Wafanyakazi Wanaogoma Sahara Media Waeleza Masaibu Yao

Wafanyakazi wanadai kwamba kuna watu wana malimbikizo ya madeni ya mishahara ya zaidi ya miezi 25.

subscribe to our newsletter!

Mwanza. Wafanyakazi wa kampuni ya Sahara Media wapo kwenye siku ya tatu ya mgomo wao unaolenga kumshinikiza mwajiri wao alipe stahiki zao ambapo baadhi ya wafanyakazi wamesema inajumuisha malimbikizo ya mishahara ya miezi zaidi ya 25.

Mgomo huo ulianza hapo Januari 3, 2023, na kufahamika kwa jamii kutokana na vituo vya habari vya Star TV, Radio Free Africa na Kiss FM, vinavyomilikiwa na kampuni hiyo, kusitisha matangazo yake na kuanza kupiga tu muziki muda wote.

Mwandishi wa habari hii alifika katika ofisi za kampuni hiyo zilizopo Ilemela, jijini Mwanza majira ya asubuhi ya Januari 3 na kushuhudia hali iliyoashiria kwamba kuna kitu kisicho cha kawaida kinachoendelea.

Nje ya geti la ofisi hiyo, The Chanzo ilikuta kundi kubwa la wafanyakazi mbalimbali wa kampuni hiyo, waliokiri kwamba wako nje kwani kuna mgomo ulikuwa unaendelea ofisini hapo.

Baada ya ukinzani mfupi na mlinzi wa ofisi, mwandishi wa habari hii aliweza kuingia ndani ya ofisi za kampuni hiyo na kukuta wafanyakazi wengi zaidi wakiwa wamekaa katika eneo wanalotumia siku zote kwa ajili ya chakula.

Wafanyakazi wengi waligoma kuzungumza na The Chanzo, wakiielekeza izungumze na Aloyce Nyanda, waliyemwita kiongozi wa mgomo huo. Nyanda, ambaye ni mtangazaji wa Star TV, hata hivyo, aligoma kuongea chochote, huku akimshauri mwandishi aachane na habari hiyo.

SOMA ZAIDI: ‘Sheria Kandamizi Zinavifanya Vyombo vya Habari Visitekeleze Wajibu Wao Ipasavyo’

Sharbano Abubakar, ambaye ni afisa rasilimali watu msaidizi, aliiambia The Chanzo kwamba hakuna mgomo wowote ofisini hapo, akitaja uwepo wake kama ushahidi wa kauli yake, huku akikataa kujibu maswali mahususi ya mwandishi.

Licha ya kukanusha huko, The Chanzo inafahamu kwamba kuna mgomo unaoendelea katika ofisi za Sahara Media, hali inayoendelea kuathiri shughuli za kampuni, ikiwemo uzalishaji wa vipindi kwenye vituo vyake vitatu vya habari.

Mpaka wakati wa kuandika habari hii, leo Alhamisi, Januari 5, 2023, bado Star TV inaendelea kupiga tu muziki, huku vipindi kwenye Radio Free Africa na KISS FM vikiwa vimerudi, huku ripoti za kuaminika zikisema kwamba uzalishaji wake unafanywa kwenye ofisi zilipo Dar es Salaam.

Ni majanga matupu

The Chanzo ilifanikiwa kuzungumza na baadhi ya wafanyakazi walio kwenye mgomo kwa masharti ya kutowataja majina yao, ambapo wamefunguka kuhusiana na msingi wa mgomo huo ambao haujulikani utaisha siku gani.

“Hivi sasa, kuna watu wanadai hadi Shilingi milioni 60,” alisema mmoja ya wafanyakazi walio kwenye mgomo. “Kwa mfano, mwaka jana kuna watu wamelipwa miezi mitatu tu ndani ya mwaka mzima. Ukienda hata [Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii] NSSF hakuna hela, yaani ni majanga matupu.”

Mfanyakazi huyo alisema wamelazimika kugoma baada ya njia za mazungumzo zilizolenga kutatua tatizo hilo kugonga mwamba, licha ya kwamba mpaka viongozi waandamizi wa Serikali wanafahamu masaibu yao.

SOMA ZAIDI: Serikali, Wadau Wabainisha Changamoto Zinazoikabili Tasnia ya Habari Tanzania

Wafanyakazi hao wameiambia The Chanzo kwamba baadhi ya wenzao wanadai mishahara ya miezi zaidi ya 25, na kilichosababisha kufikia kudai miezi hiyo mingi ni kutokana na mfumo uliokuwa unatumika kulipa mishahara.

“Kwa mfano, mimi nikilipwa mwezi wa kwanza nikiwa natokea RFA, kwa mfano, baada ya wiki kadhaa, au mwezi unaofuata, watalipwa Star TV, mwezi mwingine tena wanalipwa KSS FM,” anafafanua mmoja ya wafanyakazi.

“Kwa hiyo, hadi mzunguko uishe unakuta miezi mitatu hadi minne mtu hujalipwa. Kwa hiyo, hayo madeni yanakuwa yanaongezeka,” alisema.

Wafanyakazi hao, hata hivyo, walisema kwamba tatizo la maslahi yao kutokupewa kipaumbele na mwajiri wao huyo ni la siku nyingi, linaloenda mbali zaidi hadi mwaka 2012.

“Mwaka jana, wafanyakazi wakaanza kulalamika, [kampuni] ikaja na ajenda ya kutaka kupunguzia watu mishahara, kama ulikuwa unalipwa Shilingi laki nane, utaanza kulipwa Shilingi laki nne, kama ni Shilingi laki sita, utalipwa Shilingi laki tatu,” alisema mfanyakazi mwengine aliye kwenye mgomo.

“Ilikuwa ni mwaka 2020 mwishoni, wafanyakazi wakagomea, wakalalamika kwenye vyombo vya Serikali, baada ya hayo malalamiko zoezi likasitishwa,” anaeleza.

Waandishi hao wanadai kwamba, mwanzoni mwa 2021, taarifa zilimfikia aliyekuwa Rais wa awamu ya tano John Magufuli, aliyetoa amri kwamba wadai wote walipwe.

Kukawa na mazungumzo na ikafikia makubaliano kwamba wawalipe watu walau asilimia 50 ya madeni yao.

Tatizo kubwa

Tatizo la Sahara Media, hata hivyo, ni kielelezo tu ya tatizo kubwa linalohusiana na malalamiko ya waandishi wa habari nchini Tanzania kwamba waajiri wao hawajali maslahi yao.

Mnamo Januari 12, 2022, kwa mfano, wakizungumza jijini Mwanza wakati wa kuaga miili ya waandishi watano waliofariki dunia kwenye ajali ya barabarani, wawakilishi wa waandishi wa habari waliiomba Serikali isaidie kuboresha maslahi ya waandishi wa habari nchini.

Wawakilishi hao walisema kwamba hata waandishi wenzao waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo walifariki wakiwa wanawadai waajiri wao, hali iliyomfanya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye kutoa siku saba kwa waajiri hao kulipa madeni hayo.

SOMA ZAIDI: Wanahabari Epukeni Makosa Haya Mnapokitumia Kiswahili

Pia, akizungumza kwenye Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022 lililofanyika jijini Dar es Salaam hapo Disemba 17, 2022, Nape aliahidi kwamba kwenye mwaka huu wa 2023, Serikali itaweka nguvu kwenye kulinda na kutetea maslahi ya waandishi wa habari.

“Mwaka unaofuata tutaweka nguvu za kutosha kwenye suala la maslahi ya waandishi wa habari na uchumi wa vyombo vya habari, ikiwemo mikataba ya waandishi wa habari ili kuongeza ari katika utendaji wa kazi,” Nape alinukuliwa akisema.

“Ukitaka maslahi ya waandishi yakae vizuri [ni] lazima uhakikishe uchumi wa vyombo vya habari unakaa vizuri, ikiwemo [kwa Serikali] kulipa madeni,” alisema mbunge huyo wa Mtama (Chama cha Mapinduzi – CCM).

Rahma Juma Salumu ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka jijini Mwanza, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia barua pepe salumurahma1@gmail.com.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts