Kitaalamu, kuna aina au njia nne kuu za malezi, kwa kimombo wanasema parenting style, na wazazi hutofautiana katika njia kutumia njia hizi. Aina hizi hujenga mahusiano tofauti kati ya mzazi na mtoto, pia, hupelekea matokeo tofauti katika makuzi ya watoto.
Tuzitazame aina hizi za malezi pamoja na athari zake, kisha, tujitathmini ni aina ipi ya malezi tumekuwa tukiitumia kwa watoto wetu au ni aina ipi tungependa tuanze kutekeleza.
Mosi, ni malezi ya kidemokrasia; Haya ni malezi ambayo wazazi hutumia nguvu nyingi kujenga mahusiano mazuri na watoto huku wakiwaeleza sababu zinazopelekea sheria na maelekezo wanayowapa. Katika aina hii wazazi, hutilia maanani hisia za watoto wao na kuhakiksha wanakuwa na furaha.
SOMA ZAIDI: Tunavyoweza Kuwafundisha Watoto Kuwa Salama Wakati Wanacheza
Wataalamu wa malezi wanatuambia kuwa malezi haya ndiyo yaliyo bora zaidi kuliko aina nyingine kwani wazazi huwapa nafasi watoto kukabiliana na changamoto za maisha ili kuwajengea ujasiri. Pia, huwapa maelekezo muhimu ya kujiepusha na tabia au mienendo hatarishi na kuwapongeza watoto wao wanapoziishi tabia na maadili mema.
Wazazi hawa huwa na muda wa kutosha kuwasikiliza watoto wao na kuwaonyesha upendo kila wapatapo nafasi. Watoto wanaolelewa kupitia aina hii ya malezi huja kuwa na uwezo mkubwa wa kujiamini, mafanikio, wanakua wenye furaha na mara nyingi huishia kuwa wazazi bora kwa watoto wao huko baadae.
Mbili, ni malezi ya kimabavu; Haya ni yale ambayo wazazi huamini kuwa watoto wanahitaji uangalizi tu huku wakifuata sheria walizowaekea bila kupinga. Katika malezi haya hisia, mawazo na mitazamo ya watoto haisikilizwi. Wazazi hutumia zaidi maneno kama ‘mimi nimesema’ na ikitokea mtoto amepinga au hata kuuliza sababu, huishia kukaripiwa au kupigwa na kusisitiziwa kuheshimu na kutii maamuzi ya mzazi. Watoto wanaolelewa kupitia mfumo huu hukosa uthubutu, hawajiamini na mara nyingi ni wakatili wasiowathamini wala kujali hisia za wenzao.
SOMA ZAIDI: Je, ni Upi Umri Sahihi wa Kumpeleka Mtoto Shule ya Bweni?
Tatu, ni malezi huru; Haya ni malezi ambayo wazazi huweka sheria na maelekezo yakufuatwa na watoto wao lakini hawayatilii maanani wala kufatilia kama watoto wametekeleza maelekezo yao. Wazazi wa aina hii huwadekeza watoto na huhofia kuwakaripia wala kuwakwaza hata kidogo wakiamini kuwa watoto wao watajifunza zaidi bila kufuatiliwa.
Pia, wazazi huwasamehe watoto kila wakikosea bila kujali uzito wa makosa yao. Watoto hawa huwa hawawezi kufanya maamuzi wenyewe bila kumshirikisha mzazi hata akiwa mtu mzima mwenye familia yake.
Nne, ni malezi huria; Kwenye aina hii mzazi hafuatilii muenendo wa mtoto wake shuleni wala kwenye maisha yake ya kila siku, hawajihusishi hata kidogo na mahitaji wala maendeleo ya watoto wao. Wanatumia muda wao mwingi wakijikita na mambo yao binafsi kama ajira.
SOMA ZAIDI: Mtoto Anapaswa Kuwafahamu Wazazi Wake, Ndugu na Familia Tandaa
Mara nyingi watoto wenye wazazi kama hawa hulelewa aidha na dada wa kazi au ndugu wa karibu. Asilimia kubwa huishia kutokufanya vizuri darasani na kuwa wenye utovu wa nidhamu.
Kama umefika sehemu hii ya makala yetu, basi utakua umetambua aina gani ya malezi unaitumia kuwalea watoto wako. Je, aina hiyo inamjenga mtoto wako kuwa mtu wa aina gani? Je, umependezwa na aina yako ya malezi?
Ni muhimu kujitahidi kadri ya uwezo wako kuwa na aina ya malezi yanayojenga upendo, amani, ujasiri, uthubutu na thamani ndani ya mtoto wako bila kumsababishia madhara yoyote.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.
One Response
Nimejifunza kitu