Dodoma. Wito umetolewa kwa Watanzania kuacha kuwanyanyapaa wenzao wanaoishi na virusi vya UKIMWI, huku waathirika wa ugonjwa huo wa upungufu wa kinga mwilini wakibainisha kwamba upo uhusiano kati ya vitendo vya unyanyapaa na kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa huo hatari.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hii kwa nyakati tofauti, Watanzania waishio na virusi vya UKIMWI walitaja unyanyapaa kama moja ya matatizo sugu wanayoyapitia kwenye maisha yao ya kila siku, wakipendekeza hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya watu wanaotekeleza vitendo hivyo.
Kinachowauma Watanzania hao zaidi ni namna vitendo hivyo vinavyowachochea baadhi ya wenzao wanaoishi na virusi vya UKIMWI kueneza maambukizi ya virusi hivyo kwa makusudi kama njia ya kulipiza visasi kutokana na unyanyapaa wanaokabiliana nao kwenye jamii zao.
Dorah Mwaluko amekuwa akiishi na virusi vya UKIMWI tangu mwaka 2002 ambaye mpaka sasa, miaka 21 baadaye, hajui haswa alipata maambukizi hayo kutoka wapi.
Mama huyo wa mtoto mmoja anashukuru bado yuko hai licha ya kiwango kikubwa cha ubaguzi ambacho amekuwa akikutana nacho ndani ya kipindi hicho, ubaguzi ambao umekuwa ukimuachia hisia mbalimbali, ikiwemo ile ya kutaka kujiua.
“Ilifika mahali nilitamani kujitoa uhai wangu kwa sababu mimi nilikuwa ni tegemeo kwenye familia,” Dorah, 63, aliiambia The Chanzo. “Nilikuwa tegemeo la familia. Sasa niko kitandani ilikuwa inanisumbua sana. Nilishataka kujiua siyo mara moja wala mara mbili.”
Mkazi huyo wa Dodoma anaamini kwamba unyanyapaa unamfanya mlengwa aishi katika hali ya hasira na hivyo kumpelekea aamue kusambaza maambukizi hayo kama njia ya kupambana na hali hiyo anayokabiliana nayo katika jamii yake.
“Unyanyapaa unamfanya mtu anayeishi na maambukizi kujiona hana haki ya kuishi kama watu wengine,” Dorah, ambaye analaani usambazaji wa maambukizi kwa makusudi, alisema. “Ndiyo maana tunasema ni muhimu kwa watu kuacha hivi vitendo vya unyanyapaa kwani hupelekea athari hizo.”
Hayuko peke yake
The Chanzo iliwauliza Watanzania wengine wanaoishi na virusi vya UKIMWI endapo kama wanakubaliana na mtazamo huu wa Dorah na wote iliyoongea nao walisema wanakubaliana nao.
Kati yao ni Semeni Jonathan aliyegundulika kuishi na virusi vya UKIMWI hapo mwaka 2003 ambaye anaeleza kwamba licha ya kutaka kulipa kisasi, unyanyapaa hupelekea kuenea kwa maambukizi kwa namna nyingine pia.
Mama huyo wa mtoto mmoja anaeleza kwamba kwa sababu tayari waathirika wanakabiliana na uadui kwenye jamii zao, wengi wao wanaamua kutokuweka hali za afya zao hadharani ili kujiepusha na uadui huo, hali inayopelekea kusambaa kwa maambukizi.
SOMA ZAIDI: Anatumia Mitandao ya Kijamii Kuwatafutia Wenza Watu Wanaoishi na VVU
“Kama ni watu wana mahusiano, wengi hawako wazi kuwashirikisha wenza wao kwa kuogopa kunyanyapaliwa,” Semeni, 49, alisema kwenye mahojiano na The Chanzo. “[Mtu] anasema nikimshirikisha ataniacha, na mimi bado ninampenda, nitaenda wapi?”
“Sasa nitashiriki [mapenzi] na mwenzangu bila ya yeye kujua hali yangu ya maambukizi,” anaongeza Semeni. “Na yeye atakuwa na mimi bila kuchukua tahadhari yoyote. Katika mazingira hayo, ni rahisi sana kumpatia na yeye virusi vya UKIMWI.”
Semeni siyo kwamba anaunga mkono vitendo hivyo. Kimsingi, anavilaani kwa nguvu zote, akitoa wito kwa wenzake wanaoishi na virusi vya UKIMWI kutafuta njia nyingine ya kukabiliana na vitendo hivyo vya unyanyapaa bila kuwaathiri watu wengine wasiyo na hatia.
Namna nyingine ambayo unyanyapaa unaweza kupelekea kuenea kwa maambukizi ya virusi vya UKIMWI ni ile iliyobainishwa na Amina Abdulrahman, binti wa miaka 21 aliyezaliwa na maambukizi hayo.
“Unyanyapaa unasababisha watu wanaoishi na maambukizi vya virusi vya UKIMWI kuacha kutumia dawa, na hata kushindwa kuhudhuria kliniki kuangalia maendeleo yao,” anasema Amina.
“Ukinywa dawa inafubaza [makali ya UKIMWI], ukiacha maambukizi yanaendelea kuongezeka. Nafikiri tukijengewa uwezo na kujitambua itaondoa hali ya hofu,” aliongeza.
Tafiti zathibitisha
Tafiti mbalimbali za kisayansi zimethibitisha kwamba upo uhusiano wa moja kwa moja kati ya vitendo vya unyanyapaa na kuenea kwa maambukizi ya virusi vya UKIMWI, siyo Tanzania tu bali hata sehemu nyingine za dunia.
Kwa mfano, utafiti uliowahi kufanyika mwaka 2001 ulihitimisha kwa kusema kwamba unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI Tanzania “unatoa mchango mkubwa” kwenye kuenea kwa maambukizi hayo miongoni mwa jamii, hususan kwa kuchochea hofu kwa watu kuweka hadhi za afya zao wazi.
SOMA ZAIDI: Mtaalamu Aeleza Kila Kitu Unachopaswa Kujua Kuhusu Saratani ya Shingo ya Kizazi
Haishangazi, kwa hiyo, kuona Nadhifa Omar, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) akikiri uwepo wa uhusiano huu na namna juhudi za Serikali kukabiliana na janga hilo zinavyoathiriwa na vitendo vya unyanyapaa.
Kwenye mahojiano na The Chanzo, Nadhifa alisema hali ya unyanyapaa huwafanya waathirika kuwa na hofu ya kwenda vituo vya afya kupata huduma stahiki, ikiwa ni pamoja na kupima ili kutambua hali zao.
“Hata wale ambao tayari wanajua hali zao za maambukizi bado huwa wanahofu kwenda vituo vya karibu kuchukua dawa, wakihofia watakutana na watu wanaowafahamu, hivyo kwenda vituo vya mbali,” alisema Nadhifa.
Anaongeza kwa kusema kwamba kutokana na hofu ya kunyanyapaliwa, mtu anayeishi na virusi vya UKIMWI anaweza kuishi na mtu asiye na maambukizi na asimwambie wakati huo akiendelea na mahusiano ya kingono.
“Lakini kama angemuweka wazi mapema wangeweza kutumia njia sahihi za kujikinga na mwenza wake asipate maambukizi,” alisema Nadhifa. “Jamii inatakiwa kuacha unyanyapaa na kuchukulia VVU kama ugonjwa mwingine. Jamii ibadilike ili ifikapo 2030 tuwe tumefikia maambukizi mapya sifuri.”
Sheria mpya itungwe
Wengi walioongea na The Chanzo wamependekeza kutungwa kwa sheria kali dhidi ya watu wanaonyanyapaa watu waishio na virusi vya UKIMWI, wakionesha kujiamini kwamba endapo kama sheria hiyo itakuwepo vitendo vya unyanyapaa vitapungua.
Dorah, kwa mfano, anaamini uwepo wa sheria hii utasaidia sana kukabiliana na vitendo hivi vya unyanyapaa, na hivyo kuchangia kwenye jitihada za kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI nchini.
SOMA ZAIDI: Nimeishi na Virusi vya UKIMWI kwa Miaka 27 Bila Mwenyewe Kujijua
“Hiyo sheria itasaidia,” Dorah aliiambia The Chanzo. “Maana wakitaka kufanya kitu kama hicho, wakijua kwamba kuna sheria, nikimnyanyapaa mtu anayeishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kifungo labda ni miaka mitatu, au faini ni kiasi fulani, inaweza ikasaidia.”
The Chanzo ilimuuliza Waziri wa Katiba na Sheria Damas Ndumbaro kwenye mjadala wa hivi karibuni wa Clubhouse endapo kama anadhani kwamba Serikali inaweza kuamua kuja na sheria hii kama inavyopendekezwa na Watanzania hao wanaoishi na virusi vya UKIMWI.
Ndumbaro, ambaye pia ni Mbunge wa Songea Mjini (Chama cha Mapinduzi – CCM), alijibu kwamba hilo ni jambo gumu kulitekeleza kwani Serikali ikiamua kuja na sheria hiyo mahususi juu ya ubaguzi dhidi ya watu wanaoishi na VVU, makundi mengine pia yatakuja kutaka sheria yao mahususi.
“Kwa hiyo, lazima Katiba [ya nchi ambayo] inakataza unyanyapaa tuitekeleze na tuisimamie,” alisema Dk Ndumbaro. “Unyanyapaa umetawanyika katika sehemu nyingi. Tukisema tuwe na sheria hiyo moja kwa ajili ya kundi hilo moja tutakuwa na sheria nyingi.”
“Kwa sasa hivi Katiba yetu iko wazi kwamba ubaguzi wa aina yoyote ile hautakiwi na ni kinyume cha sheria,” aliongeza. “Na mtu yeyote anaweza akafungua kesi kupinga unyanyasaji na ubaguzi wa aina yoyote ile.”
Katika kipindi cha miaka 12 iliyopita, Tanzania imefanikiwa kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI kwa asilimia 50 na kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa wa UKIMWI kwa asilimia 50.
Asilimia 86 ya Watanzania wanaoishi na virusi vya UKIMWI wanapatiwa matibabu wakati huu. Hata hivyo, hali ya unyanyapaa imeendelea kuripotiwa kuwepo katika taifa hilo la Afrika Mashariki, huku Watanzania wakishauriwa kuachana na mila hiyo potofu.
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.