Dar es Salaam. Pengine hakuna watu waliyoyapokea kwa mikono miwili mapendekezo ya tume ya Rais ya kuchunguza mfumo wa haki jinai nchini juu ya umuhimu wa kuharakisha kesi zilizopo mahakamani kama Watanzania ambao wanaoendelea kusumbuka na tatizo hilo, hali inayoathiri upatikanaji wa haki zao kwa wakati.
Tume hiyo, iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan mnamo Januari 6, 2023, chini ya uenyekiti wa Jaji (Mstaafu) Mohamed Othman Chande, iliwasilisha ripoti yake hapo Julai 15, 2023, ambapo, pamoja na mambo mengine, iliainisha malalamiko kuhusu ucheleweshaji wa mashauri kwenye Mahakama za nchi, ikipendekeza hali hiyo irekebishwe.
Kwenye taarifa yake, tume hiyo ilibaini kwamba kuna mashauri zaidi ya 1,000 ambayo yamefunguliwa na yanasubiri kusikilizwa kwenye Mahakama Kuu pekee, ikizitaka Mahakama na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuandaa mkakati wa pamoja wa kusikiliza mashauri ambayo upelelezi wake umekamilika.
Hili, bila shaka, ni pendekezo lililowakosha wengi, wakiwemo wafanyakazi wastaafu takriban 472 wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) ambao wamekuwa wakipigania haki yao ya kupata mafao yao stahiki kwa takriban miaka 14 baada ya Serikali kuwastaafisha kwa lazima kati ya mwaka 2005 na 2009 wakiwa na umri wa miaka 55.
Kesi ya muda mrefu
Serikali inadaiwa kuchukua hatua hiyo kwa madai kwamba haikuwa na uwezo wa kifedha wa kuendelea kuwa na wafanyakazi hao mpaka wafikie umri wao wa kustaafu kwa lazima ambao ni miaka 60 kisheria.
Ingawaje awali Serikali iliahidi kuwalipa wastaafu hawa mafao yao kwenye mwaka wa fedha wa 2015/2016, mnamo mwaka 2020 Serikali hiyo iligoma kufanya hivyo, ikisema madai hayo hayana msingi.
Kufuatia uamuzi huo, wastaafu hao walifungua shauri katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ambayo iliona madai yao ni ya msingi na kuamuru walipwe.
SOMA ZAIDI: Wakulima Wadogo 852 Mbarali Waiburuza Serikali Mahakamani Wakitetea Ardhi Yao
Hata hivyo, Serikali haikufurahishwa na uamuzi huu, ikiiomba Mahakama Kuu (Kitengo cha Kazi) iufanyie mapitio uamuzi huo wa CMA, ambapo iliamua kwamba siyo Mahakama Kuu wala CMA ina mamlaka ya kutoa uamuzi kuhusiana na suala hilo.
Kufuatia uamuzi huo wa Mahakama Kuu, wastaafu hao, wakiongozwa na Katibu wao, Ayasi Solano Mbonde, walikata rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa mnamo Septemba 13, 2022, wakiitaka Mahakama hiyo ya juu ya nchi itamke kama hakimu wa Mahakama Kuu alikosea kwenye kutoa uamuzi wake kwa kuwachanganya wastaafu hao na watumishi wa umma.
Lakini ni miezi sasa tangu shauri hilo liwasilishwe Mahakama ya Rufaa na bado wastaafu hao hawajaitwa kwa ajili ya usikilizwaji wa kesi yao hiyo, hali ambayo Mbonde ameiambia The Chanzo kwamba inampa hofu kwamba wastaafu wenzake wengi wanaweza kufa wakiwa wanasubiri kupata haki zao hizo.
Kesi ihimizwe
“Tungeomba hiyo kesi yetu ihimizwe, isikilizwe haraka ili tujue ni nini hatima yetu kwa sababu kuna wajane na sisi wenyewe ni wazee hatuelewi mpaka leo ni kitu gani [kinaendelea],” Mbonde, 68, aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano naye yaliyofanyika katika ofisi za chombo hicho cha habari, Msasani, Dar es Salaam.
“Tunajua hatutashindwa mahakamani na hatutafanyiwa uovu wowote mahakamani kwa sababu tunaiamini Mahakama yetu ni mhimili huru unaojitegemea,” aliongeza. “Lakini taratibu za kesi mahakamani kuchukua muda mrefu kunatufanya tufe wote, sijui nani tena awe msikilizaji huko mahakamani.”
SOMA ZAIDI: Wadau wa Ardhi Waitaka Serikali Kuheshimu Maamuzi ya Mahakama
Kwa mujibu wa rekodi walizonazo wastaafu hawa, mpaka hivi sasa kati ya wastaafu 1,172 waliostaafu kati ya mwaka 2005 na 2009, zaidi ya wastaafu 300 wamepoteza maisha kutokana na sababu mbalimbali bila ya kupata haki zao.
Kesi ya wastaafu hawa ni moja tu kati ya kesi nyingi zinazocheleweshwa mahakamani, hali ambayo imekuwa ikiwakera wananchi na wadau wengi wa haki nchini Tanzania, akiwemo Rais Samia mwenyewe ambaye mnamo Mei 17, 2021, alikemea tabia hiyo, akisema inaathiri mchakato mzima wa upatikanaji haki Tanzania.
“Tatizo la ucheleweshwaji wa kesi katika Mahakama zetu bado lipo sana,” alisema Rais Samia ambaye kampeni yake ya Mama Samia Legal Aid imepania kutatua changamoto kama hiyo.
“Kama mnavyosema wanasheria, haki inayocheleweshwa ndiyo haki inayokataliwa,” aliongeza Samia. “Hivyo, ni imani yangu kuwa baada ya upatikanaji wa majaji hawa ucheleweshaji wa kesi mahakamani utapungua na hatimaye haki kupatikana kwa wakati.”
Serikali kujilinda
The Chanzo ilimuuliza Harold Sungusia, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), tatizo la ucheleweshaji wa kesi mahakamani linaweza likawa linatokana na nini haswa, ambapo alijibu kulingana na kesi yenyewe, kama ni ya jinai au madai.
Mwanasheria huyu alibainisha kwamba ucheleweshaji kwenye kesi za jinai unatokana na sheria zilizopo nchini, hususan kwenye utambuzi wa makosa, uchunguzi wa makosa, uendeshaji wa mashtaka pamoja na changamoto za kimahakama.
SOMA ZAIDI: Safari Yangu ya Gerezani Bila Kupitia Polisi Wala Mahakamani
Hata hivyo, Sungusia anadhani tatizo lipo zaidi kwenye kesi za madai, hali anayoihusisha na uwepo wa sheria nyingi zinazosimamia masuala ya madai, masharti ya kiufundi, ukosefu wa maadili, pamoja na mfumo wa madai dhidi ya Serikali ambapo Serikali imejihakikishia kujilinda.
“Unaweza ukaangalia mfumo mzima wa madai dhidi ya Serikali ambao wenyewe una matatizo,” Sungusia, moja kati ya mawakili wanaoheshimika Tanzania, aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano. “Serikali imejilinda sana dhidi ya madai ambayo yanaweza yakaletwa dhidi yake.”
Iwe Serikali inajilinda au la, suala la wastaafu wa TAZARA kucheleweshewa malipo ya stahiki zao wamelilalamikia sana, wakisema limeendelea kuwaathiri siyo tu kiafya na kiustawi bali pia kisaikolojia na namna wanavyojichukulia wao kama wananchi.
Imetuharibia
“Imetuharibia mambo mengi kimaisha,” Solanus Cyprian Msongamwanja, mmoja kati ya wastaafu hao, anasema
“Watoto wetu hawakwenda shule na imesababisha kuchoka, imesababisha hata ndoa zetu kuvurugika,” anaongeza mzee huyo. “Imesababisha hata watoto wetu wasiendelee na masomo na [wastaafu] wengine kufa kwa magonjwa kwa sababu hawakuwa na uwezo wa kujitibu.”
SOMA ZAIDI: Mjane wa Katibu wa Zamani wa Bunge Anayepigania Haki Yake kwa Miaka 23
Suala la kesi kuchukua muda mrefu mahakamani siyo jambo pekee lililoibuliwa na tume hiyo ya Rais kuchunguza mfumo wa haki jinani nchini na kupendekeza njia za kuuboresha
Mambo mengine ni kama vile sheria kurekebishwa ili kuziruhusu mahakama kutoa dhamana kwenye makosa ya uhujumu uchumi na marekebisho ya sheria kuondoa mamlaka ya ukamataji waliyonayo wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na viongozi wengine kwa nafasi zao.
Mengine ni kuanzishwa kwa mamlaka mpya na huru ya upelelezi inayojitegemea itakayojulikana kama Ofisi ya Taifa ya Upelelezi (OTU); pendekezo kwamba kama adhabu ya kifo isiporidhiwa na Rais kwa kipindi cha miaka mitatu, adhabu hiyo itenguke kuwa kifungo cha maisha, kutaja mapendekezo hayo kwa uchache.
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Unaweza kumfikia kupitia lukelo@thechanzo.com.