Wasanii, Chukueni Tahadhari Hii Katika Mikataba ya Matangazo

Ni muhimu sana kwa wasanii kuhakikisha mnajidhatiti kwa kuwa na uwakilishi madhubuti wa kisheria katika usimamizi wa masuala yenu ya sanaa.

subscribe to our newsletter!

Ikiwa mwaka bado ni mchanga na ikiwa tunaendelea kushiriki katika wiki ya sheria, nimelazimika kutumia kalamu na taaluma yangu kutoa rai hii kwa wasanii, wakati tunaendelea kuzifungua kurasa za kitabu cha mwaka 2023.

Kama mdau wa sanaa na msanii pia – mwandishi na mtumbuizaji wa mashairi nimekuwa nikiumia sana, panapo mawio na machweo, kila nisikiapo kilio kikubwa cha wasanii kudhulumiwa haki zao za msingi, zinazotokana na sanaa yao. Aghalabu, vilio vyao huelezwa kusababishwa na wasanii wenyewe kurubuniwa na kurubunika kuingia kwenye mikataba isiyo rafiki na isiyolinda maslahi yao kwa kiwango kikubwa.

Licha ya msisitizo ambao umeendelea kutolewa juu ya wasanii kusaka na kuwa na uwakilishi na ushauri wa kisheria katika masuala ya mikataba na masuala yeyote yanayohusiana na sanaa; bado mwangwi wa vilio vya wasanii vilio vimeendelea kutanda na kurindima katika kila kona ya jamii yetu.

Kama msanii, mdau wa sanaa na mwanasheria, katika kuadhimisha wiki ya sheria, nimelazimika kuandika kwa wasanii na jamii kwa ujumla, kusisitizia kwa wasanii kuchukua tahadhari katika kipengele cha umiliki, hususani katika mikataba ya matangazo.

Wasanii na soko la matangazo

Leo hii wasanii na watu wengi wenye aina fulani ya umaarufu wana makubaliano au mikataba na wadau mbalimbali kutengeneza maudhui (content) kadhaa wa kadhaa kwa ajili ya kutangaza bidhaa. Wapo wanaotangaza miwani, wapo wanaotangaza mavazi na wapo wengine wanaotangaza vifaa vya kielektroniki nakadhalika.

Katika mchakato mzima wa kutengeneza matangazo husika wasanii hulazimika kuumiza vichwa vyao na hupitia hatua kadhaa mpaka tangazo hilo kukamilika, ikiwemo: uundaji wa wazo, utunzi, uwasilishaji kwa muhusika, uboreshaji wa wazo na utunzi, maandalizi, utengenezaji wa tangazo lenyewe sasa na hatua nyenginezo zozote zile.

Pamoja na purukushani zote hizo, muhimu sana kuhoji iwapo kabla ya yote hayo, je mmekuwa na mikataba ya maandishi ya namna yeyote ile? Pili, je mkataba huo unaeleza nini kuhusiana na umiliki wa tangazo husika? Tatu, mkataba huo unaeleza nini kuhusiana na suala la muda wa tangazo husika?

Tutafakari kwa pamoja kwa mifano:

Msanii anapaswa kuandaa tangazo kuhusiana na ubora wa sabuni fulani au mtandao fulani wa simu au shughuli yeyote ile; naye anaandaa tangazo kwa mfumo wa wimbo au igizo na kisha analikabidhi kwa muhusika. Kampuni ambayo imepatiwa inapewa wimbo au igizo husika na inaridhishwa na tangazo hilo.

Makubaliano ni kuwa tangazo hilo husika linalomhusisha msanii huyo litaruka kwa muda wa miezi sita (labda kama tu pande zote zitaamua kuongeza muda); lakini katika mwezi wa nane, tangazo linaendelea kuchezwa redioni na mtandaoni, lakini sauti na sura inayotokea sio ya msanii wa awali, bali ni ya msanii mpya au mtu mwengine. Hapa ndipo sasa shida huanza.

Mara nyingi, hapa utakuta msanii anahamaki na kuanza kudai ya kwamba anaibiwa au ameibiwa haki yake. Msanii atasisitiza ya kwamba yeye ndiye mtunzi wa tangazo husika, hivyo yeye ndiye mmiliki wa kazi hiyo ya sanaa. Lakini je sheria ndio inasema hivyo? La hasha!

Sanaa na umiliki wa kazi ya sanaa

Katika sheria ya hakimiliki, ni dhahiri kuwa kifungu cha 15(i) kinamtambua mtunzi wa kazi ya sanaa ndiye mmiliki halisi wa kazi ya sanaa. Hata hivyo, ni muhimu kutambua kuwa sheria haisomwi kwa kuangalia kifungu au sehemu moja.

Kifungu cha 15(4) cha sheria hiyo hiyo ya hakimiliki kinafafanua zaidi na kueleza na kutambua kuwa mtunzi anaweza kutunga kazi ya sanaa kwa ajili ya mtu mwingine au kwa ajili ya taasisi fulani. Katika hali kama hii, yule aliyetungiwa kazi ndiye atakayesalia kuwa mmiliki wa kazi husika ya sanaa, labda tu kama mkataba wa makubaliano unaeleza tofauti.

Kwa mantiki hii basi, kampuni ambayo kazi fulani ya sanaa imetungwa itakubaliana kabisa na msanii kwamba yeye ndiye mtunzi halisi wa kazi husika ya sanaa; hata hivyo kampuni husika itapingana na hoja ya kwamba msanii ndiye mmiliki wa kazi ya sanaa. Hapa kampuni itasisitiza kuwa mkataba unaeleza dhahiri kuwa msanii atatunga tangazo fulani kwa namna fulani kwa ajili ya kampuni hiyo; na zaidi zaidi mkataba utaeleza kuwa kampuni ndiyo itabaki kuwa mmiliki wa tangazo husika.

Hata kama mkataba usiposema pia kuwa mmiliki itakuwa kampuni na hicho kipengele cha umiliki kikawa kimya (yani hakijaelezwa dhahiri kwenye mkataba), sheria kupitia kifungu cha 15(4) kinatoa haki ya umiliki katika mazingira haya kwa kampuni iliyotungiwa kazi husika ya sanaa. Hii inaweza kuonekana kwamba stahiki husika ya msanii alishaipata kwa kulipwa kutengeneza tangazo; na hivyo tangazo hilo linaweza kuchukuliwa kama uwekezaji wowote ule wa kampuni kwa ajili ya manufaa yake.

Kwa namna nyingine msanii aliyetunga tangazo husika kwa malipo anaweza kulinganishwa na mtangazaji aliyeingiza sauti kutangaza kipindi fulani au msanifu aliyechora nembo ya kampuni na vyote kwa pamoja sasa ni mali za kampuni. Hawa watu, hata watakapo acha kazi, ubunifu wao utaweza kuendelea kutumiwa na muajiri wao wa awali, kwani kimsingi mmiliki wa ubunifu huo mara nyingi huwa muajiri mwenyewe.

Hakimiliki na udumavu wa msanii kiuchumi

Katika taswira ya juu juu, msanii aliyepata kiasi chake fulani cha kazi kwa kufanya tangazo fulani, ni dhahiri anaweza kujiona amefanikiwa kwa namna moja au nyingine kwa “mchongo” husika. Hata hivyo, msanii huyo huyo, baadaye anaweza kukaririwa akilia kuwa wapo taasisi au watu wengine ndio wananufaika zaidi kwa kazi zake za sanaa. Wapo wengine wanaweza kumpuuza msanii huyu na kumkejeli kuwa yeye ni mfujaji na alishalipwa stahiki yake.

Hakika yote mawili yanaweza kuwa majibu sahihi. Hata hivyo ni muhimu tukatafakari tena kwa mfano wa kufungia andiko hili:

Msanii wa singeli ameingia mkataba wa kuandaa tangazo la sabuni kwa malipo ya takribani milioni 3. Naye msanii huyo ametunga wimbo kama tangazo la sabuni hiyo. Wimbo huo hatimaye umekuwa maarufu na kuipaisha sabuni husika. Baada ya miaka miwili, kwa kuwa wimbo huo huo ni mali/ miliki ya kampuni ya sabuni na yupo msanii mwingine wa singeli anayechipukia, naye anachukuliwa kuurudia wimbo huo kwa idhini ya kampuni kwa ajili ya matangazo. Naye analipwa hela, hata hivyo ni kiasi cha laki tano tu, kwa kuwa kwake yeye anahitajika kuingiza sauti tu.

Katika mfano wa namna hii, kampuni husika inaonekana inaweza kupunguza gharama ya matangazo kwa jumla jumla kiasi cha milioni mbili na laki tano, kulinganisha na gharama ya awali. Hapa bado hujapigia faida kampuni itakayoweza kujiingizia kutokana na tangazo hilo kwa awamu zote mbili. Lakini je ikoje hali ya msanii? Msanii wa awali anaikosa milioni 3 nyingineyo (au hata zaidi) naye msanii wa pili anakosa fursa ya kupata zaidi.

Hivyo basi, si dhahiri kwamba katika mazingira kama haya ambapo msanii ataendelea kudhorota kiuchumi? Ni muhimu sana kwa wasanii kuhakikisha kuwa wanajibidiisha kuelewa masuala mbalimbali ya kisheria. Ni muhimu sana kwa wasanii kuhakikisha mnajidhatiti kwa kuwa na uwakilishi madhubuti wa kisheria katika usimamizi wa masuala yenu ya sanaa.

Imeandikwa na Jasper “Kido” Sabuni ambaye ni Wakili, Mshairi na Mtunzi wa kitabu cha mashairi “Love Chronicles”; anayepatikana kupitia barua pepe jasper@springattorneys.co.tz.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts