The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

‘Mazao Yetu Yote Yamesombwa na Maji.’: Njaa Inavyowanyemelea Waathirika wa Mafuriko Mtwara

Ni wananchi takriban 12,000 kutoka kata ya Mahurunga ambao wameachwa bila chakula baada ya mafuriko kuharibu takriban ekari 2,776 za mashamba yaliyokuwa yamepandwa mazao mbalimbali.

subscribe to our newsletter!

Mtwara. Wingu la hofu na wasiwasi limetanda kwenye anga za vijiji vya Mahurunga, Kivava, na Kihimika mkoani hapa kufuatia uwepo wa uhaba mkubwa wa chakula uliosababishwa na uharibifu wa mazao mashambani kutokana na mafuriko yaliyovikumba vijiji hivyo mapema mwezi uliopita.

Ikitembelea vijiji hivyo takriban mwezi mmoja tangu wananchi wao wapatao 12,000 wakumbwe na zahama hiyo, The Chanzo ilishuhudia uharibifu mkubwa wa mali uliosababishwa na mafuriko hayo yaliyotokea Aprili 1, 2023, uharibifu uliyowaacha wananchi na utegemezi mkubwa ambao hawajawahi kuufikiria kwenye maisha yao yote.

Kwenye kijiji cha Kivava, The Chanzo ilishuhudia wananchi wakikarabati nyumba zao zilizoathiriwa na mafuriko. Inakadiriwa kwamba takriban nyumba 60 kijijini hapa ziliangushwa na maji na kupelekea watu wapatao 1,400 kubaki bila makazi, wakipata hifadhi za muda kwenye shule za msingi zilizopo kijijini hapo.

Baadhi ya nyumba zilizoharibika

Kijiji hicho chenye kaya 518 na wakazi wapatao 1,976 kilishuhudia mazao yake yote – ikiwemo mchele, mihogo, korosho, minazi, kunde, na mtama – yakisombwa na maji, hali inayohofiwa kusababisha maafa kama hatua za haraka hazitachukuliwa ukizingatia shughuli kubwa ya kiuchumi kwenye kijiji hiki na vingine vilivyoathiriwa na mafuriko hayo ni kilimo.

Hadija Mohamed ni mkazi wa kijiji hiki na miongoni mwa wanakijiji kadhaa ambao wameieleza The Chanzo kwamba hawawezi kufikiria hatma ya maisha yao kutokana na uharibifu mkubwa wa hali na mali uliosababishwa na mafuriko hayo yaliyotokana na kujaa kwa Mto Ruvuma.

The Chanzo ilimuona Hadija akiwa anatoka shambani kuangalia hali ya shamba lake hilo, akionekana kuchoka na uso wake ukiwa umesawijika, hali iliyoashiria huzuni na masikitiko aliyokuwa nayo mama huyu wa watoto watatu.

Hali yangu duni

“Mimi nililima ekari mbili za mpunga pamoja na mahindi, lakini ninavyosema leo hapa hata chakula sina,” Hadija, 45, alisema kwa sauti iliyojaa uchungu. “Nina watoto watatu. Hali yangu duni. Sijui hata cha kufanya kwa sasa.”

“Serikali, mashirika, na watu wengine tunaomba mtusaidie kuhusu suala la chakula,” aliomba Hadija. “Tunaomba mtufikie siyo kesho au keshokutwa. Kama itawezekana tupate msaada wa haraka.”

SOMA ZAIDI: Serikali ya Zanzibar Yaja na Ufumbuzi wa Tatizo la Mafuriko Eneo la Mfenesini

Kwenye vijiji vingine vya Mahurunga na Kihimika, The Chanzo iliona wana kijiji wakiwa kwenye mashamba yao kuangalia namna uharibifu ulivyotokea, wakiwa hawajui nini cha kufanya kuyarejesha mashamba hayo kwenye hali yaliyokuwepo.

Katika hali iliyodhihirisha hisia za kukata tamaa, The Chanzo ilishuhudia baadhi ya wanakijiji wakipiga goti chini na kuokota mahindi yaliyosalia baada ya miti hiyo kusombwa na mafuriko hayo yaliyodumu kwa takriban wiki moja na kuzua taharuki iliyoje.

Wananchi wengi wa maeneo haya ni wakulima wadogo ambao hutegemea kuvuna mazao yao kuanzia mwezi Aprili mpaka mwezi Julai, hali inayowaacha na chakula mpaka mwezi Januari pale msimu mpya wa kilimo unapoanza.

Hii ndiyo sababu kwa nini mafuriko haya yamewaumiza sana wananchi kwani yameharibu mazao yao ambayo walitegemea kuyatumia kwa ajili ya chakula kwa sehemu iliyobaki ya mwaka huu.

Abdalla Madiva anaishi kijiji cha Mahurunga ambaye aliiambia The Chanzo kwamba kutokana na hali hiyo, familia yake imelazimika kupunguza milo ya siku kutoka mitatu hadi mmoja ili kukabiliana na hali ya njaa wananchi wa kijiji hicho wanakabiliana nayo.

Tunakula mlo mmoja

“Mimi nyumbani kwangu pale nina familia ya watu saba na tunakula mlo mmoja jamaa yangu wala sikufichi,” Madiva, 60, anasema. “Huwa tunakula jioni tu. Asubuhi kukicha kila mtu anaingia anakohangaika. Wanaokwenda shule wanaenda shule. Jioni tukirudi unapikwa ugali mmoja basi, hiyo mpaka kesho. Hayo ndiyo maisha tuliokuwanayo.”

Mazao yaliyoharibikia shambani

Tangu kutokea kwa mafuriko hayo, Serikali na wadau kadhaa wamejitokeza kusaidia waathirika wa janga hilo, huku Ofisi ya Waziri Mkuu ikitoa msaada wa mahindi tani 24. 

Wadau wengine kama vile Benki ya NMB nayo ilijitolea kusaidia waathirika wa mafuriko hayo, ikitoa magodoro, mashuka na vifaa vya shuleni vyenye thamani ya Shilingi milioni tano kwa kaya zilizoathirika.

SOMA ZAIDI: Kinachoweza Kukwamisha Mipango ya Serikali Kukabiliana na Njaa

Nao Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania ulilipatia Shirika la Msalaba Mwekundu jumla ya Shilingi milioni 203 ili kulisaidia shirika hilo la misaada kutoa msaada stahiki kwa waathirika wa mafuriko hayo, hususan kwenye eneo la mahitaji ya msingi ya nyumbani kwa familia husika.

Mratibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu kwa mkoa wa Mtwara, Ruge Sezi, ameiambia The Chanzo kwamba kwa mujibu wa tathmini waliyofanya, suala la uhaba wa chakula miongoni mwa waathirika wa mafuriko hayo limechukua nafasi kubwa, akisema msaada mwingi unahitajika katika eneo hilo.

“Ndiyo maana kama shirika tumeamua kupeleka misaada ya mbegu mpya na vifaa vya kilimo, kama majembe na mapanga, [kwa waathirika] kutokana na taarifa tulizozipokea zinazoonesha kwamba vifaa vingi vimechukuliwa na maji,” Sezi alisema kwenye mahojiano na mwandishi wa habari hii.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mtwara Vijijini Shamsia Tamba (Chama cha Wananchi – CUF) ametoa wito kwa wadau na mashirika mengine kuendelea kujitokeza kutoa misaada kwa wananchi wa kata ya Mahurunga, akisema tathmini yake inaonesha uwepo wa tatizo kubwa la chakula.

“Serikali ipo kwenye mpango wa kupeleka msaada wa mahindi ambayo yatauzwa kwa bei nafuu ili kuwapa nafasi wananchi wote walioathiriwa na mafuriko kupata chakula,” Tamba aliiambia The Chanzo. “Ni muhimu kwa wadau wengine kuunga mkono juhudi hizi.”

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Selemani Nampanye aliiambia The Chanzo kwamba wakati wanashukuru kwa hatua hizo, misaada zaidi inahitajika kuwanusuru wananchi wake na janga la njaa linalowanyemelea.

SOMA ZAIDI: Ni Upi Mtazamo wa Wakulima Wadogo Juu ya Mabadiliko ya Tabia ya Nchi?

Nampanye, ambaye ni Diwani wa kata ya Mahurunga, alidai kwamba jumla ya ekari 2,776 za mashamba zimeteketea kutokana na mafuriko hayo, akibainisha kwamba ni ngumu kufikiria watu wa kata hiyo wataishije baada ya uharibifu huo.

“Kwa taswira ya mafuriko yale, yameathiri kata nzima, kwa maana mashamba yote ya kata ya Mahurunga hayana kitu sasa hivi,” Nampanye alisema. “Hali siyo nzuri kwa maana watu wana njaa. Wanahitaji msaada.”

Serikali kusambaza mbegu

The Chanzo ilimuuliza Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Hanafi Msabaha, ni hatua gani Serikali imepanga kuchukua kuwaokoa wananchi hao na janga la njaa ambapo alieleza kwamba mbali na misaada ya chakula inayopelekwa huko, Serikali pia inapanga kugawa mbegu za mazao ya muda mfupi ya kunde na choroko. 

Msabaha alisema kwamba mpaka sasa jumla ya kilogramu 1,000 za mbegu hizo zimepelekwa kwa wakulima wa maeneo yaliyoathirika, akiita hatua hiyo moja kati ya njia za muda mrefu za kukabiliana na hali husika.

“Tunaendelea kutafuta mbegu za mazao mengine yanayohimili ukame na ambayo yanaweza kuvunwa kwa haraka haraka,” Msabaha aliiambia The Chanzo. “Tutaendelea kugawa mbegu na tunawahamasisha [wakulima] pia waendelee kulima mihogo kwa sababu ni zao linahimili ukame.”

Kwa mujibu wa tathmini ya kitaalamu, Kata ya Mahurunga iliyopo katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji, haijawahi kukumbwa na mafuriko ndani ya kipindi cha angalau miaka mitatu iliyopita.

Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Mtwara kama mkoa kukabiliwa na mafuriko kwani mnamo Januari 14, 2021, kwa mfano, angalau nyumba 177 kutoka Mikindani mkoani humo zilisombwa na maji na kuacha makumi ya wananchi bila makazi.

Omari Mikoma ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *