The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Shule ya Kwanza ya Mtoto ni Nyumbani

Mzazi yuko na mtoto nyumbani kila uchao, hivyo badala ya kutumia muda mwingi kutoa ‘maelekezo ya tabia njema,’ ishi kwa mfano.

subscribe to our newsletter!

Utakubaliana nasi kuwa shule ya kwanza katika maisha ya mtoto ni nyumbani – wazazi, ndugu wa familia tandaa, majirani na marafiki wa familia husika. Kupitia mzazi au mlezi mtoto anapata nyenzo zitakazoongoza maisha yake yote – heshima, utii, unyenyekevu nakadhalika. Yaani wema au ubaya wa mtu mara nyingi ni matokeo ya aliyojifunza nyumbani.

Nyumbani ndiko msingi hujengwa. Bahati nzuri, ‘ualimu’ wa nyumbani unatokana na matendo zaidi ya maneno. Mtoto uko naye kila uchao hivyo badala ya kutumia muda mwingi kutoa ‘maelekezo ya tabia njema,’ ishi kwa mfano.

Unamwambia mtoto sala na ibada ni muhimu katika maisha – wewe unasali? Je, unahudhuria pamoja naye katika ibada? Kupitia maisha unayoishi utamjengea mtoto misingi ya kiakili na kiimani ili kama ilivyo kwa chakula bora awe na uwiano sawia katika maisha.

SOMA ZAIDI: Namna Sita Mzazi Anavyoweza Kuhakikisha Malezi Bora Kwa Mtoto

Mtoto anapotoka tumboni mwa mama huwa na kurasa zilizo wazi pasi na tabia za aina iwayo-yote. Isipokuwa kwa vipaji na tabia za kurithi – mzazi, au mlezi, wewe unalo jukumu la kuunda tabia na kukuza vipaji vya mtoto.

Ukiwa kama mwalimu wa kwanza wa mtoto – mwandae kwa ajili ya elimu ya shule, awali, msingi, sekondari, nakadhalika. Bahati mbaya wazazi au walezi wengi huingia katika shughuli hii wakiwa ndiyo kwanza bado vijana. Lugha za ujana na misemo iliyo mingi huwa bado inazo chembe za utovu wa nidhamu. Ukiwa mzazi – mtoto anakusikia, anakuiga. Chagua maneno.

Umoja wa wazazi au walezi ni muhimu sana. Baba na mama wawe wamoja katika kulea. Pale inapotokea tofauti baina yao kuhusu namna ya kutoa maelekezo kwa mtoto – basi na wasibishane mbele za mtoto.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Ni Muhimu Kumjengea Mtoto Tabia ya Kujitegemea Mapema

Ikiwa, kwa mfano, mama anamwadhibu mtoto na baba hakubaliani na adhabu inayotolewa – muombe mama faraghani na mzungumze juu ya hili. Ukomavu wa namna hii utasaidia kutomchanganya mtoto na jumbe zinazokinzana.

Kamwe msikwaruzane mbele za watoto. Tofauti zenu zivumiliwe mpaka mpatapo faragha mbali na watoto.

Elimu ianze umri gani hasa? Elimu inaanza akiwa tumboni – kupitia mazungumzo ya mama, mtoto anaandaliwa kuzijua sauti za watu wake wa karibu kama baba, mashangazi nakadhalika. Hii inakwambia kwamba malezi yanaanza mara tu uwapo mjamzito.

Punguza maugomvi yasiyo-lazima na ikiwezekana jenga mazingira rafiki kwa kuwa mwenye furaha wakati mwingi. Mara tu unapomtia mikononi mwako kichanga wako – anza kumsemesha. Elimu ya lugha unayotumia ndiyo lugha atakayoanza kuifahamu kichanga wako. Jenga msamiati wenye lugha za staha ili mtoto naye ajifunze hivyo.

SOMA ZAIDI: Watoto Wanaoangalia Sana TV Wanaweza Kuharibu Miundo ya Ubongo

Jifunze miongozo ya malezi. Sote tunafahamu kuwa malezi hayana shule eti ukajifunze upate kujua mbivu na mbichi. Nyakati nazo zimebadilika na watu hasa waishio mijini hawakai pamoja na familia tandaa. Hii inamnyima mzazi mpya fursa ya kupata maelekezo ya namna bora ya kulea toka kwa mama au baba yake yeye mwenyewe.

Pamoja na changamoto hizi, zipo fursa za kujielimisha kupitia vitabu, majarida, na makala mfano kama haya unayosoma muda huu. Fursa nyingine adhimu ni mtandao wa intaneti wenye maandiko ya kitaalamu na kutoka kwa wazazi wa matabaka, makabila na lugha mbalimbali kote ulimwenguni.

Jisomeshe!

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *