Utakubaliana na sisi kwamba kauli “natamani sana kupata mtoto” ni moja ya kauli ambazo hutamkwa sana na wale wenye matarajio ya kuwa wazazi au wanandoa wanaohitaji kupata watoto. Tunaamini watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu ambayo haiwezi kulinganishwa na kitu chochote.
Mara nyingi mambo hubadilika kwa baadhi ya wazazi pale wanapobahatika kupata watoto. Yaliyokuwa matamanio sasa huwa uhalisia na watoto huja na mahitaji mbalimbali, ikiwemo gharama za hospitali, chakula, malazi, mavazi, shule, nakadhalika.
Pamoja na yote haya, watoto wanabeba vipaji vingi ndani yao ambavyo vikipaliliwa vyema vitakuwa chachu ya maendeleo kwa jamii na taifa kwa ujumla. Zipo njia lukuki unazoweza kuzitumia kumjengea mwanao mazingira ya kuwa mtu katika jamii.
Maneno ya wazazi kwa watoto yana nguvu sana katika kuwawezesha watoto kufikia malengo yao katika maisha; vilevile yana mchango mkubwa sana kudidimiza vipaji vya watoto.
SOMA ZAIDI: Mahusiano Mazuri ya Wazazi ni Muhimu Katika Malezi ya Watoto
Maneno yanajenga taswira na matarajio, yanajenga na kukuza saikolojia na hivyo kushawishi namna tunavyofikiri, na mara nyingi maneno pia huathiri matendo tunayofanya, hasa namna tunavyofanya matendo hayo.
Maneno tunavyowaambia watoto na mara nyingine kwa kejeli na hasa kuwatukana huathiri sana maisha yao wanapokuwa watu wazima. Mathalani, ni kawaida kusikia watoto wakiambiwa we mpumbavu; mwizi mkubwa wewe; jinga halina akili; kichwa maji; na maneno mengine mengi ya aina hiyo.
Maneno ya namna hii humuathiri sana mtoto hata kumfanya mtoto asijiamini na kudumaza uwezo wake wa kufikiri na kudadisi. Mtoto kama huyu ni mwoga kuuliza au kujibu maswali anapokuwa darasani, kwani huingiwa na hofu ya kuonekana mjinga na pengine kuchekwa kutokana na maneno aliyoambiwa mara kwa mara kuwa hana akili.
Ni sahihi kusema kwamba watoto wengi, na hata watu wazima wa leo, wamekuwa vile walivyo, pamoja na mchango wa mambo mengine, kutokana na mchango wa maneno ya wazazi au walezi wao.
SOMA ZAIDI: Shule ya Kwanza ya Mtoto ni Nyumbani
Waswahili wanasema, maneno huumba! Fursa ya kujenga mtu makini unaipata punde unapopata mtoto. Mtoto huyo anahitaji kutiwa moyo na kuongozwa ili afikie kilele cha ubora katika kipaji alichotunukiwa na Mungu!
Bado wazazi wengi wanawapa watoto wao majina ya kejeli kutokana na wanavyofaulu darasani kwa mfano. Majina mazuri kwa watoto wanaofanya vizuri na majina ya hovyo kwa wale wanaofeli.
Tunaamini kuwa mchango wako ni muhimu katika kumwinua mtoto anayefeli darasani. Je, unazijua changamoto zake? Mara ngapi unazungumza naye na kuzitatua? Ama unampachika majina ya kukatisha tamaa ili adidimie kabisa maishani au masomoni?
Msikilize mtoto wako, mhimize kutia nia na mwambie mara zote kuwa inawezekana. Utambadilisha na atakushangaza kwa atakavyobadilika. Ndugu mzazi, mlezi na jamii kwa ujumla, hatuna budi kuwa makini sana tunapoongea na watoto, na mtoto anapokosea tutumie busara tunapowaonya hasa kwa maneno dhidi ya makosa yao.
SOMA ZAIDI: Namna Sita Mzazi Anavyoweza Kuhakikisha Malezi Bora Kwa Mtoto
Pia, kumekuwepo na tabia nyingine ya watoto kuitwa majina yasiyo yao, bila shaka umeshasikia watoto wakiitwa baadhi ya majina ya vitu au wanyama hasa watoto hao wanapokuwa wamekosea, wa mfano, mbwa wewe na mengine mengi.
Tabia hii ya baadhi ya wazazi kuwafananisha watoto wao na vitu au wanyama, si tu inawaathiri watoto kisaikolojia na kuharibu uwezo wao wa kujifunza na kukuza vipaji vyao, pia ni aina mojawapo ya unyanyasaji wa watoto hao ujulikanao kitaalamu kama ukatili wa kihisia, au emotional violence kwa kimombo.
Kama wazazi, walezi, walimu na jamii nzima, hatuna budi kuelewa kuwa watoto wanahitaji kuelekezwa na kufundishwa kwa umakini na uangalifu.
Hata wanapokosea, wazazi hawanabudi kuwaonya kwa kuwaeleza makosa yao, ubaya wa kosa na madhara ya makosa hayo bila kuwatupia maneno mabaya yatakayowaathiri zaidi kwenye maisha yao ya baadaye.
Tunasisitiza kuwatia moyo watoto na kuwafundisha wanachopaswa kufanya na faida zake, hali itakayowaandaa kujiamini na hivyo kukuza vipaji mbalimbali walivyonavyo vitakavyoleta maendeleo yenye tija katika familia, jamii, na taifa kwa ujumla.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.