Je, Wimbi la Pili la Siasa za Kijamaa Amerika Kusini Litadumu?

Itategemea na namna watakavyokabiliana na changamoto za nchi zao na zile za kidunia, kama vile sera zisizorafiki dhidi yao.

subscribe to our newsletter!

Mnamo Juni 19, 2022, matokeo ya uchaguzi nchini Colombia yalitangazwa na  mwanasiasa mjamaa Gustavo Petro kutoka muungano wa vyama vya mrengo wa kushoto, Pacto Historico, alishinda uchaguzi uliohusisha wapiga kura milioni 39 kwa ushindi wa asilimia 50.44, akimshinda mpinzani wake Rodolfo Hernandez mwenye kufuata sera za uliberali aliyepata asilimia 47.31 ya kura zote.

Uchaguzi huu ulileta msisimko sana si kwa kuwa Gustavo alikuwa Rais wa kwanza mjamaa kushinda kwenye kipindi cha hivi karibuni kwenye nchi za Amerika Kusini bali alikuwa Rais wa kwanza mjamaa kuongoza nchi ya Colombia tangu nchi hiyo ipate uhuru wake hapo Julai 20, 1810.

Ikumbukwe baada ya aliyekuwa Rais wa Venezuela Hugo Chavez kuingia madarakani mnamo mwaka 1999, miaka sita baadae robo tatu ya nchi za Amerika Kusini zilikuwa na Serikali za mrengo wa kushoto madarakani huku Colombia ikiendelea kusimama kama kiongozi wa sera za kiliberali.

Kuibuka kwa wimbi la siasa za kijamaa kulinasibishwa na kufeli vibaya kwa sera za kiliberali ambazo mchumi Reggie Strator alizibatiza  jina la “Anglo-Saxon Model of Capitalism,” zilizoanza kutekelezwa miaka ya 1950, zikiambatana na mpango wa  kuzifanya nchi za ukanda huo kuzalisha bidhaa ambazo zilikuwa zinaongoza kwa kuagizwa kutoka mataifa ya nje.

Mpango huo, uliotekelezwa kwa ushauri wa taasisi za kifedha kama vile Benki ya Dunia na Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF), uliziingiza nchi za Amerika Kusini kwenye madeni makubwa na kuzilazimisha kuingia kwenye mdororo wa kiuchumi kwenye miaka ya 1970.

Kudorora kwa uchumi wa nchi hizi kulizifanya zishindwe kulipa wadeni wake, hali iliyozilazimisha taasisi za fedha za kimataifa kuingilia kati kusaidia kile walichokiita “kuhuisha uchumi” wa mataifa husika.

Katika mchakato huo, nchi hizo zilizuiwa kujihusisha na usimamizi wa uchumi, kupunguza idadi ya wafanyakazi kwenye viwanda pamoja na  kuacha kutoa ruzuku kwenye sekta ya afya na elimu.

Kwenye kutekeleza hili, mataifa hayo yakaletewa washauri wa uchumi kutoka Marekani ambao walifahamika kama “Chicago Boys” ambao jukumu lao lilikuwa ni kuzisaidia Serikali hizi kutekeleza sera hizo mpya.

Hata hivyo, mchakato huo wa “kuhuisha uchumi” haukufanikiwa na kuziacha nchi hizo kwenye janga kubwa la umasikini na kuongezeka kwa pengo lililokuwepo kati ya matajiri na masikini.

Shauku ya mabadiliko

Hali hii ilijenga shauku miongoni mwa wananchi ya kupata viongozi wapya watakaowasaidia kutoka kwenye hali hizo.

Mnamo miaka ya 1970, vyama vyenye kufuata itikadi ya mrengo wa kushoto vikaanza kuibuka kwenye nchi mbalimbali za Amerika Kusini.

Kati yao ni kama vile Sandinista National Liberation Front (Nicaragua), Guyana Action Party pamoja na Socialist Party of Chile, chama ambacho kilifanikiwa kushika madaraka kuanzia Novemba 3, 1970 hadi  Septemba 11, 1973 pale kiongozi wake na Rais wa Chile Salvador Allende alipopinduliwa na dikteta Augistino Pinochet kwa msaada wa Marekani.

Katikati ya tawala za kijeshi katika Amerika Kusini, mnamo Februari 1999 Kepteni wa Jeshi Hugo Chavez aliyekuwa muumini wa sera za kijamaa aliweza kuchukua madaraka kwa njia ya kidemokrasia nchini Venezuela kwa kumshinda mwanamama Irene Saez kwa asilimia 56 za kura zote kupitia vuguvugu la Mapinduzi ya Ki-Bolivar.

SOMA ZAIDI: Je, Mjamaa Lula Atainusuru Demokrasia Brazil?

Ikumbuwe pia Chavez alijaribu kufanya mapinduzi ya kijeshi mwaka 1992 na kushindwa hivyo kupelekea kutiwa korokoroni na Rais Carlos Andrez Perez ambapo baadae alikuja kuachiwa kwa msamaha wa Rais Rafael Caldera.

Ushindi wa Chavez pamoja na mafanikio ya utekelezaji wa sera zake nchini Venezuela ulipanda mbegu ya mageuzi kwenye mataifa mengine ya Amerika Kusini na kupelekea vyama vingi vya kijamaa kuanza kushika dola kwenye ukanda huo.

Waliofuata nyayo za Chavez ni kama vile Ricardo Lagos (Chile – 2000), Luiz Inacio Lula da Silva (Brazil – 2002), Nestor Kirchner (Argentina – 2003), Tabare Vasquez (Uruguay – 2004), Evo Molares (Bolivia – 2005), Daniel Ortega (Nicaragua – 2006), Rafael Correa ( Ecuador – 2006 ), Michelle Bachelet (Chile – 2007), Fernando Lugo (Paraguay – 2007), Mauricio Funes (El Salvador – 2009) nakadhalika.

Ujio wa tawala hizi katika Amerika Kusini ulizaa kile kilichokuja kuitwa ‘Pink Tide.’

Mpaka kufikia mwaka 2013, mwaka ambao Chavez alifariki, kwenye mataifa 12 ya Amerika Kusini, ni mataifa mawili tu ndiyo hayakuwa na Serikali zenye mrengo wa kijamaa madarakani: Colombia na Paraguay.

Hata hivyo, mpaka kufikia 2018, ni Venezuela na Bolivia tu ndiyo zilikuwa zikiendeshwa na vyama vya mrengo wa kushoto.

Anguko la ‘Pink Tide’

Kwa kiwango kikubwa, kuanguka kwa ‘Pink Tide’ kulitokana na mambo yaliyokuwa nje ya uwezo wa nchi husika, kama vile sera zisizo rafiki dhidi yao kutoka kwa mataifa makubwa ya kidunia na taasisi kubwa za kifedha, ambazo zilijumuisha hatua kama vile nchi kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na kunyimwa kwa mikopo ya maendeleo.

Sababu nyengine inayotajwa ni anguko la uchumi la mwaka 2008 ambalo liliiathiri China, aliyekuwa mshirika mkubwa wa maendeleo wa nchi hizi, ambaye hatua yake ya kulinda unchumi wake usiathiriwe zaidi na anguko hilo zilikuwa na athari ya moja kwa moja kwa nchi hizo zilizokuwa zikiendeshwa na wanasiasa wa mrengo wa kushoto.

China ilikuwa mwokozi kwa chumi za nchi hizo hususan kutokana na ukweli ulioelezwa hapo juu kwamba mataifa mengi ya magharibi, ikiwemo Marekani, hayakuwa na sera rafiki kwa tawala hizo za wanasiasa wa mrengo wa kushoto hali iliyozilazimisha nchi hizo “kuangalia mashariki.”

SOMA ZAIDI: Ushindi Wa Arce Ni Ujumbe Kwamba Kuteleza Morales Sio Kushindwa Kwa Ujamaa Bolivia 

Matokeo yake, nchi hizo zilipunguza kasi ya uwekezaji na utoaji wa mikopo hasa yenye riba nafuu.

Kubwa lililoathiri zaidi, hata hivyo, ni upunguzaji wa manunuzi ya mafuta, chuma, shaba na gesi asilia hali ambayo yenyewe ni athari za anguko la uchumi wa kidunia iliyozilamisha nchi nyingi za Amerika Kusini kuwekeza zaidi kwenye sekta za elimu na afya.

Mgogoro wa Libya wa mwaka 2011 pia unatajwa kuchochea anguko la wimbi la kwanza la tawala za kijamaa kwenye Amerika Kusini kwani kuanguka kwa taifa hilo la Afrika Kaskazini kufuatia uvamizi wa vikosi vya Umoja wa Kujihami (NATO) kulizipunguzia fursa nchi hizi kwenye soko la mafuta kwa kuwepo kwa usambazaji haramu wa mafuta kwenye soko la dunia.

Kwa sababu hizi na nyingine nyingi viongozi wengi wa siasa za mrengo wa kushoto walilazimika kufunga virago vyao na kuachia madaraka kwa viongozi wengine, wengi wao wakiwa ni wale wanaowakilisha siasa kali za mrengo wa kulia.

Ilianza na Fernando Lugo (Paraguay-2012) na kuendelea kwa Alvaro Colom (Guatemala-2012),Mauricio Funes (El Salvador-2014), Cristina Fernandez de Kirchner (Argentina-2015), Jose “Papa” Mujica (Uruguay-2015), Ollanta Humala (Peru-2016), Dilma Rouseff (Brazil-2016), Rafael Correa (2017) nakadhalika.

Historia kujirudia?

Hata hivyo, hivi sasa tunashuhudia sababu zilezile zilizopelekea kuibuka kwa wingi kwa tawala za kijamaa katika Amerika ya Kusini zikichochea mabadiliko kwenye nchi nyingi za ukanda huo, zikiviweka madarakani vyama vinavyofuata siasa za mrengo wa kushoto na kupelekea wadadisi kuhoji endapo kama dunia inashuhudia kurudi kwa ngwe ya pili ya ‘Pink Tide.’

SOMA ZAIDI: Kapteni Traoré Kurejesha Fikra za Sankara Burkina Faso?

Sababu hizi ni pamoja na kutanuka kwa pengo kati ya walionacho na wasiokuwa nacho; ukandamizaji mkubwa wa haki msingi za binadamu, ikiwemo haki-jamii; kutengwa kwa makundi fulani ya kijamii, kama vile wenyeji wa mataifa husika; na utekelezaji sera zenye kuwanufaisha matajiri na kuwaangamiza masikini.

Hizi ni changamoto kubwa ambazo viongozi wapya wa siasa za mrengo wa kushoto wamezitaja kama matatizo makubwa yanayozikabili nchi zao na kuapa kuendesha mapambano makali kuhakikisha kwamba wanazitatua na, kama Rais mpya wa Brazil Luiz Inácio Lula da Silva alivyosema, “kurejesha tabasamu” kwa wananchi.

Swali kubwa lililobaki ni kwamba je, kizazi hiki kipya kitaweza kukabiliana na mitikisiko ya kisiasa, kiitikadi na kiuchumi na kulifanya wimbi hili kuwa endelevu au, kama ilivyokuwa kwa watangulizi wao, wataruhusu nguvu za kidunia ziliwalazimishe kumwaga manyanga na kukimbia mapambano ya kujenga dunia mpya yenye kuzingatia haki na ustawi wa kila mmoja?

Wakati, wanasema waungwana, utajibu!

Ezra Yona Nnko ni mchambuzi wa uchumi na siasa za kimataifa. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ezra.nnko@gmail.com au +255 765 571917  / +255 784 527018. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts