The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Je, Wanahabari Walipe Vyanzo Vyao Vya Habari?

Ni kinyume na maadili ya uandishi wa habari kwa mwanahabari kukilipa chanzo chake cha habari.

subscribe to our newsletter!

Ungekuwa ni mwandishi wa habari, ungelipa fedha kwa ajili ya kupata taarifa kutoka chanzo cha habari? Au kama ungekuwa mwananchi, ungehitaji mwandishi akulipe kila wakati anapokuhoji ili kupata taarifa fulani kutoka kwako? Na je, unadhani haya yote mawili – kulipa au kulipwa – ni sawa?

Haya ni maswali magumu ambayo nimekuwa nikijiuliza mwenyewe kwa siku za hivi karibuni kama mwandishi wa habari kutokana na uzoefu ambao nimekuwa nikiupata kila wakati nikienda mitaani na kuzungumza na wananchi ili kupata uzoefu wao kuhusiana na mambo mbalimbali ya kitafaifa yanayotokea nchini.

Zaidi ya mara moja imeshawahi kutokea kwamba mwananchi anadai ili aweze kuzungumza chochote ni lazima nitoe fedha mfukoni na nimpatie. Kiwango kinaweza kuwa kidogo kama Shilingi 1,000 au kikubwa kama Shilingi 15,000. Kila wakati hali hii inapojitokeza huwa natatizika sana, nikishindwa kujua namna bora zaidi ya kujikwamua kwenye hali hiyo.

Wananchi wanadai kwamba msingi wa wao kuomba malipo ni kwa sababu kwa kuwahoji wao mimi nafanya kazi ambayo mwisho wa siku inaniingizia kipato, hali inayowafanya wahisi kuongea na mimi bure ni kama kunichangia hicho kipato huku wao wakibaki hawana kitu kabisa.

Hii ndiyo maana imeshawahi kutokea kulipa wananchi ili tu niweze kuzungumza nao kuhusu habari fulani niliyokuwa naifanyia kazi. Si kitu ambacho nimewahi kukifurahia na si kitu ninachopenda kukifanya hata kidogo kama mwandishi wa habari. 

Ukiukwaji wa maadili

Moja kati ya sababu zinazonifanya nisipende ni kwa sababu nadhani uamuzi huo ni ukiukwaji mkubwa wa maadili ya uandishi wa habari.

Maadili na miiko ya taaluma ya uandishi wa habari haimruhusu mwandishi kutoa fedha kwa chanzo cha habari kwa ajili ya kupata taarifa fulani kwani kufanya hivyo ni kumshawishi, hali inayoathiri uhuru wa mtu husika kutoa mawazo yake. 

Kama mwandishi wa habari, nikimuuliza mtu ni ipi tathmini yake juu ya utendaji kazi wa Rais Samia Suluhu Hassan nitataka afanye hivyo kwa kutumia maarifa yake aliyoyapata kutoka nyanja mbalimbali bila kuathiriwa, au kushawishiwa, na kitu chochote kile kwenye mchakato wake mzima wa kueleza tathmini yake hiyo.

SOMA ZAIDI: Waandishi Mwanza Watathmini Hali ya Uhuru wa Habari

Kwa kumlipa, mzungumzaji anaweza kuzungumza vitu ili kuniridhisha tu mimi niliyemlipa na pengine siyo kwamba anaviamini kutoka moyoni vitu hivyo anavyovizungumza. 

Hilo likitokea, dhana na dhima nzima ya upashanaji habari inakuwa imeingia dosari kwani kama mwandishi napaswa kuwapa wasomaji wangu habari zinazotokana na uzoefu halisi wa watu ninaozungumza nao na siyo habari za kubuni na kusadikika.

Inaweza kuwa hatari pia. Fikiria kama mwandishi wa habari atapita mitaani na kugawa fedha kwa wananchi ili wamseme mwanasiasa au kiongozi fulani kwa ubaya kama sehemu ya mradi wa kumuharibia kisiasa? Au awalipe wananchi fedha waseme bidhaa za kampuni fulani ili kuiathiri kampuni hiyo kimauzo na kibiashara?

Hilo likitokea siyo tu dhana na dhima ya upashanaji habari itakuwa imeingia dosari kama nilivyoeleza hapo juu bali pia hata dhana nzima ya kidemokrasia inayohitaji wananchi kuongozwa kwa ridhaa zao, au mteja kununua bidhaa x kwa ridhaa yake binafsi, inasita kufanya kazi.

Kimsingi hiki ndicho walimu wa uandishi wa habari kwenye taasisi za elimu ya juu huwafundisha wanafunzi wao, kwamba wasilipie kupata taarifa. 

Nilimuuliza Njonjo Mfaume, Mhadhiri wa Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kwa nini haikubaliki kulipa kwa ajili ya kupata taarifa.

“Halikubaliki kwa sababu unapokilipa chanzo cha habari unashusha kuaminika kwa ile habari yenyewe kwa sababu watu wanaweza wakasema kwamba kalipwa ndiyo maana kasema hivi,” Mfaume aliniambia. “Labda kule kumlipa ndiyo kumeshawishi kusema kile alichosema ili akuridhishe.”

Kuchochea mabadiliko

Kinachonitoa kitandani na kwenda ofisini kila siku kama mwandishi wa habari ni imani kwamba nina nafasi na uwezo wa kuchochea mabadiliko chanya ninayoyataka kuyaona yakitokea kwenye jamii yangu na kwenye nchi yangu kwa ujumla.

Ninachokitarajia sana kutoka kwa wananchi ninaowafanyia kazi ni kunipa ushirikiano kwenye mchakato mzima wa kuchochea haya mabadiliko, ni kunishika mkono pale ninapokwenda mtaani kuwashika mikono ili kusukuma gurudumu la mabadiliko. 

SOMA ZAIDI: Vyuo vya Uandishi wa Habari Virejee Mitaala Mara kwa Mara

Muda mwingine inawezekana ni suluhu za matatizo yanayowakabili wananchi, hivyo nahitaji kufahamu wananchi wanadhani ni nini wanatakiwa kufanyiwa ili kumaliza tatizo husika. 

Kitendo cha wananchi kudai nilipie ili waweze kunipa uzoefu wao juu ya mambo mbalimbali yanayowaathiri ni kama kisu mgongoni na ni lazima nikiri kwamba ni moja kati ya vitu vinavyonifanya nihoji kama kile ninachofanya nahitaji kuendelea kukifanya. 

Nahisi kusalitiwa, kutothaminiwa, na mchango wangu kwenye kuchochea maendelea kwenye jamii yangu kutoeleweka vya kutosha. Kupitia kazi yangu, najihisi kama kiunganishi, kazi yangu ikiwa ni kuchukua maelezo ya upande mmoja na kuyapeleka upande wa pili kwa ajili ya ama kupata majibu au ufafanuzi wake. 

Hofu yangu ni kwamba kama upande mmoja utataka kulipwa ndiyo utoe maelezo yake kazi hii muhimu niliyoamua kuifanya – ya kuwa kiunganishi – nitashindwa kuifanya na hivyo kukwamisha mchango ninaoweza kuutoa kwenye jamii yangu.

Watafuta taarifa wengi

Hali hii ya wananchi kuomba fedha ili waweze kuongea inaweza kuwa inasababishwa na uwepo wa watafuta taarifa wengi ambao wote huelekea huko huko mitaani kwa ajili ya kuongea na wananchi.

Siyo kila mtu anayekwenda mtaani kuongea na mwananchi ni mwandishi wa habari. Wengine, inafahamika, wanatoka mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), ambao kwa bahati mbaya au nzuri, hawafungwi na maadili yanayowafunga waandishi wa habari.

SOMA ZAIDI: Zanzibar Mbioni Kuzifanyia Marekebisho Sheria Zinazolalamikiwa na Wadau wa Habari

Vilevile, kwa sababu si kazi zao za kila siku kama ilivyo kwa wenzao waandishi wa habari, wale kutoka kwenye NGOs wanaweza kumudu gharama za kuwalipa wananchi ili wapate taarifa wanazotaka, hali ambayo mara nyingi huwa tofauti kwa waandishi wa habari ambao kwa kiasi kikubwa tunafanya kazi kwenye mazingira magumu kifedha.

Kwa kumalizia, suala hili lote linahusu dhana nzima ya uhuru wa mwandishi wa habari na vyombo vya habari. Kama mwandishi ataweza kulipa ili apate taarifa, unawezaje kuwa na uhakika kama mwandishi huyu huyu hatapokea taarifa ili achapishe au apotezee taarifa fulani?

Mwisho wa siku ni kuhusu maadili, kama nilivyozungumza hapo awali.  Maadili ndiyo moyo wa uhuru wa vyombo vya habari na waandishi wao. Maadili ndiyo yanatakiwa yamuongoze mwandishi anafanyaje anapokuwa kwenye hali fulani.

Jukumu la kila mtu

Na ni muhimu tukafahamu kwamba mapambano ya kuhakikisha uhuru wa habari si mapambano ya waandishi wa habari tu. Ni mapambano ya kila mwanachama wa jamii yetu kwani vyombo vya habari haviwanufaishi wanahabari tu bali jamii nzima kwa ujumla.

Kwa hiyo, ni muhimu kwa kila mwanajamii kushiriki kikamilifu katika mapambano haya, ikiwemo kwa kujiepusha na vitendo vyote ambavyo vinaweza kuuweka mashakani uhuru wa mwanahabari na chombo chake.

SOMA ZAIDI: Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Ina Maana Gani Kwako Kama Mwananchi?

Ningeshauri fursa ikijitokeza ya kuongea na mwandishi wa habari mwananchi ajitokeze na kufanya hivyo bila kudai malipo ya kifedha kutoka kwa mwandishi. Mifano ipo lukuki ya namna sauti moja ilivyoleta mabadiliko makubwa sana kwenye jamii zetu yenye thamani ya mabilioni ya fedha.

Barabara zimejengwa kwa wananchi kuzungumza; vivyo hivyo kwa shule kupatiwa walimu na madawati; zahanati kukarabatiwa na kupatiwa vifaa tiba; na watuhumiwa wa uhalifu kutiwa nguvuni baada ya wanajamii kuweza kujitokeza na kupaza sauti zao kupitia vyombo vya habari.

Kwa hiyo, kuna thamani kubwa sana ya kuzungumza kupitia vyombo vya habari. Ikitokezea huwezi kuzungumza, ni sawa, lakini ni ombi langu kwamba usiache kupaza sauti yako eti kwa sababu tu mwandishi amegoma kukupa Shilingi 1,000!

Lukelo Francis ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia lukelo@thechanzo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Sio sawa kwa mwandishi kumlipa source, kwa sababu sisi wasomaji tutajuaje kama alichosema source ni mawazo yake au ni kile mwandishi alichotaka kisemwe??

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts