The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mchakato wa Katiba Mpya Tanzania: Yajayo Yanafurahisha

Rais Samia ameonesha njia, kilichobaki ni sisi viongozi wa kiserikali, kisiasa, kijamii na kidini kuunga mkono na kusaidia kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya.

subscribe to our newsletter!

Nimefuatilia mwenendo wa siasa za Tanzania tangu katikati ya mwaka 2021 kwa furaha kubwa. Ingawa changamoto bado zipo, na hakuna nchi ziliwahi kuishiwa na changamoto, siasa za Tanzania kwa sasa zinaelekea kuanza kujenga maelewano, mshikamano na tija siyo tu ya kisiasa bali pia ya kijamii na kiuchumi. 

Hotuba za hivi karibuni za Rais Samia Suluhu Hassan kwa Watanzania kupitia matukio kadhaa zinarejesha rasmi imani ya umma kuwa Tanzania inaweza kujenga siasa safi na za kistaarabu. Matukio mawili ni vema nikayajadili kidogo.

Kwanza, katika mkutano aliouitisha na kuuhutubia ukihusisha vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu, Rais Samia aliweka bayana msimamo wake na kutangaza rasmi kufuta kifungo cha mikutano ya hadhara ya kisiasa na kijamii, huku akionya kuwa fursa hiyo isichezewe kwa kuanza kuitumia vibaya. 

Niliulizwa na jopo la wanadiplomasia fulani kuwa, mbona Rais Samia anaweka tena masharti kwa ruhusa ya mikutano? Majibu yangu yalikuwa ya kuuliza swali pia – kwani wapi huwa kuna uhuru usiokuwa na mipaka? 

Nilishauri, na ninarudia kufanya hivyo,: mikutano ya hadhara lazima ifanyike kwa busara na hekima kubwa ili tusijikute tunazalisha fujo na vifo kutokana na mikutano hiyo. 

Aidha, Rais Samia amehutubia mabalozi na wanadiplomasia mbalimbali wanaoziwakilisha nchi na taasisi zao nchini katika kusanyiko maalum la kila mwaka la wanadiplomasia lililofanyika wiki hii. 

Katika hotuba yake fupi, Rais amesisitiza kuwa Tanzania itaendeshwa kwa misingi ya demokrasia ya mazungumzo na mashauriano. 

Katika hali inayoonesha kuungwa mkono, Rais Samia alishangiliwa sana mwishoni mwa hotuba yake hiyo.

Gumzo la Katiba Mpya

Katika yaliyojiri kwenye mkutano wa Rais na wanasiasa, kulikuwepo suala la Katiba Mpya. Hili limekuwa ni gumzo la muda mrefu tangu mchakato wa Katiba Mpya udorore mwaka 2014. Kwa maneno ya Rais, mchakato wa Katiba Mpya sasa utafufuliwa na kukamilishwa. 

Akifafanua zaidi, Rais Samia amekiri kuwa mahali pa kuanzia na namna ya kuanza imekuwa ni changamoto kiasi kuwa alilazimika kuomba subira ili atafute njia sahihi. 

Ni katika muktadha huo ndipo Rais aliunda kikosi kazi kilichoongozwa na gwiji wa Sayansi ya Siasa, Profesa Rwekaza Sympho Mukandala na kuratibiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini. 

Furaha yangu ni kuwa Rais Samia anaonekana kuelekea kupata majibu juu ya namna ya kuukamilisha mchakato wa Katiba, hususan namna ya kuanza kukamilisha na wapi pa kuanzia. 

Kwa maneno yake mwenyewe, kunahitajika kamati ya watu wachache itakayotazama na kuelekeza namna bora ya kukamilisha mchakato huo. 

SOMA ZAIDI: Hatua Tano Muhimu Kufikia Upatikanaji wa Katiba Mpya Tanzania

Kwa tafsiri yangu, Rais Samia amesikiliza na kukubaliana na maoni ya asasi kadhaa na wadau wa Katiba Mpya ambao walipendekeza kuundwe Kamati ya Wataalam wa masuala ya Katiba ili waweze kukaa, kwa mwezi mmoja hivi, kuwianisha na kutafuta urari kati ya yaliyomo katika Rasimu ya Katiba Mpya, iliyoandaliwa na kuzalishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Sinde Warioba, na ule waraka unaoitwa Katiba Inayopendekezwa ambao ilitokana na Mchakato wa Bunge Maalum la Katiba lililoketi Dodoma mwaka 2014. 

Kwa bahati mbaya, si Rasimu ya Katiba wala Katiba Inayopendekezwa peke yake inaweza kuwa mahali pazuri pa kuanzia kwa sasa.

Wapo watu wanaosema kuwa kwa kuwa sheria iliitaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwa Bunge Maalum la Katiba, na kwa kuwa hilo lilishatendeka, basi Rasimu kwa sasa ilishapitwa na wakati na haiwezi kuwa mahali pa kuanzia. 

Aidha, wako Watanzania wanaotoa hoja kuwa ingawa Bunge Maalum la Katiba lilikuwa na mamlaka ya kuzalisha Katiba Inayopendekezwa kutokana na rasimu iliyowasilishwa kwao na Tume ya Warioba, matukio ya mwaka 2014 ya kususa na kutoka nje kwa wajumbe wote wa kambi rasmi ya upinzani chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), pamoja na baadhi ya wajumbe waliowakilisha Asasi za Kiraia, yalipelekea zao la Mchakato wa Bunge Maalum la Katiba kukosa uhalali wa kimaridhiano pamoja na kuwa uhalali wa kisheria ulikuwapo. 

Ni kwa sababu hiyo, wataalam wa masuala ya maridhiano ya kikatiba wameshauri timu ndogo ya wataalam ipewe kazi ya kukaa na nyaraka hizi mbili na kuziwianisha ili kuzalisha Rasimu ya pamoja itakayopelekwa kwa wananchi kuipigia Kura ya Maoni, au kura ya maamuzi kama ijulikanavyo katika mifumo ya Jumuiya ya Madola. 

Katika hili, nimefarijika sana kumsikia Mheshimiwa Rais akichukua msimamo huu unaopendekezwa na wataalamu.

Mchakato uanze sasa

Katika yote hayo, mchakato wa Katiba Mpya unapaswa kuanza sasa. Katika ndoto zangu, namuona Waziri wa Katiba na Sheria akiandaa barabara ambamo mchakato huu wa Katiba Mpya utapitia katika hatua hizi za kuukamilisha. 

Barabara hiyo ndiyo ambayo itatumika kuandaa Miswada ya Sheria zinazohusika na ukamilishaji wa mchakato huu wa Katiba Mpya. Kwa waliosahau, zipo sheria mbili zinazoongoza Mchakato wa Katiba Tanzania. 

Kwanza, kuna Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na. 83 iliyopitishwa na Bunge mwezi Novemba mwaka 2011. Katika kuhakikisha kuwa mchakato unaenda sawa, sheria hii ilifanyiwa marekebisho mara kadhaa baada ya kutungwa.

SOMA ZAIDI: Othman Masoud Ataka Haya Yazingatiwe Kwenye Mchakato wa Katiba Mpya

Kwa mfano, miezi mitatu tu baada ya kutungwa kwa sheria hiyo, Bunge lilipitisha marekebisho yaliyopata idhini ya Rais Jakaya Kikwete mnamo Februari 28, 2012. 

Baada ya kuanza matumizi, sheria ililetwa tena bungeni kwa ajili ya marekebisho mengine mara tatu mwaka 2013. 

Kwa mwaka huo pekee, Bunge lilipitisha Sheria Na. 7, 9 na 11 zikirekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyotungwa miaka miwili tu kabla ya hapo. 

Kutokana na marekebisho yaliyofanyika mara nyingi ndani ya muda mfupi, iliamuliwa kuwa kufanyike uunganishaji wa marekebisho yote ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba katika sheria moja kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha Sheria ya Mapitio ya Sheria Sura ya 4 ya Sheria za Tanzania.

Kwa bahati mbaya, sheria hii ya Mabadiliko ya Katiba, pamoja na marekebisho yote niliyoyazungumza, imepitwa na wakati na haiwezi kutumika tena pasipo maboresho wakati huu tunapohuisha Mchakato wa Katiba Mpya. 

Sheria nyingine inayoongoza Mchakato wa Katiba Mpya, hususan itakapofika muda wa Kura ya Maoni, ni Sheria ya Kura ya Maoni ya Mwezi Disemba 2013. Sheria hii nayo inayo maeneo kadhaa yanayostahili maboresho ili wakati wa kura ya maoni ukifika mambo yawe shwari.

Mchakato uwe wa wananchi

Yatosha kusema kwa sasa kuwa nchi yetu ina maprofesa wa nadharia ya katiba lakini kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, Watanzania ndiyo maprofesa wake kiuhalisia. 

Kama ambavyo magwiji wengi hunena, uandishi wa Katiba Mpya si suala la wanasheria na wanasayansi ya siasa bali ni suala la wananchi. 

Hata hivyo, ili wananchi waweze kushiriki kikamilifu, kunahitajika elimu pana ya uraia kuhusu michakato na maudhui ya Katiba, pamoja na uongozi thabiti wa kimchakato. 

SOMA ZAIDI: Twaha Mwaipaya: Rais Samia Hawezi Kukwepa Hitaji la Katiba Mpya

Ni imani yangu kuwa tamko la Rais Samia kuridhia kuchukua mtindo wa kuunda kamati ndogo maalum ya kuwianisha (harmonize) maudhui ya Katiba, Rais ameamua kuunda uongozi wa mchakato wa Katiba kiasi ambacho sisi wengine tutakuwa na kazi ya kuelimisha, kuhamasisha na kushiriki. 

Siku za nyuma tulikosa bahati ya wananchi kuweza kushirikishwa na ninaweza kusema bila kusita kuwa hapakuwa na ushiriki mpana wa wananchi katika michakato yote iliyozaa Katiba tano ambazo Tanzania imekuwa nazo tangu Uhuru: Katiba ya Uhuru mwaka 1961; Katiba ya Jamhuri mwaka 1962; Katiba ya Muungano mwaka 1964 na Katiba ya Mpito ya Mwaka 1965. 

Hata Katiba ya ‘Kudumu’ ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo ndiyo inayotumika hadi sasa ilikosa msingi huo wa ushiriki mpana wa Watanzania. Katika marekebisho yake mara 14 tangu 1977 hadi 2005, Katiba hii iliwahi kujaribu kushirikisha Watanzania wa kila mkoa kwa mapana ya kiasi chake mwaka 1983/4. 

Hata hivyo, tatizo moja lililojitokeza wakati huo ni kwamba chama pekee cha siasa wakati huo, Chama cha Mapinduzi (CCM) ndicho kiliratibu mchakato wa maboresho ya Katiba kiasi kwamba kuna mambo ambayo hayakuruhusiwa kuhojiwa, au kutolewa mchango katika mchakato huo, kwa mujibu wa imani za CCM. 

SOMA ZAIDI: Ben Ishabakaki: Katiba Mpya Italeta Mageuzi Kwenye Mfumo wa Utoaji Haki Tanzania

Watu wengi waliamini kuwa wakati wa mageuzi ya kisiasa na kuruhusiwa kuanza kwa mfumo wa vyama vyingi vya siasa mwaka 1992 kungeambatana na mchakato wa Katiba Mpya ili kuleta mageuzi halisi ya kikatiba, sambamba na mageuzi ya kisiasa na kiuchumi ya miaka ya 1980 na 90. 

Kwa kuwa hilo halikutokea, fursa ya sasa iliyoanza na Rais Kikwete mwaka 2011 na inakamilishwa na Rais Samia mwaka 2023 ndiyo fursa kwa kila Mtanzania kushiriki katika historia ya kuandika Katiba ya Watanzania wote.

Ni imani yangu kuwa mchakato wa kuandaa Miswada ya Marekebisho ya Sheria zinazoongoza mchakato wa Katiba Mpya Tanzania utaanzishwa mapema hivi karibuni, ili tusiendelee kupoteza muda. 

Lini mchakato unaweza kukamilika?

Kwa makadirio yangu, endapo Baraza la Mawaziri litaelekeza Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Sheria ya Kura ya Maoni, inawezekana kabisa kuandaa Miswada hiyo miwili na kuipeleka bungeni kwa hatua ya kusomwa kwa mara ya kwanza mwezi Aprili mwaka huu. 

Baada ya maoni ya wananchi katika ngazi ya kamati, sheria zote mbili zinaweza kupitishwa kabla ya kukamilika kwa Bunge la Bajeti mwezi Juni mwaka huu. 

Kazi ya uhamasishaji, uelimishaji na maandalizi ya Kura ya Maoni kuhusu Rasimu itakayokuwa imetayarishwa na Kamati Maalum ya Rais ikifanyika vema mwaka 2023, itakuwa inawezekana kabisa kufanya Kura ya Maoni ifikapo katikati ya mwaka 2024. 

Kwa uzoefu wangu, kupitishwa kwa Katiba Mpya mwaka 2024 hakutamaanisha mwisho wa matumizi ya Katiba ya sasa ya mwaka 1977 au ile ya Zanzibar ya mwaka 1984. 

SOMA ZAIDI: Ismail Jussa: Sikubaliani na Hoja Kwamba Mchakato wa Katiba Mpya Uanze Baada ya 2025

Nchi nyingi huhitaji muda usiopungua miezi 24 ili kukamilisha maandalizi ya utekelezaji wa Katiba Mpya ambao huhitaji mabadiliko ya sheria mbalimbali, kanuni, mifumo na taratibu ili kuendana na matakwa ya Katiba Mpya.

Katika kozi moja niliyoisoma kuhusu sheria na mifumo ya uundaji wa Katiba Mpya katika chuo kikuu kimoja nchini Hungary, nilibaini kuwa Katiba inaweza kupitishwa lakini utekelezaji wake ukasubiri kuandaliwa kwa sheria na mifumo ya utekelezaji wake.

Katika Kuhitimisha, ningependa kusema kuwa Mheshimiwa Rais ameonesha njia, dhamira na nia ya kuleta utawala wa kidemokrasia ya Katiba nchini Tanzania. Kilichobaki ni sisi viongozi wa kiserikali, kisiasa, kijamii na kidini kuunga mkono na kusaidia kukamilisha sehemu iliyobaki. 

Ndiyo maana nimekuwa nikitoa wito kwa Watanzania waliokuwa wamelazimika kuondoka nchini kutokana na uminyaji wa demokrasia kurejea ili tusaidiane kujenga nchi. 

Kama ujumbe niliousoma wiki hii kupitia mtandao wa Twitter utakuwa ni wa kweli, nafurahi kusikia kuwa Mtanzania gwiji wa uchambuzi wa sheria, Tundu Lissu anarejea nchini Tanzania mnamo siku ya Jumatano, Januari 25, 2023, akiwasili Dar es Salaam kwa shirika la ndege la Ethiopia kutokea Ubelgiji kupitia Addis Ababa. Hii ndiyo raha ya kufungua milango ya majadiliano na mikutano!

Mheshimiwa Lissu, na ninaamini wengine walioko nje ya Tanzania kwa sababu za mazingira duni ya kufanya kazi ya siasa kutokea Tanzania siku za nyuma, sasa wanaanza kurejea ili kuja kushirikiana na Watanzania wote kujenga nchi. 

Nachukua fursa hii kuwakaribisha wote nyumbani.

Kipekee, nampongeza Mheshimiwa Rais, viongozi wote walioshiriki kushauri mwelekeo wa kisiasa nchini tangu Juni 2021 na wanahabari kwa kazi nzuri ya kuelimisha na kuhamasisha mnayoifanya. 

Natumaini hakutakuwa na mtu yeyote wa kuikwamisha kazi na juhudi hizi zinazoendelea!

Deus Kibamba ni mtafiti na mchambuzi wa masuala ya siasa Tanzania anayefundisha utatuzi wa migogoro na uendeshaji wa mazungumzo ya amani katika Chuo cha Diplomasia. Anapatikana kupitia +255 788 758581 na dkibamba1@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *