The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wadau Wataka Mikataba ya Uwekezaji Katika Bandari Iwekwe Wazi

Inafuatia kauli ya Rais Samia kwamba mikataba ya uwekezaji iliyosainiwa ilizingatia maoni ya Watanzania kuhusu mkataba kati ya Tanzania na Dubai.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kushuhudia uwekaji saini kwenye mikataba mitatu ya uwekezaji kati ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Serikali na kampuni ya lojistiki ya Dubai, DP World, juu ya uendelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam, wadau wameitaka Serikali kuweka wazi mikataba hiyo kwa Watanzania.

Hafla ya uwekaji saini kwenye mikataba hiyo ilifanyika jana, Oktoba 22, 2023, katika Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma, ikiwa ni takriban miezi sita tangu Bunge liridhie mkataba kati ya Tanzania na Dubai unaoipa DP World kuchukua baadhi ya operesheni katika Bandari ya Dar es Salaam.

Hatua ya kusainiwa kwa mikataba hiyo pia inakuja wakati ambapo wananchi na makundi mbalimbali nchini yamekuwa na maoni mbalimbali kuhusiana na mkataba huo, huku kambi ya wanaoupinga ikichuana vikali na ile ya wanaoupongeza. 

Kwenye hotuba yake hapo jana, Rais Samia alisema Serikali ilisikiliza maoni ya kila mdau juu ya namna bora ya kuboresha mashirikiano hayo kati ya Tanzania na Dubai, akiunda timu maalum ya wataalamu iliyochambua maoni yote ya wadau ili kuhakikisha Tanzania inafaidika na mashirikiano hayo.

Hata hivyo, baadhi ya wadau waliotoa maoni yao punde baada ya mikataba hiyo kusainiwa, wameitaka Serikali kuweka wazi mikataba hiyo ili Watanzania waone kama kweli Serikali imechukua maoni ya wadau kama ambavyo Rais Samia amedokeza. 

SOMA ZAIDI: Mkataba wa Bandari: Matukio Muhimu Kuhusu Suala Linalogawa Maoni ya Watanzania

Moja kati ya watu waliotoa wito huo ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA (Tanzania Bara), Tundu Lissu, ambaye amekuwa mstari wa mbele kupinga mkataba huo, aliyetilia mashaka maelezo ya Rais Samia kama Serikali yake imezingatia maoni na ushauri wa Watanzania katika kuboresha mkataba huo.

Lissu, ambaye amezungumza akiwa nchini Marekani kwenye mkutano na Watanzania wanaoishi nchini humo, alisema ni ngumu kuamini maneno ya Rais Samia bila ya Serikali yake kuweka mikataba hiyo hadharani ili wananchi wote waione na kufanya maamuzi wenyewe.

Sijaona nakala

“Kuna kitu ambacho mimi sijakiona, kama kuna mtu miongoni mwenu amekiona anisaidie,” alisema Lissu kwenye mkutano huo. “Sijaona nakala hata moja ya hiyo mikataba. Mimi sijaiona, mitandaoni haijawekwa.”

“Kwa haya maneno mazuri ya mikataba kuzingatia sheria na kuzingatia maoni yetu, kwangu mimi nitaamini nikiona,” aliongeza Lissu. “Kwa hiyo, haya maneno mazuri haya, kwamba maoni yetu yamezingatiwa, pendekezo langu kwenu daini uthibitisho na uthibitisho [ni] kuchapishwa kwa mikataba yenyewe.”

SOMA ZAIDI: Sakata la Bandari: Je, Serikali Imepoteza Imani ya Wananchi?

Kwa upande wake, chama cha ACT-Wazalendo kimesema kwenye taarifa yake ya jana Jumapili kwamba licha ya baadhi ya mapendekezo yake kuchukuliwa, ikiwemo uwepo wa ukomo wa kuvunjwa mkataba, inaamini kwamba ni muhimu wa Serikali kuweka hadharani mikataba hiyo.

Wakati wa hafla ya utiaji saini hapo jana, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, alisema kwamba mikataba hiyo itakuwa na muda wa miaka 30, akiondosha utata uliokuwa umetanda miongoni mwa Watanzania waliokuwa na wasiwasi kwamba mkataba kati ya Tanzania na Dubai haukuwa na ukomo.

“ACT-Wazalendo tulipendekeza mikataba hii ya utekelezaji iwekwe wazi kwa umma,” inasema taarifa hiyo iliyosainiwa na Naibu Katibu wa Uenezi, Habari na Mawasiliano kwa Umma wa chama hicho, Janeth Rithe.

“Bado ni msisitizo wetu kuwa Serikali ina wajibu wa kuweka wazi kwa umma mikataba hii mitatu iliyosainiwa leo [Jumapili] kwa lengo la kuendesha Serikali kwa uwazi na kuongeza uwajibikaji,” iliongeza taarifa hiyo.

Naye Wakili Peter Madeleka, ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa mkataba wa bandari, amebainisha kwamba ili kuzihakiki kauli za Serikali kwamba maoni ya wadau wote yamezingatiwa, Serikali haina budi kuiweka wazi mikataba hiyo. 

Tunaomba nakala

“Wakati huo, tuliokuwa tunatoa maoni ya kizalendo, tulikuwa gerezani na wengine walipewa kesi za uhaini,” alisema Madeleka kwenye mtandao wa X, zamani Twitter. “Kama mmezingatia maoni, basi tunaomba nakala za hiyo mikataba.”

SOMA ZAIDI: Sakata la Bandari: Kamati Yaahirisha Kupokea Maoni ya Marekebisho ya Sheria za Maliasili Ikitaka Ufafanuzi wa Serikali

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, nadhani watu hawana wasiwasi wa kupoteza ajira, bali wana wasiwasi na kilichoandikwa kwenye mikataba kuhusu ajira,” aliandika Madeleka mtandaoni. “Uwazi wa mikataba hiyo ndiyo itathibitisha uhakika wa ajira bandarini.”

Mpaka wakati wa kuandika habari hii, The Chanzo haikuwa inafahamu kwamba mikataba hiyo imewekwa wazi kwa umma wa Watanzania. The Chanzo ilitembelea tovuti ya Bunge na ile ya TPA lakini ilishindwa kuona kama mikataba hiyo imechapishwa.

Wito kwa Serikali kuweka wazi mikataba ya uwekezaji inayoingia na wawekezaji umekuwa ukitolewa mara kadhaa na wadau wanaoamini kwamba hatua hiyo itasaidia kuongeza uwazi na uwajibikaji kwenye uwekezaji unaofanyika nchini.

Sauti za kudai uwazi kwenye mikataba zimeenda mbali zaidi na kuitaka Serikali iweke wazi mikataba ya mikopo inayoingia na wakopeshaji, kama ambavyo CHADEMA ilifanya mnamo Disemba 15, 2022.

Katibu Mkuu wa chama hicho cha upinzani nchini, John Mnyika, aliwataka wana CHADEMA kuchukua jitihada za kudai uwazi kwani kuna hatari kubwa za mikataba ya mikopo ya Serikali kutowekwa wazi. 

SOMA ZAIDI: Jenerali Ulimwengu: Sakata la Bandari Limeonesha Tumepoteza Uwezo Kujadiliana kwa Hoja

“Hatari kubwa zaidi ni juu ya nchi yetu na rasilimali zake kwa sababu, kwa bahati mbaya, mikataba ya mikopo inayokopwa kwa wingi mkubwa haiwekwi hadharani,” alisema Mnyika.

“Sisi tupo kimya kama taifa, hatudai mikataba kuwa wazi,” aliongeza kiongozi huyo. “Hatudai kuulizia hizi pesa zilizokopwa zimetumika kwenye nini chenye tija, na kiasi gani, ambayo inarudisha ile bila kulazimika kuingia kwenye hatari ya mbele kama taifa.”

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam unaweza kumfikia kupitia lukelo@thechanzo.com.  

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *