Hivi, katika kuperuzi kwako Instagram, TickTock, Facebook au hata WhatsApp, ulishawahi kuona picha au video ya mtoto mdogo akiwa mtupu bila nguo? Je, uliwaza nini ulivyoona picha au video hiyo?
Bila shaka, kama wewe ni mtu unayejali ulinzi, usalama na utu wa mtoto, basi picha hiyo ilikushtusha na kukufanya ujiulize kwa nini mzazi, au mtu yeyote yule, alipakia picha hiyo mtandaoni.
Sheria ya Mtoto No. 21 ya mwaka 2009 inakataza na kutoa adhabu kwa mtu yeyote atakaye tengeneza, kuchapisha, au kuagiza kuchapishwa, kuonyesha, ama kuonyeshwa picha, au taswira ya mtoto aliye hai au amefariki akiwa mtupu bila nguo, akifanyiwa ukatili, au aliyefanyiwa ukatili bila kuficha utambulisho wake kama vile sura, majina yake, nakadhalika.
Sheria inatamka kwamba yeyote atakayekiuka masharti haya atakuwa ametenda kosa la jinai na atakapokutwa na hatia atalipa faini isiyopungua Shilingi 500,000 au kifungo cha miezi sita, au vyote kwa pamoja.
Lakini kiuhalisia, watu wengi, wakiwemo wazazi wenyewe, wanatenda kosa hili pasipo kujua. Mzazi unaweza kupakia video ya mtoto wake akiwa anacheza, au akifanya kitu cha kuchekesha kwa lengo la kuchekesha watu wengine, lakini hujatia maanani muonekano wa mtoto wake.
SOMA ZAIDI: Tuongee Kuhusu Matumizi ya Simu, TV na Mitandao kwa Watoto
Je, amevaa nguo inayomsitiri? Maneno, au matendo anayoyafanya yamkini ni ya kuchekesha lakini una uhakika hayatakuja kumdhalilisha baadaye? Haya ni mswali ya kujiuliza.
Wakati mwingine, mtoto amefanya kosa na kabla ya kumsahihisha, unamrekodi na kupakia video mtandaoni bila kuwaza kuwa chochote unachokiweka mtandaoni hakitafutika milele.
Mtoto wako atajisikiaje atakapoona hiyo video huko baadaye? Akienda shule, watoto wenzake watamchukuliaje? Na vipi kama hiyo video, au picha itatumika kumdhihaki akiwa mtu mzima?
Haya yote huchukuliwa kama utani, lakini mtoto wako anaweza kuathrika kisaikolojia; anaweza kuonewa shuleni na kuwa shabaha ya pedophile, au mtu anayevutiwa kufanya ngono na watoto wadogo, kwa sababu tu ya picha moja, au video uliyopeleka kwenye mitando ya kijamii.
Kadri utandawazi unavyozidi kuenea, ndivyo tunavyopaswa kujifunza na kutafuta mbinu za kuwa salama mtandaoni, na wewe mzazi ndiye mtu wa kwanza wa kumlinda mtoto wako.
SOMA ZAIDI: Je, Wazazi Tunajua Watoto Wetu Wanashinda, Kucheza Wapi?
Kabla ya kupakia video, au picha, za mtoto wako mtandaoni, tathmini lengo lako, muonekano wa mtoto wako, maudhui yake na athari zinazoweza kujitokeza hapo baadaye. Kumbuka, siyo lazima kila kitu anachokifanya mtoto wako kiende kwenye mitandao ya jamii.
Je, kuhusu zile video zinazosambaa zikionyesha watoto waliofanyiwa ukatili, au unyanyasaji, kwa lengo la kutoa elimu au kutoa taarifa? Hata kama nia ni nzuri, sheria inasimama vilevile, utambulisho wa mtoto lazima ufichwe na taarifa hiyo itolewe kwa mamlaka stahiki – Jeshi la Polisi, Ofisi za Afisa Ustawi wa Jamii na Huduma ya Simu kwa Mtoto – na siyo kuisambaza katika mitandao ya kijamii, haswa WhatsApp.
Mwisho, tukumbuke kuwa, kila mmoja wetu ana jukumu la kusimamia ulinzi na usalama wa mtoto mtandaoni. Ukiona video, au picha ya mtoto yeyote akiwa katika maudhui yaliyotajwa hapo awali, usiendelee kuperuzi tu na kusambaza zaidi, toa taarifa.
Taarifa yako inaweza kumsaidia mtoto wa mwenzako kuepukana na athari za picha na video hizo katika maisha yake ya sasa na ya baadaye.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.