Gavana Benki Kuu: Ni Muhimu Kuwa Makini Na Mikopo Ya Kibiashara

Gavana wa Benki Kuu amezungumzia umuhimu wa kuwa makini na kujilinda zaidi juu ya masharti ya mikopo ya kibiashara

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Gavana wa Benki Kuu Profesa Florens Luoga ameelezea umuhimu wa kuwa makini kwenye michakato ya Serikali kukopa mikopo ya kibiashara. Profesa Luoga ameelezea kuwa kutokana na kupanda hadhi kama nchi kuwa uchumi wa kati, hali hii inasababisha kupungua kwa  mikopo nafuu hivyo kuongezeka kwa msukumo wa kwenda kwenye mikopo ya kibiashara.

Luoga, ambaye kauli yake inakuja wakati taifa likigubikwa na mjadala mpana kuhusiana na deni la taifa, amekiambia kituo cha redio cha Clouds FM, kupitia kipindi cha Powerbreakfast leo Disemba 29, 2021, kwamba “kunaweza kuwa na madhara” pale Serikali inapokopa bila kujua masharti ya mkopo husika.

Mikopo ya kibiashara tatizo lake ni moja lazima uwe na uwezo wa kujadiliana ili isiwe na madhara, mkopo unaweza kuwa na madhara kama unakopa bila kujua masharti yake. Tena tusipokuwa waangalifu kwa wakati huu ambapo tumeingia katika uchumi wa kati, unapoingia huku, ina maana ile mikopo nafuu inaanza kuwa michache inabidi uwe makini sana unapokopa,” Profesa Luoga amefafanua.

Ugumu wa mikopo ya kibiashara

Ripoti ya tathmini ya hali ya ukopaji iliyotolewa Machi 2021, inaonyesha kuwa mpaka Juni 2020, mikopo ya kibiashara iliongezeka na kufikia asilimia 44.5 ya mikopo yote hii ikiwa ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kutokea.

Uwiano wa mikopo isiyokuwa ya kibiashara na mikopo ya kibiashara

Kuhusu ugumu wa mikopo ya kibiashara, Profesa Luoga anaelezea ugumu hasa wa mikopo huja kutokana na  masharti ambayo yanawekwa na watoa mikopo.

“Wale wanaosema weka Airport [kama dhamana] mara nyingi ni wale ambao wanatoa mikopo ya kibiashara,” alisema Profesa Luoga. “Sasa ni wewe mwenyewe kukubali ama kutokubali.”

Katika kukabiliana na hali hii Profesa Luoga anasema Serikali imejiwekea vidhibiti kadhaa katika majadiliano ya mikopo hiyo.

Anaeleza: “Hawa [wakopeshaji kibiashara] wote watakuambia kuwa katika dhamana yako tunataka Benki Kuu, airport. Unawaambia hapana. Haya masharti ni masharti hasi. Ni lazima tuweke safeguards [ulinzi]. Moja wapo ya safeguard [ulinzi unaowekwa] ni [mkopeshaji] usiniambie niweke dhamana reserve [hifadhi] za nchi sitaweka. Usiniambie niweke dhamana mali za kimkakati kama airport, bandari [au] Benki Kuu.”

Masharti mengine kutoka kwenye mikopo hiyo ya kibiashara ni pamoja na kuwa na riba kubwa.

Kwa mujibu wa Luoga, mikopo ambayo haina masharti nafuu mara nyingi ni mikopo ya kibiashara, ambapo anaeleza kwamba Serikali inaweza kukopa kutoka benki, masoko ya fedha ya kimataifa na kutoka nchi nyingine ambapo riba huwa ni ya kibiashara.

Mikopo ya kibiashara Tanzania 2019/2020

Katika Mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali ilichukua mikopo kadhaa ya kibiashara, ikiwemo mkopo wa dola za kimarekani bilioni 1.46 kutoka benki ya Standard Chartered kwa ajili ya kugharamikia ujenzi wa reli, mkopo ambao Profesa Luoga anaelezea kwamba waliweza kujadiliana na mkopeshaji kupunguza riba.

Hali ya Tanzania kukopa ikoje? 

Ripoti ya Benki Kuu inaonyesha mpaka kufikia Oktoba 2021, deni la Serikali lilifikia Shilingi trilioni 63.5. Deni la Serikali ni tofauti na deni la taifa, kwani deni la taifa linajumuisha mikopo ambayo pia inakopwa na sekta binafsi kwenye mashirika na taasisi za nje.

Hata hivyo, deni la taifa ndilo linalotoa sura nzima ya hali ya ukopeshwaji wa taifa na ikiwa kama taifa tuna deni stahimilivu. Mpaka kufikia Oktoba 2021, deni la taifa lilikua ni Shilingi trilioni 82.3, huku deni la Serikali ikiwa ni asilimia 71.6 ya deni lote.

Deni la taifa mpaka Oktoba 2021

Akiongelea juu ya ustahimilivu wa deni la taifa, Profesa Luoga amesema: “Tanzania katika bara letu ni nchi ambayo ina hadhi kubwa sana, ukichukua nchi tatu ama nne zinazoaminika katika kukuposheka Afrika mojawapo ni Tanzania.”

Vigezo ambavyo vinafanya Tanzania ibakie katika hali ya kukopesheka ni uzalishaji wake, yaani pato la taifa na uwezo wake wa kupata fedha za kulipa, kwa mujibu wa Luoga.

“Ukiangalia mikopo tuliyonayo bado hatujagusa hata kile kiwango cha kusema kuwa tuko kwenye debt stress sisi hatuko kwenye  hali nyekundu ya hatari bado tuko kwenye kijani,” anasema. “Kwa mfano, ukiangalia viwango vya debt service to revenue threshold ni 18 sisi 2020/2021 ilikuwa 14.6 tunategemea 2021/2022 kuwa 14.2 na tunategeme itashuka mpaka 12.”

Akizungumzia kuhusu pato la taifa na deni, Profesa Luoga anasema kwamba moja kati ya vipimo vya Tanzania ni kuwa viwango vya deni kwa pato la taifa [GDP] inapaswa deni lisizidi asilimia 70. Lakini ukiangalia tathmini ya mwisho ya uhimilivu wa deni ambayo ilifanyika mwezi Novemba 2020 Tanzania ilikuwa katika asilimia 27.9 ambayo ilikua ni chini ya nusu.

Pato la taifa vs deni la taifa

Ripoti ya Benki ya Dunia inaonyesha nchi ambazo zinaongoza kwa kuwa na deni kubwa kulinganisha na pato lake ni pamoja na Japan (257%), Ugiriki (238%), Italia (184%), Marekani (161%), Ureno (157%), Uingereza (154%), Hispania (148%), Ufaransa (146%), Canada (141%), Ubelgiji (141%). Akilinganisha Tanzania na nchi nyingine, Profesa Luoga anaelezea kuwa Tanzania ni ya 109, kati ya nchi 170 duniani, katika kulinganisha deni kwa pato la taifa,  hii ikimaanisha bado deni la Tanzania ni stahimilivu.

Dhamana za mikopo ninini?

Moja ya suala ambalo wasikilizaji wengi wa kipindi hicho cha asubuhi walitaka waelewe ni nini Serikali inaweka kama dhamana inapoenda kuchukua mikopo.

Akifafanua kuhusu hilo, Profesa Luoga alisema: “Asset kubwa ya Serikali ni wananchi na rasilimali za nchi. Lakini asset nyingine ya muhimu zaidi ni ubora wa utawala wa Serikali kwa sababu Serikali isipokuwa na uwezo mzuri wa kutawala na kusimamia uchumi ina maana itaingiza nchi katika mdororo wa kiuchumi lakini ukiwa na serikali imara ambayo inasimamia uchumi vizuri inamaana nchi inaendelea kukua.”

Kwa mujibu wa Profesa Luoga, wakopeshaji wanaangalia uongozi wa nchi katika kujihakikishia kuwa hakutakuwa na mdororo wa uchumi kutokana na uongozi mbovu. Lakini pia kama Serikali ina rasilimali za kutosha. Anaongeza: “Serikali moja inategemea uwezo wake rasilimali ilizonazo, mbili je, ina rasilimali fedha foreign reserve ambazo zinaweza kuhimili hilo deni?”

Kwa nini  Tanzania itaendelea kukopa?

Akielezea kuhusu ni nini kinatoa msukumo wa kukopa, Profesa Luoga anaelezea mikopo huwa inatokana na mipango kwa ajili ya miradi ya maendeleo na si matumizi ya kawaida.

Serikali inapoenda kukopa inaangalia vitu vingi,” anasema. “Moja [ni] malengo ya kukopa kwa sababu hatuendi kukopa kwa sababu hatuna pesa, tunaenda kukopa kwa sababu ya mipango tuliyojiwekea, hatuendi kukopa kama Serikali kwa ajili ya kula lakini tunapotaka kutengeneza assets ambayo itatumika mpaka vizazi vijavyo.”.

Kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan alisisitiza jana, Disemba 28,2021, kwamba Serikali itaendelea kukopa, Profesa Luoga naye anatilia mkazo na kuelezea sababu za msingi.

“ukitumia pesa ya ndani peke yake [kwenye miradi] lazima utapandisha kodi na utafanya wananchi wachangie kwa njia nyingine ambayo ni gharama na itakuchukua muda mrefu badala ya kutekeleza mradi katika miaka mitatu au minne utautekeleza kwa miaka 20,” anasema na kuongeza:

“Kwa sababu unategemea uchukue pesa za ndani kwahiyo hata huo mradi hautakuwa na manufaa kwako papo hapo. Unapokopa unaenda kufanya miradi ambazo zitaendelea kuzalisha na kwasababu zitaendelea kuzalisha ina maana uhimilivu wako wa deni unaendelea kuwa mzuri.”

Moja ya maswali ambayo Profesa Luoga aliulizwa na wasikilizaji ni inakuwaje inafikia mpaka tunasikia nchi nyingine bandari, au viwanja vya ndege vinataka kuchukuliwa na wakopeshaji watendaji wanakuwepo wapi?

Akifafanua juu ya hilo, Profesa Luoga anaelezea nafasi yake juu ya usimamizi wa mikopo na mfumo mzima wa usimamizi wa mikopo Tanzania, akisema: “Gavana ni mshauri na anakuwa  ya kamati ya madeni ya taifa (National Debt Management Committee) ili mda wote aweze kuhusika kutoa taarifa mwenendo wa deni ukoje ili serikali ifanye maamuzi.”

Profesa Luoga anaelezea pia kuwa kamati hiyo inaongozwa na Katibu wa Wizara ya Fedha, huku kukiwa na wataalamu wengine mbalimbali, “Na katika ile kamati mnaangalia kuwa madeni yenu yasiuze nchi ndo maana nchi haiwezi ikaweka rehani watu ama haiwezi ikaweka rehani rasilimali zake na itahakikisha kuwa itazitumia ili serikali iendelee kupata kipato.”

Moja ya tatizo kubwa linaloelezewa na wachambuzi wengi ni pale mamuzi ya kisiasa yanapozidi utashi wa wataalamu ambao uwezo wao ni kutoa ushauri tu kwa serikali. Tathmini ya mikopo inaonyesha kuwa kuna uwezekano mkubwa mikopo ya kibiashara ikaendelea kuongezeka, ni kwa namna gani Serikali inaweza kuendelea kujenga uwazi juu ya mikopo hii na mingine, masharti, malengo, pamoja na mlolongo mzima wa upatikanaji wake.

Wachambuzi wengi wanapongeza uwazi ulionyeshwa na Serikali juu ya mkopo wa hivi karibuni toka IMF na kuitaka serikali kuendeleza aina hiyo ya uwazi kwenye mikopo yote.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts