The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wananchi Dar Waendelea Kukilalamikia Kiwanda Kilichopigwa Faini na NEMC Kwa Uharibifu wa Mazingira 2016: ‘Hakuna Mabadiliko’

Kiwanda cha NIDA Textile Mills (T) LTD kinadaiwa kutiririsha maji taka kwenye Mto Kibangu, hali inayolalamikiwa kuwaathiri wananchi wa karibu.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Wananchi wa maeneo ya Mabibo na Kigogo jijini hapa wameendelea kukilalamikia kiwanda cha NIDA Textile Mills (T) LTD kilichopigwa faini na Serikali mwaka 2016 kwa kutiririsha maji machafu kwenye Mto Kibangu, wakisema uchafuzi huo bado unaendelea na kutishia afya na ustawi wao.

Kiwanda hicho cha nguo, kilichopo pembezoni mwa mto huo unaotiririka katikati ya mitaa ya Mabibo na Kigogo, kinadaiwa kutiririsha maji taka hayo na kuyafanya maji ya mto huo, ambayo yamekuwa yakitumiwa na wananchi kwa shughuli mbalimbali, ikiwemo kufulia, kutokuwa salama tena kwa matumizi ya nyumbani.

Wakiongea na The Chanzo iliyotembelea mitaa hiyo kwa nyakati tofauti hivi karibuni, wananchi wanaoishi pembezoni mwa mto huo wamelalamikia kitendo hicho cha kiwanda hicho, wakidai kwamba kumekuwa na kesi nyingi za wananchi kuharibika miguu, hali wanayodai inatokana na uchafuzi huo kwenye mto.

“Tuna kero kubwa sana juu ya maji haya ya [kiwanda cha] NIDA,” Christina Edward, mkazi wa Mabibo, mtaa wa Ngekewa, aliiambia The Chanzo wakati akiwa nje ya nyumba yake iliyopo mita kadhaa tu kutoka kwenye mto huo. 

Christina Edward, mkazi wa Mabibo, Mtaa wa Ngekewa, akizungumza na mwandishi kando kando ya Mto Kibangu. PICHA | LUKELO FRANCIS

“Maji [haya] yanatuathiri sana mpaka yanafikia hatua ya kuharibu mazingira yetu,” aliongeza mwananchi huyo. “Ukipita humo ndani ya maji, ukiweka mguu tu, yaani ukitoka pale na kuchubuka juu, yaani hatuna amani juu ya maji [haya].” 

“Hali ya hapa siyo nzuri kutokana na hiki kiwanda,” Najma Fanilimo, mkazi mwingine wa mtaa huo, alilamika. “Kiwanda hiki kinazalisha mali huko ndani, lakini tunaoathirika sana ni sisi huku wananchi.”

“Kuna muda wakizalisha mali zao huko ndani kuna moshi unatoka ni mkali sana, ule moshi unatuathiri watu wengi, siyo watoto wadogo tu hata sisi watu wazima,” aliongeza mwananchi huyo. “Tunaomba Serikali itusaidie.”

Kukata tamaa

Lakini licha ya kulalamika kwa miaka mingi kuhusiana na usumbufu wanaoupata kutokana na vitendo vya kiwanda hicho, wananchi hawa wamelalamika kwamba mamlaka husika zimeshindwa kuingilia kati, wakisema wameshakata tamaa kuripoti usumbufu unaotokana na kiwanda hicho.

Kombo Mohamed Rijebi, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kigogo Mkwajuni, aligoma kuzungumza na The Chanzo kuhusiana na kadhia hiyo, akisema ameshazungumza sana, akipaza sauti za wananchi kuhusu jambo hilo, lakini mamlaka husika zimeshindwa kuchukua hatua stahiki.

SOMA ZAIDI: Haya ni Baadhi ya Madhila Wanayopitia Wafanyakazi wa SBC Tanzania

“Historia ya pale imenichosha,” alisema mtumishi huyo wa wananchi. “Washakuja waandishi wa habari wengi, washakuja sijui NEMC, washakuja nani, lakini hatuoni mabadiliko ya aina yoyote. Sasa na sisi sasa hivi tunaona bora tunyamaze kimya kwa sababu tunaona hakuna tena linalofanyiwa kazi.”

Sehemu ya kiwanda cha NIDA ambayo maji taka yake hutoka na kuingia kwenye Mto Kibangu. PICHA | LUKELO FRANCIS.

NEMC ni kifupi cha Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, mamlaka ya Serikali yenye jukumu la kusimamia utunzaji endelevu wa mazingira nchini. Kwenye majukumu yake, NEMC husimamia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya 2004 ambayo inataja uharibifu wa mazingira kama kosa kisheria.

Kifungu namba 187 cha sheria hiyo kinatamka kwamba mtu yeyote ambaye “atamwaga kichafuzi chochote cha mazingira, kinyume na masharti ya sheria hii, atakuwa ametenda kosa,” na akipatikana na hatia atatozwa faini isiyopungua Shilingi milioni tatu na isiyozidi shilingi milioni 50, au kifungo kisichozidi miaka 12 jela, au vyote kwa pamoja.

Lakini wananchi wamelalamika NEMC kushindwa kukichukulia hatua kiwanda hicho licha ya ukweli kwamba mamlaka hiyo ilishawahi kukikuta kiwanda hicho hicho kukiuka matakwa ya sheria hiyo hapo mwaka 2016 na kukipiga faini ya Shilingi milioni 30.

Ukiukwaji huo wa sheria uliokuwa ukifanywa na kiwanda hicho ulibainika mnamo Agosti 4, 2016, baada ya aliyekuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina, akiambatana na aliyekuwa Mratibu wa Mazingira kutoka NEMC, Jafari Chimgege, kutembelea kiwandani hapo.

Kwenye ziara yao hiyo, watendaji hao waandamizi wa Serikali walibaini mapungufu mbalimbali ya miundombinu katika kiwanda hicho, ikiwemo maji taka kutiririka katika Mto Kibangu, na kuwapelekea kukitoza kiwanda hicho faini hiyo ya Shilingi milioni 30.

Kiwanda cha jibu

Mnamo Agosti 25, 2023, The Chanzo iliutafuta uongozi wa NEMC, Kanda ya Ubungo na Kinondoni, na kuuliza ni kwa nini mpaka sasa wameshindwa kuyafanyia kazi malalamiko hayo ya wananchi.  Uongozi huo uliomba kupatiwa wiki mbili ili kulitolea maelezo suala hili, lakini mpaka wakati wa kuchapisha habari hii, ulikuwa haujafanya hivyo.

Ulipotafutwa kujibu tuhuma hizo kutoka kwa wananchi, uongozi wa kiwanda hicho ulisema haufahamu uwepo wa malalamiko hayo ya wananchi, huku afisa mmoja kutoka kwenye kiwanda hicho aliyekataa kutoa jina lake kwa The Chanzo akisema kwamba kama malalamiko yangekuwa na ukweli, Serikali ingekwisha kukichukulia hatua.

SOMA ZAIDI: NEMC Kufanyia Kazi Madai ya Uharibifu wa Mazingira Unaofanywa na Kiwanda cha Wachina

Abel Dugange ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shahidi wa Maji, shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na utetezi wa matumizi sahihi ya rasilimali maji na ambalo limekuwa likifuatilia kwa karibu mgogoro uliopo kati ya wananchi wa Mabibo na Kigogo na kiwanda hicho cha NIDA Textile Mills (T) LTD.

Kwenye mahojiano na The Chanzo, Dugange alisema kwamba mamlaka zenye jukumu la kusimamia utunzaji mazingira kushindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo inachangia kwa kiwango kikubwa uchafuzi wa mazingira kushamiri nchini, hali aliyosema ni hatari kwa Tanzania kama taifa.

“Hiki kiwanda kinacholalamikiwa kimeshapigwa faini mara moja au mbili,” Dugange alisema. “Kwa hiyo, tunadhani pengine tatizo linachukua muda mwingi kutatuliwa kwa sababu kuna watu wana mahusiano na watu waliopo kwenye maamuzi, pengine, hatujui, ndiyo maana hali inakuwa hivi.”

Dugange, ambaye mwaka 2021 shirika lake lilichukua maji ya Mto Kibangu na kuyafanyia vipimo vya kimaabara vilivyoonesha kwamba maji hayo yameathiriwa na kemikali, alitoa wito kwa wananchi kutokuacha kupaza sauti kuhusiana na changamoto hiyo, akisema ni muhimu sauti nyingi zipazwe ili mamlaka husika zisikie.

Waandamana

Ikiwa ni sehemu ya jitihada zao za kupaza sauti kuhusu suala hilo, mnamo Julai 31, 2023, wananchi wanaoishi pembezoni mwa Mto Kibangu na kiwanda cha NIDA Textile Mills (T) LTD walifanya maandamano kuelekea kwenye kiwanda hicho, wakikitaka kuacha kutiririsha maji taka hayo kwenye mto huo.

Waandamanaji hao, ambao walikuwa kama 20, walikwenda nyuma ya kiwanda hicho ambapo maji hayo yanatiririshwa, wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe zilizoitaka Serikali kukichukulia hatua za kisheria kiwanda hicho kwa uharibu wake wa mazingira.

SOMA ZAIDI: Serikali, Wananchi Wavutana Kuhusu Uhalali wa Kukalia Eneo la Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo – RAZABA

“NEMC mko wapi, NEMC njooni huku muone maisha ya watu wanavyopata tabu, njooni huku tena. Mvifuate hivi viwanda wawaoneshe wanatibu maji wapi kabla hawajayaleta kwenye mto,” alisema Sakina Abdul, mmoja wa waandamanaji hao. 

“Oneni wenyewe maji wanayotiririsha hapa, hawayatibu, wangekuwa wanayatibu viumbe tungeviona, watu wasingepata athari,” aliongeza mwananchi huyo. “Maji ni uhai, lakini kwa sasa maji si uhai.”

Lukelo Francis na Hadija Said ni waandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Kwa mrejesho, wanapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com na hadijasaid826@gmail.com, mtawalia.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *