge baada ya kukosoa hatua ya Serikali “kukopa sana,” akionya kwamba kuna siku Tanzania “itapigwa mnada” kutokana na madeni.

Deni kuendelea kukua

The Chanzo iliwauliza wachambuzi wa masuala ya kiuchumi kama wanadhani mjadala huu wa deni la taifa utaendelea kwa mwaka 2023 na jibu lao lilikuwa ndiyo, wakibainisha kwamba kutokana na miradi mingi ya kimkakati inayoendelea kujengwa nchini, hawaoni Serikali ikiacha kukopa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania ya Novemba 2022, mpaka kufikia Oktoba 2022, deni la taifa la Tanzania lilikuwa ni Dola za Kimarekani milioni 39,006.1 (takriban Shilingi trilioni 91 za Kitanzania), ambalo ni sawa na ongezeko la Dola za Kimarekani milioni 544.8 (takriban Shilingi trilioni 1.2), kwa mwezi.

Kwa mujibu wa Benki Kuu, asilimia 70.5 ya deni hilo ni deni la nje, ambalo ni sawa na Dola za Kimarekani milioni 27,482.2, ikijumuisha deni la Serikali na lile la sekta binafsi. Wachumi wanaamini kwamba deni hili litaongezeka, badala ya kupungua, 2023.

SOMA ZAIDI: Maboresho ya Bandari ya Tanga ni Fursa kwa Wananchi na Uchumi

Moja kati ya wachumi hao ni Dk Humphrey Moshi, gwiji la uchumi nchini, aliyeiambia The Chanzo kwenye mahojiano naye kwamba haoni deni hili likipungua ndani ya mwaka huu ulioanza, akitaja miradi mikubwa inayotekelezwa hivi sasa na Serikali kama sababu ya yeye kuwaza hivyo.

Baadhi ya miradi hii ni kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (SGR); ujenzi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP); mradi wa Kuimarisha Ujifunzaji katika Elimu ya Awali na Msingi (Boost); pamoja na miradi mingine kama hiyo ya maendeleo.

“Miradi hii mingine inachukua miaka miwili, mitatu, minne [au] mitano na hapa sasa hivi, kwa mfano, tumeona kama mradi wa reli, juzi juzi tumeona Rais [Samia Suluhu Hassan, akisaini, ile ya kutoka Tabora mpaka Kigoma. Sasa hicho siyo kitu ambacho kitaisha kesho,” alisema Dk Moshi.

Hoja ya Dk Moshi inaungwa mkono na Dk Vicent Mughwai, Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anayetabiri kwamba mwenendo wa deni la taifa kwenda juu mwaka 2023, pia akihusisha hali hiyo na miradi hiyo mikubwa ya maendeleo.

“Nafikiri [kasi ya kukopa] itaendelea kwa sababu, tukiangalia hata mwenendo unavyoonesha, mwenendo unaonesha kwamba ukopaji umekua ukienda juu kwa miaka kumi mfululizo,” alieleza msomi huyo. “Kwa hiyo, kila mwaka deni la taifa linapanda.”

Kama Mtendaji Mkuu wa Serikali, Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kukiri kwamba ni kweli Serikali inakopa, akibainisha kwamba anafanya hivyo kwa sababu mapato ya ndani hayatoshi kufanikisha juhudi za maendeleo.

Mara ya hivi karibuni kabisa kutetea sera yake hiyo ya kukopa ilikuwa ni Januari 3, 2023, wakati wa kikao chake na viongozi wa vyama 19 vyenye usajili wa kudumu nchini Tanzania, kilichofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam.

“Nasemwa kwa mengi,” Rais Samia alisema kwenye hotuba yake. “[Watu] wanasema, ‘Anakopa sana.’ Ndiyo, nakopa ili kuleta maendeleo makubwa. Na mnayaona. Na kila pesa tunayopokea tunaeleza tumeielekeza wapi, kwa mfano, kwenye SGR.”

Deni ni himilivu?

Utetezi mkubwa wa Serikali, hata hivyo, umekuwa ni kwamba deni la taifa bado ni himilivu, hoja ambayo siyo ngeni kwenye masikio ya Watanzania kwani huisikia mara kwa mara pale viongozi waandamizi wa Serikali na CCM wanapotoa ufafanuzi kuhusiana na suala hilo nyeti.

Lakini siyo Serikali tu ambayo haikubaliana na madai kwamba Tanzania imeshakopa sana kiasi ya wananchi wake kuwa na wasiwasi wa nchi yao “kupigwa mnada” kama Ndugai alivyoonya, wapo pia wachumi huru wasiokubaliana na mtazamo huo.

Deus Ngaruko ni profesa wa uchumi wa jamii kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) ambaye ameiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalum hivi karibuni kwamba deni la taifa la Tanzania halipo katika hatua inayotishia uchumi wa taifa hilo la Afrika Mashariki.

SOMA ZAIDI: Mbeya Katikati ya Mtanziko wa Kulinda Maslahi ya Kiuchumi na Kujikinga na Ajali za Barabarani

“Tanzania ni nchi inayokopesheka kulingana na vigezo vya kimataifa,” alisema Profesa Ngaruko. “Tunakopesheka vizuri tu. Kwa hiyo, deni la taifa halijatishia maisha ya uchumi wa Tanzania. Tuna vigezo vyote vya kimataifa [vya kukopesheka].”

The Chanzo ilimuuliza Dk Theresia Busagara, Mhadhiri wa Biashara na Uchumi kutoka UDSM, shida ya mikopo haswa ni nini ambapo alijibu kwamba mikopo haina shida endapo kama itaelekezwa kwenye shughuli muhimu za kiuzalishaji mali.

“Inategemea pesa tulizichukua na kwenda kuzipeleka wapi,” alieleza msomi huyo. “Kwa sababu, tunapozungumzia uzalishaji wa umeme, matarajio ni kwamba tutaenda kuzalisha umeme ambao tutauza nje, maana yake ule mkopo unaweza ukajilipa.”

Umakini zaidi unahitajika

Hata hivyo, bado wachumi wametaka kuwepo kwa umakini kwenye ukopaji ili kuinusuru Tanzania kutumbukia kwenye madhara makubwa kama yaliyozikumba nchi zingine zilizoshindwa kulipa madeni yake, ikiwemo kushindwa kabisa kulipa madeni hayo.

Dk Mughwai, kwa mfano, anasema hadhani kwamba ni kitu kizuri kwa nchi kujilimbikizia madeni, akisema hali hiyo “siyo afya kwa uchumi wa nchi.”

“Mikopo hiyo imekuwa ni mingi sana, kiuchumi ni kitu ambacho siyo kizuri,” anabainisha msomi huyo. “Yaani, uchumi unaweza ukaporomoka kama nchi ikiwa na madeni sana. Ukikopa, unaweka dhamana. Ukishindwa kulipa, unapoteza hizo mali. Iko hivyo hivyo kwa nchi.”

SOMA ZAIDI: Gavana Benki Kuu: Ni Muhimu Kuwa Makini Na Mikopo Ya Kibiashara

Profesa Moshi, kwa upande wake, anasema kwamba wakati ni kweli kwamba mikopo haikwepeki, basi angalau Serikali ijitahidi kuchukua mikopo yenye masharti nafuu ili kupunguza mzigo kwenye uchumi wake.

Mchumi huyo ameielezea mikopo yenye masharti nafuu kuwa ni kama ile yenye riba ndogo, muda mrefu wa kupumzika kabla ya kuanza kulipa na muda mrefu wa kulipa mikopo hiyo.

“Tukope lakini kitu cha msingi ni kwamba ni lazima tuhakikishe deni letu linaendelea kubaki kuwa himilivu,” alishauri Profesa Moshi. “Na ukitaka deni liwe himilivu ni lazima ukope kwa masharti nafuu.”

Hadija Said ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Dar es salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia barua pepe hadijasaid826@gmail.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Asante Hadija Said. Je umezungumza na NGO na asasi za wanahabari? Je wao wanamtetea mwezao Hando au wanajipendekeza kwa serikali? Si lazima ukubaliane na Hando ila ni vizuri kulinda uhuru wetu wa kutoa mawazo bila ya matusi wala kashfa. Hii ndio kazi ya NGO na asasi
    Tusiwe wanafiki

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *