The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ushindi Wa Arce Ni Ujumbe Kwamba Kuteleza Morales Sio Kushindwa Kwa Ujamaa Bolivia

Bolivia imetoa fundisho kwamba sera za kijamaa zinatekelezekaikiwa viongozi watakuwa waadilifu na kipimo ni mafanikio yaliyopatikana kwenye Uchaguzi Mkuu wa Bolivia.

subscribe to our newsletter!

Wasoshalisti nchini Bolivia na  wajamaa sehemu nyengine Amerika Kusini na Kati  wamesherehekea ushindi unaotajwa kuwa wakihistoria baada ya  uchaguzi wa Rais  Jumapili iliopita, Octoba 18, 2020. Ni ushindi wa mgombea wao Luis Arce, sahibu wa chanda na pete wa Rais wa zamani wa Bolivia Eva Morales na wa Chama  cha Kisoshalisti cha Movement for Socialism (MAS), au Vuguvugu kwa Ajili ya Ujamaa MAS.

Morales  alikuwa  Rais wa kwanza  wa Bolivia kutoka jamii ya wakaazi asilia wa nchi hiyo aliyechaguliwa mwaka 2006.  Morales aliyekuwa kiongozi wa chama cha wafanyakazi kabla ya kujibwaga kwenye siasa, alipata umaarufu mkubwa hasusani miongoni mwa wakaazi asilia (indigeneous people) kutoka  maeneo ya  vijini ya nchi hiyo ya Amerika ya Kusini.

Baada ya kuitumikia Bolivia kwa miaka 14 kama kiongozi wake mkuu, Morales aliyapa kisogo  matokeo ya  kura ya maoni  ya 2016  yaliounga mkono hoja ya kuwepo kwa ukomo wa mihula ya uraisi nchini humo. Mwaka jana, 2019, Morales  akagombea  kipindi cha nne. Tume ya Uchaguzi ilipomtangaza  tena kuwa mshindi dhidi ya mpinzani wake Morales akapata upinzani mkubwa kutoka kwa wahafidhina na shinikizo kutoka nchi ya Marekani pamoja na viongozi wa kihafidhina kutoka  Jumuiya ya Mataifa ya Amerika, OAS.

Evo Morales aliendelea kusakamwa pia na vyombo vya ulinzi vya Bolivia, ikiwemo polisi. Baadhi ya vigogo jeshini nao walijiunga na wimbi hilo. Akiwa amebanwa kila kona, Morales akalazimika kujiuzulu na kwenda uhamishoni kwanza nchini Mexico na baadae Argentina.

Wahafidhina waunda Serikali

Spika wa Bunge Jeanine Anez akakimbilia kuchukua madaraka kwa mujibu wa Katiba. Bibi huyu mhafidhina aliyeiongoza serikali ya mpito, aliingia kwa mbwembwe na kutangaza hatua kadhaa za kuachana na sera za kijamaa zilizoasisiwa na Morales na chama chake cha MAS.

Katika uchaguzi huo  ulioitishwa Jumapili, Oktoba 18, Anez alijitangaza mgombea lakini baada ya kuona dalili za kushindwa alijiengua akisema ni  hatua ya kuzuia kuzigawa kura za wahafidhina na hivyo kumuachia uwanja  mhafidhina  mwenye msimamo wa wastani Carlos Mesa.

Mesa alikuwa na nafasi zaidi kuliko Anez. Ilitumainiwa kuwa pindi uchaguzi ukiingia duru ya pili watakuwa na nafasi ya kumshinda Luis Arce, mrithi wa Morales kutoka chama cha MAS. Hata hivyo, mambo hayakuwa kama walivyotarajia kwani matokeo yalimpa Arce ushindi wa moja kwa moja.

Ushindi wa Arce unaweza kuwa na maana nyingi. Moja inaonekana kwamba raia wengi wa Bolivia, wakiwemo wajamaa, huenda walimkataa Morales asijiongezee muhula mwengine lakini hawakuzikataa sera za chama chake cha kisoshalisti.

Hilo wamelidhihirisha bayana katika uchaguzi wa Oktoba 18 kwa kumpa ushindi mnono mgombea wao Arce ambaye wapinzani wake wamedai aliteuliwa na swahiba yake Morales.

Fundisho kwa nchi za kijamaa

Wabolivia wamezingatia matunda waliyovuna tangu Morales alipoingia madarakani. Hawakusahau madhila ya miongo mingi chini ya  tawala za kijeshi, kidikteta na kihafidhina ambazo zilikandamiza haki za binadamu na kutojali maisha ya walio wengi katika  taifa hilo masikini.

Bolivia  imetoa fundisho la kuwa sera za kijamaa zinatekelezeka, ikiwa viongozi watakuwa waadilifu na kipimo ni mafanikio yaliyopatikana. Ndio maana  mgombea wa Chama cha Kisoshalisti Arce akachaguliwa na kukirejesha chama hicho madarakani.

Na amini kwamba hili pia litakuwa funzo kwa watawala na vyama vyengine vya mrengo wa kushoto katika Amerika Kusini na Kati ambavyo vishindwa kujenga mustakbali mwema na raia wa nchi hizo na kutumbukia katika dimbwi la  ubadhirifu wa mali za umma na kujitajirisha, kinyume na  walichokuwa wakikipigania  kabla ya kuingia madarakani.

Mfano mmoja ni nchi ya Nicaragu, nchi ya Amerika ya Kati, na kiongozi wake Daniel Ortega, aliyegeuka mtawala wa kimabavu na aliyelewa madaraka. Viroja vya  Ortega ni pamoja na kumteuwa mkewe kuwa  makamu wake wa Rais. Miongoni mwa waliompinga alikuwa mtu niliyemhusudu binafsi Comrade Ernesto Cardenal aliyewahi kuwa waziri wa utamaduni, mwanazuoni wa kikatoliki aliyehasimiana wakati mmoja na Kanisa alipolishitumu lilikuwa likiyafumbia macho maovu ya  watawala wa kidikteta katika Amerika Kusini. Cardenal  aliyendelea  kumkosoa Ortega kwa kwenda kinyume na malengo ya mapinduzi alifariki mwaka jana, 2019.

Ushindi wa Arce utakuwa umepokelewa kwa furaha na serikali za mrengo wa kushoto katika kanda hiyo, kama Mexico, Argentina, Venezuela na Cuba ambazo zilikiunga mkono chama cha  MAS. Wote watakuwa wanayaangalia matokeo kuwa ni kurejea kwa Ujamaa katika eneo hilo.

Ushindi huu ni pigo kubwa kwa wahafidhina nchini Bolivia, lakini pia ni pigo kwa  utawala wa Raisi wa Marekani Donald Trump na washirika wake katika kanda ya Amerika kama Brazil na Chile walioshadidia na kushinikiza Morales aondoke madarakani. Trump na Rais wa  Brazil Jair Bolsonaro, mfuasi wa siasa  kali za kizalendo za mrengo wa kulia aliyepewa jina la Trump wa Amerika Latino, walishangiria alipojiuzulu Evo Morales  mwaka 2019.

 

Mohamed Abdulrahman ni mwandishi wa habari mstaafu na mtangazaji gwiji wa kimataifa. Alishawahi kuwa Naibu Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani, DW, katika idhaa yake ya Kiswahili. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni mamohamed55@hotmail.com au kupitia akaunti yake ya Twitter ambayo ni @mamkufunzi. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *