The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

CAF Imetuonyesha Uamuzi Wetu ni Janga

Tunahitaji mkakati wa kitaifa wa kuinua viwango vya waamuzi wetu wa soka ili tusomeke kimataifa.

subscribe to our newsletter!

Wakati fulani huko nyuma, ilikuwa ni tatizo kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika kutokana na idadi ndogo ya timu zilizokuwa zinatakiwa.

Awali, ilikuwa timu 12, na baadaye ikawa timu 16, hivyo kupenya kwenye kundi lenye nchi kama Nigeria, Cameroon, Ghana, Senegal, Algeria, Misri, Morocco na Tunisia ilikuwa kazi ngumu.

Lakini baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kulegeza utaratibu wake, sasa imekuwa ni habari kubwa tena kufuzu. Kuwa na fainali zenye timu 24 kati ya mataifa 54 Afrika, ni takriban nusu ya mataifa ya Afrika yanashiriki fainali hizo. Hivyo, kukosa kufuzu ndiyo tatizo kubwa kwa sasa.

Hivyo, habari kubwa inahamia katika mambo mengine kama hili la wiki tuliyoimaliza la nchi kushindwa kuwa na mwamuzi hata mmoja kwenye orodha ya waamuzi watakaochezesha fainali hizo za mwaka 2023 zitakazofanyika Januari mwakani nchini Ivory Coast.

Ilikuwa habari kubwa nchini kwa sababu orodha hiyo ndefu haina jina hata moja la mwamuzi Mtanzania na imeendeleza utamaduni huo wa nchi yetu kutokuwa na waamuzi wenye sifa za kusimamia mashindano hayo makubwa barani Afrika.

Tatizo la msingi

Ukibaini kwamba hata Nigeria imeshindwa kutuma waamuzi kwenye fainali hizo kwa mara ya pili mfululizo, unaweza kujifariji kuwa si Tanzania pekee. Lakini ukituliza kichwa na kufikiria kwa makini, utaona kuwa kuna tatizo la kimsingi linalosababisha waamuzi wetu wasifikie viwango vinavyohitajika.

Mjadala umekuwa mkubwa nchini kutokana na hali ya uamuzi ilivyo kwenye mechi za Ligi Kuu na hata za madaraja ya chini. Vituko vimetawala na hatua huchukuliwa kwa baadhi ya matukio tu.

Tukio kubwa la hivi karibuni ni lile la yule mwamuzi msaidizi katika mechi ya fainali ya Ngao ya Jamii aliyeshindwa kutoa uamuzi mara tatu baada ya kipa kuondoka katika mstari wa goli wakati wa mikwaju ya penati. Hadi leo hakujatoka tamko lolote la mamlaka ya waamuzi wala Shirikisho la Soka (TFF).

SOMA ZAIDI: Kocha Amrouche Ametoa Majibu ya Kapombe, Tshabalala, na Fei Toto Uwanjani

Hilo ni moja ya matukio mengi yanayotokea bila ya hatua zozote kuchukuliwa na ndiyo malezi yanayodekeza waamuzi wetu kiasi kwamba hawaoni kama wanawajibika kwa wananchi na mashabiki wa soka, bali kwa viongozi wanaowapanga kuchezesha mechi na matokeo yake ni kuporomoka kwa viwango vyao.

Uwajibikaji

Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) lilianza kujaribu utaratibu wa kuwalazimisha waamuzi kutoa maelezo kwa mashabiki uwanjani kuhusu maamuzi wanayofanya ili wawajibike zaidi. FIFA ilijaribu utaratibu huo wakati wa fainali za Kombe la Dunia za Wanawake na ulionekana kuwawajibisha zaidi.

Kampuni ya Waamuzi wa Mechi za Soka la Kulipwa England nayo imeanza kuwajibika kuomba radhi kwa klabu ambazo maamuzi ya marefa yameziathiri. Hii inaongeza uwajibikaji kwa waamuzi kwa kuwa kampuni hiyo haiwezi kuvumilia kuomba radhi mara nyingi kwa vitendo vya waamuzi wake.

Hizi zote ni hatua za kutaka kuboresha kabisa nyanja hiyo ambayo ni muhimu sana kwenye soka. Uamuzi mbovu, au uamuzi wa upendeleo, huondoa ile hali ya ushindani na kukatisha tamaa watu tofauti, wakiwemo wamiliki wa klabu, wawekezaji, mashabiki na watangazaji.

Tumeona hata Tanzania, mmiliki wa klabu ya Gwambina, Alexander Mnyeti, alivyoamua kuiondoa klabu yake Ligi Daraja la Kwanza kutokana na maamuzi ya ajabu ajabu. Mbali na kuiondoa kabisa kwenye soka, Mnyeti pia aliamua uwanja alioujenga kwa ajili ya soka, utumike kwa masuala mengine, mwenyewe akisema hata kwa ajili ya malisho ya mifugo.

SOMA ZAIDI: Kocha Adel Amrouche Awajibike Kwa Watanzania

Hadi leo baada ya CAF kutoa orodha hiyo ya awali hakujatokea tamko lolote kutoka mamlaka husika kuonyesha kusikitishwa au maelezo yoyote kuhusu orodha hiyo. Suala hilo limechukuliwa kuwa la kawaida na iwapo mamlaka zitatakiwa zitoe maelezo, nahisi zitatumia mfano huo wa Nigeria kuonyesha kuwa ni jambo la kawaida.

Weledi

Wakati Shirikisho la Soka (TFF) linaanza kutumia waamuzi vijana, niliwahi kuandika kuwa wamewahishwa sana kwa kuwa kwa mwamuzi hadi kufikia kuchezesha mechi za mashindano ya juu ya nchi anahitaji uzoefu wa angalau miaka mitano kwenye ligi za chini.

Haikuwa kitu kibaya kuanza kuzalisha kizazi kipya cha waamuzi, lakini ilitakiwa wapitie njia zilezile ambazo huwakuza kiweledi.

Lakini watoto wale wadogo wakapewa majukumu makubwa na kila walipokosea walikutana na mkono wa chuma, baadhi wakifungiwa kwa hadi miaka miwili bila ya kuwepo na programu zozote za kuwasaidia kujifunza pale walipokosea na kupewa mechi za madaraja ya chini, huku wakifuatiliwa maendeleo yao.

SOMA ZAIDI: Kukosa Uvumilivu Kunaigharimu Azam FC?

Matokeo yake, vijana wadogo wanapokosea bila ya kuwa na programu maalumu ya kuwasaidia, wanaharibika kabisa na hivyo uamuzi kuendelea kuwa wa hovyo.

Wakati tunaelekea mwishoni mwa msimu uliopita, takribani waamuzi 20 walifungiwa kwa makosa mbalimbali. Baadhi wamemaliza adhabu zao, lakini katika mechi zao za mwanzo tangu wamalize adhabu, wakafanya tena makosa makubwa. Kwa mtindo huo tutafika kweli?

Mambo ya posho

Kumekuwepo na madai kuwa shirikisho linaamua kutumia waamuzi hao vijana kwa kuwa wale wakongwe wanadai walipwe posho zao kwanza hivyo haliwataki. Mmoja amefungua kesi mahakamani mkoani Mwanza akidai malipo.

Kwa mtindo huo, hatuwezi kuwa na waamuzi wanaoweza kuaminiwa na CAF na hata FIFA. Labda tunaweza kusema hawapewi nafasi ya kuonekana, lakini hao wanaoitwa kuchezesha mechi za mashindano ya klabu ya CAF, au yale ya timu za taifa, wanafanya nini kuthibitisha ubora wao?

SOMA ZAIDI: Kanuni Mpya TFF Inaua Uchumi wa Wachezaji

Hiyo ndiyo nafasi ambayo inatumiwa vizuri na waamuzi kutoka Somalia, Eritrea, Djibout na Ethiopia kiasi kwamba inakuwa rahisi kuwaingiza kwenye kanzidata ya mashirikisho hayo na kuitwa kwenye mashindano makubwa.

Kwa kifupi, bado hatuna programu maalumu ya nchi kwa ajili ya kuboresha uamuzi wetu. Tunadhani mafunzo yanayotolewa na CAF na FIFA ndiyo pekee yanayoweza kuinua kiwango cha waamuzi wetu. Hapana!

Orodha ya CAF imetuonyesha kuwa uamuzi wetu ni tatizo kubwa na hivyo tunahitaji mkakati wa kitaifa wa kuinua viwango vya waamuzi wetu ili tusomeke kimataifa.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *