Rasimu ya Sera ya Elimu imetolewa na hivi sasa inaendelea kujadiliwa, huku moja ya suala tete na tata likiwa ni lugha ya kufundishia. Kwenye rasimu hii, wataalamu na viongozi wetu hawajaona umuhimu wa kufanya mabadiliko yoyote ya msingi kwenye eneo hilo ukilinganisa na ilivyokuwa.
Sera inatamka kwamba lugha ya taifa ya Kiswahili itatumika kufundishia katika elimu ya awali na elimu ya msingi, isipokuwa masomo ya lugha za kigeni na katika shule zitakazoomba kutumia lugha ya Kiingereza kufundishia.
Lugha ya Kiingereza itatumika kufundishia kuanzia ngazi ya sekondari ya chini, isipokuwa somo la Kiswahili, masomo ya lugha za kigeni na katika shule za sekondari na vyuo vitakavyoruhusiwa kutumia Kiswahili kufundishia, sera hiyo inaeleza.
Kiswahili pia kitatumika kufundishia somo la Historia ya Tanzania na Maadili ili kujenga na kuendeleza mila, desturi, na utamaduni wa Mtanzania katika ngazi zote za elimu na mafunzo.
Hoja zimejengwa kutetea matamko hayo ya kisera na hata maprofesa lakini bado kuna matatizo ya msingi, kubwa ni ubaguzi na matabaka katika misingi ya wenye nacho na wasiyo nacho.
Tatizo la msingi la sera hii ni kuwa watoto wa kimaskini, ambao ndiyo wengi wanaosoma katika shule za umma, wanafundishwa kwa lugha ya Kiswahili halafu ghafla wakifika kidato cha kwanza wanaanza kusoma masomo yote kwa Kiingereza, isipokuwa Kiswahili, Historia na Maadili.
Hapo, mtoto anajikuta anapambana na lugha asiyoifahamu vema huku pia akitakiwa kufahamu vema maudhui.
Tuliosoma huko, tunajua mapambano tuliyopitia hadi walau tukatoboa. Si rahisi. Tulikariri, tulikariri na tukakariri tena. Tulikariri hadi is, was, that, na which achilia mbali misamiati migumu ya fani mbalimbali.
Kile ambacho mwenye msingi mzuri katika lugha anakisoma kwa mara moja na kukielewa, sisi ilibidi tukariri mara kadhaa ili kikae kichwani na ufanye marejeo mara kwa mara ili usisahau.
Uhalisia ni tofauti
Kinadharia, ilitarajiwa kuwa somo la Kiingereza linalofundishwa shule ya msingi litatosha kumuandaa mwanafunzi akiingia sekondari kuelewa masomo ambayo yataanza kutolewa kwa Kiingereza. Uhalisia, hata hivyo, ni tofauti.
Hatuna walimu wa Kiingereza wazuri na wa kutosha kumpa mwanafunzi stadi ya kusoma, kusikiliza, kuongea na kuandika Kiingereza kiasi cha kuweza kukitumia kwa ajili ya kupokelea maarifa.
Bila shaka, kama somo, Kiingereza kitafundishwa muda mchache tu na tuzingatie pia katika mazingira ya kijamii ya Kitanzania, Kiingereza hakitoki nje ya darasa na kutumika katika jamii.
SOMA ZAIDI: Hatua Zilizobaki Ili Kiswahili Kiwe Lugha ya Kufundishia Tanzania
Matokeo ya hali hiyo niliyoitaja ni mitihani ya kidato cha nne, inayoletwa kwa Kiingereza, kuwa migumu mno kwa vijana wetu waliopitia mfumo huu wa kuanza na Kiswahili na kisha Kiingereza.
Mtihani, kimsingi, ni mawasiliano unayoyafanya na anayekupima kumuonesha unajua, na mawasiliano hayo yanahitaji lugha. Ndoto za vijana wengi huishia kidato cha nne kwa sababu tu ya kushindwa kujieleza.
Tatizo hili haliwakuti wale wengine waliofuata mfumo wa Kiingereza. Wao walianza kusoma masomo yote kwa Kiingereza tangu chini. Hii ina maana wakiingia sekondari ya chini wanaendelea tu na masomo mapya kwa lugha wanayoifahamu.
Unaweza kuuliza, kama kuna chaguo kati ya mifumo hii miwili kwa nini ni tatizo hali ya kuwa watu wana uhuru wa kuamua kupeleka watoto katika mfumo wanaoutaka?
Ingekuwa rahisi hivyo kama mifumo yote ingekuwa bure. Shule za Kiingereza, hata zile za Serikali, zinalipiwa na wazazi wengi wa kawaida hawamudu kulipa.
Hapo ndiyo matabaka hujengeka katika elimu kwani watoto wa wenye fedha wana faida ya kumudu Kiingereza lugha ya kufundishia ngazi za juu za elimu na hivyo wana nafasi kubwa ya kufaulu kidato cha nne.
Mapema ndiyo bora
Tafiti za kisayansi zinaonesha kuwa muda bora wa mtu kujifunza lugha ni kabla ya miaka 10. Mapema zaidi, kwa hiyo, ndiyo bora zaidi.
Kwa hiyo, ni wazi kuwa wale walioanza na Kiingereza tangu awali hadi msingi na wakaendelea nacho sekondari wana faida kubwa huko mbele ambako lugha hiyo imefanywa ndiyo ya kufundishia.
Kwa hali hii utaona kuwa mifumo hii miwili tofauti inawapa faida baadhi ya kufanikiwa katika elimu kwa kuwa na msingi mzuri wa lugha huku wengine, watoto wa kimasikini, wakibaki patupu.
Hili halionekani kwa sababu kwa bahati mbaya sana mijadala hii ya lugha ya kufundishia inachangiwa zaidi na haohao wa daraja la juu na kati ambao watoto wao kamwe huwakuti katika shule za umma au za binafsi za daraja la chini.
SOMA ZAIDI: Kutweza Kiswahili ni Ishara ya Kujidharau, Kutojiamini
Mimi sioni mantiki ya kuwa na mfumo huu wa lugha mchanganyiko, yaani Kiswahili ngazi ya msingi na Kiingereza huko juu. Tuchague mfumo mmoja, na kwa sababu najua kwa uhakika tabaka la juu na kati halitaki Kiswahili, basi pia tusiwachagulie wengine Kiswahili kisa tu ni maskini.
Najua hoja za kubakisha Kiswahili kama lugha ya kufundishia ngazi ya msingi ni za ‘uzalendo,’ ‘kuenzi tunu ya taifa’ na nyingine za kihisia, sasa iweje faida hizo ziende kwa tabaka la chini tu ambao hawamudu kupeleka watoto shule za Kiingereza?
Viongozi wa Serikali waache kujificha katika hoja hizi za kihisia za kukifanya Kiswahili lugha ya kufundishia ngazi ya msingi na watimize wajibu wao wa kufanya uwekezaji utakaosaidia watoto wa kimaskini wapate elimu ya kiwango cha kuridhisha.
SOMA ZAIDI: Wanahabari Epukeni Makosa Haya Mnapokitumia Kiswahili
Kwa hiyo, Serikali iamue tu lugha ya kufundishia iwe ni Kiingereza kuanzia shule za awali, msingi, sekondari hadi elimu ya juu na kisha ifanye jitihada za kuwekeza katika kuimarisha ufundishaji wa lugha hiyo, ikiwemo kuajiri walimu wa Kiingereza wenye sifa wa kutosha.
Mifumo miwili
Vinginevyo, Serikali inaweza pia kuamua kuwa na mifumo miwili juu mpaka chini. Kama mwanafunzi atasoma elimu ya awali na msingi kwa Kiswahili, pia kuwe na muendelezo huko juu kiasi kwamba mwanafunzi awe huru kusoma na kutahiniwa kwa Kiswahili katika ngazi ya sekondari, vyuo vya kati hadi elimu ya juu.
Najua wapo wanaosema Kiswahili hakiwezekani kutumika katika elimu, hususan ya juu. Huo ni uongo. Kuna jukwaa linalojadili masuala ya kiufundi katika fani mbalimbali kama Bunge? Lakini wanajadili kwa Kiswahili na kuelewana.
Haijawahi kutokea kwa sababu mswada fulani unahusu mambo ya sayansi za anga, vinasaba, sheria na kadhalika, basi ujadiliwe kwa Kiingereza!
SOMA ZAIDI: Namna Fasihi ya Kiswahili Ilivyo Changa Kidhima Licha ya Kuwa Kongwe Kihistoria
Kwa hiyo, watakaoamua kupita mkondo huu wa Kiswahili kitupu, wafundishwe Kiiingereza kama somo na kama hakiwatoshi wataenda kukitafuta wenyewe popote.
Tusilazimishe mwalimu wa baolojia, hesabu, au jiografia afanye jukumu ambalo siyo lake la kusomesha mtoto lugha ya Kiingereza kisa hajaandaliwa mapema wakati ana jukumu zito zaidi la kumpa maarifa ya somo husika huyu mtoto ili aweze kuyatumia katika maisha yake.
Hivyo, nasisitiza, hii habari ya lugha mseto, ngazi ya msingi kwa Kiswahili na ngazi za juu kwa Kiingereza, haifai kwani inawanyima fursa ya kufaulu kwa sababu tu mitihani ipo kwenye lugha wasiyoifahamu.
Hapo tunapima uelewa au lugha? Umewahi kuingia darasani halafu unalijua jibu lakini siyo kwa Kiingereza, lugha ambayo ndiyo inatakiwa kujibia? Tuulizeni tuliopitia.
Upande mwingine, huu mfumo unawanyima wengi kupata ufahamu mzuri wa kuyaeelewa maarifa kwa kina hadi kuweza kuyatumia kwenye maisha.
Kwa msingi huo, si haki kabisa kumkosesha mtoto fursa katika miaka sahihi ya kujifunza lugha halafu umlazimishe aitumie kugha hiyo kujipatia maarifa yanayolenga kumuandaa kukabiliana na changamoto za maisha wakati huohuo ukimshindanisha na wengine waliopata faida kwa sababu tu wazazi wao wana pesa.
Hebu viongozi wajiweke kwenye nafasi ya wale maskini halafu wafikirie katika nafasi hiyo, kama hawana pesa ya kumpeleka mtoto shule ya Kiingereza ya binafsi, wangependa Serikali iwafanyie nini kuhusu sera ya lugha?
Njonjo Mfaume ni Mhadhiri wa Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa mrejesho, wasiliana naye kwa meseji kupitia +255 735 420 780 au mfuatilie Twitter kupitia @njonjoOKAY. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.