Katika makala hii tutaangazia watoto wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (VVU) kwa watoto walio katika umri wa kujitambua na kuweza kujihudumia na namna wazazi wanavyolichukulia suala hili katika harakati za kuwahudumia watoto wao.
Tunaposema watoto wenye umri wa kujitambua na kujihudumia tunamaanisha watoto wenye umri kuanzia miaka nane na kuendelea, kwani kuanzia umri wa miaka nane hadi umri wa miaka 12, watoto huanza kuelewa, kufikiri na kuona mantiki katika jambo, aghalabu kwa uchahe tu hasa katika mambo wanayoweza kuona au vitu wavyoweza kugusa.
Katika umri huu, watoto huwa na uwezo mkubwa wa kuona mitazamo, maoni na kuzingatia hisia za wengine.
Watoto huweza kupata maambukizi ya VVU kwa njia tofauti, ikiwemo kuambukizwa wakati wa kuzaliwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ambayo ni njia kuu kabisa kwa watoto, hasa wa umri mdogo kabisa.
Wengine huambukizwa kwa kuchangia vitu vyenye ncha kali na waathirika wa VVU kama vile nyembe, vipini na sindano, kugusa damu ya mtu aliyeathirika endapo atakuwa na mchubuko sehemu ya mwili wake, kuongezewa damu ya mtu aliyeathirika, au kwa kushiriki ngono bila kutumia kinga.
SOMA ZAIDI: Upi Ni Umri Sahihi Kwa Mtoto Kumiliki Simu ya Mkononi?
Tukisema kushiriki ngono wengi watajiuliza mtoto wa umri mdogo inawezekana vipi akashiriki ngono? Takwimu zinaonesha kuwa watoto wanaanza kujihusisha na ngono kabla hata ya kutimiza miaka 10.
Mtoto anapofikisha umri wa miaka 4-6 anatakiwa aanze kupewa taarifa kidogo kidogo juu ya hali yake ya maambukizi.
Anapofikia miaka 8-10 na anapoonekana ana uwezo wa kuelewa masuala mbalimbali ya maisha na uwezo wake wa kumudu masomo darasani umeimarika, mtoto huyo pia atakuwa na uwezo wa kuelewa masuala ya afya na jinsi kinga inavyofanya kazi mwilini, hivyo anaweza kupewa taarifa kamili kuhusu hali yake ya maambukizi ya VVU.
Ni jukumu la mzazi, au mlezi, kuhakikisha afya ya mtoto wake iko salama kwa kumpeleka katika kituo cha afya pale inapotokea mabadiliko ya kiafya na kuhakikisha mtoto anapata matibabu.
Katika kutekeleza jukumu hili, wazazi wengi wamekuwa na dhana potofu ya kuwaficha watoto hali yao ya kiafya baada ya kugundua watoto wameathirika.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Siku 1,000 za Mwanzo za Mtoto Ni Muhimu?
Kuna taratibu maalum za kuzingatia zinazotolewa na wataalamu wa afya baada ya kugundua mtoto, au mtu mzima, kaathirika na virusi vya UKIMWI kama vile kuhudhuria matibabu ya dawa za kupunguza makali ya virusi, kuhudhuria kiliniki kwa ajili ya uchunguzi wa mara kwa mara, kuhudhuria semina za ushauri nasaha na kuelimishwa namna ya kujikinga na maambukizi mapya.
Tunamuelezaje mtoto?
Ni muhimu mzazi, au mlezi, kwa kushirikiana na mtoa huduma kuandaa mpango wa namna ya kumueleza mtoto hali yake ya maambukizi ya VVU, kabla ya mtoto huyo kupata habari hiyo kutoka vyanzo vingine.
Kusikia habari kuhusu hali yake ya maambukizi kutoka kwa mtu mwingine kunaweza kumfanya mtoto ajisikie vibaya na atingwe na msongo wa mawazo na hata kupelekea kuchukua maamuzi yasiyofaa kama vile kujiua, kuacha shule, kuacha dawa, au hata kutokuwa na imani na wazazi wake. Ni vizuri kuongea na kumwambia mwanao mambo yanayomuhusu na kumfariji.
Mtoto aelezwe ukweli kuhusu afya yake huku akifundishwa namna ya kujikinga na kuwakinga wenzake. Mtie moyo wa kukubaliana na hali halisi ya mabadiliko ya kiafya yanayoweza kujitokeza mara kwa mara na namna ya kujihudumia.
Tujenge tabia ya kuamini watoto wetu kuwa wana uwezo mkubwa na wakipatiwa muongozo mzuri wanaweza kufanya makubwa kujilinda na kuwalinda watoto wenzao.
SOMA ZAIDI: Fahamu Kwa Nini Watoto Wachanga Hucheua
Wazazi, au walezi, wanapaswa kuzungumza na watoto wao juu ya ugonjwa huu kwa njia inayolingana na umri wao ili isiwatishe. Watoto wanahitaji kujua kwamba siyo kosa lao, wao ni wagonjwa na wanapaswa kumeza dawa kila siku.
Mzazi amtie moyo mwanae kuwa hayuko mwenyewe katika kukabiliana na ugonjwa huu. Msaada wa kijamii, kifedha, na kimhemko au kisaikolojia kwa familia nzima ni wa umuhimu pia.
Watoto wenye VVU na UKIMWI wanaweza kwenda shule salama. Ila wanaweza kukabiliwa na unyanyasaji na ubaguzi ikiwa wanafunzi wengine na walimu hawana uelewa mzuri wa jinsi VVU vinavyosambazwa.
Uhamasishaji na mipango ya elimu husaidia kuvunja unyanyapaa wa VVU ili watoto wawe na marafiki na kuhisi wanapendwa na wako sawa na watoto wengine.
Makala hizi za maelezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.