Dodoma. Wakulima wa korosho mkoani Lindi na wale wa pamba mkoani Simiyu wameelezea malalamiko yao juu ya mfumo wa stakabadhi ghalani wakizitaka mamlaka husika kufanyia kazi malamiko hayo.
Wakati wakulima wa korosho wameulalamikia mfumo huo kwa kuwacheleweshea malipo yao, wenzao wanaolima pamba mkoani Simiyu wamelalamikia kutokufikiwa na mfumo huo na hivyo kuziomba mamlaka zinazohusika kutatua changamoto hizo.
Wakulima hao walielezea malalamiko hayo wakati wa mahojiano na The Chanzo yaliyolenga kupata tathmini yao ya utaratibu huo unaowawezesha wakulima, pamoja na mambo mengine, kukusanya mazao yao katika Ghala Kuu ili kuuza kwa pamoja kupitia minada ya pamoja kwa lengo la kupata bei nzuri.
Hatua hiyo ilitokana na hatua ya Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala kutoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu yake jijini Dodoma mnamo Februari 15, 2023, ambapo, pamoja na mambo mengine, ilibainisha kwamba baada ya kuanzishwa kwa mfumo huo, uzalishaji wa mazao umeongezeka kwa takribani asilimia 12 kwa mwaka.
Kwenye taarifa yake hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala Asangye Bangu alisema kwamba mfumo huo pia umepelekea kuongezeka kwa mapato ya Serikali kwenye makusanyo ya fedha zitokanazo na tozo zinazotozwa kwenye mazao yanayofanyiwa biashara.
“Tumeona ongezeko mpaka la asimia 200 kutoka kwenye makusanyo yaliyokuwa yakitumika halmashauri nje ya mfumo na baada ya kuingia kwenye mfumo,” alisema Bangu. “Hii ni kwa nini? Ni kwa sababu mazao yakipitishwa kwenye mfumo yanakusanywa mahali pamoja, yanauzwa katika utaratibu unaojulikana na unaokubalika.”
“[Mfumo huu] umekuwa ni kichocheo cha ubora wa mazao,” aliongeza Bangu. “Mkulima anapopeleka mazao ambayo ni mabovu hayataweza kupokelewa kwenye ghala. Maana yake hayataweza kuingia kwenye biashara na maana yake hutaweza kuuza.”
Ucheleweshaji wa malipo
Lakini wakizungumza na The Chanzo, baadhi ya wakulima wameukosoa utaratibu huo, hususan linapokuja suala ucheleweshaji wa malipo.
Swalehe Mtwawite ni mkulima wa korosho kutoka kijiji cha Namtubwa, wilayani Liwale, mkoani Lindi, ambaye alidai kutopata malipo kwa wakati, hali inayowalazimisha kuuza kwa mfumo usiyo rasmi ili waweze kujikimu kimaisha.
SOMA ZAIDI: Wakulima Wadogo 852 Mbarali Waiburuza Serikali Mahakamani Wakitetea Ardhi Yao
“Yaani hilo la ucheleweshaji wa malipo ni tatizo, mpaka mkulima anaichukua fedha inachukua zaidi ya mwezi mmoja,” alisema Mtwawite. “Kwa mfano, mimi nikipeleka korosho leo ghalani, korosho zikipimwa siyo siku hiyo hiyo itasafirishwa, hapana. Inatakiwa ibaki pale mpaka zitimie tani kadhaa ambazo zitakuwa zinasafirishwa kwa pamoja.”
Naye Mohamed Issa, mkulima wa korosho kutoka kijiji cha Namihu wilayani humo alisema kwamba msimu wa korosho unapokaribia kufungwa wanaambiwa korosho zitauzwa kwa bei ya daraja la pili bila ya wao kufahamu bei halisi ya kila kilo moja ya korosho ambayo wameuza.
“Tunaingiziwa hela tu kwenye akaunti zetu, utakuta Sh1,300 kwa kilo moja ya korosho daraja la pili,” anaeleza mkulima huyo. “Halafu wanasema hizo hazifai. Sasa wanapeleka wapi kama hazifai, yaani kitu kibovu unakinunuaje?”
Kwa upande wao, wakulima wa pamba mkoani Simiyu wamelalamikia kutokufikiwa na mfumo wa stakabadhi ghalani, wakiiomba Serikali iwafikishie mfumo huo ili na wao waweze kunufaika na faida zake.
“Mfumo huu kweli bado huku haujafika,” Nkuba Mjika, mkulima wa pamba kutoka mkoani Simiyu, aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalum. “Ila kwa muda wa nyuma ulikuwa unafanyiwa majaribio kwa baadhi ya vijiji, kwa maana ya kwamba kweli walikuwa wanaiweka pamba ghalani baada ya muda fulani bei ikiwa nzuri ndiyo inauzwa.”
SOMA ZAIDI: Tozo, Pembejeo Zinavyowatesa Wakulima wa Korosho Mtwara
Mkulima mwengine, Malisha Mhangilwa, alisema: “Kwanza kwa sisi huku tuna hamu nao sana huo mfumo kwa kuwa bado haujatufikia, tunashindwa tufanyaje. Mpaka Serikali kufanya hivyo [ina maana] manafuaa [ya mfumo] yatakuwepo.”
Changamoto za bei
Kwenye taarifa yake hapo Februari 15, Bangu alikiri kuwepo kwa changamoto za bei kwenye zao la korosho, hali aliyoihusisha na ongezeko la wakulima wa zao hilo la biashara nchini, akisema wao kama mamlaka husika wanatafuta namna za kibunifu za kukabiliana na changamoto hiyo.
Kuhusu wakulima wa pamba kutokufikiwa na mfumo huo, Bangu alikiri kwamba hilo ni kweli lakini kwenye msimu unaoendelea wa kilimo wakulima hao watafikiwa na mfumo huo.
Tangu kuanza kutumika kwa Sheria ya Stakabadhi za Ghala, mfumo umetekelezwa katika mazao 11 yaliyoleta makusanyo zaidi ya kilogramu bilioni 2.3 hadi kufikia robo ya kwanza ya mwaka 2021/22, kwa mujibu wa Bangu.
Mazao hayo ni Alizeti, Choroko, Dengu, Kahawa, Kakao, Korosho, Mahindi, Mbaazi, Mpunga, Soya na Ufuta.
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.