Dodoma. Jesca Makuya si mtu anayesahau haraka, hususan kama suala husika ni lile lililoumiza hisia zake. Mama huyu angekuwa na watoto watano isingekuwa kwa watu ambao mpaka wakati wa kuandika makala haya hawajatambulika kuuchukua uhai wa binti yake, Farida Makuya, binti wa miaka 16 aliyeuwawa kikatili mnamo Oktoba 4, 2022.
Mnamo Agosti 3, 2023, The Chanzo ilimtembelea Jesca, 45, nyumbani kwake Mtumba, jijini Dodoma, na kumkuta mama huyo mrefu, mwembamba akiwa jikoni kwake akisonga ugali, huku jua la saa nne asubuhi likionekana kuipa Mtumba, sasa maarufu kama Mji wa Serikali, ung’avu na uchangamfu.
Baada ya kumaliza kupika, Jesca, ambaye kifo cha binti yake kimemfanya aache shughuli iliyokuwa inamuingizia kipato ya kuuza pombe ya kienyeji, aliingia ndani mwake na kukaa kwenye kigoda, tayari kwa kusikiliza ni maswali gani nimepanga kumuuliza mara hii ikiwa ni mara ya pili tangu tukio hilo la kusikitisha liikumbe familia yake. Mara ya kwanza ilikuwa ni Juni 8, 2023.
Vipi kuhusu kesi ya mauaji ya binti yako, umepata taarifa za watuhumiwa kukamatwa? The Chanzo ilimuuliza mama huyu aliyekuwa anasikiliza kwa umakini ulioje. Hapo ilikuwa tayari ni miezi nane imepita tangu binti yake ashambuliwe akiwa nyumbani kwao na watu wasiojulikana.
Watu hao waliingia ndani, wakampiga binti huyo, halafu wakamtoa ndani kwa kumburuza, na kwenda kumtupa nyuma ya nyumba yao. Jesca ilibidi afuate alama za mburuzo kugundua binti yake ametupwa nyuma ya nyumba yao.
Damu zilikuwa zikimvuja sana binti huyo, na jitihada za kuokoa maisha yake ziligonga mwamba kwani alifariki akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
“Tangu muda mlipokuja [mara ya kwanza], sijajua nini kinaendelea,” alisema Jesca aliyeonesha dalili za kukata tamaa. “Hapa nasikia wameshikwa [watu], wametajana, lakini wenye hela zao wamejiwekea dhamana na wametoroka kesi zao, hawapo, mpaka sasa hivi wanawatafuta. Ombi langu kwa Serikali hilo suala walifanyie kazi.”
Jesca Makuya, mama aliyepoteza binti yake, Farida Makuya, akifuta machozi alipokuwa akisimulia namna alivyogundua kifo cha binti yake kwenye mahojiano na The Chanzo. PICHA | Jackline Kuwanda.
Mnamo Juni 21, 2023, Kamanda wa Polisi wa Dodoma, Martin Otieno, aliiambia The Chanzo kwamba watu wanne wanashikiliwa kwa kuhusika na mauaji hayo na kwamba kesi ilikuwa inaendelea mahakamani. Hata hivyo, Otieno hakutoa majina ya watu hao, wala kutaja Mahakama ambapo kesi hiyo ilikuwa inaendelea.
Jesca anasema kwamba mauaji ya kikatili ya binti yake yamemuachia maumivu makali ambayo hadhani kama anaweza kupona.
SOMA ZAIDI: Wanawake Wawili Wauwawa Kikatili Zanzibar. Familia, Wanaharakati Wataka Uwajibikaji
“Alikuwa darasa la saba, na alikuwa anatarajia kuingia kwenye mtihani kesho yake,” alieleza Jesca. “Mwanangu wamemkatisha ndoto zake. Sijui angekuja kuwa nani. Hata kama asingenisaidia mimi, angesaidia wadogo zake.”
Mauaji ya binti yake yamemjaza Jesca siyo majonzi tu bali hata woga. Mama huyu aliiambia The Chanzo kwamba kwa sasa hawezi kufanya kazi yoyote kwa kuhofia kwamba akiondoka watoto wake wengine watadhurika.
“Huo hapo ni udongo nimeurundika lakini nashindwa kutengeneza vyungu,” alisema mama huyo. “Nikitoka, watoto wangu nitawaacha na nani? Tunaomba Serikali kwa kweli itusaidie, [wahalifu] wakishashikiliwa wasiwe wanawaachia.”
Mauaji ya kikatili
Farida, binti yake Jesca, ni mmoja tu kati ya mabinti kadhaa waliouwawa kikatili wakati wimbi la mauaji hayo lilipoikumba Mtumba, moja kati ya kata 41 zinazounda Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kuanzia mwishoni mwa mwaka 2022.
Hakuna takwimu rasmi zinazoonesha idadi ya mabinti waliouwawa kwenye wimbi hilo. Hata hivyo, uchambuzi wa The Chanzo wa taarifa zilizokuwa zikiripoti mauaji hayo unaonesha kwamba mabinti kadhaa walipoteza maisha baada ya kushambuliwa, huku wengine wakikutwa na umauti baada ya kufanyiwa vitendo vingine vya ukatili, kama vile ubakaji.
Kwenye orodha hiyo yumo binti wa darasa la sita katika shule ya Msingi Mtumba ambaye alibakwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, kisha kukatwa mapanga na kutelekezwa akiwa hajitambui.
Machi 6, 2022, aliuawa Lyidia Mgogoro, 41, aliyeuwawa akiwa njiani kuelekea kazini majengo ya Mji wa Serikali. Agosti ya mwaka huo huo, tukio jingine la mkazi wa Mtumba liliripotiwa, likihusisha binti aliyekatwa mapanga na vijana wawili hadi kufa.
Sarah Njani ni mkazi wa Mtumba ambaye yeye na wenzake walinusurika kudhuriwa na watu hao, ambao ni vijana wakiume, baada ya kijana kuwavamia na kutaka kumbaka mmoja wao, lakini alilazimika kukimbia baada ya watu kuja kufuatia kelele za akina mama hao.
Sarah Njani ni mkazi wa Mtumba ambaye anasema alinusurika kubakwa baada ya kupiga kelele zilizoita watu na kumkimbiza kijana aliyetaka kuwadhuru. PICHA | Jackline Kuwanda.
Mama huyo wa mtoto mmoja aliiambia The Chanzo Juni mwaka huu kwamba tukio hilo lilitokea Aprili 4, 2022, majira ya saa saba walipokuwa shambani kuvuna karanga ambapo kijana huyo alitokea akiwa na nia ya kutaka kuwadhuru.
“Wanakujeruhi tu, hata ukiwa na simu na hela huwa hawana shida nayo, wanakujeruhi tu basi wanakuacha,” Sarah, 45, aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano hayo. “Hatuna amani sasa hivi, hata kukata kuni porini tunashindwa.”
Usalama waimarika
The Chanzo ilipotembelea Mtumba mapema mwezi Agosti mwaka huu, wananchi wengi walielezea kuimarika kwa hali ya usalama, japo upo woga miongoni mwa wanawake, hususani wa kuwa nje ya makazi yao baada ya saa mbili usiku.
Tiliza Adrea ni mkazi wa Mtumba ambaye licha ya kukiri kutokuwepo kwa ripoti za wanawake kuuwawa na kufanyiwa vitendo vya kikatili kwa siku za hivi karibuni, mama huyo wa mtoto mmoja anabainisha kwamba wanawake kijijini hapo hawako salama kiasi cha kufanya shughuli zao kwa uhuru.
SOMA ZAIDI: Watoto 1,173, Wanawake 185, Wanaume 3 Wafanyiwa Ukatili Zanzibar 2022
“Hata saa nyingine nyumbani unalala na haulali usingizi,” Tiliza, 47, aliiambia The Chanzo. “Unalala unawaza kama kuna mtu atakuja kukugongea na kukufanya kitu kibaya, licha ya kwamba hakuna kitu kama hicho kilichotokea kwa siku za hivi karibuni.”
Francis Felix ni Mtendaji wa Kata ya Mtumba ambaye ameihusisha hali ya utulivu inayoripotiwa na wananchi wake na hatua ambazo mamlaka za nchi zimechukua kuidhibiti hali hiyo, ikiwemo kukamatwa kwa watu kadhaa wanaohusishwa na vitendo hivyo.
Kwenye mahojiano yake kwa njia ya simu na The Chanzo hapo Agosti 10, 2023, Felix alibainisha kwamba ofisi yake mara kadhaa imepokea wageni kutoka vyombo vya ulinzi na usalama vikiomba ushirikiano wake kwenye kuwasaka na kuwatia mbaroni wale wote waliokuwa wakihatarisha hali ya usalama kwenye eneo la Mtumba.
“Walikuwa wanawafuatilia [hawa washukiwa] kwenye simu kwa kukamata mawasiliano yao,” Felix anasema. “Wengine waliwapeleleza watu kwenye pombe walikuwa wanawasikia wakizungumza. Unakuta mtu anaweza akaropoka amezungumza kitu amemtaja mtu bila kujua basi wanawakamata. Walikuwa wanafanya kazi kwa umakini sana.”
Licha ya uwepo wa taarifa hizi za washukiwa kukamatwa, The Chanzo imeshindwa kuthibitisha kwamba kweli watu waliokuwa wanahusika na matukio hayo ya kihalifu wamefikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Baada ya Kamanda Otieno kushindwa kutupatia majina ya watu wanaoshikiliwa kwa kuhusika na uhalifu huo, mnamo Juni 22, 2023, The Chanzo iliitafuta Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka kuuliza kama ina taarifa zozote za watuhumiwa wa mauaji ya Mtumba kufikishwa mahakamani, ikijibu haina taarifa hizo.
Hofu
Kuna hofu miongoni mwa wadau wanaopinga ukatili wa kijinsia kwamba endapo kama washukiwa wa matukio haya watakuwa hawafikishwi mbele ya vyombo vya sheria na haki kutendeka, juhudi za kukomesha aina hiyo ya uhalifu zitashindwa kuzaa matunda yanayokusudiwa.
Hofu hii inatokana na ukweli kwamba nchini Tanzania matukio ya ukatili wa kijinsia, hususan yale yanayowalenga wanawake, yameripotiwa kushamiri kwa siku za hivi karibuni kama ambavyo ripoti mbalimbali zimekuwa zikionyesha mara kwa mara.
Kwa mfano, ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2022 iliyopewa jina la Tathmini ya Ukatili wa Kijinsia Tanzania ilionesha kwamba asilimia 40 ya wanawake wote chini Tanzania walio na umri kati ya miaka 15 na 49 waliripoti kuwahi kufanyiwa ukatili wa kimwili katika maisha yao.
Licha ya tatizo kuwa na ukubwa huo, ripoti hiyo inaonesha kwamba ni mashauri machache sana ya ukatili wa kijinsia ndiyo hufikishwa mahakamani, hali iliyohusishwa na kukosekana kwa ushahidi, kushindwa kukusanya au kuhifadhi ushahidi wa tukio, uchunguzi mbovu, au rushwa.
Anna Henga ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ambacho kwenye ripoti zake za kila mwaka za haki za binadamu kimekuwa kikibainisha tatizo la ukatili wa kijinsia chini, amekiri kwamba upo uhusiano kati ya kesi hizi kutowajibishwa na kushamiri kwake.
Hali hii imewasukuma wadau, wakiwemo LHRC wenyewe, kupendekeza hatua madhubuti kuchukuliwa dhidi ya wale wote wanaothibitika kujihusisha na ukatili wa kijinsia, wakienda mbali zaidi na kutaka sheria mahususi itungwe ili kuonesha umakini kwenye kukabiliana na janga hilo.
SOMA ZAIDI: Ulawiti Unavyowajaza Hofu Wazazi Kuhusu Hatma ya Watoto wa Kiume Tanzania
“Kwa takwimu zetu za ukatili wa kijinsia, [waathirika] namba moja ni watoto na namba mbili ni wanawake,” Henga ameiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalumu. “Tunahitaji Sheria ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia kuonesha umakini wa kukabiliana na madhila haya.”
Haki itendeke
Lakini wakati wadau wakisubiri sheria hiyo mahususi itungwe, Jesca ameendelea kuisihi Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama kuhakisha kwamba watu wanaoshukiwa kujihusisha na ukatili wa kijinsia wanafikishwa mbele ya vyombo vya sheria, na wakithibitika hatua stahiki zichukuliwe.
Mama huyu anadhani suala kubwa linalofanya washukiwa wa vitendo hivyo kutowajibishwa ni uwepo wa rusha, akitoa wito kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuingilia kati kuhakikisha kwamba haki inatendeka.
“Serikali itusaidie, habari ya rushwa waache, [watu] wanatoa hela, wanatolewa. Wakishatolewa, wanakuja kuendelea na tabia zao,” alishauri Jesca.
“Hapa tunasema kwamba wametulia, lakini bado watakuja kuendelea,” alitahadharisha mama huyo. “Wanataka kupoe baadaye wanaendelea. Kwa sababu wanawaachia na wanapokea hela. Tunaomba Serikali iangalie habari ya rushwa, sisi tunaangamia.”
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.