Bahi/Dodoma. Wazazi wenye watoto njiti wilayani hapa wameelezea kufurahishwa na hatua ya Serikali kuanzisha Kitengo cha Watoto Njiti katika Hospitali ya Wilaya ya Bahi, wakisema uwepo wa kitengo hicho umesaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa maisha ya watoto wao.
Kitengo hicho kilichoanzishwa hapo Julai 2022 kinaripotiwa kusaidia watoto njiti angalau 36 tangu kuanzishwa kwake, hali iliyosaidia kuwapunguzia usumbufu wazazi hao ambao hapo zamani walilazimika kupelekwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya huma hiyo.
The Chanzo ilitembelea kitengo hicho hapo Februari 6, 2023, kufahamu maendeleo yake ambapo ilikutana na wazazi kadhaa wa watoto njiti walioelezea ni kwa namna gani uwepo wa kitengo hicho umesaidia kuleta nafuu kubwa kwao.
Grace Iman ni mama wa mtoto mmoja aliyejifungua mtoto wake kabla ya wakati akiwa na kilo moja tu. Kuwepo kwa huduma ya watoto njiti katika Hospitali ya Wilaya ya Bahi imesaidia kuokoa maisha ya mtoto wake.
“Nilijifungua kabla ya wakati katika Kituo cha Afya cha Chipanga,” Grace, 21, aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalum. “Nilitakiwa nimpeleke [mtoto] kwenye huduma nzuri kupata matibabu [nikapewa rufaa kuja hapa] hospitali na sasa hivi anaendelea vizuri.”
Ng’waru Luhende, 39, mama mwenye watoto 10, anasema alijifungua mtoto wake akiwa na kilo moja na baada ya kupelekwa kitengo cha huduma kwa watoto njiti mtoto wake ameongezeka kilo na kufikia kilo 1.6.
“Namshukuru Mungu sasa hivi mtoto wangu anaendelea vizuri,” anasema Ng’waru.
Naye Paulina Eliamini, 19, mama wa mtoto mmoja aliyejifungua katika Kituo cha Afya ya Bahi na kupewa rufaa kujifungulia katika hospitali ya wilaya, anasema alijifungua mtoto akiwa na gramu 800 na sasa ana kilo moja, kitu ambacho anashukuru.
Kupunguza gharama
Mecktilds Limited, Muuguzi Mkuu katika Hospitali ya Wilaya ya Bahi, anakiri uwepo wa kitengo hicho umesaidia kuokoa maisha ya watoto kwa uharaka lakini pia kupunguza gharama ambazo zilikuwa zikitumika kwa rufaa kwenda Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.
“Huduma hii pia imesaidia kupunguza vifo vitokanavyo na watoto wachanga,” Limited aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano naye. “Lakini hata kupunguza gharama kwa familia zenye hawa watoto [kwani] wanachukua muda mrefu kuwa hospitali. Hivyo, tumepunguza gharama kwa familia kwa ajili ya kutoa huduma za watoto hawa.”
SOMA ZAIDI: Fanya Hivi Mtoto Wako Akipata Tumbo la Chango
Mtaalamu huyo alieleza ni kwa nini ni muhimu kwa mtoto njiti kupatiwa huduma kwa haraka, akisema watoto hao wako hatarini kupoteza joto kwa haraka, kupata magonjwa haraka, wana changamoto za kushuka kwa sukari kwa haraka, na kwamba wakipata changamoto hizi ni rahisi kupoteza maisha.
Huduma kitengoni hapo hutolewa bure ukiacha gharama za huduma ambazo mama anazitegemea kama vile chakula ambazo hubebwa na familia.
Limited alielezea sababu kadhaa za mtoto kuzaliwa njiti, zikiwemo sababu zinazohusisha magonjwa ambayo mama mjamzito anaweza kuwa nayo kama vile presha, upungufu wa damu, uvimbe tumboni.
“Mtoto ili akue vizuri ni lazima mfuko wa uzazi uwe unatosheleza kubeba mtoto,” alieleza mtaalamu huyo. “Mama anapokuwa tayari ana uvimbe nafasi inakuwa ndogo kwa mtoto, hali inayopeleekea mtoto kuzaliwa kabla ya wakati.”
Kuvuta sigara, unywaji wa pombe na lishe duni ni baadhi ya sababu ambazo Limited ameziita za kimazingira zinazoweza kupelekea mtoto kuzaliwa njiti pia.
Maradhi kama malaria, kaswende na magonjwa mengine pia yanaweza kupelekea mtoto kuzaliwa kabla ya wakati.
SOMA ZAIDI: Zaidi ya Watoto 1,000 Dodoma Wana Uzito wa Ujifunzaji Shuleni
“Watoto hawa wanahitaji kupimwa mara kwa mara, tumeona ni rahisi sana kupoteza joto wakiwa kwenye mazingira ya kawaida,” anasema Limited.
“Ni rahisi sana kupoteza sukari [kwa] kushuka,” anaongeza. “Kwa hiyo, wanahitaji wapimwe mara kwa mara. Wakipoteza joto ni rahisi sana kupata shida katika upumuaji, wanabadilika haraka ukilinganisha na watoto wengine.”
Wito kwa Serikali
Limited anadhani Serikali inahitaji kuwekeza zaidi, hususan kwenye kuongeza vifaa tiba, ili kuwasaidia watoto njiti nchini kupata huduma bora.
“Tunahitaji kuwekeza zaidi kwa ajili ya hawa watoto njiti,” Limited anashauri.
“Hapo mwanzo ilikuwa ni changamoto kuwaokoa watoto hawa. Kupitia maboresho yaliyofanyika tumeokoa watoto wengi,” aliongeza mtaalam huyo.
“Hawa watoto wanahitaji vifaa kuwasaidia katika matibabu.”
Nchini Tanzania, takwimu zinaonesha kwamba asilimia 17 ya watoto huzaliwa kabla ya muda wa mimba kukomaa.
Jackiline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anayepatikana Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.