The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wananchi Buhongwa Wafurahia Kuimarika kwa Huduma Kituo cha Afya Bulale

Ni baada ya miradi mitatu iliyogharimu mamilioni ya fedha kukamilika na kuanza kufanya kazi, ikiwafurahisha wananchi.

subscribe to our newsletter!

Mwanza. Wananchi wa Bulale, kata ya Buhongwa, wilaya ya Nyamagana, mkoani hapa wamefurahia kuimarika kwa huduma za afya zinazotolewa katika Kituo cha Afya cha Bulale, wakisema hali hiyo siyo tu imewapunguzia gharama za matibabu bali pia imewaepusha kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo.

Kuimarika kwa huduma hizo kunatokana na kukamilika kwa miradi mitatu kituoni hapo, ukiwemo ule wa chumba cha upasuaji uliogharimu Shilingi milioni 124.7, jengo la mionzi uliogharimu Shilingi milioni 49.6, na jengo la kufulia uliogharimu Shilingi milioni 26.9.

Miradi hii ni baadhi ya miradi ambayo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aiinishe kwenye ripoti yake ya Machi mwaka huu ambayo imeshindwa kutumika licha ya Serikali kuikamilisha kwa kutumia fedha nyingi za walipa kodi.

Ni kati ya miradi mbalimbali katika vituo vya afya vilivyokamilika kwa thamani ya Shilingi bilioni 4.93 katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 16 ambayo ilishindwa kuanza kutumika kama ilivyotarajiwa, huku CAG akitaka hatua za haraka kuchukuliwa ili miradi hiyo ianze kutumika.

The Chanzo inaweza kuthibitisha kwamba miradi mitatu katika Kituo cha Afya cha Bulale imeanza kufanya kazi, ikisaidia kwa kiwango kikubwa katika kuboresha huduma za kiafya kwa wakazi wa eneo hilo na maeneo ya jirani.

SOMA ZAIDI: Vituo vya Afya vya Tozo za Miamala Vyashindwa Kuwahudumia Wananchi Mbeya, Songwe

Kuanza kazi kwa miradi hiyo kunafuatiwa na uzinduzi wake uliofanyika Julai 15 Julai, 2023, na kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023, Abdallah Shaibu Kaimu, wakati Mwenge huo ulipopita Nyamagana, Mwanza.

Mariam Kahinda ni mama wa watoto watatu ambaye ameiambia The Chanzo kwamba kuanza kufanya kazi kwa huduma za upasuaji na mionzi katika Kituo cha Afya cha Bulale ni ukombozi kwa akina mama wajawazito wanaoishi karibu.

“Zamani tulikuwa tunahangaika,” anasema Mariam anayejishughulisha na biashara ya mboga na matunda. “Ukibeba mimba uende mpaka Buhongwa, au ukitaka kujifungua mpaka uende Butimba. Sasa hivi mimi naona hali ni nzuri, watu wanahudumiwa hapa karibu. Hatuangaiki tena.”

Mwananchi mwingine, Samweli Renatus, anasema huduma hizi zimeleta tabasamu kwa wanawake na wanaume wa Bulale.

“Tuna furaha kwa sababu huduma ziko karibu, ukipata tatizo unakimbia haraka haraka,” anaeleza baba huyo wa watoto wanne. “Ukiona kama wameshindwa hapa, unaona gari inakuja kuwachukua, wanapiga simu.”

SOMA ZAIDI: Huduma za Afya ya Akili Ziingizwe Kwenye Huduma za Mama na Mtoto

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, kata ya Buhongwa inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wakazi jijini Mwanza, ikiwa na jumla ya watu 67,254 ambao sasa wanategemewa kunufaika na maboresho ya huduma hizo za afya katika Kituo cha Afya cha Bulale.

Lakini siyo wananchi wa Bulale na kata ya Buhongwa tu wanaotegemewa kunufaika na kuimarika kwa huduma katika Kituo cha Afya cha Bulale bali hata wananchi wa Misungwi wanaripotiwa kutafuta huduma kituoni hapo kwani kipo karibu na wao.

Diwani wa kata ya Buhongwa, Joseph Kabadi, ameieleza The Chanzo kwamba wananchi wa maeneo jirani wanavyonufaika na huduma katika kituo cha afya Bulale. 

“Kituo hiki cha afya kinahudumia watu wengi sana,” Kabadi anaeleza. “Wengine wanatoka nje ya kata ya Buhongwa, wilaya jirani ya Misungwi maeneo kama Idetemya.”

Kabadi alikiri kwamba kukamilika kwa miradi hiyo kunawasidia wakazi wa Bulale na kata ya Buhongwa kwa ujumla, akitoa wito kwa wananchi kuwapa ushirikiano wa kutosha wafanyakazi wa kituo hiki ili kutoa huduma bora na zenye uhakika.

SOMA ZAIDI: Walazimika Kujifungulia Nyumbani Baada ya Kituo cha Afya Kukosa Wahudumu

Wadau wanaamini kwamba kufanya kazi kwa miradi hii ambayo CAG aliiainisha katika ripoti yake kutasaidia kupunguza hasara itokanayo na kupungua kwa thamani ya fedha iliyotumika katika miradi hiyo kutokana na uchakavu pale inapoanza kutumika pamoja na kuyafikia malengo yaliyokusudiwa.

Alex Makaro ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Mwanza. Unaweza kumpata kupitia matonyingamakaro@gmail.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *