The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Vyuo vya Uandishi wa Habari Virejee Mitaala Mara kwa Mara

Vyombo vinavyopokea waandishi kutoka vyuo vinasema wengi hawawezi hata kuandika utangulizi wa stori. Lakini pia inasemwa hao waandishi hata tafakuri tunduizi hawana.  

subscribe to our newsletter!

Uandishi wa habari ni taaluma kama taaluma nyingine lakini pia siyo kama taaluma nyingine. Ndiyo, ili uwe muandishi unasomea, unapewa leseni ya kukuruhusu kufanya kazi, na kuna mamlaka ya kitaaluma zinasimamia maadili. Katika hayo, kuna mfanano na taaluma nyingine, ingawa pia yanabishaniwa.

Wapo wanaoamini uandishi wa habari hauwezi kuwa taaluma kwa sababu hata wasiosomea wanafanya hiyo kazi, na ukiwazuia unaingilia haki yao ya kikatiba kama iivyoainishwa katika ibara ya 18, kifungu (a) hadi (d), ya Katiba ya Tanzania. 

Hakuna mtu amefungwa, au kuzuiwa, kwa kufanya kazi za uandishi wa habari bila leseni na hata hilo Baraza la Habari halina meno. Lakini tuyaache hayo. Huo ni mjadala wa siku nyingine.

Niliposema uandishi wa habari ni zaidi ya taaluma nyingine ni kwa sababu ni shughuli yenye uhusiano na kutimilizwa haki ya kiraia ya kuhabarishwa. Uzito wa jukumu la vyombo vya habari umefanya viitwe Mhimili wa Nne, vikifanya kazi ya kuchunga mihimili mingine: Serikali, Bunge, na Mahakama.

Vyombo vya habari ni daraja muhimu linalowezesha mawasiliano kati ya Serikali na wananchi. Pia, vinaibua ajenda na kuwezesha taifa kuongea kwa kuwa jukwaa la mijdala.

Hebu waza maisha yangekuwaje bila kuwepo vyombo vya habari! Demokarasia, ambayo inahitaji raia wenye taarifa sahihi ili kuchagua kati ya mibadala ya sera, vyama na viongozi; demokrasia inayohitaji taifa kuongea, ingetekelezekaje? Ni kwa sababu hiyo, vyombo vya habari huru ni moja ya misingi ya demokrasia.  

Mabadiliko ya teknolojia

Ukiacha upande huo wa uwajibu unaoonesha umuhimu wa taaluma, uandishi wa habari pia ni taaluma inayoathiriwa na mabadiliko ya teknolojia. Kabla ya uvumbuzi wa teknolojia yeyote, jamii mbalimbali zilikuwa na mifumo ya kuhabarishana: ngoma, moshi, miluzi, mbiu, nakadhalika.

Yakaja makaratasi yaliyoruhusu taarifa kuandikwa kwa mkono na kubandikwa maeneo ya jumuiya, kisha ikaja teknolojia ya machapisho iliyoruhusu uanzishwaji wa magazeti, ikaja redio, televisheni, na sasa intaneti na yaambatanayo mengine katika mitandao ya kijamii.

SOMA ZAIDI: ‘Sheria Kandamizi Zinavifanya Vyombo vya Habari Visitekeleze Wajibu Wao Ipasavyo’

Vifaa vya kazi navyo vimebadilika sana na kuwa vya kidijitali kutoka analojia. Kila uchao zinatengenezwa kamera za picha mnato na za video, vinasa sauti, kumpyuta, mitambo ya uchapaji, aina mpya na za kisasa zaidi. 

Kwa sababu ya kukua kwa teknolojia, simu janja sasa ni kifaa kinachojitegemewa cha kazi, kikitumika kuandika habari, kurekodi sauti, na kupiga picha za ubora wa juu, za mnato na za video.

Kwa upande mwingine, teknolojia imezaa changamoto mpya nyingi, ikiwemo mitandao ya kijamii kutweza nguvu vyombo vikuu na inayoruhusu kila Tom, Dick, and Harry kukusanya na kusambaza habari kiasi kwamba baadhi zinaaminika, zinapewa uzito na kufanyiwa rejea siyo tu na wanajamii bali hata hao waandishi wenyewe wenye taaluma zao.

Hali ya kila mtu kuweza kukusanya na kusambaza maudhui imezalisha habari nyingi za uzushi. Hivi karibuni tu kulikuwa na taarifa ya Achraf Hakimi, mchezaji wa soka wa timu ya PSG ya Ufaransa, raia wa Morocco, eti alikuwa na kesi ya kudaiwa talaka na mkewe huku pia mke huyo akidai nusu ya mali za mchezaji huyo. 

Kwa mshangao mkubwa wa mke huyo, ikagundulika mahakamani kuwa Hakimi hana hata ndururu kwa sababu mali zote zilikuwa kwenye jina la mama yake!

Mpaka Aprili 20, 2023, pale mtandao wa The African Report ulipoondoa sintofahamu hiyo kwa kufafanua ukweli halisi twiti ya lugha ya Kifaransa ya jarida la First Mag iliyoanzisha uzushi huo ilishasambazwa zaidi ya mara 15,000 na kupokea ‘likes’ 97,000, achilia mbali twiti zilizofasiri habari hiyo kwa lugha zote uzijuazo Afrika.

Hatari ni kwamba habari hiyo ilipokelewa, ikatangazwa, ikachapwa, na kusambazwa na vyombo vikuu vya habari vya ndani hapa Tanzania na nje. Waandishi mahiri wanaojulikana kwa ubobevu katika taaluma nao wakaibeba habari katika akaunti zao za mitandao ya kijamii.

SOMA ZAIDI: Mambo Muhimu ya Kufahamu Kuhusu Muswada Mpya wa Sheria ya Huduma za Habari Tanzania

Achilia hilo la habari za ushushi, maendeleo makubwa katika sekta nyingine yanaongeza changamoto zaidi kwa taaluma ya uandishi wa habari kujiimarisha ili kuripoti habari hizo kiweledi zaidi. Hii ni dunia ya takwimu, biashara, uwekezaji, mizunguko ya fedha – haya yote yanahitaji upeo wa juu zaidi wa kiuandishi.

Ipo pia changamoto kubwa ya ufinyu wa mapato kwa vyombo vya habari kuweza kujiendesha. Hayo yote niliyoyataja hapo juu yanasema kuhusu umuhimu wa taaluma hii ya habari, nguvu ya mabadiliko ya teknolojia yanayoathiri fani hii, na changamoto kubwa zinazohitaji wanahabari waandaliwe vema kumudu majukumu yao.

Mitaala ya vyuo vya habari

Kwa kuwa waandishi wanaandaliwa katika vyuo vya habari, taasisi hizo za kielimu zinapaswa kujua uzito wa majukumu hayo mazito yanayowakabili hao wanaoandaliwa. 

Pia, kwa upande mwingine, taasisi hizo za kielimu zinapaswa kuzingatia mabadiliko ya kiteknolojia ya haraka yanayotokea na kuathiri taaluma hii. Kadhalika, vyuo vizingatie changamoto za sekta ya uhabarishaji umma, nilizozijadili hapo juu ambazo zinatakiwa kupatiwa majibu.

Ukichanganya hayo yote matatu – uzito wa majukumu, mabadiliko ya teknolojia, na changamoto mpya – utaona kuwa taasisi za elimu ya habari zinapaswa kujipanga kwelikweli kuandaa watu mahiri.

SOMA ZAIDI: Zanzibar Mbioni Kuzifanyia Marekebisho Sheria Zinazolalamikiwa na Wadau wa Habari

Kuna mawanda mapana katika elimu lakini mimi nataka kuzungumzia zaidi mitaala kwa sababu hiyo ndiyo miongozo yenyewe katika shughuli ya utoaji elimu. 

Nadhani kuna umuhimu mkubwa wa vyuo vya habari kufanya marejeo ya mitaala na kuiboresha mara kwa mara. Sambamba na hilo, zinahitajika tafiti za kutosha kwa sababu uboreshaji wa mitaala unahitaji kujibu mapendekezo yanayotokana na tafiti.

Maboresho mapana na ya kina ya mitaala yanatakiwa kuanzia kwenye aina ya programu zenyewe zinazofundishwa, hadi kwenye masomo yanayotolewa kwenye kila programu husika, na mpangilio wa hayo masomo – lipi lianze, lipi lifuate, na mwisho kwenye miongozo ya masomo (course outlines). 

Nikitumia uzoefu wa vyuo vichache ninavyovifahamu, naona kuna udhaifu mwingi.

Sioni msisitizo wa kutosha kwenye kuwaelekeza waandishi kujua dhima yao katika jamii na nchi. Wakati nikifundisha somo la uandishi wa habari za uchunguzi, mwanafunzi mmoja alihoji kwa nini kazi hiyo wasiachiwe polisi; na hapo tayari alishasoma masomo ya awali juu ya uandishi na dhima yake. Ni wazi kuna kitu alikikosa. 

SOMA ZAIDI: Serikali, Wadau Wabainisha Changamoto Zinazoikabili Tasnia ya Habari Tanzania

Hadi hii leo baadhi ya programu hazina masomo ya uandishi wa habari wa mitandaoni pamoja na vikorombwezo vyake, uandishi ambao unazidi kupata umuhimu, kukua na kuajiri watu wengi, hata uandishi wa takwimu (data journalism) pia haufundishwi katika vyuo vingi. 

Siku hizi kuna masomo ya uandishi wa kuthibitisha taarifa kwa kutumia programu maalumu za mtandaoni, pia haufundishwi. Uandishi huu unasaidia kupambana na uenezaji wa habari za uzushi na za kuungaunga – kama ile Hakimi.

Suala la uchumi wa vyombo vya habari na utawala nalo halijapewa kipaumbele, licha ya kuwa ni changamoto kubwa. Tunafahamu kuwa yapo magazeti na hata radio nzuri zilikufa kwa sababu zalishindwa kujiendesha. Mitaala ingefaa ijibu changamoto hii pia.

Masuala mengine ya msingi

Licha ya vyuo kushindwa kwenda sambamba na mabadiliko ya kidijitali na changamoto zitokanazo, udhaifu mwingine wa mitaala unaonekana kwenye masuala mengine mengi ya msingi. 

Mathalan, wakati tunakazana kuwafundisha wanafunzi ujuzi katika masuala ya uandishi, hatuwaongezei ufahamu katika masuala ya sekta muhimu ambazo maudhui yake watakakwenda kuyaandika.

Kwangu mimi, mtaala bora ni ule unaowapa wanafunzi fursa ya kusoma masomo kama sayansi ya siasa, uchumi, sosholojia, sheria kidogo, nakadhalika. 

SOMA ZAIDI: Wanahabari Epukeni Makosa Haya Mnapokitumia Kiswahili

Tena, vyuo viandae masomo hayo kwa mtaala maalum wa waaandishi na siyo kuwachanganya na wengine wenye tahsusi zao kwa sababu hawa waandishi kwanza wana mahitaji maalumu na muda wao ni mchache. 

Mfano, kozi ya uchumi kwa waandishi ibebe masuala ya msingi ya kumsaidia mwandishi kuelewa nadharia, masuala, na lugha za kiuchumi wakati anaandika habari hizo, iwe hivyo pia kwa masomo mengine pia.

Suala la lugha nalo lafaa kuangaliwa. Katika Tanzania ambayo pengine hadi asilimia 95 ya vyombo vilivyopo ni vya Kiswahili, si sahihi kufundisha wanafunzi kuandika habari na makala kwa lugha ya Kiingereza pekee. 

Siyo tu hakuna uhalisia, lakini ni vigumu kujua huyu mwanafunzi anakwama kwenye lugha au maarifa yenyewe ya kiuandishi. Hebu mitaala ielekeze kuwa mwanafunzi anaweza kufanya kazi za kiuandishi anazofundishwa kwa lugha apendayo, Kiingereza au Kiswahili.

SOMA ZAIDI: Haki ya Kupata Taarifa: Uzoefu wa Mwandishi wa Chombo cha Habari cha Mtandaoni

Suala jingine la msingi katika mtaala ni mpangilio wa masomo na pia maudhui yenyewe. Najua vyuo ambavyo kila mwalimu ana fursa ya kubadili muongozo wa somo aonavyo, na matokeo yake kila mwalimu anakuja na mambo yake kiasi kuwa siyo tu yanatofautiana bali mengine yanaenda nje ya lengo la somo. 

Hebu vyuo vya habari vifanye kazi zake kisayansi. Uholela wa miongozo unapelekea baadhi ya topiki kujirudia.

Upo mjadala wa miaka nenda rudi juu ya uwiano gani ni bora wa masomo kati ya nadharia na stadi za kazi. Vyombo vinavyopokea waandishi kutoka vyuo vinasema wengi hawawezi hata kuandika utangulizi wa stori. 

Lakini pia inasemwa hao waandishi hata tafakuri tunduizi hawana, ni makondoo tu. Haya ni masuala ya kutafakari sana tukirejea mitaala.

Njonjo Mfaume ni Mhadhiri wa Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa mrejesho, wasiliana naye kwa meseji kupitia +255 735 420 780 au mfuatilie Twitter kupitia @njonjoOKAY. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *