The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Zanzibar Yachunguza Tukio la Mtuhumiwa Kufariki Mikononi Mwa Vyombo vya Ulinzi

Kijana huyo anadaiwa kupigwa na maafisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya hadi kupoteza maisha.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, Kanali Burhani Zuberi Nassoro ameiambia The Chanzo kwamba mamlaka hiyo inafanya uchunguzi juu ya tukio lililohusisha kifo cha mtuhumiwa akiwa mikononi mwa maafisa wa mamlaka hiyo, tukio lililoacha simanzi kubwa visiwani hapa.

“Ni kweli  tulimshikilia mtuhumiwa kwa ajili ya mahojiano na uchunguzi zaidi na kwa sasa uchunguzi unaendelea juu ya tukio hio na tutatoa taarifa pale uchunguzi utakapokamilika,” alijibu kwa ufupi Kanali Nassoro, huku akikataa kujibu maswali mengine ya mwandishi.

Mtuhumiwa huyo, aliyetambulika kwa jina la Hamed Mohammed Rashid, 45, mkazi wa Kinyasini, wilaya ya Kaskazini B, mkoa wa Kaskazini, Unguja, anadaiwa kufariki kufuatia kipigo kikali kutoka kwa maafisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar waliofika nyumbani kwake kwa ajili ya upekuzi maalumu.

Salma Said Saleh, mke wa marehemu, aliiambia The Chanzo kwamba usiku wa Septemba 26, 2023, majira ya saa tatu usiku, watu watatu walivunja mlango wa nyumba yao na kuingia ndani, wakiwa na mpira mnene wa maji, bunduki na bakora, wakijitambulisha kama askari wa kupambana na madawa ya kulevya, wakisema wamepata taarifa kwamba kwenye nyumba hiyo kulikuwa na madawa ya kulevya.

“Walichakura sana na kisha kuanza kumpiga mume wangu na huo mpira kisha wakanipiga na mimi,” alisimulia Salma huku akitokwa na machozi. Familia ya kijana huyo inasema wakati ni kweli alikuwa akitumia madawa ya kulevya, hakuwahi kujihusisha na uuzaji wake.

Baada ya kukosa walichokuwa wakikitafuta, maafisa hao wanadaiwa kumchukua Hamed, mke wake na rafiki yake Hamed aitwaye Ali Muhammad Mbarouk aliyekuwepo hapo nyumbani na kuwapeleka Kidimni, wilaya ya Kati, mkoa wa Kusini, Unguja ambako kuna kituo watuhumiwa wa madawa ya kulevya huhifadhiwa kwa ajili ya upelelezi.

Muonekao wa mikono ya Ali Mohammad rafiki wa Hamed aliyekamatwa nae ikionekana kuvimba mkono wa kulia.Mlango wa nyumba ya Hamed ambao ulivunjika na kurekebishwa.

Wapokea maiti

Salma, mkewe na Hamed, alitoka siku ya pili baada ya kufikishwa kituoni hapo, yaani Septemba 28, wakati Ali alitolewa Oktoba 2, 2023. Wakati wawili hao walitoka wakiwa hai, Hamed, aliyetoka Oktoba 1, alitoka akiwa amefariki, hali ambayo familia yake inaamini ilitokana na kipigo alichokuwa akipewa.

Abdallah Mohamed Rashid, kaka wa marehemu, aliiambia The Chanzo kwamba walifika kwenye kituo hicho mnamo Septemba 27 kwa ajili ya kumuwekea dhamana ndugu yao, lakini maafisa hao wa madawa ya kulevya walikataa, wakisema bado wanamuhitaji Hamed kwa ajili ya uchunguzi.

SOMA ZAIDI: Askari wa Uhifadhi Kilwa Wadaiwa Kukiuka Haki za Binadamu Wakihamisha Wananchi Kwenye Ardhi Yenye Mgogoro

“Nilimuona akiwa hoi, amechoka na dhaifu,” alisimulia Abdallah, ambaye anadai maafisa hao pia walimkatalia kumtibu mdogo wake. “[Hamed] alisema, ‘Kaka nitoe humu, nitakufa, mwambie baba awape wanachotaka mnipeleke hospitali, naumia.’”

Familia hiyo haikuweza kumpeleka kijana wao hospitali. Badala yake, walipokea simu kutoka kwa Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja, ikimtaka Abdallah afike hospitalini hapo kuangalia mwili wa ndugu yake.

Kabla ya kufikishwa Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja, Hamed alipelekwa kwanza Hospitali ya KMKM iliyopo Bububu, kisiwani Unguja ambapo Seif Mohammed Rashid, ndugu yake Hamed, alifika na kuuona mwili wa ndugu yake akiwa tayari amefariki.

“Alipotolewa na kuwekwa kwenye kitanda, niliona kabisa ndugu yangu ameshakufa,” Seif ameiambia The Chanzo. “Nikasema, inawezekanaje wanamchukua akiwa hai kisha wananipa maiti?”

Dk Machano Silima Ali ni daktari wa dhamana wa wagonjwa wa nje wa Hospitali ya KMKM alikiri kwenye mahojiano na Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) kwamba walimpokea Hamed akiwa tayari amefariki.

SOMA ZAIDI: Safari Yangu ya Gerezani Bila Kupitia Polisi Wala Mahakamani

“Ila kufika pale inaonesha katoka damu za mdomo, tulipomkagua tulimuona hivyo kashakufa tukampeleka Mnazi Mmoja,” Dk Machano aliiambia ZBC. “[Ilikuwa] ni majira ya 2:45 usiku na aliletwa na Mamlaka ya Kuzuia Madawa ya Kulevya.”

Mohamed Rashid baba yake Hamed Mohamed akiwa nje pembeni mwa nyumba yake huko Kisongoni -Kinyasini Unguja

Matumizi ya nguvu

Familia ya Hamed inaamini kwamba sababu kubwa ya kifo cha ndugu yao ni matumizi ya nguvu yasiyokuwa na ulazima wowote yaliyofanywa na maafisa wa madawa ya kulevya, yaliyohusisha kipigo na mateso kwa ndugu yao huyo na kupelekea kifo chake.

“Nilipofungua mwili niliona damu kwenye pua na kwenye masikio,” Abdallah anasimulia, akizungumzia alipofika Mnazi Mmoja kuchukua mwili wa ndugu yake. “Nikaomba uchunguzwe nini kimesabisha kifo chake, hivyo nilitolewa kisha nikaitwa, nikaomba wamgeuze huku mgongoni, nikaona mgongoni kuna alama ya rangi buluu kama damu na kwenye nyao zimepasuka na kuvimba.”

Hemed Swelu ni baba mdogo wa Hamed ambaye alikuwa miongoni mwa watu waliouosha mwili wake kabla ya kwenda kuzikwa, alikiri kwa The Chanzo kwamba wakati wa zoezi hilo waliukuta mwili wa Hamed ukiwa na alama za kuvimba na maboje.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, Ali Aziz Masoud, alithibitisha kupokea mwili wa Hamed, na kubainisha kwamba ripoti ya uchunguzi juu ya kifo chake tayari imekabidhiwa kwa Jeshi la Polisi.

SOMA ZAIDI: Takribani Mwaka Tangu Wapendwa Wao Wauwawe Kikatili, Familia Hizi Zataka Haki Kutendeka

Abdalla Abeid ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na haki za binadamu na ustawi wa vijana Zanzibar ZAFAYCO ambaye amelitafsiri tukio hilo kama uvunjifu wa haki za binadamu, akitoa wito kwa mamlaka za nchi kufuata sheria wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Kaburi la Hamed Mohamed ambalo liko kwenye shamba la familia nyuma ya nyumba yake huko Kisongoni -Kinyasini Unguja.

“Tumepata taarifa za tukio hilo na tumesikitika sana,” Abeid aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano. “Tunafuatilia kwa karibu ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka. Ni muhimu kwa askari kufahamu kwamba kutafuta haki haimainishi kuvunja haki, na tumekuwa tukiwafundisha hivi.”

Matumizi ya madawa ya kulevya ni tatizo kubwa visiwani Zanzibar, hali iliyoipelekea Serikali kwenye sehemu hiyo ya Jamhuri ya Muungano kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya mapema mwaka 2022 ili kuongeza jitihada za kukabiliana na janga hilo.

Najjat Omar ni mwandishi wa Habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *