Mwanza. Mgogoro baina ya wafanyakazi na uongozi wa kampuni ya Sahara Media Group Limited hauoneshi dalili za kuisha hivi karibuni baada ya taarifa kuibuka kwamba kampuni hiyo imewasimamisha kazi wafanyakazi kwa madai kwamba hakutakuwa na uzalishaji wa vipindi kupisha maboresho ya kiufundi.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusiana na jambo hilo, Afisa Rasilimali Watu wa kampuni hiyo Sharbano Abubakar aligoma kuthibitisha au kukanusha ukweli wa taarifa hizo akisema yeye binafsi hahusiki na mambo hayo. Juhudi za kupata majibu kutoka ngazi za juu za kampuni hazikuzaa matunda.
Lakini baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo inayomiliki Star TV, Radio Free Africa (RFA) na Kiss FM wameieleza The Chanzo kwamba kwa mujibu wa tangazo walilopewa ni kwamba hakutakuwa na uzalishaji wa vipindi kuanzia Januari 18, 2023, kupisha maboresho.
Tangazo hilo lilikuja siku chache baada ya wafanyakazi wafanyakazi wa kampuni hiyo kuendesha mgomo wa takriban siku tano, kutoka Januari 2 mpaka Januari 7, 2023, wakishinikiza kulipwa kwa stahiki zao na mwajiri wao huyo.
SOMA ZAIDI: Wafanyakazi Wanaogoma Sahara Media Waeleza Masaibu Yao
Kwa mujibu wa mmoja ya wafanyakazi wa kampuni hiyo aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, mgomo huo ulikoma baada ya wafanyakazi na uongozi wa kampuni kukubaliana kwamba wafanyakazi wote walau walipwe mishahara mitatu ndani ya mwezi huu wa Januari.
Hata hivyo, uongozi wa kampuni uliyakiuka makubaliano hayo kwani mapaka sasa wamelipa mshahara mmoja tu na makubaliano yalikuwa kwamba ifikapo Januari 16 mishahara yote mitatu iwe imelipwa.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa wetu, mara baada ya uongozi kusikia fununu za wafanyakazi kuulizia mustakabali wa mishahara yao ndipo ulipoamua kutoa tangazo kwa waandishi wa Star TV kwamba hakutakuwa na matangazo yoyote yatakayokuwa yanarushwa kutokea ndani zaidi ya yale yanayotengenezwa nje.
“Waliitisha kikao cha dharura kwamba kuanzia sasa vipindi vya Star TV vitakuwa vinazalishiwa nje, yaani vile vipindi vinavyolipiwa pamoja na taarifa ya habari, wakiwataka wafanyakazi wote kubaki nyumbani mpaka pale watakapopatiwa taarifa nyengine,” kilisema chanzo chetu cha habari.
“Mara baada ya taarifa hiyo, wafanyakazi wakaanza kuhoji kuhusu mustakabali wa madeni yao, wakisema wanachotaka wao ni kulipwa madeni yao, na kwamba mambo ya uzalishaji wa vipindi wao hayawahusu,” kiliendelea kueleza chanzo chetu hicho cha habari.
Kufuatia malalamiko hayo kutoka kwa wafanyakazi, uongozi ulibadili msimamo wake na kuwataka waandishi wa habari waje ofisini huku mchakato wa kufanyia maboresho uzalishaji wa vipindi ukiendelea.
“Lakini ni janja janja tu zinazoendelea kwa ajili ya kuwadhulumu waandishi,” kilisema chanzo hicho cha habari. “Kosa la waandishi ni kuulizia madeni yao ya nyuma. Sasa hivi wameamua waje ofisini kukaa tu bila kufanya vipindi.”
Akizungumzia mgogoro huo, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi Tanzania (COTWU) Hamza Juma aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalum kwamba njia inayotumiwa na kampuni ya Sahara Media kumaliza mgogoro na wafanyakazi wake siyo njia sahihi.
“Njia iliyotumika kimsingi siyo sahihi kwa sababu unaposema watu waboreshe vipindi haina haja ya kuvifungia,” alisema. “Ni kama vile uwaambie watu wajenge nyumba mpya halafu ukabomoa ile wanayoishi muda huo, kinachotakiwa ni nyumba mpya ijengwe wahamie halafu ya zamani ibomolewe.”
Hamza alisema kinachowashangaza wafanyakazi ni kuona vipindi vinasitishwa halafu wanapohoji wanaambiwa inabidi uboreshwaji wa vipindi ufanyike.
“Unapoondoa vipindi ina maana waliokuwa wanaviandaa wakifika ofisini wanakaa tu bila kufanya kazi yoyote,” anasema Hamza.
“Maboresho huwa yanafanyika lakini siyo kwa mtindo kama huu,” aliongeza. “Lakini kwa sababu ni mamlaka ya muajiri kaamua kufanya alichokifanya, kwa sababu hajamtimua mtu, basi wafanyakazi wanapaswa kuwa watulivu.”
Rahma Juma Salumu ni mwandishi wa habari kutoka Mwanza, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia barua pepe salumurahma1@gmail.com.