The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Hivi Ndivyo Watu Wenye Kigugumizi Wangependa Uongee Nao

Imani kwamba watu wenye kigugumizi wana hasira hutokana na kutokujua namna nzuri ya kuongea nao.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Mwanzilishi wa Chama cha Mitindo Maalum ya Uzungumzaji Tanzania (CHAMMUTA) Ally Baharoon amebainisha namna bora ambazo watu wanaweza kuongea na watu wenye kigugumizi bila kuathiri saikolojia za watu hao.

Baharoon, anayefanya kazi zake jijini Dar es Salaam na Zanzibar, na ambaye anasema amekuwa na kigugumizi tangu akiwa na umri wa miaka mitano, alibainisha hayo wakati wa mahojiano maalumu na The Chanzo yaliyofanyika jijini hapa hivi karibuni.

Akizungumza katika mahojiano hayo, Baharoon, ambaye pia ni mwandishi, alisema kwamba kitu cha muhimu cha kuzingatia wakati wa kuzungumza na mtu mwenye kigugumizi ni kuhakikisha kwamba unamtazama machoni.

“Hii ni kwa sababu, wakati unaangalia chini na sehemu nyingine wakati unazungumza, kwa fikra za haraharaka za binadamu tunaona kama tunamsaidia kuepukana na aibu, kwa kweli imekuwa ni kinyume,” alisema Baharoon.

“Kwa sababu, wakati unamtazama machoni mtu mwenye kigugumizi, unampa ishara kwamba bado upo naye na unamsikiliza,” aliongeza mdau huyo. “Kwa hiyo, hiyo inamsaidia kujenga hoja na kujiamini zaidi kuendelea na mazungumzo hayo.”

Kitu cha pili cha kuzingatia wakati wa kuzungumza na watu wenye kigugumizi, ambao kwa tathmini ya Baharoon ni asilimia moja ya watu wote waliopo nchini, ni kuhakikisha kwamba akikwama unahakikisha usimmalizie maneno au sentesi.

“Ni suala la kuvuta subira kidogo na kumpa nafasi ya yeye kumalizia mwenyewe,” anabainisha Baharoon.

Baharoon pia alisema kwamba njia nyengine ni kuhakikisha kwamba mtu mwenye kigugumizi awe na sehemu ya kuona kwamba ile changamoto yake haikucheleweshi wewe.

“Mara nyingi unapomuona mtu mwenye kigugumizi unaona kama kuna haja ya kumuambia niko na wewe [au] vuta pumzi,” anasema. “Lakini vitu vyote hivi anakuwa anafahamu. Kwa hiyo, wakati unasema hivyo kisaikolojia anakuta yeye anakuchelewesha wewe.”

Kutokujua namna bora ya kuzungumza na watu wenye kigugumizi, kwa mujibu wa Baharoon, hupelekea watu kuwa na imani potofu dhidi ya watu hao, kama imani kwamba watu wenye kigugumizi ni watu wenye hasira.

SOMA ZAIDI: Kijana Huyu Anataka Kutokomeza Upweke Walionao Watu Wenye Kigugumizi Tanzania

“Hiki ni kitu ambacho kimejengwa na jamii,” alisema Baharoon. “Kwa sababu, watu wenye kigugumizi huwa wanakatizwa katikati ya maongezi yao. Kwa hali ya kawaida, mtu yeyote ambaye haachiwi amalize ujumbe wake lazima atakuwa na hasira.”

Baharoon amekosoa tabia ya baadhi ya watu, hususan waandishi wa habari, ya kukinasibisha kigugumizi na taswira mbaya, hali ambayo amesema imekuwa na athari kubwa za kisaikolojia kwa watu hao.

“Mara nyingi unakuta mtu anatumia neno kigugumizi kumaanisha kitu kimefeli,” alisema Baharoon. “Utakuta kwenye vitu ambavyo havihusiani na kigugumizi linawekwa kuleta maana ambayo inaleta taswira mbaya. Kwa mfano, utasoma kichwa cha habari kinasema Manchester United imepata kigugumizi katika ligi ya Uingereza. Hiyo siyo sawa.”

Mdau huyo anayejaribu kuishawishi jamii kuwachukulia watu wenye kigugumizi kama binadamu wengine anasema ni muhimu sana kwa mabadiliko kutokea kwani watu hao wanakabiliwa na changamoto kadhaa zinazosababishwa na hali yao hiyo.

Changamoto kubwa, kwa mujibu wa Baharoon, ipo kwenye sehemu za ajira ambapo watu wengi wenye kigugumizi hukosa ajira kutokana na dhana kwamba wanakuwa wamekosa ukamilifu fulani wa akili.

“Mara nyingi waajiri wanaona mtu mwenye kigugumizi yuko taratibu kupata maarifa na kutatua shida,” anaeleza mdau huyo. “Kwa hiyo, huwa hapewi ajira za kutegemewa sehemu nzuri. Sehemu za ajira zinakosa watu wenye kigugumizi kwa sababu ya dhana potofu.”

Kwenye eneo la mapenzi na ndoa pia, Baharoon anakiri kukutana na kesi nyingi ambapo mtu anakataliwa kupewa mke au hata kuolewa kwa sababu jamii inadhani kigugumizi kinarithishwa.

“Niseme tu hiyo ni dhana potofu,” anaeleza. “Kigugumizi hakirithishwi. Mara nyingi, tumekuta mzazi ana kigugumizi mtoto hana au mtoto ana kigugumizi mzazi hana. Vitu hivi vimekuwa na shida kwa sababu jamii imejenga kuona kwamba kigugumizi ni kama kipingamizi fulani.”

Kutokana na changamoto hizi, Baharoon anasema yeye na chama chake, kwa kushirikiana na wadau wengine, wanatarajia kwenye mwaka huu wa 2023 kujikita zaidi kwenye eneo la uelimishaji, hususan miongoni mwa wazazi na walezi.

“Wito wangu kwa jamii ni kuhakikisha kwamba mtoto ukiona anapata shida ya kigugumizi, hakikisha unampa nafasi ya kumaliza maneno yake na siyo kumkatisha,” alisema Baharoon.

“Kwa upande wa Serikali, kwa kweli Serikali inahitaji kuhakikisha kwenye ajira watu wenye kigugumizi hawatengwi, au hawakataliwi fursa ya kufanya kazi, kwa sababu ya changamoto ya kigugumizi,” aliongeza.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *