The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tunawezaje Kunufaika na Uwepo wa Watu Kama Joe Chialo, Waziri Jijini Berlin Mwenye Asili ya Tanzania?

Serikali inachukua jitihada gani ili watu kama Chialo watoe mchango kwenye ujenzi wa nchi?

subscribe to our newsletter!

Tuna ugeni mkubwa sana hapa nchini kwetu hivi sasa, na huu si mwingine bali ule wa Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, Dk Frank-Walter Steinmeier. 

Rais huyo, akiwa na msafara wake, aliwasili nchini Novemba 30, 2023, kwa ziara ya siku tatu na kupokelewa na Januari Makamba, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 

Rais Steinmeier anatarajiwa kutembelea Songea, mkoani Ruvuma, mnamo Novemba 1, 2023, ambako atatembelea Makumbusho ya Vita ya Maji Maji pamoja na Shule ya Msingi ya Maji Maji iliyopo wilayani humo. 

Ikumbukwe kuwa kwenye mkoa huo, Vita ya Maji Maji ilirindima kati ya mwaka 1905 hadi 1907 ambapo Mmatumbi, Kinjekitile ‘Bokero’ Ngwale, ‘aliwapiga fiksi’ wenzake baada ya kuwafanyia usangoma kwenye miili yao na kuwaambia risasi za Wajerumani zitageuka maji zikiwagusa tu na hivyo hazitawaua. 

Hata hivyo, takriban Waafrika 200,000 wanakisiwa kupoteza maisha kwenye vita hiyo inayosifika kwa kuweka msingi wa harakati za baadaye za ukombozi dhidi ya wakoloni.

SOMA ZAIDI: Elizabeth Maruma Mrema: Mfahamu Mtanzania Aliyetajwa Miongoni Mwa Watu 100 Mashuhuri na Jarida la TIME

Joe Chialo

Kwenye msafara huo, Rais Steinmeier ameongozana na wawekezaji kutoka makampuni makubwa 12 na viongozi wa Serikali. Kwenye msafara huo pia yumo ‘Mtanzania’ Joe Chialo ambaye ni Waziri wa Utamaduni huko Berlin, Ujerumani.

Chialo aliukwaa uwaziri huo mwaka huu, Aprili 2023, na kuandika historia mujarab, akiwakilisha chama cha Christian Democratic Union (CDU). Chialo, ambaye ni mwimbaji, alizaliwa mwaka 1970 huko Bonn,  Ujerumani. Ana mke na binti mmoja. 

Chialo ni mtoto wa marehemu Balozi Isaya Bakari Chialo aliyewahi kuwa Balozi wetu nchini Ujerumani, China, na Japan. 

Wazazi wa Chialo mdogo walikuwa wakiizunguka dunia kuhudumu ubalozini, hivyo ikabidi wamuache na kaka yake skuli ya bweni ya kikatoliki ya Salesian Don Bosco iliyopo jirani na jiji la Cologne ambako ndiko kijana huyo alipata elimu yake.

Baada ya skuli, Chialo alisomea Siasa, Historia na Sayansi ya Siasa katika elimu yake ya chuo kikuu kabla ya kuachana na mambo ya kubundi ili kuuitikia wito wake wa kuwa mwanamuziki.

SOMA ZAIDI: Mtanzania Afariki Marekani Baada ya Kushambuliwa na Risasi

Chialo ni raia wa Ujerumani ingawa mwanzoni haikuwa rahisi kwa yeye kuipata hadhi hiyo. Akiwa na mwili uliojengeka vyema kutokana na kuwa mtu wa mazoezi, Chialo pia aliwahi kuwa ‘bouncer’ katika klabu ya Nuremberg Discotheque.

Baada ya kumaliza chuo mwaka 1997, Chialo alianza kujihusisha na muziki ambapo alijiunga na lebo ya Sony Music na akawa mwimbaji wa Blue Manner Haze. Mwaka 2002, Chialo alijiunga Universal Music, kampuni kubwa ya muziki ulimwenguni, na kuhamia Berlin. 

Mnamo mwaka 2020, Chialo akachaguliwa kuwa Makamu wa Rais Mtendaji, au Executive Vice President kwa kimombo, wa kampuni hiyo ambapo majukumu yake makubwa yalijumuisha kuwatafutia ‘michongo’ wanamuziki wa Afrika huko Ujerumani na Ulaya kwa ujumla.

Chialo alijiunga na CDU mwaka 2016 baada ya kufurahishwa na uamuzi kuntu wa Angela Merkel, Chansela mstaafu wa Ujerumani, na ambaye alikuwa mwana-CDU, mwaka 2015 wa kuwakaribisha wahamiaji waliokuwa wakikimbia vita nchini Syria.

Kwenye tawasifu yake, Chialo anajitambulisha kama ‘a proud Afropolitan.’ Mwaka 2019, alipewa heshima ya kuwa kwenye jopo la majaji wa Ujerumani kwenye ‘The 2019 Eurovision Song Contest.’

SOMA ZAIDI: Kitila Mkumbo: Hoja za Wanaopinga Uraia Pacha Hazina Mashiko

Baada ya kuhudumu kwa miaka mingi kama Balozi, baba yake Chialo mdogo, Balozi Chialo, alirejea nchini na kisha akastaafu. Mama yake Chialo mdogo ni Theopista Chialo, ambaye, pamoja na kaka zake, wote wanaishi hapa Tanzania.

Je, kuna Watanzania wengine kama Chialo huko nje ya nchi? Je, kama taifa, tutafaidikaje kuwa na mwenzetu kama waziri huko Berlin, ambao ndiyo mji mkuu wa Ujerumani?

Je, wanamuziki wa Tanzania, hususan wa Bongofleva, wametumiaje uwepo wa Chialo kujipatia ‘michongo’ kimuziki? Je, Chialo atatusaidiaje kurudisha mafuvu ya Watanzania waliopelekwa Ujerumani, akiwemo shujaa mwanamke wa Kinyaturu, Liti Lerti Kidanka? 

Shujaa huyu aliwasambaratisha Wajerumani kwa kutumia nyuki hadi aliposalitiwa na hatimaye kukamatwa, kukatwa kichwa na kisha kupelekwa Ujerumani. 

Uwanja unaotumiwa na timu ya Singida Fountain Gate FC wa CCM LITI umepewa jina hilo kwa heshima ya shujaa huyu!

Mzee wa Atikali ni mwandishi na mchambuzi kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia +255 754 744 557. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *