The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ukata Unavyokwamisha Matumizi ya Nishati Mbadala Dodoma

Wadau wataka gharama za nishati mbadala zipunguzwe ili Watanzania wengi waweze kuzimudu.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Margareth Petro ni mama wa watoto watano anayeishi wilayani Bahi mkoani Dodoma ambaye amekuwa akitumia nishati ya kuni kupikia tangu utoto wake. Haikupita siku bila kutumia nishati hii licha ya kufahamu athari zake.

Margareth, mjane, anayetegemea kilimo na biashara ndogo ndogo kuendesha maisha yake, anasema ni vigumu kwa yeye kumudu gharama za kununua gesi, hali inayomfanya kuendelea kutumia kuni mpaka sasa.

Margareth, 42, hata hivyo, anawakilisha kundi kubwa la wanawake wengi vijijini ambao wanategemea kuni na mkaa kupikia.

Matumizi haya makubwa ya kuni na mkaa yamezidi kuteketeza misitu nchini, hali inayochochea kwa kasi athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi ambayo athari zake zinakuja tena kuwaathiri wakulima na wafugaji.

Kwa sasa katika wilaya anayokaa Margareth, kuna upungufu wa maeneo ya kukatia kuni. Maeneo mengi yanamilikiwa na watu binafsi, hivyo kuwalazimu watembee umbali mrefu kutafuta kuni porini wanakokutana na wadudu hatari, wakiwemo nyoka.

“Nakumbuka kuna kipindi niliwahi kujikata na shoka,” anaeleza Margareth kwenye mahojiano na The Chanzo. “Nilivyokata kuni kipande cha mti kiliruka kwa nguvu ikabidi niachie shoka ambalo nilikuwa nakatia kuni likaja kunikata pajani.”

“Ukienda kukata kuni  kwenye eneo ambalo siyo lako yule mtu akikukuta, mwenye eneo, ni shida kubwa,” aliongeza mama huyo. “Anaweza akakunyang’anya kuni. Tunaomba Serikali ipunguze bei ya gesi ili na sisi masikini tupate na tuweze kuzitumia.”

Si wanawake tu walioathirika na uhaba wa nishati safi. Bahati Ernest, 40, baba wa watoto watatu anasema amekuwa akikata kuni tangu utoto wake, hali inayomfanyia apitie madhila kama ambayo hupitia wanawake wanaposaka kuni.

“Tunaomba watutengenezee gesi kwa watu wa hali ya chini,” anashauri Bahati akieleza kuwa naye anapenda kutumia nishati safi. “Tunaweza tukajitahidi na sisi tukanunua.” 

SOMA ZAIDI: Gharama Ya Gesi Sababu Matumizi Ya Kuni, Mkaa Kushamiri Dar es Salaam

Wakati usio wa kilimo, Margareth huwa anafanya biashara ya kuuza vikapu ambapo kwa siku hupata faida ya Sh2,000. Jirani yake, Esther Paulo, 49, mama wa watoto sita, huuza kuni kwa siku na kupata Sh2,000.

“Unajua kuni tunakata sisi wenyewe, tunabeba kutoka porini, tunakuja, tunaweka, ndiyo tunapika,” anasema Esther. “Maisha yanaruhusu niendelee kupikia kuni hizo. Labda nipate ajira zaidi iniongezee kipato ili ninue gesi.”

Kwa aina ya shughuli za kiuchumi wanazozifanya akina mama hawa, hapana shaka wakifanya biashara zao hizo kila siku huenda wakaingiza Sh60,000 kwa mwezi, sawa na Sh720,000 kwa mwaka.

Kiwango hicho cha fedha wanachopata kutokana na kazi zao nje ya kilimo, ambacho ni cha msimu, ni robo tu ya wastani wa pato la mtu la Sh2,701,039 kwa mwaka nchini kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Fedha na Mipango mwaka 2021.

Hali hiyo ya kiuchumi inafanya matumizi ya gesi, au umeme, kupikia kuwa ni anasa. 

Kwa mfano, gesi ya kupikia wilayani Bahi kama vile Taifa Gas kilo 15 inauzwa kwa Sh65,000 mpaka Sh70,000 na mtungi mdogo kwa Sh45,000 wa kilo sita . Kwa upande wa Oryx Gas, mtungi wa kilo 15 unauzwa kwa Sh98,000 mdogo wa kilo sita ukiuzwa kwa Sh50,000.

Na gesi ya O Gas mtungi mkubwa wa kilo 15 unauzwa kwa Sh80,000, huku mtungi mdogo wa kilo sita  ukiuzwa kwa Sh48,000.

Uelewa bado mdogo

Hata hivyo, si watu wote Tanzania wanaelewa umuhimu wa matumizi ya nishati mbadala ya kupikia na wanaweza kumudu kununua nishati hiyo ambayo inajumuisha gesi ya kupikia, umeme, au bayogesi kutokana na ukata.

Anna Daudi, 100, mama wa watoto saba wilayani Bahi ni miongoni mwa watu wasiyojua umuhimu wa matumizi gesi wala na athari za kuni na mkaa.

Alisema toka enzi wamekuwa wakitumia kuni kupikia na hakuna athari zozote ambazo amewahi kuziona, jambo linaloonesha kuwa elimu zaidi inahitajika kuhusu athari za nishati zisizo rafiki kupikia.

“Nyinyi mnasema kwamba kuni  zina athari, mbona toka zamani vipofu hawakuwa wengi?” anahoji Anna. “Sasa hivi tunaona vipofu wengi na ni watoto wadogo wanapofuka, kwa ajili ya nini?”

Kwa mujibu wa Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi kwa mwaka 2017-2018 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Wizara ya Fedha na Mipango, matumizi ya kuni ni makubwa mkoani Dodoma kwa asilimia 62.9, huku matumizi ya mkaa yakiwa ni asilimia 28.4 na matumizi ya gesi yakiwa ni asilimia 1.1 tu.

Hii inamaanisha kuwa kaya 63 kati ya 100 mkoani Dodoma zinatumia kuni, juu kidogo ya wastani wa kitaifa wa kaya 61, huku kaya 29 kati ya 10 zikitumia mkaa kwa ajili ya kupikia. Ni kaya moja tu kati ya 100 zinatumia gesi kupikia, jambo linalotishia mustakabali wa kukabiliana na uchafuzi wa mazingira nchini.

Utafiti huo unaonesha kuwa chanzo kikuu cha nishati ya kupikia Tanzania Bara ni kuni kwa asilimia 60.9, ikifuatiwa na mkaa asilimia 28.8, gesi ya viwandani asilimia 3.2, umeme  asilimia 2.1, mafuta ya taa asilimia 1.3, na sola asilimia 1.1.

Matumizi ya kuni yanatumika zaidi maeneo ya vijijini kwa asilimia 84.8 kuliko maeneo ya mijini kwa asilimia 17.4, huku mkaa ukipatikana zaidi katika maeneo ya mijini kwa asilimia 60.5 kuliko vijijini kwa asilimia 11.5.

Athari za matumizi ya kuni, mkaa

Wataalam wa afya na mazingira wanabainisha kwamba watu wanaotumia nishati ya kuni na mkaa kupikia wako hatarini kuathiri mfumo wao wa upumuaji kama hatua za haraka hazitachukuliwa.

“Kwa sababu mtu anayepika jikoni ule moshi mwingine unakuwa na kemikali za sumu,” anaeleza Thomas Chali, mtaalamu wa mazingira, wakati wa mahojiano haya. “Unachokiingiza kwenye mfumo wako wa upumuaji kinaingia hadi kwenye mwili wako.” 

SOMA ZAIDI: Daktari Bingwa Muhimbili Awasihi Watu Kuacha Kutumia Kuni, Mkaa Kupikia

Mtaalamu huyo alisema ili nishati iweze kutumika ni lazima iwe inapatikanika kwa urahisi na kununulika, jambo ambalo kwa wananchi wenye kipato cha chini, kama wanaoishi Bahi, ni ngumu kuhimili.

“Ni muhimu kubuni nishati ambayo inaweza kupatikana kwa wingi, inaweza kuwafikia watu karibu,” anasema Chali kwenye mahojiano yake na The Chanzo

“Sawa tuna gesi inauzwa kwenye mitungi, inaweza ikawa inapatikana, lakini ikawa siyo nafuu kwa mtu kununua,” anaongeza. “Kwa sababu Watanzania walio wengi mitaani siyo watu wenye pesa nyingi za kuwekeza kwenye ununuzi wa gesi.”

“Inapaswa kuwepo na namna bora ya kumuwezesha mwananchi kuweza kumudu gesi.”

Kwa mujibu wa WHO, magonjwa yanayosababishwa na moshi husababisha vifo vya watu milioni 4.3 kila mwaka duniani, vikiupiku ugonjwa wa malaria na kifua kikuu, huku takribani watu bilioni tatu katika nchi zinazoendelea wakitegemea kuni, au mkaa, kwa ajili ya kupikia.

Si athari za kiafya pekee zinazotokana na matumizi ya kuni na mkaa. Athari nyingine ni pamoja na uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti.

Afisa Mazingira Wilaya ya Bahi Wiliam Mpangala alisema ukataji wa miti unapofanyika unasababisha jangwa.

“Tunajua kuwa mvua zinatokana na uwepo wa miti,” anasema Mpangala akiongea na The Chanzo. “Kwa hiyo, ukataji wa miti kwa ajili ya kupata nishati ya mkaa na kuni vinaathiri sana ulimwengu. Lakini pia vinasababisha uharibifu wa anga la juu. Na pia unapoondoa uoto wa asili unaleta mmonyoko wa ardhi.”

SOMA ZAIDI: ‘Usalama wa Maji ni Usalama wa Nchi’

Mpangala anasema kutokuwepo kwa nishati mbadala za kutosha inachangia jamii ya Bahi kuendelea kutegemea nishati ya kuni na mkaa kupikia.

“Kwa wilaya ya Bahi, tuna shida hiyo ya kutegemea nishati ya kuni na mkaa kwa sababu bado hatuna nishati mbadala za kutosha kama gesi,  solar, makaa ya mawe na mkaa mbadala,” anasema Mpangala.

Kukabiliana na hili, Mpangala anasema wanahamasisha vikundi vya kijamii vya vijana kujifunza teknolojia ya utengenezaji wa nishati ya mkaa mbadala, akisema: “Tunawahamasisha ili waweze kupata mikopo kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii waweze kuwezeshwa na kuweza kutengeneza mikaa mbadala.”

Aliiomba Serikali iweke ruzuku kwenye gesi iweze kupunguza gharama za manunuzi ya nishati hiyo ili kila mtu aweze kumudu kuinunua, huku akitaka gesi iwekwe kuanzia mtungi wa kilo tatu mpaka kilo tano, hali ambayo anaamini itapunguza sana kiwango cha matumizi ya kutegemea matumizi ya kuni na mkaa.

Serikali yatoa kauli

Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Mazingira, kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk Thomas Bwana anadhani wakati tafakuri za namna ya kupunguza gharama za nishati mbadala zikiendelea, ni muhimu kwa wananchi kuboresha mazingira yao ya kupikia ili kuepuka athari zitokanazo na nishati chafu.

“Watu wengine wanavyopika vijijini wawe na sehemu ambayo iko wazi, moshi unaweza ukatembea,” Dk Bwana aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano naye. “Vijijini kwetu [unakuta] mafiga yapo ndani ya nyumba. Kwa hiyo, hali hii tunajaribu kuipunguza.”

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) NEMC Dk Samuel Gwamaka aliambia The Chanzo kwamba mikakati waliyonayo kama baraza ni kuelimisha wananchi kuachana na ukataji wa miti hovyo ili waweze kutumia njia mbadala.

Dk Gwamaka alisema pia kwamba wakati huo huo wanaendelea kuhakikisha kwamba nishati mbadala na majiko ya gesi yanakuwa rafiki na umeme  unapatikana kwa karibu  kwenye maeneo ya wananchi.

“Serikali imefanya juhudi kuhakikisha kila mahali mtu anayetaka kuwekewa umeme umeme unakuwa hauko mbali kutoka sehemu aliyoko,” Dk Gwamaka aliiambia The Chanzo

“Hiyo ni moja ya juhudi za kujaribu kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa kwa upande wa jamii, hususan maeneo ya vijiji,” aliongeza. 

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari mkoani Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *