The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Serikali Kuchunguza Madai ya ‘Upigaji’ Ujenzi wa Kituo cha Polisi Butiama

Ukigharimu jumla ya Shilingi milioni 802, ujenzi wa kituo hicho cha polisi umezua gumzo miongoni mwa Watanzania waliowengi.

subscribe to our newsletter!

Mwanza. Serikali imesema kwamba inachunguza madai ya ‘upigaji’ wa fedha za umma katika ujenzi wa Kituo cha Polisi Daraja B wilayani Butiama, mkoani Mara baada ya kuibuka taarifa kwamba jumla ya Shilingi milioni 802 zilitumika kujenga kituo hicho, hali iliyoibua maswali mengi miongoni mwa Watanzania.

Akiongea na waandishi wa habari hapo Jumatatu, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Jumanne Sagini alisema wizara hiyo inayohusika na usimamizi wa Jeshi la Polisi imeunda tume maalumu kuchunguza ujenzi huo ili kujiridhisha kabla ya kuchukua hatua yoyote ile.

“Kwa hiyo, hii timu iliyoundwa na Wizara ya Mambo ya Ndani inakwenda kujiridhisha,” Sagini, ambaye pia ni Mbunge wa Butiama (Chama cha Mapinduzi – CCM), aliwaambia wanahabari. “Je, hivyo viwango vilivyowekwa vya milioni 802 kwa aina ya jengo liliojegwa pale, ni sahihi? Kama siyo sahihi, huyu aliyefanya hivyo alikuwa na dhamira gani?

Mkandarasi wa ujenzi wa kituo hicho cha polisi, SP Masiva Mfinanga, alisema hapo Novemba 18, 2023, wakati Sagini alipotembelea ujenzi huo, kwamba mradi huo una thamani ya Shilingi milioni 802, ambapo ujenzi ulianza rasmi Mei 6, 2023, na unategemewa kukamilika mwishoni mwa mwezi Disemba 2023.

Kufuatia taarifa hiyo, Watanzania wengi nchini, hususan kwenye mitandao ya kijamii, walionesha kushangazwa na matumizi hayo makubwa ya fedha za umma katika ujenzi wa Kituo cha Polisi.

SOMA ZAIDI: Je, Ubadhirifu Serikalini Unaweza Kudhibitiwa? Wataalamu Wanaamini Hivyo

Jengo linalozungumziwa lina ukubwa wa mita za mraba 737 na jumla ya vyumba 31 na vyoo 15, likitarajiwa kubeba ofisi za OCD, OCCID, DTO na OCS. 

Pia, lina mahabusu sita zenye uwezo wa kuchukua watu kati ya 50 na 60, ikiwemo mahabusu mbili za watoto chini ya miaka 18, kwa wanaume na wanawake, mahabusu kwa ajili walemavu, na mahabusu za watu wazima kwa jinsia zote mbili.

Kufuatia kelele za walipakodi, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mtanda, alifanya ziara kwenye mradi huo na kutoa ufafanuzi wa jinsi pesa hizo zilivyotumika, akikanusha madai kwamba ujenzi huo umegharimu kiasi cha milioni 802, akisema kwamba kiasi hicho ni makadirio ya mradi wote mpaka pale utakapokamilika.

Mtanda alisema kwamba mpaka sasa mradi huo umetumia kiasi cha Shilingi milioni 366 na siyo Shilingi milioni 802 kama inavyodaiwa, akieleza kwamba Serikali imeshatoa Shilingi milioni 500 kwa msimamizi wa mradi huo ambaye ni Kamanda wa Jeshi la Polisi (RPC) wa mkoa wa Mara na Shilingi milioni 302 bado haziidhinishwa.

Mtanda aliongeza kwamba kati ya Shilingi milioni 500 iliyotolewa na kuingizwa kwenye akaunti ya benki ya RPC Mara, kiasi cha Shilingi milioni 43 zimetumika kuwalipa wananchi wa eneo hilo waliopisha ujenzi huo, huku kiasi cha Shilingi milioni 91 ikiwa haijutumika kwenye mradi bado. 

SOMA ZAIDI: Ripoti ya CAG: Je, Ufisadi Unatokana na Udhaifu wa Serikali au ni Tatizo la Kijamii?

Kiasi cha Shilingi milioni 48 kimeombwa kwa ajili ya malipo ya gharama za ufundi, gharama za uhifadhi mafuta kwa ajili ya mradi, na kumlipa msambazaji na gharama za umeme. Licha ya malipo hayo kuidhinishwa, bado hayajalipwa, huku kiasi cha Shilingi milioni 42.4 kikiwa hakijatumika kwani bado unaendelea, Mtanda alibainisha.

Lakini akizungumza kwenye mkutano wake na wanahabari hapo Jumatatu, Sagini alisema kwamba tume iliyoundwa itaenda kuchunguza kwa kina iwapo matumizi yaliyotolewa yanaendana na uhalisia.

“Ndiyo maana tumeweka timu ya wataalamu wabobezi kwenye eneo hilo la ukaguzi na eneo la ukadiriaji majengo,” alisema Sagini. “Mtu wa kawaida tu ukiona unaweza usielewe. Lakini kwa sababu tumetuma wataalamu, taarifa yao itatusaidia tuweze kufanya uamuzi.”

Matonyinga Makaro ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Mwanza. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia matonyingamakaro@gmail.com. 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *