Mwanza. Tabia ya kutokujali miongoni mwa wakazi wa jiji hili imetajwa kama kichocheo kikubwa cha kukithiri kwa utupaji holela wa nepi na taulo za kike, hali ambayo wataalamu wametahadharisha inatishia afya za watu lakini pia usalama wa vyanzo vya maji na usafi wa mazingira kwa ujumla.
Tathmini fupi iliyofanywa na The Chanzo katika mitaa mbalimbali ya jiji la Mwanza iligundua kwamba utupaji holela wa nepi na taulo za kike ni tatizo kubwa katika jiji hili la pili kwa ukubwa nchini Tanzania, huku aina hizo za taka zikionekana zikizagaa kwenye maeneo mbalimbali.
Moja kati ya maeneo ambayo tatizo hili linaripotiwa kwa ukubwa zaidi ni kata ya Kirumba katika wilaya ya Ilemela ambapo The Chanzo ilishuhudia nepi na taulo za kike zikiwa zimetapakaa katika maeneo mbalimbali, hali ambayo imekuwa ikiwakera wakazi wengi wa eneo hilo.
Moja kati ya wananchi hawa ni Ramadhani Shabani Magege, Mjumbe wa Serikali ya Mtaa na Kaimu Mwenyekiti wa Kirumba, ambaye alisema tatizo hilo limekuwa ni la muda mrefu, likileta athari kadhaa, ikiwemo kuziba kwa mabomba ya maji, hali inayoleta usumbufu kwa wananchi.
“Tatizo hili linatokea mara nyingi katika chemba zilizopo maeneo ya nyumba za kulala wageni, wanatupa uchafu huo sana,” Magege alisema. “Tuna chemba korofi kama tatu zinaziba kila siku. Kuna chemba moja ipo hapo Mwembe Sangara ambayo ni sugu kabisa. Chemba hiyo mara nyingi sana huwa inaziba. Nyingine ipo mtaa wa Mbugani, Sokoni na mtaa wa Vijana.”
SOMA ZAIDI: NEMC Kufanyia Kazi Madai ya Uharibifu wa Mazingira Unaofanywa na Kiwanda cha Wachina
Wananchi mbalimbali wa kata ya Kirumba wamelalamikia utupaji huo holela wa nepi na taulo za kike, wengi wao wakisema hivyo si vitu vya kutupwa kiholela bali kwa umakini ili kuepusha kuwaudhi wengine.
Mkazi wa kata hiyo Jamila Masu aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano kwamba haridhishwi kuona taka hizo zikitupwa kiholela kwani ni uchafu unaokera wengine na pia zina madhara ya kimazingira.
“Mitaro inajaa huo uchafu, sana sana,” Masu, 33, alisema. “Nepi za watoto imekuwa ni kitu cha kawaida tu kuzikuta kwenye mitaro.”
Kitogo Laurence ni Afisa Mazingira kutoka Shirika la Utunzaji wa Mazingira na Maendeleo ya Kiuchumi (EMEDO) lenye makao yake makuu jijini Mwanza ambaye alisema kwamba utupaji holela wa nepi na taulo za kike ni hatari kwa mazingira kwani taka hizo haziozi.
SOMA ZAIDI: ‘Usalama wa Maji ni Usalama wa Nchi’
“Mvua zikinyesha, [hizo taka] zinabebwa, zinapelekwa ziwani [ambako] zinaenda kuharibu mazalia ya viumbe hai na kuua mfumo mzima wa ikolojia ya Ziwa [Victoria],” alisema kwenye mahojiano na The Chanzo. “Serikali wana wajibu wa kuhakikisha wanaweka mazingira sahihi kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi [juu ya] utunzaji wa taka hizo.”
Pascal Malimani, Kaimu Afisa Afya Mkoa wa Mwanza, amesema ipo haja ya kudhibiti utupaji holela wa nepi na taulo za kike kwani kushindwa kufanya hivyo kunatishia afya za wakazi wa eneo husika.
Malimani alisema kwamba tafsiri kwamba kinyesi cha mtoto hakina madhara ni tafsiri potofu, akisisitiza kwamba jamii inapaswa kuelewa kwamba kinyesi, au taka inayomtoka mtoto, pia inaweza kusababisha madhara.
“Kama mtoto alikuwa na magonjwa kama kichocho au kipindupindu, au vimelea vyovyote vya magonjwa ya kuhara, basi watumiaji wa maji yale watadhurika,” alisema mtaalamu huyo, akizungumzia maji yaliyoathiriwa na utupaji wa nepi.
Jarome Ansgary Kayombo, Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Kanda ya Ziwa, amesema sehemu ya tatizo hilo inachangiwa na uwekezaji mdogo uliofanywa na jiji katika ukusanyaji taka.
SOMA ZAIDI: Hali ya Uchafu Mbeya Yazisukuma Mamlaka Kuibuka na Mikakati Mipya
“Kwa mfano, tukisema tuzichome, hatuna mashine za kuchomea za kutosha,” alisema Kayombo. “Lakini pia hatuna teknolojia ya kuweza kuharibu hizi taka ili zisizidi kurundikana.”
“Ukijiuliza kama halmashauri zetu zina uwezo wa kuwa na gari zaidi ya tatu kwa ajili ya ukusanyaji taka, kwa maana apitie vitu vinavyooza, ambavyo haviozi, apitie taka hatarishi, unakuta uwezo wa halmashauri zetu ni changamoto, gari ni chache,” aliongeza Kayombo kwenye mahojiano yake na The Chanzo.
Kayombo pia alisema mbali na uwekezaji huo hafifu, bado tatizo linachochewa na Watanzania wengi kutokuwa na utamaduni wa kuzichambua taka katika makundi mbalimbali kwa ajili ya utunzaji mzuri, akitoa wito kwa wananchi kujenga utamaduni huo.
“Kwa nchi yetu hatuna ule utamaduni wa kutenga taka, kuna taka zinazooza zikae tofauti, kuna zisizooza zikae pembeni na kuna taka hatarishi ambazo zinaweza kuleta madhara zikae sehemu moja,” alisema. “Nadhani ni utamaduni ambao inabidi tujijengee ili kusaidia utunzaji wa mazingira yetu.”
Rahma Salumu ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Mwanza. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe: salumurahma1@gmail.com.