Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan leo amemuapisha Balozi Iddi Ali Siwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, akichukua nafasi ya Said Hussein Massoro aliyeteuliwa kuwa Balozi.
Hii ikiwa ni takribani miezi nane toka Rais Samia amteue Said Massoro aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu na Mkurugenzi wa Shughuli za Ndani wa idara hiyo nyeti kuwa Mkurugenzi Mkuu Januari 3, 2023.
Balozi Siwa amekuwa mtumishi wa umma tangu mwaka 1977 na kati ya mwaka 2001 hadi 2014 aliweza kushika nafasi ya Afisa Mambo ya Nje Mkuu katika ofisi ya ubalozi wa Tanzania Abu Dhabi iliyopo nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu, Moscow nchini Urusi na baadaye Berlin nchini Ujerumani.
Mwaka 2014 Rais Jakaya Mrisho Kikwete alimteua kuwa balozi wa Tanzania nchini Rwanda, kipindi ambacho kulikuwa na mvutano mkali wa kidiplomasia kati ya Serikali ya Tanzania na Rwanda, hali iliyofikia mpaka kuwa na wasiwasi kwamba mvutano huu ungeweza kufikia pabaya.
Ni wakati huu, katika kipindi fulani, utayari wa kijeshi wa Tanzania uliwekwa katika hali ya juu, huku maneno mazito kutoka kwa viongozi waandamizi wa nchi hizo mbili yakitolewa katika vyombo vya habari.
Wakati Balozi Siwa akipokelewa na Rwanda Aprili 1, 2015, hii ni baada ya Rais wa Rwanda Paul Kagame kuchukua muda mrefu kumpokea kama balozi, Balozi Siwa alieleza kwamba, “uhusiano wa Tanzania na Rwanda ulipitia katika kipindi kigumu, lakini ni wakati wa kusahau yaliyopita na kuganga yajayo.”
Hali ya Rwanda na Tanzania iliendelea kuimarika, huku moja ya mafanikio makubwa chini ya Ubalozi wa Siwa ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kufungua ofisi zake nchini Rwanda, nchi ya tatu kutoa biashara nyingi zaidi kwa Tanzania, takribani tani milioni 1.4 zinaenda Rwanda kila mwaka.
Ni kawaida ya Tanzania kwa baadhi ya maeneo yanayozunguka mipaka ya Tanzania na maeneo ambayo yamekuwa na changamoto mbalimbali kama Rwanda, Burundi, DRC, Msumbiji, mabalozi wanaoteuliwa hutoka katika vyombo vya ulinzi na usalama. Machi 21, 2018, Rais John Magufuli alimteua Ernest Mangu kumrithi Balozi Siwa.
Balozi Siwa alivyorudi nyumbani baada ya kumaliza majukumu yake Septemba 20, 2018, aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), majukumu ambayo amekuwa akiyafanya mpaka alivyoteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Usalama leo Jumatatu, Agosti 28, 2023.
Wengine waliowahi kushika nyadhifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa ni Emilio Charles Mzena, Lawrence Gama, Hassy Kitine, Dkt. Agustine Mahiga, Luteni Jenerali Imrani Kombe, Apson Mwang’onda, Othman Rashid, Dkt. Modestus Kipilimba na Kamishina wa Polisi Diwani Athumani Msuya.
Mabadiliko yanamaanisha nini?
Mabadiliko haya yanakuja takribani miezi miwili toka Tanzania ifanye mabadiliko makubwa katika Sheria ya Idara ya Usalama wa Taifa mnamo Juni 8, 2023; sheria ambayo haikuwahi kufanyiwa marekebisho toka mwaka 1996.
Mabadiliko haya ya sheria yamefanya Idara ya Usalama wa Taifa kuripoti moja kwa moja kwa Rais, tofauti na hapo mwanzo ilipokuwa inaripoti kwa Waziri. Pia, sheria inaweka jukumu linalofanywa na idara hiyo katika kulinda viongozi rasmi kisheria na kuruhusu idara hiyo kushirikiana na vyombo vingine vya kijasusi vya kimataifa.
Sheria hiyo pia iliweka muundo mpya na kuweka kuwa kutakuwa na wakurugenzi wasaidizi wawili, mmoja kutoka Zanzibar na mwingine kutoka Tanzania Bara, pamoja na mabadiliko mengine.
Kuna namna mbili za kuangalia mabadiliko haya, moja ikiwa ni kuimarisha utendaji wa taasisi hii kulingana na mabadiliko ya sheria yaliyofanyika. Lakini pili ni Mamlaka ya Uteuzi kutaka kuona uelekeo fulani, ndani ya taasisi hiyo nyeti, na mamlaka hiyo yaani Rais, kuona namna pekee ya kufikia hapo ni kupitia kubadilisha uongozi.
18 Responses
Pamoja na mabadiliko ya sheria ya usalama wa Taifa, na kumfanya Mkurugenzi wake kuripoti moja kwa moja kwa Rais, bado sheria haijampa nguvu Mkurugenzi wa taasisi hiyo!
Kutokana na UNYETI wa idara hiyo, kulikuwa na haja, baada ya kuteuliwa kwa Mkurugenzi, ilipaswa ATHIBITISHWE na bunge, na baada ya hapo afanye kazi akiwa HURU! Na hivyo UTENGUZI wake pia URIDHIWE na bunge! Usalama wa Taifa wanatakiwa KUMPA TAARIFA, KUMSHAURI, KUMUONGOZA, KUANGALIA USALAMA wa Raisi na si Raisi kuwapa maelekezo juu ya mambo ya USALAMA WA NCHI!
Ukifuatilia hii panga pangua ya Wakurugenzi kwa muda mfupi, utagundua kuna tatizo katika mfumo mzima wa UTEUZI na UTEKELEZAJI wa MAJUKUMU ya Wakurugenzi wa idara hiyo nyeti kwa taifa letu! Hatuwezi kubadilisha Wakurugenzi wa TISS kama wakuu wa mikoa! Jambo hili si afya kwa usalama wa nchi yetu!
Tukiteua Mkurugenzi, tumuache afanye kazi yake, na si kumuelekeza cha kufanya! Tukumbuke kuwa viongozi wa kisiasa wa kitaifa huja na kuondoka, lakini suala la usalama wa nchi ni la kipekee! Idara isifanye kazi kutokana na mtazamo wa kiongozi aliyepo madarakani bali kwa kusimamia na kutekeleza malengo ya kuanzishwa kwake! Vinginevyo tutakuwa na Wakurugenzi wastaafu wa TISS kama wakuu wa mikoa wastaafu! Jambo ambalo halipo katika nchi nyingine!
✅✅✅✅ good say
Facts Sana mkuu Ishu ya ulinzi Wa Taifa ni ishu nyeti Sana na ni ishu ambayo Kila Nchi Duniani inahaha kutafuta fedha ili kuimarisha Ulinzi na usalama wa Taifa,Nchi yetu Kuna mahali viongozi wanahitaji kuwa makini hususani kwenye idara nyeti hii Kwa Sababu ndiyo Ina taarifa nyingiii kuhus usalama wa Taifa letu,So kubadilisha viongozi Kila baada ya muda italeta changamoto …. Nakubaliana na wazo lako
Makini hii
Binafsi nimpongeze na kumtakia Majukumu mema. Mh Balozi Siwa. Naimani pia katika jukumu jipya lilo ongezwa maboresho ya Katiba juu ya mashirikiano na Mashirika ya Kimataifa ya kijasusi. Kutimiza Sera yetu ya kigeni yaani( Tanzania foreign policy of 2021) na kutetea maslai ya Taifa. Katika kuchanganua mambo na kumshauri Mh.Rais
Hongera balozi idi Siwa nakutaka mafaniko mema ya kazi yako Kwani usalama ndio kiini Cha maendeleo Kwa ujumla
Kasome katiba yetu juu ya Mamlaka ya nchi na kiuongozi yanatoka kwa nani …ni wananchi kama ni hivyo kiongozi wa juu kulingana na katiba yetu imempa mamlaka ya kuwa amri jeshi mkuu wa Vyombo vya ulizni na usalama ikiwemo TISS , huo uhuru unaotaka utoke wapi ? Ukiruhusu haya kuna siku vichaa fulani watakutana na kufanya mapinduzi ya hovyo ..mfano Sudani Leo kinawaka kwa sababu inayofanana na maoni hapo juu
Bravo
Much Congratulations Balozi Siwa for your New Appointment
Habari nilikuwa ninashida ya nsada wa kuwa miongoni mwa mtumishi wa iyo idara
acheni upumbavu ninyi ivi mnafaham kwel swaala la ulinzi na usalama wa taifa hili upo mikononi mwa nani? rais ndiye mwenye jukumu la kuhakikisha taifa hili liko salama na yy ndie atakaelaumiwa endapo taifa hili litaingia pabaya kiusalama na wala sio mkurugenzi wa TISS . mwacheni rais afanye itakavyompendeza yeye juu ya usalama wa taifa hii . wapo viongozi waliowekewa kinga na ni muhimu sana watu hao kuwa na kinga mfano , Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali {CAG}. huyu mtu lazima awe huru ili aweze kutekereza majukumu yake .haiwezekani lawama apewe mwengine endapo jambo fulani litaharibika alaf utekelezaji wa jambo hilo apewe mtu tofaut na atakaebeba rawama hizo. huu ni upumbavu mkubwa sana. kila moja atumbue kua usalama wa taifa unawagusa watu wote waliopo kwenye taifa husika. hivyo basi kama munaona inafaa mkurugenzi wa TISS awe huru basi achaguliwe na wananchi .
Wachangiaji naomba tu mjue kuwa issue za masuala yahusuyo ULINZI na USALAMA haipashwi kufanyiwa Siasa au kuwa mada za kujadili mitandaoni kwani huko ni kutaka kuleta au kuchochea hoja za kumnyima mh Rais na Amiri jeshi Mkuu kutekeleza majukumu yake kikatiba.
ULINZI na USALAMA ni TAALUMA KAMILI sio kila mtu anaweza kufanya.Nashauri hii mada isiendelee Kwa uelekeo wa kuona Amiri Jeshi Mkuu anakosea.
Naomba kuwasilisha Kwa wahusika.
Sawaa
Nataka KAZI usalama wa Taiga plz
Taifa letu litadumishwa na sisi wenyewe mungu bariki viongozi wetu
Upo sawa ila muundo wake ni wa zamani za ukoloni hivyo lazima uripoti sehemu
Usalama
Wa taifa
Kafanya vyema kiongozi wetu