Ni kitu cha kawaida kama mzazi au mlezi kushuhudia watoto, hasa wale waliofuatana, wakigombana mara kwa mara na wakati mwingine hata kupigana au kufanyiana vitendo vya kukomoana.
Hali hii ni ya kawaida lakini huwapa wazazi wakati mgumu sana hasa pale watoto wanaposhindwa kukaa kwa amani, na mzazi hujikuta akiwa msuluhishaji muda wote.
Wengi wetu tunaweza kukumbuka matukio mbalimbali ya kugombana na ndugu zetu pindi tulivyokuwa watoto na mambo gani wazazi wetu waliyokua wanatueleza. Watoto wana uwezo wa kukusoma na kutumia udhaifu wako mzazi kwenye jambo fulani kama mwanya wa kuwaonea wenzao.
Kama una watoto wawili au zaidi, ingawa wote ni wanao, mara nyingi kuna mmoja au wawili wanaokuwa karibu na wewe zaidi ya wengine na wakisema kitu unakichukulia hatua. Basi watoto wako wengine wanakua wanajua kuwa mama au baba “anamsikiliza na kumjali fulani zaidi yetu.”
Hii ni hali ya kawaida kwa watoto wanapokua wakitafuta utambulisho wao, ila mzazi unapaswa ujitahidi kuuziba mwanya huo.
SOMA ZAIDI: Ifahamu Nguvu ya Maneno ya Mzazi, Mlezi Katika Vipaji vya Mtoto
Mara nyingine, mzazi hujikuta akiegemea na kumtetea mtoto mmoja, huku akiona kwamba mwenzake ndiye mkorofi. Pengine kumbandika mtoto majina kama ‘mtundu’ au ‘mkorofi’ bila kujua kuwa kumuita majina hayo, kunampa nafasi ya kuwa mkorofi zaidi.
Inawezekana kuwa yeye huwa siyo mwanzilishi wa kila ugomvi na hana namna ya kujitetea kwa kuwa imeshajulikana kuwa yeye siku zote ni mkorofi.
Hivyo basi, kama mzazi au mlezi, epuka kuwa muamuzi wa mashitaka yao kila wakikwaruzana; epuka kumpa mtoto jina kutokana na tabia yake; na epuka kupendelea upande mmoja zaidi maana wote wanastahili kupendwa, kusikilizwa na kuthaminiwa.
Pia tufahamu kuwa, ugomvi wa mara kwa mara huwaathiri watoto kisaikolojia, hasa wale wanaokuwa wanyonge kwa wenzao. Huwaathiri kimasomo, huathiri mahusiano yao na wengine, huwafanya wasijiamini na kuwa na hisia kuwa wao ni wakosaji kila mara.
Ugomvi ukizidi sana, huweza kupelekea msongo wa mawazo, hali ambayo inaweza kumsababisha mtoto kujidhuru, kukimbia nyumbani ama kutaka kwenda kuishi na ndugu mwingine wa karibu.
SOMA ZAIDI: Mahusiano Mazuri ya Wazazi ni Muhimu Katika Malezi ya Watoto
Pale watoto wakigombana au kufarakana, jitahidi kujiwekea mfumo mzuri wa kusuluhisha mashtaka kwa haki bila kupendelea upande mmoja. Jaribu kuwaachia wenyewe wasuluhishane kwa usimamizi wako pasipo kuwahukumu.
Unaweza kuwakalisha chini na kuwasikiliza na kisha kuwauliza, “Je, kama wewe ungefanyiwa hivyo, ungejisikiaje?” Au, “Ni namna gani ungependa kushirikiana na mwenzio?” na kuwasistizia waombane msamaha pasipo kujali nani mwenye kosa.
Unaweza pia kuweka sheria kuwa kila wakizozana wanapata adhabu wote kama kuosha vyombo, kutokuangalia televisheni, kufagia uwanja au adhabu nyingine kulingana na uwezo, uelewa na umri wao.
Ni muhimu sana kuwajengea watoto umoja; waeleze umuhimu wa undugu na kuishi kwa amani, waeleze namna unavyojisikia pale wanapopigana na kuzozana kila mara na uwaambie namna unavyofurahi wakicheza pamoja kama ndugu.
SOMA ZAIDI: Shule ya Kwanza ya Mtoto ni Nyumbani
Wafundishe watoto kuombana msamaha kwa mifano, ukiwakosea waombe msamaha na wao watakuiga wakikukosea au wakikoseana. Si rahisi ila ni fundisho jema litakaowajenga kuwa watu wazima bora siku za usoni.
Mwisho, kumbuka kuwa haya mafundisho hayatatekelezwa haraka; yatachukua muda ila yatabaki akilini mwao. Siku zote watakua wakijua kuwa wanapaswa kuishi kwa amani na upendo.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.