Wakati akizindua tovuti ya hifadhi ya nyaraka za Dkt.Salim Ahmed Salim, leo katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere,Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kuazishwa kwa tovuti maalum ya serikali itakayotoa nyaraka mbalimbali za kumbukumbu za viongozi.
Tovuti ya nyaraka za Dkt.Salim Ahmed Salim, ni tovuti inayoangalia maisha ya mwanadiplomasia huyo nguli; historia yake binafsi, elimu, historia ya kazi toka alivyoteuliwa kuwa balozi mpaka alivyoshika nyadhifa za juu kimataifa na hata nchini.
Hulka ya Dkt Salim kuandika na kuhifadhi kumbukumbu ya kila kilichotokea imeweza kugeuka mali adimu iliyowezesha tovuti hiyo kuazishwa.
Katika uzinduzi huo Rais Samia alieleza kuwa baada ya kusikia kwamba familia imeamua kuchukua jukumu hilo la kuweka kumbukumbu ya Dkt Salim, aliagiza serikali kutoa usaidizi muhimu kufanikisha suala hilo.
“Wanafamilia waliponiandikia kutaka nishiriki kwenye mradi huu na baadae kuzindua limenishtua kidogo nikasema kwa nini wanafamilia?, alieleza Rais Samia mbele ya washiriki waliohudhuria uzinduzi huo.
“Kwa hiyo nikamuambia Katibu Mkuu Kiongozi, kawaida kazi hii inatakiwa kufanywa na serikali lakini wanafamilia wameanza, naomba serikali ilibebe jambo hili na tulikamilishe kwa mafanikio makubwa,” aliongeza Rais Samia, katika hotuba yake aliyomtaja Dr Salim Ahmed Salim kama kiongozi mwadilifu.
SOMA:Mfuko wa Utafiti wa UVIKO-19 wa Amne Salim: Watafiti Wamebaini Nini?
Agizo la Rais Samia
Akitoa neno la shukrani baada ya uzinduzi wa tovuti hiyo mtoto wa tatu wa Dr.Salim, ambaye pia aliongoza mchakato huo kwa upande wa familia, Ahmed Salim anaeleza kuwa walipitia takribani picha 12,000 na nyaraka nyingi kuweza kuandaa tovuti hiyo.
“Huu mradi tuliuanza Oktoba 2021 na tulipitia maandiko mengi na picha kama 12,000,” alieleza Ahmed katika uzinduzi huo uliohudhuriwa na marafiki pamoja na wadau wengine waliofanya kazi kwa karibu na Dkt Salim Ahmed Salim.
Rais Samia ametambua jitihada za familia ya Dr.Salim, na kutoa agizo kwa serikali kuanzisha tovuti maalum itakayoweka historia mbalimbali za viongozi.
“Hivyo basi pamoja na jitihada hizo twende sasa tukatengeneze tovuti ya serikali ya kuweka kumbukumbu za viongozi wetu kama tulivyooneshwa na kaka yetu Dr.Salim Ahmed Salim,” alisema Dr.Samia.
Kwa sasa, wakati taasisi mbalimbali za serikali kama Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) huwa na nyaraka mbalimbali za kihistoria, utaratibu wa kupata nyaraka hizi umeendelea kutajwa na wadau mbalimbali kuwa sio rafiki.
Ili kupata baadhi ya nyaraka kama hotuba za viongozi, humhitaji mtu kuandika barua kwa mtendaji wa shirika hilo baada ya barua kupitiwa na ombi kukubaliwa ndipo hapo ndipo huweza kulipia kupata nyakara hizo.
Kama agizo la kuandaa tovuti malum litatekelezwa inamaanisha nyaraka hizi zitaweza kupatikana kiurahisi kabisa kwa wadau wote.
Chuo Cha Diplomasia Kufhamika Kama Chuo Cha Kidiplomasia Cha Dr Salim Ahmed Salim
Katika uzinduzi huo Rais Samia pia alitangaza kuwa Chuo Cha Diplomasia kilichopo Kurasini Dar es Salaam sasa kitabadilishwa jina na kuitwa kwa jina la Dr Salim.
“Kwa sababu mcheza kwao hutuzwa na tumesema alikua Mwanadiplomasia mahiri tumekubaliana kukipa chuo kile cha kidiplomasia jina na sasa rasmi kitakuwa kinaitwa Dr. Salim Ahmed Salim Centre of Foreign Relation,” aligusia Rais Samia.
Chuo cha Diplomasia kilianzishwa mwaka 1978 kupitia ushirikiano kati ya serikali ya Tanzania na serikali ya Msumbiji, kikiwa na lengo la kuwajengea uwezo na kuwezesha nchi hizo mbili kupata wataalamu wa diplomasia na anga za kimataifa.
Katika uzinduzi huo Rais Samia alithibitisha kuwa kwa sasa chuo hiko kinamilikiwa na Tanzania kwa asilimia 100 na kwamba serikali iko mbioni kufanya mageuzi makubwa katika chuo hiko.