The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Maafisa Waandamizi wa Serikali Wadaiwa Kuhongwa Mabilioni ya Fedha na Iliyokuwa Acacia

Taarifa inaonesha kampuni hiyo ilikuwa inalipa takribani Shilingi bilioni tatu kwa mwaka kwa maafisa wa kikosi kazi nyeti kinachohusika na usalama wa nchi.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Acacia, kampuni ya uchimbaji madini iliyokuwa na shughuli zake nchini Tanzania kabla ya kuingia kwenye mgogoro mkubwa na Serikali, inadaiwa kutumia takriban Shilingi bilioni tatu (Dola za Kimarekani milioni 1.2) kwa mwaka kulipa maafisa waandamizi wa Serikali kati ya 2008 na 2015, uamuzi ambao maafisa wa kampuni hiyo walilamika kwamba ulikuwa kinyume na sera zake dhidi ya rushwa na ufisadi.

Kwa mujibu wa barua pepe ambazo gazeti la nchini Canada la The Globe & Mail imezipata, Acacia, iliyokuwa moja ya kampuni kubwa za uchimbaji madini ya dhahabu nchini, ilikuwa ikilipa mabilioni hayo kwa watumishi wa umma waliokuwa wakifanya kazi kwenye kikosi kazi maalum cha ulinzi na usalama wa taifa, kinachojulikana kama NTF, au Tanzanian National Law Enforcement Taskforce.

Barua pepe hizo ziliibuliwa hadharani kwa mara ya kwanza kwenye kesi inayoendelea katika Mahakama Kuu ya Haki ya nchini Uingereza ambapo raia wa Tanzania wanaishitaki kampuni ya Barrick Gold, ambayo sasa imechukua umiliki wa Acacia, kwa madai walinzi wa kampuni hiyo wamekuwa wakipigaa risasa na kuwauwa ndugu zao.

SOMA ZAIDI: Mahakama Uingereza Kusikiliza Kesi ya Raia 10 wa Kitanzania Dhidi ya Barrick

Barua pepe hizo zinaonesha kwamba Acacia ilikuwa ikilipa hongo hizo kwa maafisa wanaokadiriwa kufika 60 waliokuwa wakifanya kazi NTF, ambacho kazi zake zinajumuisha kupambana na uhalifu mkubwa kama vile ugaidi na ufisadi na ambacho mkuu wake wake huripoti moja kwa moja kwa Rais wa nchi.

NTF inadaiwa kuundwa na maafisa kutoka Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa, na Jeshi la Wananchi.

Kikosi kazi nyeti

NTF kimekabidhiwa kazi ya kulinda miundombinu nyeti ya Serikali na ile ya sekta binafsi nchini, ndiyo maana pia kikawa kinahusika na kutoa huduma kwa Acacia, ambapo kulingana na mahitaji ya kampuni hiyo, NFT ilikuwa na vitengo vitano, kila kimoja kikiwa na maafisa kati ya watatu mpaka saba.

Vitengo hivi vinapatikana Kahama, ambapo vipo viwili, Tarime, Mwanza, na kitengo cha tano kikifanya kazi kwenye maeneo ambayo Acacia ilikuwa na maslahi nayo.

Kwa mujibu wa barua pepe zilizopatikana na gazeti la The Globe & Mail, malipo kwa kikosi kazi hicho yalikuwa tofauti na malipo ambayo Acacia ilikuwa ikilipa kwa Serikali kwa ulinzi ambao Tanzania ilikuwa ikitoa kwenye migodi na vituo vyake vya kazi.

Malipo ya Acacia kwa maafisa wa kikosi kazi hicho yalijumuisha malipo ya fedha za kujikimu, au per diems, ambapo barua pepe hizo zilizowekwa hadharani zinaonesha kwamba viwango vyake vilizidi viwango vya malipo ya posho ya kijikimu vilivyowekwa na Serikali kwa watumishi wake.

Mbali na malipo hayo ya fedha za kujikimu, maafisa wa kikosi kazi hicho wanaripotiwa pia kulipiwa malazi, chakula, na mafuta ya gari.

Ukiukwaji wa sera

Mazungumzo ya maafisa waandamizi wa Acacia yaliyofichuka baada ya barua pepe zao kuwekwa hadharani yanaonesha kwamba maafisa hao walikuwa na wasiwasi juu ya malipo hayo waliyokuwa wakifanya kwa maafisa wa Serikali, huku wengine wakikiri kwamba utaratibu huo unakiuka sera za kampuni zilizowekwa kupambana na rushwa na ufisadi.

Nick Rowell, moja ya viongozi waandamizi wa kampuni hiyo, kwa mfano, alisema kwenye barua pepe yake kwa wenzake kwamba malipo hayo kwa maafisa wa NTF yaliifanya Acacia “kutokuendana na sera zake juu ya kuzuia rushwa.” Kwenye barua pepe yake ya awali, Rowell alitaka malipo hayo “yasitishwe mara moja.”

Kiongozi mwingine mwandamizi wa kampuni hiyo, Peter Geleta, alisema kwamba baadhi yao wamekuwa wakilalamikia kuhusu malipo hayo kwa miezi 18, akiongeza, “Na ni wazi kwangu kwamba baadhi ya watu wetu wenyewe wamekuwa wakiulinda huu utaratibu.”

Hata hivyo, kulikuwa na hofu kwa baadhi ya viongozi wa kampuni hiyo juu ya namna malipo hayo yanavyoweza kusitishwa, huku wengine wakigusia ukubwa na nguvu ambazo kikosi kazi hicho kinazo, kikiwa na mafungamano na vigogo kwenye nafasi nyeti Serikalini.

Kwa mfano, mshauri wa masuala ya ulinzi wa kampuni ya Acacia, A.D Firth, alishauri kwamba kikosi kazi hicho kimekuwa kikilinda maslahi ya Acacia kwa kipindi cha muda mrefu, akisema, “Mabadiliko yoyote ya kimahusiano [kati ya Acacia na kikosi kazi] ni lazima yafanyike kwa umakini mkubwa siyo tu kwa sababu za kisiasa bali pia kiutendaji.”

Malipo hayo, ambayo barua pepe hizo zinaonesha kwamba yalikuwa yakizidi kuwa makubwa kila uchao, na ambayo yalikuwa hayajumuishwi kwenye bajeti ya ulinzi ya Acacia, yaliendelea mpaka Septemba 2015.

‘Hatuhusiki’

Ilipotafutwa na gazeti la The Globe & Mail, Barrick Gold, ambayo inamiliki na kuendesha migodi miwili nchini Tanzania, ule wa Bulyanhulu na North Mara, iligoma kujibu maswali kuhusu barua pepe hizo za ndani za Acacia.

Hata hivyo, msemaji wa kampuni hiyo, Kathy du Plessis, alikiambia chombo hicho cha habari kwamba Acacia ilikuwa na bodi na menejimenti huru mpaka pale Barrick ilipoibinafsisha hapo mwaka 2019.

Msemaji huyo alisema kwamba si Acacia wala Barrick walikuwa na udhibiti juu ya kikosi kazi hicho, au polisi, akiongeza kwamba kikosi kazi hicho hakikuhusika kwa namna yoyote ile kwenye ukiukwaji wa haki za binadamu ambao raia hao wa Tanzania wameifikisha Barrick mahakamani.

Kwenye kesi yao hiyo dhidi ya Barrick Gold, raia hao wa Tanzania wanadai kwamba kushindwa kwa soko hilo kufuata sheria zake zenyewe kwenye kutoa ithibati kwa dhahabu chafu kumekuwa na athari kubwa kwenye maisha yao.

“Tuna imani kwamba madai yaliyofikishwa mbele ya Mahakama ya hapo London hayana msingi wowote, na tunasubiri kwa Mahakama hiyo kupata fursa ya kuitolea uamuzi hii kesi na kuliweka hili jambo pembeni,” alisema du Plessis.

Kampuni ya Barrick Gold imekuwa ikikosolewa vikali na wanaharakati wa haki za binadamu na mazingira kwa madai ya uvunjifu wa haki za binadamu, hususan kwenye mgodi wake wa North Mara, uliopo mkoani Mara.

Mbali na kesi hiyo inayoendelea katika Mahakama ya London, Barrick pia inakabiliwa na kesi nyingine huko nchini Canada ambapo Watanzania 21 wameiburuza kampuni hiyo kortini, wakiishutumu kwa ukiukwaji wa haki za binadamu.

Barrick siku zote imekuwa ikikanusha vikali madai haya ya uvunjifu wa haki za binadamu, huku Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Mark Bristow akisema kwenye taarifa yake ya Disemba 13, 2022 kwamba kampuni yake ni kampuni inayoheshimu haki za binadamu na kudhamiria juhudi za maendeleo kwa taifa.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts