Mwanza. Tukiwa tumebakiza siku chache kuukamilisha mwaka 2023, yapo matukio mengi yaliyotokea mwaka huu kwenye medani za siasa na kwa namna moja ama nyingine kuikutanisha Serikali na vyama vya upinzani kwenye meza moja huku baadhi yakizifanya pande hizo kuendelea kuhasimiana.
Moja ya tukio kubwa lililotokea mapema Januari 3, 2023 ni lile na kuondolewa kwa marufuku ya mikutano ya hadhara nchini. Kuondolewa kwa marufuku iliyowekwa tangu mwaka 2016 kuliviwezesha vyama vya upinzani kuifurahia haki hiyo ya kikatiba.
Baada ya zuio hilo kuondolewa vyama vya siasa kama vile CHADEMA, ACT Wazalendo pamoja na CUF vilipongeza uamuzi huo na kuanza kufanya mikutano yake sehemu mbalimbali nchini kwa ajili ya kutangaza na kunadi sera zao kwa wananchi.
SOMA ZAIDI: Maswali Fikirishi Kuhusu Falsafa ya 4R ya Rais Samia
Kuondolewa kwa zuio la kufanyika kwa mikutano ya hadhara halikuwa tukio pekee lililowapatanisha Serikali ya Chama Cha Mapinduzi na vyama upinzani. Yapo matukio mengine ambayo nayo pia yalionekana kuwapatanisha.
Rais Samia kuwa mgeni rasmi kwenye tukio la BAWACHA
Katika hali ambayo haikuwa imezoeleka Rais Samia Suluhu Hassan aliridhia kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ulioandaliwa na Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA).
Tukio hilo lilitokea Machi 8, 2023 huko mkoani Kilimanjaro ambapo Rais Samia alikwenda kwenye mkutano huo baada ya kupewa mwaliko na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe.
Kitendo hicho kilionesha jinsi pande hizo mbili zinavyoweza kuwa kitu kimoja katika baadhi ya mambo licha ya uwepo wa upinzani mkubwa dhidi ya hatua hiyo ndani ya vyama vya CCM na CHADEMA.
Alipokuwa akihutubia mkutano huo Rais Samia ambaye aliambatana na baadhi ya viongozi wa Serikali alitilia mkazo ajenda ya maridhiano na kutolipa kisasi na aliwataka wanachama wa CHADEMA kusahau yaliyopita na kuendeleza ushirikiano wa kulijenga taifa la Tanzania.
Uteuzi wajumbe ZEC
Hatua nyingine iliyowaunganisha upinzani na Serikali hususani kwa upande wa Zanzibar ni hatua ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi kuteua wajumbe 6 wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
SOMA ZAIDI: Tumechelewa Kupata Katiba Mpya Kabla ya Uchaguzi, Basi Tuboreshe Hii Iliyopo
Miongoni mwa walioteuliwa ni pamoja na watu wanaokubalika na vyama vya upinzani visiwani humo ikiwemo ACT Wazalendo ambacho ni chama kikuu cha upinzani na mshirika wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Katika orodha ya wajumbe hao walikuwepo Awadh Ali Said na Juma Haji Ussi ambao ni wananchama wa ACT Wazalendo na Halima Mohamed Said mwanachama wa chama cha upinzani ADA-TADEA.
Kufuatia uteuzi huo ACT Wazalendo ilitoa taarifa ya kuunga mkono uteuzi uliofanywa na Rais Mwinyi huku ikiwahimiza wajumbe hao kutimiza wajibu wa kusimamia sheria na kutenda haki.
Tundu Lissu kurejea nchini
Mnamo Januari 25, 2023 Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu, alipokelewa na maelfu ya Watanzania kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere wakati akitokea nchini Ubeligiji alipokwenda kuishi kwa sababu za kiusalama baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Kitendo cha Lissu kurejea kilitokana na matamko yaliyokuwa yakitolewa na Rais Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani akiwataka Watanzania waliondoka na kwenda kuishi uhamishoni kurejea nchini kwani mazingira ya sasa ni salama.
Kivutio kingine kikubwa kilichotokea ni pale siku ya mapokezi yake vyombo vya ulinzi na usalama vilivyoshiriki kikamilifu katika kuhakikisha usalama wa Watanzania waliojitokeza kumpokea Lissu.
SOMA ZAIDI: Je, Demokrasia ni Sharti Au Matokeo ya Maendeleo ya Kiuchumi?
Lissu aliondoka nchini kwenda nchini Kenya kwa matibabu kwa mara ya kwanza Septemba 7, 2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana.
Januari 6, 2018 alihamishiwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi hadi Julai 27, 2020 aliporejea nchini na kuwania nafasi ya Rais kupitia tiketi ya CHADEMA ambapo aliibuka mshindi wa pili katika uchaguzi huo uliolalamikiwa kutokuwa huru na wa haki. Hata hivyo Novemba 10, 2020 mara baada ya uchaguzi mkuu, Lissu aliondoka nchini kwenda Ubelgiji kwa madai ya kuhofia usalama wake.
Si Lissu pekee aliyerea nchini mwaka huu akitokea uhamishoni. Mwanachama mwingine wa chama cha CHADEMA aliyerejea ni pamoja na Godbless Lema, aliyekuwa mbunge wa jimbo la Arusha Mjini na mbunge wa kamati kuu ya chama hicho na Ezekiel Wenje mmoja wa viongozi wa kanda ya Serengeti wa CHADEMA na aliyewahi kuwa mbunge.
Licha ya mambo hayo ambayo yaliwapa tabasamu la pamoja pande hizi mbili, lakini baadhi ya mambo yafuatayo yaliwafanya waendelee kuishi kuhasimiana;
Sakata la mkataba wa bandari.
Kwa muda wa takribani miezi mitano suala hili lilizitikisa siasa za Tanzania. Hiyo ni baada ya Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi kuridhia mkataba wa uendelezaji wa bandari ya Dar es Salaam. Mkataba huo ulikuwa ni baina ya Tanzania na Serikali ya Dubai chini ya kampuni ya DP World.
SOMA ZAIDI: Rais Samia Ameanza Kujitafuta Upya, Chonde Asijipate kwa Magufuli
Suala hili liliwagawa Watanzania, Serikali ilionekana kulipigia chapuo suala hili kwa kile ilichodai DP World inakwenda kuongeza ufanisi wa bandari hiyo. Hata hivyo chama cha upinzani cha CHADEMA hakikuunga mkono mpango huo ambao ulielezwa kuwa ni wa kuuza rasilimali hiyo muhimu kwa nchi.
Si tu CHADEMA waliopinga mpango huo, Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (TEC) nalo pia lilipinga kwa kile walichodai kuwa Serikali inapaswa kutoa kipaumbele kwa Watanzania kumiliki na kuendesha nyezo kuu za uchumi wa nchi.
Baadhi ya mambo yaliyoibua mjadala katika mkataba huo ni jinsi zabuni ya kumpata muwekezaji zilivyotolewa na kikomo cha kuendesha baadhi ya shughuli kwenye bandari hiyo.
Baadhi ya wanaharakati walioonekana kupinga suala hili walijikuta katika wakati mgumu baadaya ya kukamatwa mara kadhaa na polisi na kufunguliwa kesi. Baadhi ya wanaharakati hao ni pamoja Wakili Boniface Mwabukusi, Dk Wilbroad Slaa pamoja na Mdude Nyagali.
Hata hivyo licha ya upinzani mkubwa juu ya mpango huo, Oktoba 22, 2023 Rais Samia Suluhu alishuhudia utiaji sahihi wa mikataba mitatu ya uwekezaji kati ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Serikali na DP World, akisema Serikali imezingatia maoni ya wadau wote waliozungumza kuhusu suala hilo kabla ya kusainiwa kwa mikataba hiyo.
Kuvunjika kwa mchakato wa maridhiano
Mwaka 2022 mchakato wa maridhiano ulianza kati ya Serikali ya CCM na vyama vya upinzani. Mazungumzo hayo yalipokewa vizuri na wapenda demokrasia nchini baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kukaa meza moja na vyama hivyo ili kusikiliza hoja zao.
Hata hivyo mwaka huu wa 2023, mchakato huo umeelezwa kukwama kabla ya muafaka wa maridhiano hayo kupatikana, ambapo kila upande umekuwa ukimyoshea mwenzake kidole kama chanzo cha kukwama huko.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema kwamba haridhishwi na namna mazungumzo yao yanavyoendelea kutokana na upande wa CHADEMA kutokuzingatia misingi ya kuingia katika makubaliano hayo. Kinana alisema wakati wanaingia kwenye mazungumzo hayo na CHADEMA, walikubaliana kufanya siasa za kistaarabu, kujenga hoja na kujibiwa kwa hoja, jambo alilosema wenzao wameliacha na kuanza kutukana viongozi majukwaani.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tanzania Bara Tundu Lissu yeye alikinyoshea Chama cha Mapinduzi (CCM) kidole kuwa kimekataa kuendelea kwa maridhiano kwa sababu chama hicho kimetupilia mbali mapendekezo yote 11 ambayo CHADEMA iliyawasilisha mbele ya vikao vyao na kukubalina.
Lissu alifafanua kuwa mapendekezo yote iliyokuwa imeyawasilisha yamekataliwa kwa maandishi jambo ambalo linaonesha CCM hawapo tayari kwa maridhiano.
Lissu alieleza kuwa CHADEMA itakuwa tayari kwa mazungumzo endapo Rais Samia na chama chake watabadilisha msimamo wao. Lissu alidai haikuwa dhamira ya CHADEMA kujiondoa kwenye mchakato huo lakini kitendo cha mapendekezo yao yote kukataliwa kimewaondolea imani dhidi ya kuendelea mjadala huo.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema maridhiano hayo hayana tija kwa Taifa kwa kuwa yanahusisha kundi dogo la watu walio ndani ya vyama hivyo, badala yake yangehusisha pia wadau wengine kama vile asasi za kiraia.
Matonyinga Makaro ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Mwanza. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia matonyingamakaro@gmail.com