Unaweza kusema kwamba mchakato wa kuandika Katiba Mpya Tanzania umegubikwa na lugha gongana, au talking past each other kama wanavyosema Waingereza. Yaani, mnadhani mnazungumza jambo moja, kumbe mantiki hazishabihiani kabisa.
Vyama vyote vya siasa vimesema vinaitaka Katiba Mpya. Lugha gongana ipo kwenye safari ya kuipata. Kila upande una picha ya peke yake kuanzia jinsi ya kuanza mchakato husika hadi maudhui ya nyaraka hiyo muhimu.
Vyama vya siasa vinatazamana jicho kwa jicho, havisikilizani sikio kwa sikio. Hotuba za wanasiasa zinadhihirisha kuwa Katiba ni muhimu zaidi kwa ajili ya uchaguzi.
Vyama vya upinzani vinaamini Katiba nzuri, itakayotambulisha Tume Huru ya Uchaguzi, itaviwezesha kukiondoa chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM) madarakani. Taswira yoyote ya kukawiza mchakato, wanaitafsiri kuwa hila ya chama hicho kutaka kuendelea kubaki madarakani.
Mnamo Juni 22, 2022, Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), ilitoa tamko kutaka mchakato wa Katiba Mpya ufufuliwe haraka iwezekenavyo, ikisema kufanya hivyo ni kuweka mbele maslahi mapana ya kitaifa.
Tangu wakati huo, hata hivyo, maswali yamekuwa mengi kuhusu dhamira ya chama hicho. Je, ni kweli wanahitaji Katiba Mpya au walitoa tamko kupunguza joto? Awali ilionekana CCM hawakuwa radhi kwa mchakato wa Katiba Mpya.
SOMA ZAIDI: Mchakato wa Katiba Mpya Tanzania: Yajayo Yanafurahisha
Upande wa pili, yaani vyama vya upinzani na wanaharakati, walikuwa wakisukuma madai ya Katiba Mpya kwa shinikizo kubwa. Ndiyo sababu inadhaniwa CCM walikubali mchakato kupoza joto.
Sasa weka makundi matatu ya wanaotaka Katiba Mpya: wanasiasa na matakwa ya kisiasa; Wazanzibari wanaotamani Katiba bora itakayoondoa kile wanachokiona ni ukandamizwaji na unyonywaji; na Watanzania wanaotaka Tanzania iwe na misingi bora ya kuishi kwa kila Mtanzania.
Kisha mlete kwenye muktadha aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro, aliyesema mchakato wa Katiba unaanza mwezi huu wa Septemba 2023 kwa utoaji wa elimu ya Katiba kwa miaka mitatu, akisema kwamba asilimia 50 ya Watanzania hawaijui Katiba iliyopo, ile ya mwaka 1977.
Nia ovu
Namleta Askofu Nelson Kisare wa Kanisa la Mennonite Tanzania. Mnamo Agosti 10, 2023, katika mkutano wa Jukwaa la Katiba na wadau wa Katiba, ambao nilipata fursa ya kushiriki, Askofu Kisare alisema jambo muhimu kuhusu Katiba ni nia. Kama nia ni ovu, mivutano itatawala.
Katika mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya Seychelles, Dar es Salaam, Askofu Kisare alitolea mfano ujenzi wa Mnara wa Babeli ambapo zoezi hilo lilishindwa kufanikiwa baada ya Mungu, kwa kuona lengo lilikuwa ni kuufikisha mbinguni, aliwavuruga waliokuwa wanaujenga na hivyo hawakufanikiwa.
Mnara wa Babeli ni simulizi kwenye Kitabu cha Mwanzo 11 kwenye Bibilia ambapo Mungu anawafanya binadamu wasizungumze lugha moja ili wasielewane katika dhamira yao ya kuunda jengo la kufika mbinguni.
SOMA ZAIDI: Othman Masoud Ataka Haya Yazingatiwe Kwenye Mchakato wa Katiba Mpya
Katiba ni msahafu wa nchi; ni nyaraka ya mwafaka wa mtindo wa maisha katika nchi. Kwa tafsiri hiyo, hakuna kitu kinapaswa kuwaweka Watanzania pamoja na kwa maelewano makubwa kama Katiba.
Kwa nini sasa Katiba haifanyi Watanzania wazungumze lugha moja? Jawabu lipo kwenye hekima za Askofu Kisare. Nia si kuifanya Tanzania kuwa na mazingira bora ya kuishi, bali kuna kona na mianya ya kisiasa vinatafutwa. Mungu hawezi kubariki!
Safari ya Katiba Mpya
Januari 2023, Kikosi Kazi cha Kuratibu Maoni ya Demokrasia, kilikabidhi ripoti kwa Rais Samia Suluhu Hassan. Ukisoma ripoti hiyo mstari kwa mstari, utabaini kuwa zaidi ya asilimia 90 ya mapendekezo yao yalitaka mabadiliko ya Katiba, japo walitumia lugha ya kuzunguka.
Mwaka 1992, Tanzania ilirejea kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa, Katiba haikuandikwa upya, isipokuwa ilifanyiwa marekebisho machache. Desemba 18, 2010, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, aliahidi bungeni kuanzisha mchakato wa Katiba.
Ahadi ya Kikwete ilikuwa jibu la kilio cha muda mrefu kuhusu nchi kupata Katiba Mpya. Alitimiza ahadi, mchakato ulianza. Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitekeleza wajibu wake. Disemba 2013, tume ilikabidhi rasimu kwa Kikwete.
SOMA ZAIDI: Hatua Tano Muhimu Kufikia Upatikanaji wa Katiba Mpya Tanzania
Kisha, mchakato ukavurugika kwenye Bunge la Katiba mwaka 2014. Kwa mantiki hiyo, Watanzania walishiriki mchakato, shida ikaletwa na siasa. Hila na majaribio ya wanasiasa kuingiza konakona kwenye Katiba, ikawa sababu ya mvurugiko.
Akiandika kwenye dibaji ya kitabu A Practical Guide to Constitution Building, au Muongozo Kivitendo Ujezi wa Katiba kwa Kiswahili cha mwaka 2011, Rais wa Pili wa Mauritius, Cassam Uteem, alisema kwamba neno ukatiba, au constitutionalism kwa kimombo, linaweza kutafsiriwa na maneno machache ambayo ni “ukomo wa mamlaka.”
Kwa kuchukua tafsiri ya Rais Uteem, aliyeiongoza Mauritius kwa miaka 10, kuanzia mwaka 1992 mpaka 2002, unapata jawabu kwamba nchi inaweza kwenda vizuri kwa kuwa na ukatiba. Yaani kutambua na kuheshimu haki, wajibu na mipaka kutoka mtu mmoja hadi mwingine.
Ukatiba
Ukatiba ukiwaingia wanasiasa vema, watabaini kuwa Katiba ni ya nchi, kwa hiyo wajibu mkuu ni kuweka mazingira sawa kwa wananchi wote. Si kutoa upendeleo kwa kikundi au jamii fulani.
Ukatiba ni kufahamu kuwa Katiba ni nyaraka inayofaa kuongoza nchi vizuri kwa miongo mingi mbele kama si karne kadhaa zijazo. Uelewa huo ungekuwa wa pamoja kwa taifa zima, Katiba isingekuwa inagawa watu, bali ingewaunganisha zaidi.
Ubinafsi na hila za kujipendelea kisiasa ndiyo tatizo kuu. Hayo yasipopatiwa tiba, Katiba itaendelea kuwa na michakato yenye kuahirishwa vipindi baada ya vipindi.
SOMA ZAIDI: Jaji Mathew Mwaimu: Tanzania Kuwa na Katiba Mpya ni Jambo Jema
Mnamo karne ya 17, Uingereza iliweka rekodi ya kuwa nchi ya kwanza duniani kuwa na Katiba. Hata hivyo, Katiba yao si ya maandishi, huitwa Katiba ya Kimila. Mataifa ya Israel na New Zealand, nayo pia Katiba zao ni za kimila.
Kwa Uingereza, pale Mfalme au Malkia anapozindua Bunge ndiyo Katiba. Kisha, Bunge hutumia taji la ufalme kutunga sheria ambazo huziongoza nchi. Pamoja na mazingira hayo, huoni Uingereza ikiwa na matatizo ya kikatiba. Ni kwa sababu wana kiwango kizuri cha ukatiba.
Mnamo Julai 4, 1776, Marekani walijitangazia uhuru. Baada ya hapo, waasisi wa taifa hilo, kabla ya kuvamia madaraka, walianza kuandika Katiba yao, kwa ajili ya kuvifaa vizazi vingi baada yao.
Mwaka 1789, ndipo Katiba ya Marekani ilikamilika. Sababu ni moja: waasisi wa Marekani walikuwa na kiwango cha juu cha ukatiba.
Hapa kwetu Tanzania, watu wanautazama mchakato wa Katiba kwa uchu wa madaraka au fursa za kisiasa, hali inayopelekea lugha gongana mithili ya jinamizi la Mnara wa Babeli, na kutia mashaka kama kweli Katiba Mpya, kama Watanzania wanavyoitaka, itapatikana kwa wakati muafaka.
Luqman Maloto ni mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia thisluqman@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.