The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ni Majukumu Yepi Ya Kitaifa Yanamzuia Dkt. Mpango Kuonekana Hadharani?

Sidhani katika hali ya kawaida Dkt. Mpango angeacha kutoa pole au kusafiri hadi Hanang kuwapa pole waathirika wa maafa.

subscribe to our newsletter!

Siku zote wahenga wanasema siri huzua tetesi, tetesi huzua uzushi, na uzushi huzua taharuki na sintofahamu. Maneno haya napenda sana kuyazingatia kwa sababu babu yangu naye alipenda sana kuitumia busara iliyopo kwenye maneno haya ya wahenga kuwasihi watoto wake.

Ni mwezi sasa Makamu wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. Philip Isdor Mpango hajaonekana hadharani.  Jambo hili hasa kwenye mitandao ya kijamii limepelekea kuzua  tetesi ambazo nazo zimeanza kuzua uuzushi wa aina mbalimbali.

Hatujui nini kitafuata baada ya uzushi unaonednelea kwenye mitandao ya kijamii, pengine ndiyo itapelekea kile wahenga waliona kuwa mwishowe uzushi huzua taharuki na sintofahamu.

Sitaki kuwa sehemu ya kusambaza tetesi na uzushi, lakini tukubaliane na ukweli kwamba si kawaida kwa kiongozi mkuu wa kitaifa kutoonekana hadharani kwa zaidi ya mwezi.

SOMA ZAIDI: Aidan Eyakuze: Ni Wajibu wa Wananchi Kusimamia Uwazi, Uwajibikaji Serikalini

Pamoja na kwamba siku chache zimepita tangu Watanzania kuelezwa kwamba anaendelea na majukumu ya kitaifa.  Lakini hatujui ni majukumu gani, wala anayafanyiaa wapi? Hatufahamu kama tunapaswa kumuombea kiongozi wetu au kumpongeza kwa majukumu mazito yanayomfanya asionekane hadharani kwa zaidi ya mwezi.

Ukipitia tovuti rasmi ya Ofisi ya Makamu wa Raisi utaona kwamba mara ya mwisho kuwekwa taaria yoyote inayo muhusu yeye moja kwa moja ni Oktoba 28, 2023. Taarifa hiyo ina kichwa cha habari “Dkt. Mpango: Taasisi za fedha ziwezeshe mikopo viwanda vidogo kukuza uzalishaji” 

Katika mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter) kwenye ukurasa wa Makamu wa Raisi napo mara ya mwisho kuchapishwa  taarifa zake ni Oktoba 28, 2023 alipokua kwenye ziara ya kikazi mkoani Njombe. 

Ukiachana na taarifa iliyosambaa Disemba 4, 2023 ikimuonesha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akilaani tetesi zinazoendelea mitandaoni kuhusu kutoonekana hadharani kwa Dkt. Mpango, Disemba 5, 2023 tena lilisambaa bango likimuonyesha Dkt. Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kongamano la 14 la Kimataifa la Sayansi iliokua lifanyike Arusha kati ya tarehe 6 hadi 8 Disemba, 2023. 

SOMA ZAIDI: Waandishi Mwanza Watathmini Hali ya Uhuru wa Habari

Watanzania wakasubiri kwa shauku kumuona Makamu wa Raisi. Kwa bahati mbaya tarehe ikafika na badala yake Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki akamuwakilisha Makamu wa Rais. Waziri Kairuki akautaarifu umma ya kwamba kaagizwa na Makamu wa Raisi kumuwakilisha na kwamba alikua akiendelea na majukumu mengine ya kitaifa. 

Kongamano hilo liliandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) ambayo ni ya Serikali. Swali ni kwamba ina maana TAWIRI ambayo ni taasisi ya Serikali ilikua haijui kwamba Makamu wa Raisi hatakuepo na badala yake wakachapisha bango lenye picha yake masaa machache kabla ya tukio?

Wiki hii pia, taifa limeshuhudia maafa makubwa ya mafuriko yaliyotokea wilayani Hanang, mkoa wa Manyara yaliyosababisha vifo vya watu takribani  75 na majeruhi zaidi ya 115. Maafa haya yalisababisha hadi Rais Samia Suluhu Hassan akatize ziara yake ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE)  na kulazimika kurudi nchini kuungana na Watanzania wengine kuwafariji waathirika wa maafa hayo. 

Hata hivyo, Makamu wa Rais, ambaye tunaambiwa anaendelea na majukumu yake ya kitaifa, hajaonekana hadharani kutoa pole wala kutuma ujumbe wa pole kutoka alipo. Makamu wa Rais ni mtu mkarimu sana. 

Sidhani katika hali ya kawaida Dkt. Mpango angeacha kutoa pole au kusafiri hadi Hanang kuwapa pole waathirika wa maafa. Je, ni majukumu gani ya kitaifa yanamzuia Dk. Philip Mpango kutoa hata pole?

Binafsi, sijui ni nini kinaendelea, lakini ni dhahiri kwamba kuna kitu kinaendelea ambacho wananchi hatukifahamu. Katika zama hizi za mitandao, ni vigumu sana kudhibiti uvumi, kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Kwa uelewa wangu mdogo, hakuna kazi zozote ambazo Makamu wa Raisi anazofanya ambazo zitamlazimu kuzifanya kwa kificho kama shushushu. 

Lakini ni  vigumu kuelewa kwa nini wananchi wanapaswa kufichwa kwa sababu zozote zile. Katika suala hili, sidhani ni lazima tukajifunze ughaibuni, hapa Tanzania kabla ya utawala wa awamu ya tano, hata ilipotokea viongozi wakuu wa nchi wanakabiliwa na changamoto ya maradhi wananchi walipewa taarifa.

Hayati Benjamini Mkapa mwaka 2003 akiwa madarakani alienda Uswisi kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa mguu uliokua ukimsumbua. Raisi Mkapa alikaa takribani miezi mitatu akipatiwa matibabu. Katika kipindi hicho tulitaarifiwa kuhusu safari ya raisi kwenda kutibiwa, tulipewa mrejesho wa mara kwa mara jinsi matibabu yalivyokua yanaendelea, tukapewa na gharama zilizotumika kumtibia. 

Kumbuka kwamba kipindi hicho ilikuwa ni wakati hamna mitandao ya kijamii ambapo Serikali ingeweza kutuficha lakini wakaamua kufanya vile ambavyo ilipaswa kufanywa kwa Serikali yake iliyojitanabaisha kwa uwazi.

Sasa kama Dk Mpango anaugua, na nasisitiza sina hakika kwa sababu hakuna taarifa zozote zilizotolewa kama ni mgonjwa, basi ningeshauri Serikali yetu ingetuweka wazi. Kama ilivyokuwa miaka ya nyuma walipougua viongozi wetu kama Mwalimu Nyerere, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.

Kama nilivyosema awali, hadi sasa zinazosikika zaidi ni tetesi tu. Hakuna anayejua zaidi ya wale wanaojua, au kama ule msemo wa kimombo unaosema “those who know, know.” Sisi wananchi tutaendelea kumuombea huko alipo, tukitarajia kumuona tena hadharani hivi karibuni, akiendelea na majukumu yake ambayo yanamruhusu kuwasiliana na wananchi anaowaongoza. 

Kama mwananchi wa kawaida, nimalizie tu kwa kuisihi Serikali yetu kupitia msemo usemao kwamba iwapo hutaidhibiti hadithi, basi hadithi itakudhibiti.

Thomas Joel Kibwana ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na uhusiano wa kimataifa. Unaweza kumpata kupitia thomasjkibwana@gmail.com  au Twitter kama @tkibwana. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *