Mfuko wa Utafiti wa UVIKO-19 wa Amne Salim: Watafiti Wamebaini Nini?

Baadhi ya watafiti walionufaika na ufadhili huo waeleza matokeo ya tafiti zao.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Jumla ya tafiti nane zimeweza kuzalishwa na watafiti mbalimbali kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) kufuatia ufadhili uliotolewa na familia ya aliyekuwa Waziri Mkuu Salim Ahmed Salim uliolenga kuenzi kifo cha mke wake, Amne Salim, aliyefariki kwa ugonjwa wa UVIKO-19 hapo Oktoba 20, 2020.

Ukipewa jina la Mfuko wa Utafiti wa UVIKO-19 wa Amne Salim, familia ya Dk Salim ilitoa Shilingi milioni 100 kwa ajili ya kufadhili tafiti mbalimbali juu ya janga la UVIKO-19, kwa lengo la kuwawezesha watunga sera na wafanya maamuzi kulifahamu janga hilo vizuri na kama Tanzania inaweza kutumia uzoefu wa UVIKO-19 kukabiliana na majanga mengine.

The Chanzo imezungumza na watafiti watatu walionufaika na ufadhili huo kwa lengo la kufahamu tafiti zao zilihusu nini na matokeo gani waliweza kupata, ikiwa ni sehemu ya kueneza matokeo hayo kwa jamii.

Mmoja kati ya watafiti hawa ni Profesa Karim Manji, daktari bingwa wa watoto kutoka MUHAS, ambaye utafiti wake ulihusu UVIKO-19 kwa akina mama waliokuwa katika umri wa uzazi, kutoka visiwa vya Unguja na Pemba. Hapa Profesa Manji anaeleza kwa kina:

 

UVIKO-19 na akina mama

“Kwa hiyo, utafiti huu uliangalia hizo vichembe ambavyo vinatokana na kinga baada ya kupata ugonjwa wa UVIKO-19. Katika tafiti yangu hapo Unguja, tulipima akina mama 500 katika wilaya na kata zote za Unguja. Tulitumia kata 25. Kila kata ilitoa akina mama 20 waliokuja kupima afya zao kwa kawaida. 

“Na tukawapima kitu kinachoitwa IGG na IGM, Immunoglobulin G na Immunoglobulin M. Immunoglobulin G inaonekana kwenye damu pale ambapo mtu amewahi kupata ugonjwa huo, na IGM ni pale ambapo ugonjwa huo ni wa sasa, yaani ameupata hivi karibuni, ni imara. 

SOMA ZAIDI: Fahamu Kuhusu Ugonjwa wa Homa ya Virusi vya Marburg

“Katika utafiti wetu, tuliona kwamba asilimia 88 ya akina mama wa Unguja na asilimia 92 ya akina mama kutoka Pemba walikuwa tayari wana IGG. Hiyo inaashiria kwamba tayari walishapata ambukizo hilo katika miaka hiyo ya nyuma toka [UVIKO-19] imeanza. Ila hatuna uhakika kama ilikuwa hata kabla ya hiyo mwaka 2020 [UVIKO-19 iliporipotiwa].

“Pamoja na hayo, IGM, ambayo ni ambukizo la hivi karibuni, ilionekana kwa asilimia 1.79, yaani takriban asilimia mbili. Hiyo inaonesha kwamba UVIKO-19 bado ambukizo linaendelea kuwepo.

“Kwa hiyo, tulifikiri tuone pia kuhusu chanjo. Tuliona katika utafiti wetu kutoka hawa akina mama 100 wa Unguja na 100 wa Pemba, asilimia 30 tu ndiyo waliopata chanjo hiyo [ya UVIKO-19]. 

“Kwa hiyo, utafiti huu umeonesha kwamba chanjo bado tuko mbali katika kufanyika Unguja na Pemba. Na sababu kubwa ya kutokuchanja ilikuwa siyo kwamba wao hawataki au vipi. Tatizo ilikuwa ni upotoshaji, yaani taarifa zilizowafikiwa kutoka vyombo tofauti na kutoka kwenye mitandao ya kijamii, inaonekana kwamba wametaarifiwa vingine na ile iliyokuwa ya kisayansi.

“Na hivyo, Serikali inabidi ifanye mikakati maalum, ya makusudi, ya kuweza kuhamasisha watu, kwa kutumia vyombo vya habari, na vyanzo vyote vingine, ambazo zitaweza kuwahamasisha watu wapate chanjo.”

SOMA ZAIDI: Sababu Zatajwa Dodoma Kuongoza Ukamilishaji Chanjo ya UVIKO-19

Upatikanaji taarifa changamoto

Mtafiti mwengine aliyenufaika na ufadhili huo ni Godwin Pancras, mhadhiri kutoka MUHAS, ambaye utafiti wake ulikuwa umejikita kwenye masuala ya taarifa, au upatikanaji wa taarifa, katika maeneo ya vijijini kuhusu chanjo ya UVIKO-19.

Pancras na wenzake walienda mkoa wa Geita kwa ajili ya utafiti wao ambapo, pamoja na mambo mengine, waligundua namna ilivyokuwa changamoto kwa jamii za vijijini kupata taarifa sahihi kuhusiana na UVIKO-19. Hapa Pancras anaeleza kwa undani:

“Kwa hiyo, katika kipengele hicho hicho cha kukubalika kwa taarifa, tukagundua kwamba namna taarifa, au kampeni ilivyoendeshwa, ya kuhamasisha watu kuchanja UVIKO-19, ilikuwa na hayo mapungufu makubwa matatu: la kwanza, ni kupatikana kwa hiyo taarifa, [ilikuwa] ni changamoto. 

“Kupatikana hapo tunamaanisha vyombo mbalimbali vilivyokuwa vinatumika kwenye kuhamasisha watu. Kwa Tanzania hapa, kampeni zilikuwa zinasikika kwenye maredio makubwa ambayo tunachukulia kwamba yanasikika Tanzania nzima. 

SOMA ZAIDI: Trilioni 3.6 Kugharamia Mpango wa Serikali Kukabiliana na Madhara ya UVIKO-19

“Lakini watu wa vijijini wana vyombo vyao vya kupata habari, kwa mfano, kwa redio tunasema zile local radio stations. Watu ambao wanaongea lugha yao. Watu ambao wanaishi maisha yao.

“Kwa hiyo, kwa kifupi, [tuligundua] kwamba hamna mtu ambaye anakataa kuchanja, sema ni yale maswali magumu waliyonayo [kuhusu chanjo], taarifa, au zile kampeni zilizokuwa zinaendeshwa, hazikuweza kujibu hayo maswali magumu.

“Kwa hiyo, tukashauri kwamba ili kukabiliana na upatikanaji wa taarifa [na] kukubalika, ni kwamba Serikali kwanza, au wadau, walitakiwa, ile taarifa ambayo inawahamasisha watu itoke kwa watu. Yaani, tunasema iendeshwe katika ngazi ya jamii.”

UVIKO-19 na tiba asili

Mtafiti mwengine aliyenufaika na ufadhili huo ni Dk Mourice Mbunde, mhadhiri kutoka MUHAS, ambaye utafiti wake ulijikita kwenye tiba asili, huku yeye na wenzake wakiangalia namna mbalimbali za asili ambazo wananchi walizitumia kukabiliana na UVIKO-19.

Dk Mbunde na wenzake walifanya utafiti wao huo kwenye mikoa miwili, Dar es Salaam, ambapo walienda katika wilaya za Ubongo pamoja na Ilala, na Kanda ya Ziwa, mkoa wa Mwanza, katika wilaya ya Nyamagana pamoja na Magu.

Kwenye utafiti wao huo, Dk Mbunde na wenzake waligundua kwamba matamko yaliyokuwa yanatolewa na viongozi wakuu wa Serikali kuhusu matumizi ya tiba asili yaliwashawishi wananchi wengi kutumia njia hiyo kukabiliana na UVIKO-19. Hapa, Dk Mbunde anaelezea kwa kina:

SOMA ZAIDI: Afya Moja Ni Nini Na Kwa Nini Ujali Kuhusu Ufanisi Wake?

“Na katika hayo, tukaja tukagundua kwamba jamii, sehemu kubwa ya jamii, ilikuwa inatumia vitu kwa kuchanganya. Kwa hiyo, wanatumia zaidi ya njia moja kukabiliana na zile dalili [za UVIKO-19]. Kwa hiyo, anaweza akaanza nyumbani akajifukiza, akamaliza akanywa, akimaliza anaenda kununua ‘antibiotics’ aliyosikia. Kwa hiyo, njia zote anatumia.

“Tulibaini kwamba jamii ilipata matokeo chanya, sehemu kubwa ya jamii ilipata matokeo chanya kwenye vile vitu walivyovitumia. Na katika hilo linadhihirika kwa sababu wengine walisema labda anapata shida kabisa kupumua lakini baada ya kujifukiza akajiona amepata nafuu ya haraka.

“Upande wa matokeo hasi hatukupata sana japo kilichoibuka ni hofu na mashaka ya usalama wa hiyo mifumo, au hizo njia, walizotumia. Kwa maana kwamba sehemu kubwa ya jamii wanasema kwamba hawakuwa na uhakika wa usalama [wa] kile walichokuwa wanakitumia kwa sababu kilikuwa hakijapitishwa na mamlaka yoyote.

“Ni muhimu sana [kwa] jamii kupewa taarifa sahihi juu ya aina za tiba zilizofanyiwa utafiti ambazo zinaweza kuwa na faida kwenye miili lakini pia zinazoweza kuleta ufanisi na usalama kwenye miili ya [watu]. 

“Na jambo jengine ambalo tunashauri ni kwamba [ni] muhimu kuwekeza sasa kwenye hizi tiba asili ambazo zilionesha kusaidia kwenye kipindi cha kukabiliana na UVIKO-19 ili kubaini sasa kama je, zilileta ufanisi halisi pamoja na kuwa na usalama?”

Wazawa wafadhili tafiti

Akizungumza na The Chanzo ofisini kwake kuhusiana na umuhimu wa watu binafsi kufadhili tafiti, Naibu Makamo Mkuu wa Chuo cha MUHAS Profesa Bruno Sunguya alisema ni muhimu kwa wazawa kufadhili tafiti, akibainisha kwamba utegemezi wa wafadhili wa nje huicheleweshea Tanzania maendeleo.

“Tumezoea – miaka mingi – tumezoea kwamba wafadhili wa tafiti, wafadhili wa maendeleo, basi wamekuwa ni ndugu zetu ambao ni washirika wa kimaendeleo ambao ni kutoka nje ya nchi,” alisema Profesa Sunguya kwenye mahojiano hayo. 

SOMA ZAIDI: Kutibu Wanyama Wetu Ni Kulinda Afya, Ustawi Wetu Kama Binadamu

“Sasa haya yanachelewesha maendeleo ya nchi. Yanachelewesha uwezo wa nchi kuweza kupambana na matatizo ambayo yanaweza kuwa makubwa. Tukichukulia mfano mkubwa wa UVIKO-19, nchi zote ziliathirika. 

“Kwa hiyo, ilikuwa ni ngumu sana kwa nchi moja kutoa msaada kwa nchi nyingine wakati na yenyewe inapambana na hali yake. Kwa hiyo, katika muktadha kama huo, ni muhimu sana kwa wafadhili wa ndani, au raia, familia, au watu wanaoguswa, wenye uwezo kuweza kutoa mchango wao katika mapambano kupitia sayansi. 

“Kwa hiyo, mfano ambao familia hii [ya Salim Ahmed Salim] imeonesha, ni mfano wa kuigwa. Lakini pia ni suala ambalo linaweza likawa endelevu la namna ambavyo tunaweza tukahamasisha familia na watu mbalimbali kuweza kutoa mchango wao katika kuendeleza tafiti, kuendeleza sayansi, na kuendeleza maendeleo ya nchi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts