The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Watoto Wanaoangalia Sana TV Wanaweza Kuharibu Miundo ya Ubongo

Tafiti zinaonesha kwamba kutumia muda mwingi kwenye televisheni sehemu ya ubongo inayohusika na uelewa haikui bali husinyaa.

subscribe to our newsletter!

Kuangalia sana televisheni kunaweza kubadilisha muundo wa ubongo wa mtoto na hivyo kumletea madhara. Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Tohoku kilichopo katika jiji la Sendai, nchini Japan. 

Utafiti huu uligundua kuwa kadiri mtoto anavyotumia muda mwingi zaidi kuangalia televisheni ndivyo madhara ya mabadiliko kwenye ubongo wake yanavyozidi kuwa makubwa.

Watafiti hawa walifuatilia maisha ya watoto 276 wenye umri kati ya miaka mitano na 18, ambao huangalia televisheni kwa takribani masaa manne kwa siku, huku wastani wa jumla ya muda wanaotumia kwenye televisheni kwa pamoja ukifikia hadi masaa mawili kila mmoja wao.

Watafiti hao wanasema ukweli ni kwamba kuangalia televisheni ni tofauti na kujifunza vyombo vya muziki, kusoma vitabu, nakadhalika kwani uzoefu katika kuangalia televisheni hakuongezi ujuzi kama ilivyo kwa vitabu nakadhalika bali hufinyamiundo ya ubongo inayohusika na ufahamu. 

Kwa kutumia muda mwingi kwenye televisheni sehemu ya ubongo inayohusika na uelewa haikui bali husinyaa kwa kukosa changamoto mpya kwani televisheni hubakia kuwa ni jambo hilohilo na kuunyima ubongo kukua.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Ni Muhimu Mzazi Kumuomba Mtoto Wake Msamaha?

Kwa kumalizia, watafiti hawa wanaeleza kuwa kuangalia televisheni huhusishwa moja kwa moja na ukuaji na maendeleo ya sehemu ya ubongo wa mtoto inayohusika na ufahamu. 

Hivyo, wataalamu hawa wanashauri kwamba wazazi, au walezi, wanapaswa kuwa waangalifu na kuzingatia athari hizi katika muda wanaotenga kwa ajili ya watoto wao kuangalia televisheni.

Ingawa tafiti kama hizi haziwezi kutoa majibu ya moja kwa moja juu ya madhara na athari ya televisheni hapa kwetu Tanzania, – kijamii, kielimu na hata kidini – bado zina nafasi kubwa ya kutupa picha ya nini kinaendelea katika bongo za watoto wetu kwa kukaa kwenye televisheni muda mrefu. 

Kikubwa tunachokiona hapa ni kupangilia muda mtoto anaokaa kuangalia televisheni kwa siku. Muda kati ya saa moja hadi saa moja na nusu kwa siku unatosha kabisa kumpa mtoto ‘elimu’ kutoka katika vipindi vya televisheni kwa siku.

SOMA ZAIDI: Fahamu Kwa Nini Watoto Wachanga Hucheua

Mifano ipo ya watoto kushinda kutwa kwenye televisheni hasa wakati wa likizo ama wakiwa wametoka shule kila siku! Hii ni hatari kwani watoto, kama binadamu wengine, wanahitaji kujifunza kuhusiana na binadamu wenzao kupitia michezo, kuwatembelea marafiki na ndugu na kujuliana hali. 

Vinginevyo tutakuwa tunaandaa taifa la watu wasioujua ‘utu’ wala kuuthamini kwani hawakukuzwa kuishi na watu.

Kwa upande mwingine, ni muhimu pia kujibu swali la watoto huwa wanaangalia nini katika televisheni? Watoto katika umri mdogo sana wanaanza kuangalia mambo yasiyoendana na umri wao na yasiyo-maadili. 

Je, unajua kwamba unaweza kudhibiti na kupangilia mtoto wako anachoangalia kila siku kwenye televisheni? Visimbuzi vingi sasa vinakuja na mifumo ya kukusaidia mzazi kupanga nini mwanao aangalie hata kama haupo nyumbani. 

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Siku 1,000 za Mwanzo za Mtoto Ni Muhimu?

Hivyo, unawajibika kutenga muda kupangilia jambo hili kwani unaweza ukawa unampoteza mwanao bila wewe mwenyewe kujua kupitia vipindi potofu vinavyoonyeshwa kutwa katika televisheni wakati ukiwa kazini ama mihangaikoni.

Usiiache televisheni ikufundishie mwanao maadili kwani tafiti zinaonyesha kwamba televisheni ni mojawapo ya vitu vinavyochangia kwa kiasi kikubwa mmomonyoko wa maadili katika jamii zetu za leo kama hakuna uangalizi makini.

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts