The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Twaha Mwaipaya: Rais Samia Hawezi Kukwepa Hitaji la Katiba Mpya

Kada huyo wa CHADEMA anasema wao kama chama hawatabweteka kufuatia kauli ya CCM kwamba Katiba Mpya inahitajika bali wataendelea kuchochea uhuishwaji wa mchakato huo.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Mratibu wa Uhamasishaji wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) Twaha Mwaipaya amesema kwamba kwa kazi ambayo baraza hilo imekuwa ikiifanya kwenye kuchochea uhuishwaji wa mchakato wa Katiba Mpya nchini ana imani kwamba nyaraka hiyo muhimu itapatikana kabla ya mwaka 2025.

Mwaipaya alitoa tathmini yake hiyo wakati wa mahojiano na The Chanzo yaliyofanyika katika ofisi ya chombo hicho cha habari Msasani, Dar es Salaam hapo Julai 28, 2022, ambapo alitoa maoni yake kuhusiana na masuala kadhaa ya kitaifa, ikiwemo hitaji la Katiba Mpya na mageuzi ndani ya Jeshi la Polisi.

“Kitendo cha watu waliokwamisha mchakato wa Katiba Mpya, wakafika sehemu wakazungumza kuhusu Katiba Mpya, wakati wao walisema sio kipaumbele chao, sio hatua ndogo, ni hatua kubwa,” alisema Mwaipaya wakati wa mahojiano hayo.

Alikuwa akizungumzia hatua ya chama tawala Chama cha Mapinduzi (CCM) kujitokeza hadharani hapo Juni 22, 2022, na kuitaka Serikali kufufua mchakato wa Katiba Mpya, ikisema mazingira ya sasa yanahitaji Katiba Mpya kwa “maslahi mapana ya taifa.”

“Na sisi hatujaridhika, hatujabweteka wala kauli yao haiwezi ikatufanya sasa tuachane na kudai Katiba Mpya, tukabweteka,” alisema Mwaipaya wakati wa mahojiano hayo. “Tunaendelea kuzungumza na Watanzania, tunaendelea kujiandaa sisi kama vijana wa Kitanzania, tunajua mstakabali mkubwa wa Watanzania ni vijana.”

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo. Endelea …

The Chanzo: Twaha, tunashukuru sana kwa kutenga muda na kuja kuzungumza na sisi. Nakumbuka kwamba mara nyingi tumekuwa tukipanga lakini mambo mengine yanaingiliana, yanaingilia kati. Labda unaendeleaje?

Twaha Mwaipaya: Ninamshukuru Mungu. Mungu amenijalia afya yangu imekuwa njema mimi na familia yangu pamoja na viongozi wote ambao tunafanya nao kazi. Mungu ametupa afya njema. Niko salama kabisa.

The Chanzo: Na ningependa kuanza moja kwa moja mahojiano yetu haya na hiki ambacho kimejitokeza juzi tu hapa. Kuachiwa huru kwa wale vijana saba kule Mbeya wa CHADEMA ambao walikuwa wanakabiliwa na kesi mbili tofauti za mauaji. Wewe binafsi uliupokeaje uamuzi wa Mahakama wa kuwaachia huru wale vijana wenzenu, wanachama wenu wa BAVICHA?

Twaha Mwaipaya: Kibinadamu, kwa hali ya kawaida, lazima mtu yeyote anapokuwa gerezani na akitoka unaipokea vizuri. Lakini mimi nimejisikia fahari kwa sababu nimeshafika gereza la Songwe kuwatembelea zaidi ya mara nne. Mara ya kwanza tulifanya ziara ya kuwatembelea wafungwa wa kisiasa sisi kama Baraza la Vijana wa CHADEMA taifa pamoja na Mwenyekiti Mheshimiwa John Pambalu.

Tulizunguka nchi nzima kupita kila gereza kuwajulia hali na kuwafariji, na kuwatia moyo, wafungwa wote wa kisiasa ambao kesi zao zilianza baada ya uchaguzi au kabla ya uchaguzi wa mwaka 2020. Tulifika gereza la Songwe na wale ambao wameachiliwa jana ni miongoni mwa watu zaidi ya sitini ambao wengine waliachiliwa mwanzoni.

Alikuwepo Meya mstaafu wa mji mdogo wa Tunduma. Alikuwepo kijana wetu aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana mkoa wa Songwe hapo mwanzo Ayubu Segunamo. Kwa hiyo, hawa ambao wametoka ni baadhi tu ya wale watu ambao walikuwa bado wamesalia gerezani na wamekaa gerezani zaidi ya mwaka mmoja na miezi nane kwa kesi za kiuchaguzi ambazo sisi mara kadhaa tulikuwa tumeiomba Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia Mheshimiwa Rais kwamba watu hawa wanastahili uhuru kwani tunajua kesi za uchaguzi mara nyingi zinakuwa ni kesi za kisiasa.

Haiwezekani watu sitini wakatuhumiwa kumuua mtu mmoja, hata huo mwili utakuwa na majeraha mangapi? Kwa hiyo, namshukuru Mungu wapo huru lakini najua wana maumivu makubwa. Wamekaa mwaka mmoja gerezani, wanafamilia, wana wake [zao], wana watoto na si tu walikuwa wapo wanaume peke yake lakini kulikuwa na wanawake ambao pia wamekaa gerezani zaidi ya mwaka mmoja.

Kwa hiyo, ni maumivu tunayapokea kwa furaha kama wanaharakati na kama wanasiasa. Lakini najua familia zimewapokea lakini bado inawezekana watoto wao wanavyowaona sasa hivi wazazi wao wamerudi nyumbani wakapata uchungu mkubwa kwa sababu muda mrefu wamekaa wenyewe, wamepitia mateso makubwa.

Huenda watoto wengine wakawa wameacha shule kwa sababu walikuwa hawana matunzo ya baba na mama kwa sababu baba yake alikuwa yupo magereza. Kwa hiyo, ni maumivu na ni furaha. Inawezekana kwa familia ikawa vilio kwani inamaanisha kuna baadhi ya mambo makubwa hayakwenda sawa. Unajua wazazi wanapokuwa hawapo nyumbani mambo mengi familia inapitia.

The Chanzo: Kabisa.

Twaha Mwaipaya: Ndio.

The Chanzo: Na hapo uligusia kwamba ni takribani vijana sitini wa CHADEMA walikuwa wapo kwenye magereza tofauti tofauti.

Twaha Mwaipaya: Gereza moja la Songwe lilikuwa na vijana sitini peke yake.

The Chanzo: Gereza moja tu. Na kwa uelewa wako, kwa ufahamu wako, ni wangapi mpaka sasa wanaendelea kusota magerezani?

Twaha Mwaipaya: Tulikuwa tuna wafungwa wa kisiasa zaidi ya 400 ambao walikuwa wapo magerezani, na mimi nikiwepo miongoni mwao, ambapo nimekuwa gereza la Singida baadaye nikawa gereza la Dodoma.

Mpaka sasa sisi kama Baraza la Vijana wa CHADEMA tunawatambua vijana wetu pamoja na magereza mabalimbali ukienda kwenye gereza la Iringa mjini sasa hivi yupo Mwenyekiti wa mkoa wa Njombe wa Baraza la Vijana ndugu yetu George Sanga na wenzake wawili ambao wapo gerezani zaidi ya siku 600 sasa.

Wamekuwa gereza la Njombe na sasa hivi wamesafirishwa kuelekea gereza la Iringa Mjini, wana kesi ya mauaji. Walituhumiwa kumuua kiongozi wa CCM kipindi cha uchaguzi na siku chache kabla ya kurejesha fomu George Sanga alikuwa ni Diwani wetu wa Kata ya Ramadhan kuanzia 2015 mpaka 2020 na 2020.

Alirejea tena kugombea tena nafasi yake ya udiwani kama ambavyo alikuwa Diwani hapo mwanzo na akiwa kwenye hatua za kurejesha fomu, siku ya kurejesha fomu, alikamatwa na Jeshi la Polisi na baadaye akatoweka katika mazingira ya kutatanisha. Baadaye tulipokea taarifa kwamba yupo mikononi mwa polisi na anatuhumiwa kwa kesi ya kumuua kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi.

Mpaka leo tunapozungumza yeye na wenzake wapo gerezani na George Sanga mara nyingi nimefika gereza la Njombe kwenda kumtembelea hata katika ziara yetu ya kutembelea wafungwa wa kisiasa wa magereza tulifika gereza la Njombe tukazungumza nae akalalamika sana.

Mguu wake wa kulia alipigwa sana George hata sasa hivi ukimuona anavyotembea anachechemea mguu wake wa kulia mpaka sasa haujapona vizuri kutokana na kipigo kikali alichopigwa na Jeshi la Polisi.

Polisi walikuwa wanataka akiri kama zile tuhuma ambazo amepewa ni za kwake lakini George Sanga ilimuwia vigumu sana kuzikubali tuhuma hizo japo kuwa alipitishwa katika mateso makubwa. Walipigwa vibaya mpaka sasa yupo gerezani.

George Sanga anafamilia. Ana watoto. Ana wazazi. Lakini pia George Sanga sisi ni kiongozi mwezetu. Kwa hiyo, mara nyingi nimekuwa nakutana na mke wake na familia yake na kama chama tumejitahidi kadri ambavyo tunaweza kuisaidia familia yake ili kuitia faraja kwani mke zaidi ya mwaka sasa hajamuona mume na watoto hawajamuona baba.

Ni maumivu makubwa ambayo hatuwezi tukayaelezea sisi kama wanasiasa. Lakini kwenye magereza yetu bado kuna wafungwa wa kisiasa ambao tunaendelea kuzungumza na Mama Samia, au na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, awaachilie huru.

Ukienda pale Mbeya kuna kijana wetu anaitwa Gerald amefungwa maisha. Gerald anatuhumiwa kwa kuchoma moto ofisi ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi, [na] amefungwa maisha.

Ukienda kule Kishapu kuna wanachama wetu wa CHADEMA nane wamefungwa maisha. Watu wa Kishapu walituhumiwa kwa kesi ya ubakaji. Yaani watu 8 walituhumiwa kwa kumbaka mtu kwenye kituo cha kupigia kura. Yaani siku ya kupiga kura walituhumiwa walibaka mtu ndani ya kituo na katika maelezo yao walisema walikuwa wanabaka kwa kupokezana.

Sasa unaweza ukajiuliza siku ya kupiga kura ile purukushani watu kwenda kupiga kura lakini bado mtu anaweza akakamatwa kwenye kituo cha kupigia kura akabakwa na watu nane na watu hao mpaka leo Kishapu wamefungwa maisha.

Hiyo haijawahi kuwa mwisho na wala haiwezi kuwa mwanzo. Najua sisi viongozi wa chama cha upinzani tunapitia mengi. Gereza ni mlango wa kutengenezwa [kisiasa]. Mimi Mwaipaya yule ambaye mwanzo aliyeingia gerezani na sasa ni tofauti.

The Chanzo: Sawa sawa na ninataka kukuuliza kwa kuhusianisha na mchakato unaoendelea sasa ambao unaitwa ni wakutafuta maridhiano ya kisiasa nchini na nilikuwa nataka kupata maoni yako kama unadhani hatua hii ya kuachiwa kwa vijana hawa saba kutoka gerezani inaweza kuwashawishi baadhi ya vijana wenzako ndani ya CHADEMA kwamba nia ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye kutafuta hicho kinachoitwa maridhiano ni ya dhati?

Nakuuliza hivi kwa sababu tumeona baadhi ya vijana ndani ya CHADEMA wakijitokeza hadharani kuonesha masikitiko yao wakionesha nia sio nzuri, hususani wakitolea mfano jinsi Serikali inavyowachukulia wale Wabunge 19 ambao hawana chama.

Unadhani ni kwa kiasi gani hatua hii ya kuachiwa vijana saba wa CHADEMA inaweza ikawashawishi nyinyi ndani ya CHADEMA kwamba nia ya kutafuta maridhiano inayoendelea ni nia ya dhati, ni nia ya kweli?

Twaha Mwaipaya: Asante. Kwanza ifahamike kwamba watu ambao wameachiliwa hawajapewa zawadi ya uhuru wao. Walistahili kuwa huru. Hawakustahili kuwa gerezani.

Kwa hiyo, kitendo cha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na baada ya kukutana na chama cha CHADEMA na Chama cha Mapinduzi hata ukimsikiliza Mheshimiwa Katibu Mkuu John Mnyika, alizungumza na vyombo vya habari, kwamba kati ya mambo mengi ambayo wamezungumza jambo la kwanza kati ya hayo ilikuwa ni kuwaachilia huru wafungwa wa kisiasa.

Kwa hiyo, wanahaki ya kuwa huru. Walikuwa wanahaki ya kuwa huru. Walikuwa wanahaki ya kuishi na familia zao. Walikuwa wanahaki ya kuendelea kutekeleza majukumu yao kwani tunapokwenda kwenye uchaguzi watu ambao wanapitia madhila siyo Chama cha Mapinduzi peke yake hata CHADEMA.

Sisi tumepitia majaribu makubwa akiwemo kama mdogo wake wa John Heche aliuawa na Jeshi la Polisi kule Tarime. Ukienda Zanzibar kuna Wazanzibari zaidi ya 20 waliuawa kwenye uchaguzi wa mwaka 2020.

Hawa pia wanandugu na wana watoto. Wanawake waliowaacha je, nani atawalipa fidia zile familia na nani atarejesha ile furaha ya familia na wazazi na watoto nao wakashangilia?

Kwa hiyo, maridhiano ambayo yanaendelea na wafungwa wa kisiasa kuachiliwa huru siyo hisani. Sisi tunaamini kabisa aliyeko kule ni kwa sababu ya kisiasa.

The Chanzo: Siyo hisani lakini unadhani inaweza ikawashawishi baadhi ya watu ambao wanawasiwasi kwamba nia ya Rais ni ya dhati?

Twaha Mwaipaya: Hatuhitaji Rais akutane na mtu yeyote, afanye maridhiano ili mtu yeyote ashawishike, au aone Rais anafanya vizuri. Sisi tunahitaji Rais ajenge misingi ya nchi yake.

Tunahitaji kutengeneza misingi ya kidemokrasia. Tunahitaji tutengeneze misingi ya haki. Tunahitaji tutengeneze misingi ya mapatano katika taifa letu la Tanzania. Na Rais kama anaipenda nchi yake ya Tanzania inatakiwa ajenge misingi mema kwenye nchi yake ya Tanzania ili sisi kama Watanzania na wananchi tuhakikishe kabisa tuone haki inatendeka wakati wowote bila kutafuta wa kumpongeza.

Kwani tukiwa tuna sheria njema zinazoongoza nchi hatutatafuta mtu wa kumpongeza bali sheria na Katiba na zitatuongoza kutenda haki kwenye nchi yetu ya Tanzania. Kwa hiyo, haya ambayo yanaendelea sisi tunahitaji Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aijenge Tanzania ya kesho na nina amini kama Rais anataka kukumbukwa kwenye nchi yake ya Tanzania, atakumbukwa kwa misingi mema atakayoijenga kuanzia hivi sasa.

Na jambo la kwanza peke yake ambalo litamfanya atakumbukwa ni kurejesha misingi ya haki kwenye taifa na misingi ya haki haiwezi kurudi bila kurejesha mchakato wa Katiba Mpya, bila Katiba Mpya hatutakuwa tuna misingi imara ya haki.

The Chanzo: Mtazamo wako binafsi wa mchakato wa maridhiano ni upi, au msimamo wako ni upi, unadhani ni jambo zuri?

Twaha Mwaipaya: Maridhiano ni jambo jema kama pande zote mbili ambazo zinaridhiana zina nia njema. Na tumeona maridhiano wakati yanaendelea bado kuna mambo mengine makubwa yanaendelea, ikiwemo mimi mwenyewe katikati ya maridhiano nilikamatwa na Jeshi la Polisi na kufichwa kusikojilikana na Watanzania wakanililia ili wanione.

Kwa hiyo, hatuwezi kukata tamaa. Hata mimi wakati yamenitokea haya sikukilaumu chama changu ni kwa nini kinafanya maridhiano wakati kuna watu wanaumia. Sisi tunataka turidhiane, tupatane, pande zote mbili, upande wa Chama cha Mapinduzi, CHADEMA tumepitia madhila makubwa kama chama lakini na upande wa Serikali ambapo ni watawala wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi.

Tunataka badaye asipatikane mtu wa kulaumiwa kwamba sisi kama CHADEMA tulikubali kukaa na Chama cha Mapinduzi mezani, kukubali kutafua maridhiano ya taifa ili upande wa Serikali wawe na amani, upande wa wapinzani wawe na amani na upande wa wananchi wawe wana amani.

Kwa hiyo, sisi hatujakwenda kutaka maridhiano na Chama cha Mapinduzi kwa sababu ya kutafuta sifa au kuonekana. Sisi tunataka tuandike historia. Ipo kesho watoto wetu watakuja kutuuliza, ni kwa nini hamkukaa mkaelewana, mkaacha damu ikamwagika Tanzania?

Hatuhitaji tufike kwenye umwagaji damu kwenye taifa letu. Hatuhitaji tupite njia Wakenya walipita. Wakenya walimwaga damu. [Jamhuri ya Kidemokrasia ya] Congo wanamwaga damu. Hata Zambia hapo, unakumbuka mwaka 1996 wakati wakipigania Katiba Mpya na maridhiano kwenye taifa walimwaga damu.

Kwa hiyo, sisi Watanzania tunahitaji tuzungumze kama watawala itawapendeza tufanye maridhiano na tupatane. Yale mambo yote ambayo tunaamini yametukwamisha kama taifa tuyakwamue, tusonge mbele kwa pamoja na tuitengeneze Tanzania ya kesho iliyonjema zaidi.

The Chanzo: Na unadhani ili huu mchakato wa maridhiano uwe ni wenye kuwanufaisha wananchi, unadhani unapaswa uchukue sura gani, au unapaswa uhusishe nini na nini, yaani ni sura gani ya maridhiano ambayo wewe binafsi ungependa kuiona?

Twaha Mwaipaya: Tunahitaji kuona maridhiano ambayo kila mtu anayeyaangalia anaona yale ni maridhiano. Tunahitaji tupate maridhiano ya kweli. Maridhiano ya haki, siyo maridhiano ya kuviziana. Hatuhitaji sisi Chama cha Mapinduzi kituvizie CHADEMA wala hatuhitaji CHADEMA tuivizie Chama cha Mapinduzi.

Kwa sababu tunapokwenda kufanya na mambo ambayo tumepeleka mezani kwa sababu ya maridhiano ni mambo ya haki, mambo ambayo yatarejesha uhuru wa wananchi yatakuza demokrasia ya nchi na yatafanya kukuza hata uchumi wa nchi kwa sababu wawekezaji wakiona Tanzania inamaridhiano mazuri watakuja kuwekeza Tanzania.

Kwa hiyo, tunahitaji maridhiano ambayo yataisaidia nchi ya Tanzania. Maridhiano ya kweli yatakayopatanisha pande zote mbili. Tunahitaji maridhiano ambayo yataisaidia nchi ya Tanzania. Maridhiano ya kweli na yatakayopatanisha pande zote mbili. Tunahitaji maridhiano ambayo yatatusahaulisha mabaya na maovu yote ambayo yamepita.

Kwa hiyo, tunahitaji kuwa na subira lakini kikubwa kwenye maridhiano Serikali na sisi [CHADEMA] tupeane tarehe ya mwisho, tujue maridhiano yanakwisha lini. Haiwezekani tukawa tunafanya maridhiano huenda tukafika uchaguzi wa mwaka 2025 hayajakamilika.

Lazima twende kwenye safari ya maridhiano kwa mashaka. Sio kwamba hatuwaamini Chama cha Mapinduzi lakini matendo yao na kauli zao ambazo zinabadilika mara kwa mara ndiyo zinafanya tuwe na mashaka na Chama cha Mapinduzi lakini hatutaacha kuridhiana na tutaendelea kukishauri chama kama Baraza la Vijana wa CHADEMA kwamba tunahitaji tujue maridhiano haya yatafika lini.

Tunakiamini chama chetu pendwa cha CHADEMA lakini tuna haki ya kushauri na kutoa maoni yetu kwenye chama. Kwamba ifike sehemu tujue maridhiano yanakwisha lini na baada ya hapo tuanze sasa kuweka kumbukumbu sawa kama kile ambacho tumeridhiana Chama cha Mapinduzi hawawezi wakaturejesha huko tulikotoka.

The Chanzo: Asante sana. Twaha wewe ni mmoja kati ya vijana wa taifa hili ambaye umejikuta matatani kwa zaidi ya mara moja kwenye vyombo vyetu vya ulinzi na usalama na nilikuwa nataka kusikia kutoka kwako unadhani ni matatizo gani ya msingi yanavikabili vyombo vyetu vya ulinzi na usalama hapa Tanzania?

Twaha Mwaipaya: Jambo kubwa ambalo linavikabili vyombo vya ulinzi na usalama Tanzania ni maelekezo. Kumekuwa kuna changamoto kubwa sana ya ukamataji. Kumekuwa kuna changamoto kubwa sana mtu kukamatwa bila kupewa haki yake ya kuambiwa kosa lake la msingi ni lipi.

Polisi wanakuja kukukamata Mtanzania, ukihoji mnanikamata kwa kosa gani wanakwambia usitupangie kazi. Wakati sheria zinataka polisi anapokuja kukukamata akwambie kwanza anakukamata kwa kosa gani, kabla ya kukwambia anakukamata kwa kosa gani kwanza ajitambulishe yeye ni nani kama ni polisi anatokea kituo gani na anakukamata kwa tuhuma gani na akikukamata akupe haki zako zote za msingi, akuambie haki zako zote za msingi ambazo unatakiwa kufanya.

Lakini Jeshi la Polisi linakukamata halikwambii kosa lako, linakunyima kufanya mawasiliano na ndugu zako uwaambie upo wapi na unafanya nini. Mimi nimekatwa na Jeshi la Polisi sio mara moja. Nimekamatwa Singida, nimekaa vituo vya polisi, nimekamatwa Iringa.

Nimekamatwa Mbeya, tumekamatwa Mwanza kila sehemu tumekamatwa na Jeshi la Polisi matatizo ni yale yale. Siyo kwa sisi tu ambao tunakamatwa. Hata ukienda kwenye vituo vya polisi unakutana na watu wengi ambao wamekaa kwenye vituo vya polisi kinyume cha sheria.

Sheria inasema mtu ndani ya masaa 24, kama amekamatwa siku za kazi, kama amekamatwa Ijumaa basi ndani ya masaa 48, mtu huyo awe tayari ameshakwisha fikishwa mahakamani.

Lakini tunakaa kwenye vituo vya polisi-, nimeenda, nimekutana na watu kwenye kituo cha polisi Morogoro kuna wanawake nane wamekaa kwenye kituo cha polisi zaidi ya wiki tatu hawajafukishwa kwenye vyombo vya haki.

Mahakama ndiyo inaweza ikasema mtu huyo anahaki au anastahili kwenda jela au anastahili kuwa huru, ana haki ya dhamana au hana haki ya dhamana. Kwa hiyo, mfumo wetu wa Jeshi la Polisi imekuwa ni changamoto. Kwanza [polisi] hawafuati sheria kabisa.

Hawafuati kanuni za Jeshi la Polisi kama amabvyo tumeona kwenye kesi ya Mheshimiwa Freeman Mbowe. Ukamataji, utesaji na hii imekuwa changamoto kubwa sana. Kama unaweza hata mimi kiongozi wa chama cha siasa ninayejulikana unaweza ukanikamata, ukakaa na mimi ndani ya siku saba ndugu zangu wasijue, viongozi wangu wa chama wasijue, familia yangu isijue vipi kwa Watanzania wa kawaida ambao hawafahamiki?

Na hatujui wanakamatwa lini na wanapelekwa wapi. Kwa hiyo, ili tuwe tunajeshi imara tunahitaji turudi upya kuliangalia Jeshi la Polisi. Tunahitaji kutoka kwenye Jeshi la Polisi twende kwenye Huduma ya Kipolisi.

Vile vile kwenye chombo hiki ambacho kimepewa dhamana kubwa ya kulinda raia na mali zake tunahitaji kiundwe chombo ambacho ni Tume ya Utumishi ya Jeshi la Polisi ili Watanzania watakapoonewa na Jeshi la Polisi wapate sehemu, au chombo huru, cha kwenda kulalamika na kutoa maelezo yake.

Leo hii ndugu mtangazaji ukionewa na Jeshi la Polisi sehemu pekee ambayo unakwenda kutoa malalamiko ni kwa watu ambao wanatengeneza kesi ambao ni polisi. Kwa hiyo, mimi nikionewa na Jeshi la Polisi nakwenda polisi kutoa malalamiko yangu.

Sasa kama polisi wamenionea ni nani anaweza akajichunguza? Yaani kuna polisi gani ambaye anaweza akajichunguza mwenyewe na akachunguza kwa haki akatoa siri zake kwamba ni kweli amefanya kosa?

Tumeangalia hapa Dar es Salaam lilitokea sakata kubwa sana la Hamza na Hamza kwenye video yake Mungu alitupeleka mbali zaidi alimtuhumu Sirro kwenye video ile akasema nitalipiza kisasi na maneno mengi aliyasema kwenye ile video na yalionekana Watanzania waliyaona.

Baadaye Jeshi la Polisi wakapewa mamlaka ya kujichunguza wenyewe na baadaye wakaja kutwambia kwamba Hamza alikuwa ni gaidi. Sasa unakuta tunapitia katika changamoto kama hizo wale ambao tunahofu na mshaka nao wanajichunguza wenyewe.

Nikikurejeshe kule Mtwara kuna kijana mmoja ambaye polisi walituhimiwa kwamba alikamatwa na Jeshi la Polisi, akapelekwa kituo cha polisi na baadaye alikuja akaachiliwa. Alivyofika nyumbani akakumbuka kwamba kuna vitu vyake aliviacha kwenye kituo cha polisi. Alipokwenda kurejea kwenye kituo cha polisi kuchukua vitu vyake mtu yule aliuawa na Jeshi la Polisi.

Na baadae kuna askari zaidi ya saba ambao mpaka leo wapo magereza kule Mtwara wanatuhumiwa kwa kesi ya kumuua kijana yule. Sasa ile kesi ambao wanachunguza na kupeleleza ni polisi. Na unajua kabisa ndani wale polisi walivyokamatwa na kupelekwa kwenye kituo cha polisi kuna polisi mmoja ilisemekana amejinyonga na amejinyonga kwa kutumia dekio la ndani ya kituo. Hizo tuhuma zipo ni kubwa.

Sasa haya matukio yote ambayo yanatokea ndani ya Jeshi la Polisi wamepewa jukumu la kuchunguza polisi wenyewe. Sasa sisi tumekuwa na mashaka makubwa. Tumesema kwa sababu kwa kweli mwenendo wa jeshi letu la polisi sio mzuri kwa kauli zake, kwa vitendo na ambacho kinatuumiza zaidi kwenye jeshi la polisi halifuati sheria kabisa na wala mara nyingi tumesema halibadiliki, hususani yale masaa 24, masaa 48 haki ya mtuhumiwa kupewa fursa ya kuwasiliana na ndugu zake pindi ambapo anakamatwa.

Sio watu wazima, sio watoto wadogo wanashikiliwa zaidi ya siku saba. Mimi nilikuwa nipo kituo cha Dodoma, nilisema hata kwenye mazungumzo yangu ya hivi karibuni, kwamba nilikutana na mtoto mdogo anaitwa Joshua Daniel.

Joshua Daniel alikamatwa na Jeshi la Polisi alikuwa anatuhumiwa kwa wizi na baadaye ilikuja kuonekana kwamba yeye hakuhusika kabisa na wizi ule. Mwizi alikamatwa akapelekwa kituo cha polisi akaunganishwa na Joshua wakapelekwa mahakamani.

Mahakama ikamwachilia huru Joshua na yule mwizi ambaye alikuwa anatuhuma za kuiba vyuma na kumapatia Joshua mtoto mdogo aende akauze akahukumiwa yule mtuhumiwa gerezani miezi miwili lakini Joshua akaachiliwa huru na mahakama na baadaye Jeshi la Polisi lilimkamata na kwenda naye kituoni.

Mimi nimemkuta kituoni ana zaidi ya siku saba ndani ya kituo. Mahakama imeshamwachilia huru. Nikauliza sasa polisi wanamshikilia kwa kosa gani? Kwa hiyo, tumekuwa tuna changamoto kubwa.

Tuna Jeshi la Polisi ambalo asilimia kubwa limelalamikiwa kwa rushwa. Kuna usemi maarufu upo Tanzania kwamba kuingia polisi bure lakini kutoka kwa pesa. Je, kuna sheria yoyote inalipa mamlaka yoyote Jeshi la Polisi kutoza hizo fedha?

Sasa Jeshi la Polisi lijitafakari kwa nini usemi huu umekuwa maarufu wakati wao hawana sheria ya kutoza fedha kwa wananchi.

The Chanzo: Nimependa sana umezungumza kwa hisia na umezungumza vizuri sana. Wewe uliupokeaje uamuzi wa Rais Samia kumteua Camillius Wambura kama Mkuu wa Jeshi la Polisi mpya pamoja na Ramadhan Kingai kama DCI mpya? Na unadhani uteuzi wa watu hao unaweza ukafanikisha hicho ambacho wewe unakitaka ndani ya Jeshi la Polisi, kwa mfano, kufuata sheria na kujiepusha na vitendo vya rushwa? Unamatumaini kwamba hawa wanaweza wakachochea mabadiliko yoyote chanya ndani ya Jeshi la Polisi.

Twaha Mwaipaya: Nianze kwa Camillius Wambura ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi wa sasa.

Ikumbukwe kwamba Mheshimiwa Tundu Lissu, ambaye alikuwa mnadhimu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni na sasa hivi ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo taifa na alishawahi kuwa mgombea wa Urais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania, alipewa kesi na Jeshi la Polisi, ilikuwa inaitwa [kesi ya] dikteta uchwara, ilikuwa ni kesi maarufu nchini Tanzania ambayo ilikuwepo mahakamani pale Kisutu.

Na Camillius Wambura, akiwa ZCO wa mkoa wa Dar es Salaam, alikuwa anaishikilia kesi ile na kesi ile kila mmoja alijua ilikuwa haina maslahi yoyote ya umma na Mheshimiwa Tundu Lissu kesi ile alishinda na akaachiliwa huru na Mahakama kwamba kesi ile haikuwa na mashiko na upande wa Jamuhuri ukasema haukuwa na nia ya kuendelea na kesi ile.

Na nikikurejesha nyuma Camillus Wambura amewahi kuhudumu mkoa wa Arusha na Godbless Lema mara nyingi sana amemlalamikia sana kwa vitendo vyake vya kukibeba Chama cha Mapinduzi kwenye uchaguzi.

Kitendo chake cha ukamataji, alimkamata Godbless Lema alikaa ndani zaidi ya miezi minne na Lema mara nyingi amekuwa akitoa tuhuma kwamba Camillus Wambura hastahili kupewa ngazi kubwa ndani ya Jeshi la Polisi kwa sababu akionea sana hususani vyama vya upinzani.

Lakini ndani ya Jeshi la Polisi watu wote ambao wametesa sana wapinzani wamepewa vyeo. Imetokea ndani ya Mahakama pia. Sasa vyombo hivi vyote vinashirikiana kutenda haki kwenye taifa.

Ukiachana na Camillus Wambura nenda kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa sasa ambaye amepewa jukumu la kupeleleza kesi zote nchini. Kama wakina Adam Mohamed, mahakamani walitoa maoni yao, ushahidi wao kama walichukuliwa maelezo yao kwa kuteswa kama popo na wakati mwingine walimtuhumu Ramadhan Kingai kama aliwawekea bastola ili watoe maelezo [huyu mtu anawezaje kuwa DCI]?

Haya mambo makubwa yamezungumzwa ndani ya Mahakama ambapo shahidi ameapa kuilinda Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, ameapa kwa kitabu kitukufu ama Biblia au Msaafu ndani ya Mahakama.

Sasa kama mtu aliyeapa akizungumza kwamba alining’inizwa kama popo, alikamatwa, amekamatwa Moshi na mwingine kinyume kabisa na sheria mahakamani baada ya kukamatwa wakaongozana naye kwenda kuwakamata watuhumiwa wengine, wamekuja mhakamani, wamesomewa kesi ya ugaidi, wamekuja kuiambia Mahakama mateso na madhila ambayo wameyapitia.

Wamenyimwa chakula kama Watanzania wakiwa ndani ya kituo cha polisi na mtu ambaye anatuhumiwa alikuwa ni kamanda Kingai na wenzake, walitajwa mahakamani kamanda Kingai, mateso na madhila yote ambayo walipitishwa ilikuwa hivyo lakini baadaye Mheshimiwa Freeman Mbowe alilalamika kwamba Kingai alimwambia kwamba baada ya kumkamata kwamba safari hii hauchomoki.

Maneno yapo kwenye vyombo vya habari na hakuna ambaye aliwahi kuja kuyakanusha. Sasa leo Kingai, mtesaji ambaye tuhuma zake zimesemwa mbele ya chumba cha haki cha Mahakama, Watanzania wamejua wote sasa hivi Kingai sifa yake kubwa anasifika kwa ukatili na utesaji dhidi ya wakina Adam Mohamed na wenzake na genge lake na kikosi chake ambacho kilipewa jina la TaskForce lakini leo anakwenda kupewa kazi kubwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mkuu wa Upepelezi wa makosa ya jinai nchini Tanzania.

Sisi kama wadau wa haki tumesikitishwa sana na kitendo hicho. Kwa hiyo, kama Mheshimiwa Rais anasikiliza maoni ya Watanzania na huenda nchi yetu ya Tanzania viongozi wanaotawala, washauri wa Rais, vyombo vikuu vya dola kama vilikuwa vinashauriana vizuri visingeruhusu haya yaendelee kwenye taifa letu.

Lakini baada ya uteuzi wa Kingai tuliona kwenye vyombo mbalimbali vya habari, mitandao ya kijamii ambayo imekuwa kama mitandao huru ambao wanaandika kwenye mitandao ya kijamii, hawakuridhishwa kabisa na uteuzi wa Kingai.

Huenda kama Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan angekuwa ni Rais msikivu, anayesoma maoni na kusikiliza, angetengua uteuzi wa Kingai. Lakini hilo halikufanyika na hatutegemei kama linaweza kufanyika.

Kwa sababu Rais wa Tanzania, katiba yetu imempa mamlaka makubwa, anaweza akafanya kitu chochote hata wananchi wakiongea hawasikilizi, kwa sababu huenda hana ridhaa yao.

The Chanzo: Rais Samia, mbali na kumteua Kingai na Wambura, lakini pia alitangaza kuunda kamati maalumu ya watu 12 ambayo alisema itamshauri namna bora za kufanyia mageuzi au maboresho mfumo wetu wa utoaji haki hususani mfumo wetu wa utoaji haki za jinai. Wewe unadhani kama ungepata fursa ya kumshauri Rais juu ya namna bora anavyoweza kuboresha huu mfumo wetu ungemshauri nini, ungemshauri kitu gani?

Twaha Mwaipaya: Kwanza Mheshimiwa Rais kamati ambayo aliiunda ya kuchunguza kuhakikisha haki ndani ya Jeshi la Polisi inafanyika, watu wanapata haki kwa wakati, ingeanza kuwachunguza kwanza aliowateua.

The Chanzo: Ingeanza kuwachunguza akina Wambura na Kingai unamaanisha?

Twaha Mwaipaya: Ingeanza kumchunguza Camillius Wambura, anatuhuma, na Kingai anatuhuma kubwa. Ile kamati aliyoiunda kwanza ingeanza kuwachunguza watu wale na baadaye sisi kama Watanzania tungekuwa tuna imani nao na yale majibu ambayo ingetuletea, tungejua kweli imekuwa kamati ambayo itakwenda kutenda haki katika mfumo wa utoaji haki nchini.

Lakini wateule ambao wanakwenda kusimamia huo uchunguzi ambao wapo kwenye vyombo hivyo vya ulinzi na usalama hususani Mkuu wa Jeshi la Polisi ana tuhuma. Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wa nchi anatuhuma.

Sasa wale ambao sisi tunahisi wanastahili kuchunguzwa ndio wamepewa vyeo. Sasa hii kamati kwa kweli haitupi matumaini kwani hatujaoneshwa kama kweli wana nia ya dhati kurejesha mfumo wa haki nchini.

The Chanzo: Lakini ni nini ungemshauri Rais.

Twaha Mwaipaya: Ambacho ningemshauri Rais kweli tunahitaji kufanya marejeo kwenye Jeshi la Polisi lakini kuunda kamati za uchunguzi peke yake sio suluhisho la kutengeneza Jeshi la Polisi.

Tunahitaji turejee kwenye mawazo ya wananchi, kulifumua Jeshi la Polisi lote na kulisuka upya na ukisoma wananchi walitoa maoni yao kwenye rasimu ya Jaji Warioba jinsi ya kulitengeneza Jeshi la Polisi kitu pekee ambacho kinaweza kumsaidia Rais ni kurejesha mchakato wa Katiba Mpya tutapata Jeshi la Polisi lililojema kabisa Tanzania.

Tutaunda kamati nyingi lakini haziwezi kutusaidia kwani wanaochunguza ni wale wale. Mwisho wa siku wanakuja kufanya kazi ni wale wale hata hatujawahi kuona uwajibishwaji mkubwa, hususan kwenye nchi yetu ya Tanzania hata watu wenyewe binafsi kujiwajibisha Tanzania hatuna hiyo historia.

The Chanzo: Uzuri umenileta kwenye suala la Katiba Mpya. Nini kinakupa matumaini kwamba tunaweza tukawa na Katiba Mpya kabla ya kufika uchaguzi wa mwaka 2025?

Twaha Mwaipaya: Muda mwingi sana katika historia ya nchi yetu ya Tanzania hatujawahi kupata matumaini ya haki kwenye taifa letu la Tanzania.

Watu wanateswa miaka yote, watu wanadhulumiwa haki mahakamani, watu wanakosa haki kwenye vyombo vya kisheria, lakini hata ukiangalia wananchi katiba haijawapa mamlaka makubwa na Tanzania inawatu zaidi ya milioni sitini lakini mtu aliyepewa mamlaka makubwa kwenye nchi hii ni Rais.

Tunahitaji kurejea kwenye rasimu ya Jaji Warioba na kuitazama upya Katiba ya mwaka 1977. Kitu cha kwanza, nchi yetu imekosa haki. Rasimu ya Jaji Warioba wananchi walitoa maoni yao kwenye rasimu kwamba tuwe na Mwenyekiti wa Haki za Binadamu ili watu wote ambao watanyimwa haki kwenye taifa letu la Tanzania, kama wananchi wa Tanzania, basi Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu wa Tanzania apewe jukumu la kuchunguza kwa haki na Watanzania waone kwamba kunahaki inatendeka na asimamie haki za Watanzania.

Kuna watu wameuawa hatujawahi kuona kesi sehemu yoyote, kuna watu wamepotea hatujawahi kuona miili yao, kaburi wala taarifa zao, akiwemo Azory Gwanda, Ben Saanane, [Simon] Kanguye wa kule Kigoma ambaye ni mwanachama wa Chama cha Mapinduzi.

Aliuawa Alphonce Mawazo na watu wakapiga kelele sana hapa Tanzania na watu wengi wamekuwa wakiuawa kwenye chaguzi lakini hakuna chombo cha kusimamia haki ambacho kweli kimesimamia haki na haki za watu hawa zimetendeka. Kwa hiyo, tunahitaji kuwa na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu ili asimamie jambo hilo.

Vile vile, tunahitaji Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania apunguziwe mamlaka aliyonayo.

The Chanzo: Naelewa. Lakini unadhani upo uwezekano wa kuipata Katiba Mpya kabla ya kufika mwaka 2025, una matumaini kwamba inaweza ikapatikana?

Twaha Mwaipaya: Tunaimani Chama cha Mapinduzi-, sisi kama Baraza la Vijana wa CHADEMA taifa kupitia Mwenyekiti wetu Mheshimiwa John Pambalu-, unajua sisi kama baraza BAVICHA na chama chetu tulipewa jukumu tusukume ajenda kwa Watanzania kupitia chama chetu na baraza letu, tulipewa jukumu la kuhakikisha tunahuisha mchakato wa Katiba Mpya nchini.

Na wewe nadhani unajua, umesikia, kwamba sisi tumezunguka na tumefanya kazi hiyo nchi nzima na mwanzoni wakati tunaanza Mheshimiwa Rais alisema kwenye vyombo vya habari kwamba yeye kipaumbele chake cha kwanza ni kujenga uchumi mambo ya Katiba yasubiri.

Na baadaye tulipozidisha moto mkali zaidi alisema kuna chokochoko zinaendelea ambazo zilikuwa chokochoko za Katiba Mpya. Bila shaka utakubaliana na mimi Mheshimiwa Freeman Mbowe alikamatwa usiku wa kuamkia kongamano la tarehe 21 kule Mwanza ambapo lilikuwa ni la Katiba.

Sisi Baraza la Vijana wa CHADEMA tuliliandaa na Mheshimiwa Freeman Mbowe akapewa kesi ya ugaidi na baada ya hapo sisi kama BAVICHA kwa kuhuisha mchakato tulifanya makongamano nchi nzima Tanzania kwenda kuwaambia Watanzania umuhimu wa maoni yao ambayo tayari wameshayatoa kwenye rasimu ya Jaji Warioba yanatakiwa yafanyiwe kazi.

Na haikuwa kazi rahisi, wala haitawahi kuwa kazi rahisi, wala hatujaridhika kitendo cha Chama cha Mapinduzi kutoka na kuwaambia Watanzania kwamba kimekubali kuandika Katiba Mpya, kimekubali kwamba mchakato wa Katiba Mpya urejeshwe, ni kauli njema yenye matumaini lakini inamashaka makubwa, waliokwamisha mchakato wa Katiba ni Chama cha Mapinduzi.

The Chanzo: Nadhani hapo tutakuja nilitaka nikuulize hilo lakini nadhani hujanijibu. Yaani mmefanya yote haya, na ni kweli, na ndio maana upo hapa, tumekuita hapa kwa sababu tumeona hiki unachokifanya na hizi kampeni kuzunguka nchi nzima, kufanya makongamano. Lakini ndio nataka kusikia kutoka kwako baada ya kufanya yote haya bado unamatumaini tunaweza tukapata Katiba Mpya kabla ya mwaka 2025?

Twaha Mwaipaya: Nimesema kitendo cha watu waliokwamisha mchakato wa Katiba Mpya, wakafika sehemu wakazungumza kuhusu Katiba Mpya, wakati wao walisema sio kipaumbele chao, sio hatua ndogo, ni hatua kubwa.

Na sisi hatujaridhika, hatujabweteka wala kauli yao haiwezi ikatufanya sasa tuachane na kudai Katiba Mpya, tukabweteka. Tunaendelea kuzungumza na Watanzania, tunaendelea kujiandaa sisi kama vijana wa Kitanzania, tunajua mstakabali mkubwa wa Watanzania ni vijana.

Kwa hiyo, sisi tusipoandika msingi mwema wa kuiandika Katiba ya nchi haijalishi wamesema nini, sisi tutaendelea kuweka mikakati kuhakikisha tunapata Katiba Mpya Tanzania. Kama tumeweza kuhuisha mchakato sasa hivi kila mtu akizungumza matatizo ya Tanzania anasema suluhisho ni Katiba Mpya.

Tumeshafanikiwa kwa awamu ya kwanza sasa tunakwenda kwenye awamu ya pili, tutakutana tarehe 11 tutakuwa na kikao kule Shinyanga kwenda kujadili sasa tunakwendaje mbele na baada ya kongamano letu la kikao cha kamati tendaji Shinyanga na kongamano la tarehe 12 ya mwezi wa nane tukitoka tutakuja kuwaambia Watanzania sasa tunakwenda hatua gani kuhakikisha Tanzania inaandika Katiba Mpya.

The Chanzo: Sawa sawa. Pale mwanzo uligusia hatua ya Chama cha Mapinduzi kujitokeza hadharani na kuunga mkono hayo madai ya Katiba Mpya. Unadhani hatua hii ni muhimu kiasi gani katika kufanikisha mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya?

Twaha Mwaipaya: Ni hatua njema kwa kila mtu ambaye anaitakia mema nchi yake ya Tanzania kwani Chama cha Mapinduzi tangu utawala wa awamu ya tano [chini ya] Rais John Pombe Magufuli na chama chake alisema Katiba Mpya kwake sio kipaumbele, [kwamba] anajenga uchumi.

Na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuanza mapema kabisa kwenye uongozi wake alisema Katiba Mpya kwake sio kipaumbele. Lakini leo hii yeye mwenyewe ameunda kikosi kazi, kama ambacho unakisikia, mtu alisema Katiba Mpya kwake sio kipaumbele.

Hafanyi kwa mapenzi yake bali umma wa Watanzania unamlazimisha kufanya hivyo. Na sisi kama Watanzania, kama wananchi, wadau wa haki kwenye nchi yetu ya Tanzania, hatuwezi kunyamaza hata akisema hataki tutamlazimisha atake kwani amepewa mamlaka tu ya kuongoza ila hana mamlaka ya kutawala na kuhakikisha mtu yeyote hana mamlaka ya kuamua mambo kwenye nchi yake ya Tanzania.

Kwa hiyo, sisi tunahitaji Katiba Mpya na Kenya hawakupewa Katiba mkononi, waliidai wakaipata. Zambia hawakupewa Katiba mkononi, waliidai wakaipata. Hata Afrika Kusini ni vivyo hivyo.

Kwa hiyo, sisi kama tutazungumza kwa maneno hatutaelewana. Ipo siku Watanzania wakizidi kuminywa, wakizidi kuumia, hakuna mtu atakaye mwambia aende barabarani akadai Katiba Mpya na mtu yeyote. Wote tutawakuta barabarani na wataipata Katiba yao kwa sababu ndio wataamini ndio suluhisho la kutatua matatizo yao yote ya Tanzania.

The Chanzo: Twaha mimi nakushuru sana, maswali ni mengi sana niliyonayo unajua mimi ni mdadisi kusema ukweli, napenda kufahamu vitu vingi hususani kwa watu kama ninyi ambao mnafanya vitu vingi huko chini. Ningependa kumalizia na swali ambalo naweza nikasema ni binafsi kidogo. Wewe kama kijana wa Kitanzania, kama mtu ambaye upo kwenye siasa, mtu ambaye unashiriki kikamilifu kwenye harakati za kuleta mabadiliko kwenye hii nchi, ungependa kuiona Tanzania ya aina gani?

Twaha Mwaipaya: Napenda binafsi kuona Tanzania yenye demokrasia ya kweli, maendeleo ya kweli na uhuru wa kweli. Napenda kuiona Tanzania ambayo vyombo na mihimili yote inatenda haki na haki inaonekana ikitendeka.

Napenda kuliona Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania likitunga sheria kama ambavyo kazi yake na kupitisha bajeti na kuisimamia Serikali. Napenda kuliona Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kama mhimili ukijisimamia wenyewe na ukitunga sheria ambazo zinakwenda kuisaidia nchi yake ya Tanzania.

Napenda kuiona Mahakama kama mhimili wa kutenda haki, asiwepo mtu yeyote mwenye mashaka na Mahakama, kusiwepo kuna mwingiliano kati ya Mahakama na Serikali Kuu. Napenda kuiona Tanzania ya hivyo.

Napenda kuiona Tanzania ambayo viongozi wa Serikali wakizungumza wanarejea Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania [na] hawataji jina la Rais kila wakati [na] kushindwa kurejea Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwani huwezi ukaenda Kanisani ukamkuta Padri, au ukaenda Msikitini ukamkuta Sheikh, amemaliza ibada bila kutaja Msahafu au bila kutaja Biblia, haiwezekani. Tunahitaji Tanzania watu warejee Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Wakifanya hivyo wataisaidia nchi yao ya Tanzania.

Mazungumzo haya yamebadilishwa kutoka kwenye sauti kwenda kwenye maneno na mwandishi wa The Chanzo Lukelo Francis. Stephen Gimbi na Joseph Kiraty wamesimamia na kuzalisha mahojiano haya. Kwa maoni yoyote kuhusiana na mahojiano haya, wasiliana na wahiri wetu kupitia editor@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Wakati fulani unapata hisia kuwa wapinzani walipendelea Samia aendelee kukataa katiba mpya ili tu waendelee kuwa relevant, wawe na cha kufanya

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *