The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kocha Singida Amedokeza Tatizo Kubwa la Soka Letu

Tabia ya viongozi kuingilia majukumu ya makocha hailisaidii soka letu, linaiua.

subscribe to our newsletter!

Wakati kocha wa zamani wa Yanga na Singida United, Van der Pluijm akiwa hana timu, niliwahi kuwa na mazungumzo naye marefu wakati wa mechi moja ya Ligi Kuu ya soka ya Bara.

Miongoni mwa mambo yaliyokuwemo kwenye gumzo letu ni tabia ambayo tumekuwa tukiisikia ya viongozi kuingilia majukumu ya makocha, kiasi cha kutaka wachezaji fulani wawe hawakosi katika kikosi kinachoanza labda wakiwa majeruhi.

Pluijm hakutaka kuingia kwa undani sana kwenye mada hiyo, lakini akasema hicho ni kitu kibaya sana ambacho yeye hawezi kukikubali kwa jinsi yoyote na kwamba ikitokea kwake, basi ni ama ataweka rehani kibarua chake ama viongozi wakae mbali naye.

Baadaye akaajiriwa Azam Football Club, lakini hakudumu kwa maelezo kuwa alishindwa kupata matokeo mazuri katika mechi sita mfululizo za Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho. Pamoja na yote, wakati huo Azam ilikuwa inashikilia nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu nyuma ya Yanga.

Wakati fulani, kocha wa timu ya taifa, Kim Poulsen alikuwa anatatizwa na viwango vya wachezaji anaowaita timu ya taifa wakati kwenye klabu zao walikuwa wanaonekana kucheza vizuri kiasi cha kumvutia awateue timu ya taifa. 

Kupima utimamu

Poulsen aliamua kuomba sekretarieti ya TFF imnunulie kifaa maalum kwa ajili ya kupima utimamu wa wachezaji wanaoitwa timu ya taifa kabla ya kuanza kambi. Matokeo yake yalikuwa ya ajabu!

SOMA ZAIDI: CAF Imetuonyesha Uamuzi Wetu ni Janga

Mmoja wa wachezaji waliokuwa wakiimbwa sana na moja ya klabu kubwa nchini, alifeli kwenye vipimo hivyo licha ya kupewa nafasi mara tatu. Ndipo Poulsen alipoamua kuzungumza naye ajue nini hasa kimetokea hadi anashindwa kufikia sifa za utimamu wa mwili.

Kim anasema ilibidi mchezaji amwambie ukweli kwamba huko kwenye klabu yake huwa wanamdunga sindano za kupunguza maumivu ili aweze kucheza. Kumbe viongozi wa klabu yake walitaka kuhakikisha anakuwepo uwanjani hata wakati ambao ana jeraha lililokuwa linahatarisha soka lake.

Poulsen alilazimika kumuacha mchezaji huyo nyota na kuendelea na wengine aliokuwa amewaita. Ilikuwa ni jambo la kusikitisha kwamba mchezaji anachukuliwa kama mashine ambayo inahitaji mafuta kidogo ili iendelee na kazi, hata wakati ambao ilitakiwa ipate matengenezo kidogo ili ifanye kazi kwa ufanisi mkubwa.

Hivi karibuni, mchezaji nyota kutoka Nigeria, aliyeachwa wakati wa kipindi cha usajili, Nelson Okwa, aliondoka akiwa na manung’uniko aliyoyaweka bayana, lakini ilikuwa rahisi kuyapatia sababu kuwa alikuwa akitoa visingizio baada ya kuachwa.

Okwa alidai kuwa huwa anafanya vizuri mazoezini, lakini inapofikia mechi, kuna watu katika uongozi wa Simba huenda na orodha ya majina ya wachezaji wanaotakiwa kupangwa kwenye mechi husika. 

Okwa alionekana akitoa visingizio na hoja ya kumpinga ili kuzima hoja zake ilikuwa rahisi tu; alikuwa wapi siku zote? Ameona anaachwa ndiyo anatoa visingizio.

SOMA ZAIDI: Kocha Amrouche Ametoa Majibu ya Kapombe, Tshabalala, na Fei Toto Uwanjani

Ni rahisi kuielewa hoja ya kumpinga kwa sababu angeweza kuonyesha msimamo wa kupinga njama za kutopangwa hata kabla ya kutangazwa kuachwa, lakini alikaa kimya hadi janga lilipompata.

Lakini ukweli huwa haujifichi siku zote. Huwa unatafuta nafasi ya kujipenyeza hadi kujiweka bayana.

Kuingilia majukumu

Yapo maneno mengi kwamba viongozi wa klabu bado wana tabia ya kuingilia majukumu ya makocha, hasa upangaji wa timu na wanapokutana na makocha ambao wana misimamo, huwatafutia sababu za kuwatimua na malengo yao hutimia baada ya matokeo mabaya.

Huwezi kujua huwa wanatumia mbinu gani kuhakikisha makocha wenye vichwa vigumu wanapata matokeo mabaya ili nia ya kuwatimua itekelezwe. Lakini huwa inatokea hivyo na wengi wametimuliwa kwa jinsi hiyo.

Katika mazungumzo na baadhi ya viongozi, utabaini kuwa kuna mbinu inatumika kwa wachezaji ili matokeo ya kocha kichwa ngumu yawe mabaya. 

Baadhi utasikia wanasema, “Hata wachezaji wanasema hawamwelewi kocha” au wanasema, “Wanashangaa sababu za kumpanga” fulani badala ya fulani. Ukisikia kauli kama hizo unajua sumu imeshaingia kwa wachezaji na muda mfupi baadaye kichwa ngumu atatimuliwa.

SOMA ZAIDI: Kocha Adel Amrouche Awajibike Kwa Watanzania

Wiki iliyopita, kocha Mjerumani, Ernst Middendorp aliibua tena suala hilo baada ya kukubaliana kiungwana kuachana na klabu ya Singida Fountain Gate muda mfupi baada ya kuanza majukumu yake.

Kama inavyokuwa, Mjerumani huyo hakufanya vizuri katika michuano yenye muundo mpya ya Ngao ya Jamii, alipopoteza mechi zote mbili za nusu fainali na mshindi wa tatu. Kibaya zaidi, hakuanza vizuri Ligi Kuu ya Bara na ndipo ilipopatikana sababu ya kuachana naye, japo kiungwana.

Lakini katika mahojiano na kituo kimoja cha redio cha nje, Middendorp aliweka bayana jinsi viongozi wa Singida Fountain Gate walivyokuwa wakiingilia majukumu yake, hasa katika upangaji wa wachezaji.

Alisema akimpanga mshambuliaji mmoja, anaulizwa sababu za kumpanga tofauti na mwingine. Akipanga viungo wawili, anaulizwa sababu za kutowapanga viungo wengine wawili.

Alichokiona kikifuata ni viongozi kuanza kumpa majina ya wachezaji ambao wanataka wapangwe na hivyo akaamua kujitoa mapema ili hilo lisimfikie angali kocha mkuu wa Singida.

Na alisema aliweka bayana msimamo wake kwa mmiliki wa timu na menejimenti kwamba yeye ndiye anayejua wachezaji wanajituma vipi mazoezini na wapi ambao wanastahili kuanza na wanaotakiwa kuanzia benchi.

SOMA ZAIDI: Kukosa Uvumilivu Kunaigharimu Azam FC?

Maneno yake yanaibua maswali kwamba inakuwaje hao viongozi wasiende kuingilia majukumu yake mazoezini? Wanataka kuingilia majukumu yake ya kupanga timu tu na si kuiandaa?

Middendorp ametufungua vichwa ili tujua kuwa kile kinachoendelea uwanjani si kile ambacho makocha wengi wangependa kiwe. 

Bali kinachotokea kwenye viwanja vingi ni utashi wa viongozi kwa wachezaji fulanifulani tu na si mikakati ya watu waliopoteza muda wao kwenda kusomea taaluma ya ukocha na kusumbuka kubuni mbinu za kuwezesha timu zao kufanya vizuri.

Na inapotokea timu inashinda kwa kutumia vikosi ambavyo vimepangwa na viongozi, makocha ndiyo hukosa kauli kabisa, hata kama ni ushindi wa kubahatisha au ule unaotokana na maelekezo kwa waamuzi.

Utamaduni mbovu

Nilitegemea klabu ya kisasa kama Singida Fountain Gate ingekuwa inaendeshwa kisasa, lakini ndiyo imetumbukia kwenye utamaduni huohuo mbovu wa viongozi kutaka wachezaji wao ndiyo wacheze.

Kwa kweli, tunapoteza muda kama hatuachi upumbavu huu. Nauita upumbavu kwa kuwa kila mtu anajua njia sahihi ni ipi na nini kifanyike, si kama mpumbavu ambaye anaambiwa waya una umeme lakini bado anaenda kuushika.

SOMA ZAIDI: Kanuni Mpya TFF Inaua Uchumi wa Wachezaji

Middendorp amesaidia tu kudokeza tatizo kubwa lililopo katika klabu zetu. Hao makocha wengine bado hawajaamua kuwa jasiri kuzungumzia matatizo wanayopata, lakini nadhani ni makubwa zaidi ya hayo yaliyosemwa na Mjerumani huyo.

Tunahitaji kubadilika kiutendaji. Kama mtu aliomba kuwa kiongozi, basi ajihusishe na masuala ya kuongoza tu na si ya kiufundi ambayo hayajui hata kidogo zaidi ya kuwa shabiki kama wengine wote.

Kama aliomba kazi ya ukurugenzi wa ufundi, basi afanye kazi kulingana na adidu za rejea za kazi yake. 

Dunia ya leo ni ya mgawanyiko wa majukumu na hivyo kila mtu hana budi kufanya kazi kwa kadri adidu za rejea za kazi yake zinavyosema. Hapo ndipo kutakapokuwepo na weledi.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *