The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kwa Nini Unapaswa Ufikirie Mara Mbili Kabla Ya Kutumia Usafiri wa IT

Polisi na wadau wa usalama barabarani wanasema usafiri huo siyo salama kwa wasafiri.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Wito umetolewa kwa wasafiri nchini kuepuka kutumia usafiri wa gari zinazosafirishwa kutoka Tanzania kwenda nchi nyingine, maarufu kama IT, huku wadau wa usalama barabarani na polisi wakisema usafiri huo siyo salama kwa abiria.

Magari hayo ambayo safari zake huanzia katika Bandari ya Dar es Salaam kuelekea nchi kama vile za Zambia, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), huvutia wasafiri wengi kutokana na tabia yao ya kwenda kwa haraka na nauli zake kuwa nafuu.

Hata hivyo, usafiri huo umeibua wasiwasi miongoni mwa wadau wa usalama wa barabarani hivi karibuni baada ya baadhi ya gari hizo kupata ajali na kupelekea maafa makubwa kwa taifa, huku waathirika wakibaki bila msaada wowote.

Ni kutokana na maafa hayo ndipo Jeshi la Polisi limeanzisha operesheni kali ya kuwasaka madereva wa gari hizo wanaopakia abiria ambapo mnamo Disemba 29, 2022, Jeshi la Polisi mkoani Pwani liliwakamata madereva 17 wa gari hizo kwa kupakia abiria, kitu ambacho ni kosa kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani, sura ya 168.

SOMA ZAIDI: Ajali za Barabarani Zilivyoteketeza Maisha ya Watanzania 2022

Mkoa wa Dodoma ni moja kati ya mikoa ambayo magari hayo hupita – mingine ni Pwani, Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Singida, Tabora, Shinyanga, Geita na Kagera – ambapo kutokana na operesheni kali ya Jeshi la Polisi usafiri huo kwa sasa haupatikani.

Mwandishi wa habari hii alitembelea eneo ambalo gari hizo zinajulikana kupakia abiria mkoani hapa la Four Ways Nkuhungu kujaribu kuona kama angweza kupata usafiri huo kuelekea Singida lakini ilishindikana baada ya usafiri huo kutokupatikana.

Mmoja wa wapiga debe katika eneo hilo aliieleza The Chanzo kwamba usafiri huo katika eneo hilo kwa sasa haupatikani kwani umepigwa marufuku, huku Jeshi la Polisi likiweka msisitizo kwamba dereva yoyote wa IT atakayeonekana anapakia abiria basi asahau kuhusu kazi hiyo.

Hiki ni kitu ambacho Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani kutoka Jeshi la Polisi wilaya ya Dodoma Mjini Mbwiga Mwakatobe anajivunia sana, akitoa wito kwa maeneo mengine ya nchi kuendesha operesheni kali ya kuzuia magari hayo kupakia abiria.

Akiongea na The Chanzo hapo Januari 3, 2023, Mwakatobe alitoa wito kwa wananchi kuacha kutumia usafiri huo, akisema siyo salama kwani gari hizo hazijaidhinishwa kupakia abiria.

SOMA ZAIDI: MOI Yapokea Wastani wa Majeruhi Sita wa Ajali za Bodaboda kwa Siku

“Hayaruhusiwi kabisa kupakia abria kwa sababu halina bima, kwa hiyo inakuwa ni bima tu ya gari,” alisema Mwakatobe. “Na tatizo lingine gari hili linapopatwa na ajali huyo mwananchi hawezi kulipwa.

“Kwa sababu itakuwa kwa njia ya madai, kwa njia ya madai kupata haki itakuwa ni kazi. kwa sababu na yeye mwenyewe atakua anajua kile chombo hakistahili kubeba abiria na yeye amepanda kwa makusudi. Wito wangu wasipande hayo magari.

“Tukibaini wapo madereva wenye tabia hiyo tutawafikisha mahakamani au kuwapa adhabu kali ili iwe fundisho kwa madereva wengine wanaoendesha magari ya IT.”

Rama Msangi ni Mkurugenzi wa Elimu, Habari na Mawasiliano kutoka taasisi ya mabalozi wa usalama barabarani nchini (RSA) ambaye ameiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalum kwamba wananchi hawana sababu ya kutumia usafiri huo kwa usalama wao wenyewe.

“Wananchi wanapaswa wafahamu kwamba kupanda kwenye hizo gari ni kosa. Siyo gari ambazo zimeidhinishwa na mamlaka kufanya kazi ya usafirishaji wa abiria, hilo ndiyo jambo la kwanza wanatakiwa walijue,” alisema Msangi.

“Madereva wanaoendesha gari za IT pia wanatakiwa watambue kwamba pamoja na kwamba wanafanya kazi hiyo katika mazingira magumu kama wanavyosema, wanao wajibu wa kuzingatia sheria za usalama barabarani, hususan suala la mwendo.

“Kwa sababu mwendo ndiyo kitu kinachosababisha ajali nyingi sana za IT na uchovu,” aliongeza balozi huyo wa usalama barabarani.

Jackline Kuwanda ni Mwandishi wa Habari wa The Chanzo anayepatikana mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts