Kila wakati yanapoibuka malalamiko kutoka kwa vijana kuhusu ushirikishwaji hafifu kwenye uongozi wa umma hapa nchini kwetu, sauti husikika zikikosoa wale wanaoibua malalamiko hayo, zikisema ushirikishwaji wa vijana, ambao ni watu wenye umri kati ya miaka 18 na 35, upo wa kutosha Serikalini.
Lakini tujiulize, ni kweli hali ilivyo ni kama vile wadau hawa wanavyotanabahisha? Kwa tathmini yangu mimi, niliyoifanya kwa kuangalia vyombo na sekta chache tu za kimkakati, ushirikishwaji wa vijana, ambao wanasiasa hupenda kuwaita nguvu kazi ya taifa, upo kwa kiwango kidogo sana, hali isiyoakisi hali yetu halisi kama taifa.
Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 yanaonesha kwamba asilimia 50 ya Watanzania wana umri wa miaka 18 kwenda chini, huku theluthi mbili ya Watanzania wakiwa na umri wa miaka 35 kwenda chini. Hali hii haiakisiwi kwenye Baraza la Mawaziri, Bunge na Mabalozi wanaoteuliwa kwenda kuiwakilisha Tanzania duniani.
Baraza la Mawaziri
Nimeamua kuanza na Baraza la Mawaziri kwa sababu hiki ndiyo chombo kikuu cha maamuzi hapa nchini kwetu. Kwa sasa, Baraza la Mawaziri lina wajumbe 30, likijumuisha Rais, Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu na mawaziri 26.
Kwenye baraza hilo, kwa mujibu wa tathmini yangu, hakuna mjumbe hata mmoja mwenye sifa ya ujana, yaani hakuna mjumbe aliyezaliwa baada ya mwaka 1988.
SOMA ZAIDI: Vijana Wachachamaa Wakitaka Umri wa Kugombea Upunguzwe
Pia, baraza zima lina wajumbe wawili tu ambao wamezaliwa miaka ya 80 ambao ni Jerry Silaa, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, aliyezaliwa mwaka 1982, akiwa na umri wa miaka 41 na Jumaa Aweso, Waziri wa Maji, aliyezaliwa mwaka 1985, akiwa na umri wa miaka 38.
Tukitoka kwenye Baraza la Mawaziri, tuangalie Bunge ambacho ndiyo chombo kikuu cha kutunga sheria nchini. Mhimili huo wa dola una jumla ya wabunge 391, ukijumuisha wale wa kuchaguliwa, wa viti maalum, na wakuteuliwa.
Kulingana na tathmini niliyoifanya mimi mwenyewe, kati ya wabunge 391, ni wabunge 31 tu waliochaguliwa wakiwa vijana. Kati ya wabunge vijana 31, 16 wamezaliwa miaka ya 90.
Mbunge mdogo kuliko wote – Ng’wasi Damas Kamani, Mbunge wa Viti Maalum, Chama cha Mapinduzi (CCM) – alizaliwa mwaka 1996, akichaguliwa bungeni akiwa na umri wa miaka 24. Kati ya wabunge vijana 31 ni wabunge saba tu ambao ni wanaume.
SOMA ZAIDI: Sababu za Mwamko Mkubwa wa Vijana Kugombea Nafasi za Uongozi Zatajwa
Je, wanawake wanaandaliwa zaidi kua viongozi kuliko wanaume? Huu ni mjadala wa siku nyingine. Kwa leo, tumalizie kwenye sekta nyingine nyeti kwenye utawala wa umma, Mabalozi, na kuangalia ushirikishwaji wa vijana kwenye sekta hiyo.
Mabalozi
Tanzania kwa sasa ina watumishi 60 wenye hadhi za ubalozi, ikiwa na mabalozi waliopo vituoni 48 na 12 ambao wapo wizarani. Kati ya hao 60, hakuna hata mmoja mwenye sifa na vigezo vya kuitwa kijana. Na usije hapa na habari kwamba vijana hawawezi kuwa wanadiplomasia.
Ikumbukwe kwamba Salim Ahmed Salim aliteuliwa kua balozi akiwa na umri wa miaka 22 tu. Inawezekana hiyo ilikua enzi hizo, ila kama Salim aliweza kua balozi na umri mdogo wa miaka 22 na kuja kua mwanadiplomasia hodari kuwahi kutokea Tanzania, naamini wakina Salim wengine wapo wengi tu.
Hapa nimeamua kuweka mifano michache tu ili kuweza kujenga hoja yangu – kwamba ushirikishwaji wa vijana kwenye uongozi wa umma hauridhishi na kwamba Serikali na wadau wengine watapaswa kufanya jitihada zaidi kubadilisha hali hii – lakini uchambuzi kwenye sekta zingine zote za uongozi wa umma naamini utakuja na matokeo haya haya.
Hali hii, kwa vyovyote vile, inapaswa kubadilika kwani bila uwakilishi kwenye nafasi za maamuzi, ni vigumu kwa matatizo ya vijana, ikiwemo janga la ukosefu wa ajira, pamoja na changamoto nyinginezo nyingi, hazitaweza kupata ufumbuzi unaohitajika.
SOMA ZAIDI: Barua ya Wazi kwa Wanasiasa Vijana wa CCM Kuhusu Rais Magufuli
Kama vijana waliweza kuwa katika nafasi ya mbele kwenye kulitafutia taifa hili uhuru wake, na kama vijana waliweza kuhudumu katika nafasi kubwa na nyeti mara tu baada ya uhuru, ni nini kinachozuia vijana wa sasa kua na mchango huo huo? Tutafakari kwa makini!
Kuna mambo kadhaa ambayo Serikali inaweza kufanya ili kuwapa vijana nafasi za uamuzi zaidi, ikiwemo kuboresha taratibu zake za uajiri ili iwe rahisi kwa vijana kupata kazi Serikalini.
Pili, Serikali inaweza kuunda mazingira ambayo vijana wanajisikia huru kutoa mawazo yao na maoni yao. Tatu, Serikali inaweza kuwapa vijana wenye uwezo nafasi zaidi za uongozi katika Serikali.
Hatma ya taifa
Vijana ndiyo watakaokuwa wakiongoza nchi yetu katika siku zijazo. Kwa kuwapa nafasi za uamuzi sasa, tunaweza kuhakikisha kwamba hatma ya nchi yetu iko kwenye mikono ya watu walio na uwezo na maono.
Vijana wengi wenye vipaji na uwezo wanapuuziwa wakati wa kuchagua watu kwa nafasi muhimu nchini. Hii ni kwa sababu Serikali, mara nyingi, huzingatia mrengo wa kisiasa na uaminifu badala ya vipaji na uwezo wakati wa kufanya uteuzi.
SOMA ZAIDI: Haya Hapa Matukio Muhimu Kwenye Safari ya Kisiasa ya Paul Makonda
Ni muhimu kwa Serikali kuzingatia vipaji na uwezo wakati wa kuchagua vijana kwa nafasi muhimu nchini. Vijana wenye vipaji na uwezo wanaweza kuchangia maendeleo ya nchi kwa njia nyingi.
Kwa mfano, wanaweza kuja na mawazo mapya na ubunifu, wanaweza kutumia ujuzi wao na uzoefu wao kutatua matatizo, na wanaweza kuwahamasisha vijana wengine.
Vijana ni nguvu kazi muhimu na yenye uwezo mkubwa wa taifa lolote. Wao ni wabunifu, wenye nguvu, na wamejaa mawazo mapya. Wana uwezo wa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya nchi yao ikiwa watashirikishwa vya kutosha katika maamuzi muhimu.
Wakijisikia kama sauti zao zinathaminiwa, na kwamba wanaweza kuchangia katika maamuzi yanayowahusu, vijana watakuwa na uwezekano mkubwa wa kushiriki katika siasa na kuisaidia nchi yao kukua na kuendelea.
Kwa hiyo, ni muhimu sana kwa Serikali, Asasi za Kiraia na sekta binafsi kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha kwamba vijana wana nafasi ya kushiriki katika maamuzi yanayowahusu na yanayoathiri maendeleo na ustawi wa nchi yao.
Thomas Joel Kibwana ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na uhusiano wa kimataifa. Unaweza kumpata kupitia thomasjkibwana@gmail.com au Twitter kama @tkibwana. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.